Showing posts with label Speech. Show all posts
Showing posts with label Speech. Show all posts

Saturday, February 21, 2015

Wosia wa Baba Wa Taifa Kuhusu Urais - Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Mei 1, 1995

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alialikwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika kitaifa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Mei 1, 1995. Katika hotuba yake alieleza mengi, leo tunachukua kipengele cha urais, alikuwa na haya ya kusema:
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
“Naeleza baadhi ya matatizo ambayo viongozi tutakaowachagua tuwe na hakika iwapo wanayaona hivi kama sisi tunavyoyaona. Yanawauma kama sisi yanavyotuuma na kwamba, watakapofika hapo wanapopataka watusaidie kuyatatua.

“Wanayaona, yanawakera na hata watakapofika hapo, hicho ndicho kitakachowasukuma kutaka kuwa marais wetu na wabunge wetu. “Marekani walikuwa na rais wao kijana mmoja mdogo anaitwa John Kennedy. Walimpiga risasi. Marekani nao ni watu wa ajabu sana! Vijana walilaani tukio hilo kwa kuwa walikuwa wanadhani wamemchagua rais wa umri wa kama miaka arobaini na mitatu au minne hivi.

“Sasa huyo ni kijana, hata kwa hapa Tanzania leo ni kijana. Alipochaguliwa na Marekani akawa rais wao. Katika hotuba yake ya kwanza kabisa aliwambia wananchi wenzake, hasa vijana “Usiulize Marekani itakufanyia nini, jiulize wewe utaifanyia nini Marekani?”.
“Kila anayetaka kuwa mgombea wa urais/ubunge ajiulize ataifanyia nini nchi yake
“Tunataka mtu anayetaka kuwa rais wetu ajiulize anataka kuifanyia nini nchi yetu na sio nchi yetu itamfanyia nini.

“Na tunataka swali hilo ajiulize kila mtu anayetaka kuwa mgombea wa chama cho chote kuwa mbunge/rais: “Kwa nini, kwa dhati kabisa, anaumwa na umasikini wetu na umasikini huo ndiyo unaomsukuma ashughulike na mambo haya ya siasa katika ngazi hiyo ama ya ubunge ama ya urais”. Kama sivyo, hatufai!
“Mtu hapakimbilii Ikulu: Hakuna Biashara Ikulu. Mtu anayetaka kwenda ikulu kutaka faida yo yote ikulu pale, hatufai hata kidogo. Wananchi, mimi nimekaa pale Ikulu kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine ye yote, wala sidhani kuna mtu mwingine anaweza kuzidi muda huo.

“Tayari hapa tumeweka sheria. Kwa mujibu wa sheria, mtu hawezi tena kukaa Ikulu zaidi ya miaka kumi, kipindi ambacho hata hakijafikia nusu ya kipindi nilichokaa. Mimi nimekaa miaka ishirini na tatu!
“Najua, kwa mtu halisi kabisa, Ikulu ni mzigo! Hupakimbilii! Si mahali pa kupakimbilia hata kidogo; huwezi kupakimbilia Ikulu. Unapakimbilia kwenda kutafuta nini?
“Ni mgogoro; ni mzigo mkubwa kabisa! Ukipita barabarani, unakuta watu wana njaa, unaona ni mzigo wako huo. Pazito pale! Huwezi kupakimbilia na watu safi hawapakimbilii.

“Ukiona mtu anapakimbilia, na hasa anapotumia tumia vipesa kwenda Ikulu, huyo ni mtu wa kuogopa kama ukoma!
“Mtu ye yote anayeonekana anapenda sana kwenda Ikulu na hata yupo tayari kununua kura ili kumwezesha kufika Ikulu ni wa kumkwepa kama ukoma. Kwanza, hizo fedha kapata wapi.

“Mtanzania wa leo hawezi kununua watu bila kwanza yeye kununuliwa.
Na kama kanunuliwa, atataka kuzilipaje? Kazipata wapi? Watanzania wote ni masikini tu. Mtanzania anaomba urais wetu kwa hela! Amezipata wapi? “Pili, kama hajanunuliwa, kazipata wapi? Kama kakopa, atarudishaje? Ikulu pana biashara gani mtu akope mamilioni halafu aende ayalipe kwa biashara ya Ikulu? Ikulu mimi nimekaa kwa muda wa miaka ishrini na mitatu.

“Ikulu ni mahali pazito. Kuna biashara gani Ikulu?
“Rushwa na matumizi ya fedha bila utaratiba wakati wa chaguzi: Sisi Waafrika ni watu wa ajabu sana. Unajua ni wadogo, lakini nasema, ni udogo wa mawazo. Umaskini wa mawazo ni umasikini mbaya kupita wote.

