Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alialikwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye
kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika kitaifa Uwanja wa
Sokoine mjini Mbeya Mei 1, 1995. Katika hotuba yake alieleza mengi, leo
tunachukua kipengele cha urais, alikuwa na haya ya kusema:
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere |
“Naeleza
baadhi ya matatizo ambayo viongozi tutakaowachagua tuwe na hakika iwapo
wanayaona hivi kama sisi tunavyoyaona. Yanawauma kama sisi yanavyotuuma
na kwamba, watakapofika hapo wanapopataka watusaidie kuyatatua.
“Wanayaona,
yanawakera na hata watakapofika hapo, hicho ndicho kitakachowasukuma
kutaka kuwa marais wetu na wabunge wetu. “Marekani walikuwa na rais wao
kijana mmoja mdogo anaitwa John Kennedy. Walimpiga risasi. Marekani nao
ni watu wa ajabu sana! Vijana walilaani tukio hilo kwa kuwa walikuwa
wanadhani wamemchagua rais wa umri wa kama miaka arobaini na mitatu au
minne hivi.
“Sasa
huyo ni kijana, hata kwa hapa Tanzania leo ni kijana. Alipochaguliwa na
Marekani akawa rais wao. Katika hotuba yake ya kwanza kabisa aliwambia
wananchi wenzake, hasa vijana “Usiulize Marekani itakufanyia nini,
jiulize wewe utaifanyia nini Marekani?”.
“Kila anayetaka kuwa mgombea wa urais/ubunge ajiulize ataifanyia nini nchi yake
“Tunataka mtu anayetaka kuwa rais wetu ajiulize anataka kuifanyia nini nchi yetu na sio nchi yetu itamfanyia nini.
“Na
tunataka swali hilo ajiulize kila mtu anayetaka kuwa mgombea wa chama
cho chote kuwa mbunge/rais: “Kwa nini, kwa dhati kabisa, anaumwa na
umasikini wetu na umasikini huo ndiyo unaomsukuma ashughulike na mambo
haya ya siasa katika ngazi hiyo ama ya ubunge ama ya urais”. Kama sivyo,
hatufai!
“Mtu hapakimbilii Ikulu: Hakuna Biashara Ikulu. Mtu
anayetaka kwenda ikulu kutaka faida yo yote ikulu pale, hatufai hata
kidogo. Wananchi, mimi nimekaa pale Ikulu kwa muda mrefu zaidi kuliko
mwingine ye yote, wala sidhani kuna mtu mwingine anaweza kuzidi muda
huo.
“Tayari
hapa tumeweka sheria. Kwa mujibu wa sheria, mtu hawezi tena kukaa Ikulu
zaidi ya miaka kumi, kipindi ambacho hata hakijafikia nusu ya kipindi
nilichokaa. Mimi nimekaa miaka ishirini na tatu!
“Najua, kwa
mtu halisi kabisa, Ikulu ni mzigo! Hupakimbilii! Si mahali pa
kupakimbilia hata kidogo; huwezi kupakimbilia Ikulu. Unapakimbilia
kwenda kutafuta nini?
“Ni
mgogoro; ni mzigo mkubwa kabisa! Ukipita barabarani, unakuta watu wana
njaa, unaona ni mzigo wako huo. Pazito pale! Huwezi kupakimbilia na watu
safi hawapakimbilii.
“Ukiona mtu anapakimbilia, na hasa anapotumia tumia vipesa kwenda Ikulu, huyo ni mtu wa kuogopa kama ukoma!
“Mtu
ye yote anayeonekana anapenda sana kwenda Ikulu na hata yupo tayari
kununua kura ili kumwezesha kufika Ikulu ni wa kumkwepa kama ukoma.
Kwanza, hizo fedha kapata wapi.
“Mtanzania wa leo hawezi kununua watu bila kwanza yeye kununuliwa.
Na
kama kanunuliwa, atataka kuzilipaje? Kazipata wapi? Watanzania wote ni
masikini tu. Mtanzania anaomba urais wetu kwa hela! Amezipata wapi?
“Pili, kama hajanunuliwa, kazipata wapi? Kama kakopa, atarudishaje?
Ikulu pana biashara gani mtu akope mamilioni halafu aende ayalipe kwa
biashara ya Ikulu? Ikulu mimi nimekaa kwa muda wa miaka ishrini na
mitatu.
“Ikulu ni mahali pazito. Kuna biashara gani Ikulu?
“Rushwa
na matumizi ya fedha bila utaratiba wakati wa chaguzi: Sisi Waafrika ni
watu wa ajabu sana. Unajua ni wadogo, lakini nasema, ni udogo wa
mawazo. Umaskini wa mawazo ni umasikini mbaya kupita wote.
“Unaweza ukawa na almasi mfukoni, akaja tapeli na kijiwe kimetengenezwa kama almasi akakuambia “hebu tuone almasi yako.
Bwana
aa! Hii ya kwako sio almasi ni chupa tu, almasi ni hii. Kwanza nipe
bwana.” Mkabadilishana. Yeye akachukua almasi yako na akakuachia kichupa
na ukatoka hapo unashangilia kama zuzu!
“Sisi
hapa Tanzania tulikuwa tumeanza utaratibu ambao ukitumia fedha nje ya
fedha za chama na serikali na ukatumia fedha zako mwenywe katika
uchaguzi, tunakutoa. Hufai! Huo ndio ulikuwa utaratibu wetu. Tulikuwa
tunakuuliza: “hii nchi ya maskini, wewe mwenzetu una mali umeipata
wapi?”
“Mali, kwa wakati
huo, kwetu sisi ilikuwa ni sifa ya kukunyang’anya uwezo wa kugombea
uongozi Tanzania. Tulijua kwamba, kama una mali, utaficha. Leo watu
wanasema waziwazi: “Mwalimu uchaguzi wa mwaka huu utapitishwaje?”
“Marekani
wanatumia fedha nyingi sana katika uchaguzi. Nyingi sana! Kama Marekani
sasa hivi wanazungumza watunge sheria inayofanana na ile mliyoitupa
ninyi mnadhani kwa sababu ni mawazo ya masikini, haina maana. “Wakubwa
wanayafikiria mawazo hayo sasa hivi. Marekani wanafikiria uwezekano sasa
wa kutunga sheria itakayoweka utaratibu wa fedha za ugombeaji kutokana
na mfuko mmoja baada ya kugundua kwamba inapokuwa holela na kila mtu
akiachiwa lwake, inavuruga.
“Inaleta
rushwa kubwa kabisa. Unanunuliwa urais na unaweza kununuliwa na fedha
za wauza bangi na wauza baa. Wauza bangi wanaiona hatari hiyo, ninyi
haa!“Hapa tulikuwa na utaratibu mzuri kabisa tuliouanzisha mlioutupa,
mnafikiri, sisi mwaka huu fedha tu! Uchaguzi wa fedha, mtazipata wapi?
Mimi nimetoka juzi tu, mara mmetajirika kiasi hiki!
No comments:
Post a Comment