“Unaweza ukawa na almasi mfukoni, akaja tapeli na kijiwe kimetengenezwa kama almasi akakuambia “hebu tuone almasi yako. 

Bwana aa! Hii ya kwako sio almasi ni chupa tu, almasi ni hii. Kwanza nipe bwana.” Mkabadilishana. Yeye akachukua almasi yako na akakuachia kichupa na ukatoka hapo unashangilia kama zuzu!
“Sisi hapa Tanzania tulikuwa tumeanza utaratibu ambao ukitumia fedha nje ya fedha za chama na serikali na ukatumia fedha zako mwenywe katika uchaguzi, tunakutoa. Hufai! Huo ndio ulikuwa utaratibu wetu. Tulikuwa tunakuuliza: “hii nchi ya maskini, wewe mwenzetu una mali umeipata wapi?”
“Mali, kwa wakati huo, kwetu sisi ilikuwa ni sifa ya kukunyang’anya uwezo wa kugombea uongozi Tanzania. Tulijua kwamba, kama una mali, utaficha. Leo watu wanasema waziwazi: “Mwalimu uchaguzi wa mwaka huu utapitishwaje?”

“Marekani wanatumia fedha nyingi sana katika uchaguzi. Nyingi sana! Kama Marekani sasa hivi wanazungumza watunge sheria inayofanana na ile mliyoitupa ninyi mnadhani kwa sababu ni mawazo ya masikini, haina maana. “Wakubwa wanayafikiria mawazo hayo sasa hivi. Marekani wanafikiria uwezekano sasa wa kutunga sheria itakayoweka utaratibu wa fedha za ugombeaji kutokana na mfuko mmoja baada ya kugundua kwamba inapokuwa holela na kila mtu akiachiwa lwake, inavuruga.

“Inaleta rushwa kubwa kabisa. Unanunuliwa urais na unaweza kununuliwa na fedha za wauza bangi na wauza baa. Wauza bangi wanaiona hatari hiyo, ninyi haa!“Hapa tulikuwa na utaratibu mzuri kabisa tuliouanzisha mlioutupa, mnafikiri, sisi mwaka huu fedha tu! Uchaguzi wa fedha, mtazipata wapi? Mimi nimetoka juzi tu, mara mmetajirika kiasi hiki!
--

Wednesday, December 31, 2014

Salamu za Mwaka Mpya Kutoka Kwa Rais Kikwete Kwa WaTanzania

SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE 31 DESEMBA, 2014
Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Kama ilivyo ada imefikia siku ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwaka mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2015. Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa ndugu na jamaa zetu ambao hawakujaliwa kuiona siku ya leo tuzidi kuwaombea mapumziko mema. Nasi tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema atujaalie umri mrefu, afya njema na mafanikio tele kwa kila tuliombalo katika mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ndugu wananchi;
Hizi ni salamu zangu za mwisho za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi yetu. Mwakani salamu kama hizi zitatolewa na Rais wetu mpya. Mimi wakati huo nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga nikifuatilia kwenye TV na radio hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu akitoa salamu zake za kwanza za mwaka mpya, itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa kwangu.
Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza mwaka 2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko salama na hakuna tishio lolote la kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi yetu. Uhusiano wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani ni mzuri. Hakuna nchi iliyo adui au tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha usalama wa Tanzania. Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa salama.
Uhalifu Unapungua
Ndugu Wananchi;
Taarifa za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu vimepungua ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa Polisi yalikuwa 64,088 ikilinganishwa na matukio 66,906 katika mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na raia wema. Naomba ushirikiano huu uendelee mwaka ujao na miaka ijayo ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Ajali za Barabarani
Ndugu Wananchi;
Nimefarijika kusikia pia kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini nayo yanaendelea kupungua. Mwaka huu kumetokea ajali 14,048 zilizosababisha vifo vya watu 3,534 na wengine 16,166 kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali 22,383 zilizosababisha vifo 3,746 na majeruhi 19,433. Hivyo mwaka huu kulikuwa na ajali 8,335, vifo 212 na majeruhi 3,267 pungufu kuliko mwaka jana. Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo ingawa bado ni nyingi mno. Naomba yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha kupata unafuu huu mwaka huu yaendelezwe maradufu mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ugaidi
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia mabomu na kumwagia watu tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu 112 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wametiwa nguvuni. Tayari watuhumiwa 87 kati yao wameshafikishwa mahakamani na waliosalia watafikishwa wakati wo wote. Uchunguzi unaendelea ili kuwatambua wahusika wengine ambao hawajakamatwa.
Ndugu wananchi;
Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya kutambua mtandao wa ugaidi nchini na kuchukua hatua thabiti za kuudhibiti. Hali kadhalika nawashukuru raia wema waliotoa taarifa zilizowezesha haya kufanyika. Hatupaswi kubweteka wala kudhani kuwa mambo yamekwisha. Lazima tuendelee kuchukua tahadhari muda wote kwani hatujui adui anapanga kufanya hujuma gani, lini na wapi.
Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa 935 wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19 zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine, kilo 45 za cocaine na kilo 81,318 za bangi zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kukabiliana na dawa za kulevya nchini kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana. Matunda ya kazi yao tunayaona. Naomba juhudi ziongezwe maradufu mwaka ujao na miaka ijayo. Serikali itaendelea kuwaunga mkono.
Ndugu wananchi;
Kama nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu. Pamoja na kupendekeza kuongeza adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, Muswada huo pia unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye nguvu cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu ukipitishwa na kuwa Sheria tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Ujangili wa Wanyamapori
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka tunaomaliza leo mapambano dhidi ya ujangili na biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori yameimarishwa. Kwa ujumla kasi ya ujangili imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa ikilinganishwa na ndovu 219 waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473 mwaka 2012. Aidha, majangili 1,354 wamekamatwa na pembe za ndovu 542 na silaha mbalimbali 184 nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala yaani Tanzania Wildlife Agency (TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi wanyama pori na mapambano dhidi ya ujangili.
Natoa pongezi nyingi kwa askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Serikali na raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na mafanikio yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana na ujangili na biashara haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori zitaendelezwa kwa nguvu zaidi mwaka ujao 2015 na miaka inayofuatia. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu wa maendeleo wanaotuunga mkono kwa hali na mali katika mapambano haya. Naomba waendelee kutusaidia.
Hali ya Uchumi Jumla
Ndugu wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri kwa uchumi wa taifa. Uzalishaji katika sekta nyingi ulikuwa ni mzuri. Ndiyo maana tunategemea kuwa tutafikia au hata kuvuka lengo tulilojiwekea la pato la taifa kukua kwa asilimia 7.4 mwaka huu. Mwaka 2013 pato la taifa lilikua kwa asilimia 7.3. Mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014 ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwa asilimia 6.0. Hali nzuri ya upatikanaji wa chakula nchini imesaidia sana kufanya mfumuko wa bei kuendelea kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa bei utaendelea kushuka na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.
Mauzo Nje
Ndugu Wananchi;
Mauzo nje yameendelea kuongezeka. Katika kipindi kilichoishia Oktoba 31, 2014, Tanzania iliuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani milioni 8,503.9 ukilinganisha na mauzo ya dola milioni 8,332.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2013. Mapato yetu yangekuwa makubwa zaidi kama bei za kahawa, chai, korosho na pamba zisingeanguka au bei ya dhahabu nayo isingepada.
Akiba ya Fedha za Kigeni
Ndugu Wananchi;
Akiba yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekani milioni 4,251.8 kwa kipindi kilichoishia Novemba 30, 2014. Kiasi hicho kinatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje kwa miezi 4.1. Hii ni chini ya lengo letu la kuwa na akiba ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa kwa miezi minne na nusu. Hata hivyo, sina wasiwasi kabisa kwamba tofauti hii ndogo tutaweza kuiziba mwaka 2015.
Mapato ya Serikali
Ndugu Wananchi;
Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba, 2014 yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama hicho mwaka 2013 hadi shilingi bilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo yalikuwa asilimia 90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 4,459.7. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu mbalimbali zilizosababisha lengo lisifikiwe katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2014/2015. Hatua zipasazo zinaendelea kuchukuliwa kurekebisha mambo hayo ili katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha makusanyo yafikie lengo na ikiwezekana yazidi ili kufidia pengo la nusu ya kwanza.
Takwimu Mpya za Pato la Taifa
Ndugu wananchi,
Ni utaratibu wa kawaida wa nchi zote duniani kuwa na mwaka unaotumika kuwa kizio (base year) cha kukokotoa takwimu za Pato la Taifa. Ni utaratibu wa kawaida pia kwa kila baada ya muda fulani mwaka wa kizio hubadilishwa. Lengo ni kuboresha takwimu husika. Katika marekebisho hayo pia huingizwa thamani ya bidhaa na huduma mpya katika pato la taifa na kuziondoa zilizotoweka ili kutoa picha halisi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Katika miaka ya hivi karibuni nchi za Ghana (mwaka 2010), Nigeria (mwaka 2013) na Kenya (mwaka 2014) wamefanya marekebisho ya takwimu zao za pato la taifa. Na sisi Tanzania tumefanya hivyo mwaka huu (2014). Hii ni mara ya tano kwa nchi yetu kurekebisha takwimu za pato la taifa. Mara nne zilizopita ilikuwa mwaka 1966, 1976, 1992 na 2001.
Ndugu wananchi;
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekamilisha marekebisho ya takwimu za pato la taifa na kukokotoa takwimu mpya kwa kutumia mwaka 2007 kama mwaka wa kizio. Kutokana na marekebisho yaliyofanyika, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 70 kwa kutumia bei za mwaka 2007. Ukitumia bei za mwaka 2001, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 53.17. Kuongezeka kwa pato la taifa kumeongeza pia pato la wastani la kila Mtanzania kutoka shilingi 1,186,200 (sawa na US$ 742) kwa bei za mwaka 2001 hadi shilingi 1,560,050 (sawa na US$ 977) kwa bei za mwaka 2007.
Kilimo na Chakula
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini. Uzalishaji ulikuwa tani milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni 14.38 mwaka wa jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni 1.64. Kwa mujibu wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani milioni 3.25. Katika ziada hiyo, mahindi yanachangia tani milioni 1.55, mchele tani 794,000 na kiasi kinachobakia kinachangiwa na mazao mengine ya chakula.
Ndugu wananchi;
Kuna jambo moja muhimu kuhusu ununuzi wa nafaka ambalo ningependa kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga wote na mtama wote unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua sehemu ndogo tu ya nafaka ya ziada iliyozalishwa na hununua kwa ajili ya kuweka akiba ya taifa ya chakula cha kutumika wakati wa dharura ya watu kupata tatizo la njaa. Aidha, Wakala hununua kiasi kinacholingana na uwezo wa maghala yake kuhifadhi. Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni kuhifadhi tani 246,000 ingawaje tunaendelea kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa kuhifadhi tani 400,000 ifikapo 2015. Hivyo basi kwa Wakala kununua tani 292,415.41 mwaka huu ina maana kwamba kiasi cha karibu tani 50,000 zinahifadhiwa nje ya maghala kwa kutumia maturubai. Huu siyo utaratibu mzuri na haifai kuendelea nao kwani kuna hatari ya nafaka hiyo kuharibika na kuzua mgogoro mkubwa siku moja.
Ndugu wananchi;
Baada ya NFRA kununua tani 292,415.41 kuna takribani tani milioni 2.96 za nafaka ya ziada ambayo iliyobaki mikononi mwa wakulima. Mategemeo yetu ni kuwa wafanyabiashara wetu watanunua nafaka hiyo kwa ajili ya kuuza mijini na kwingineko inakohitajika. Bahati mbaya mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka wa jana, wafanyabiashara wetu hawakuweza kununua nafaka yote ya ziada ambayo Serikali haikuweza kununua kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hali hii imezua tatizo ambalo Serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara nchini hatuna budi kulitafutia majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko mengine ndani na hata nje ya nchi ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa ziada. Nimeagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa chini na kushirikiana na wafanyabiashara kulitafutia ufumbuzi suala hili lenye maslahi makubwa kwa wakulima na nchi yetu kwa jumla.
Ndugu Wananchi;
Katika mazingira haya, ninapopata taarifa ya kuwepo watu wanaotaka kuuza mahindi nje ya nchi lakini wanawekewa vikwazo na maafisa wa Serikali inanishangaza na kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya hivyo waache mara moja na badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao kufanikisha azma yao. Hali kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao wajitokeze kufanya biashara hiyo. Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo.
Miradi ya Kimkakati
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2014 utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 2015/16) umeendelea vizuri. Tunayo matumaini makubwa kwamba katika mwaka 2015 miradi mingi itakamilika.
Tuanze na Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dar es Salaam. Mradi huu unategemewa kukamilika Januari, 2015. Utakapokamilika utatuwezesha kutimiza lengo letu la kuzalisha MW 2,780 za umeme ifikapo 2016. Mipango ya kupata ardhi ya ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asili kuwa ya kumiminika (LNG) ili iweze kusafirishwa kwenda kwenye masoko, inakwenda vizuri.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati wa kusambaza umeme vijijini umeendelea vizuri na tumepata mafanikio makubwa yasiyokuwa na mfano wake katika historia ya nchi yetu. Hadi kufikia Novemba, 2014, jumla ya vijiji 3,836 vimepatiwa umeme na vingine 1,500 vinategemewa kupatiwa umeme ifikapo Juni, 2015. Hivyo basi, vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423 vya Tanzania Bara vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa na asilimia 43 ya vijiji vyote nchini vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi sasa wananchi milioni 17.3 nchi nzima sawa asilimia 36 wamefikiwa na huduma ya umeme ikilinganishwa na watu milioni 8.1 sawa na asilimia 18.4 waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015 tunatarajia watu milioni 18.2 sawa na asilimia 38 watafikiwa na umeme. Kwa upande wa vijijini mwaka 2012 watu milioni 2.3 sawa na asilimia 7 walikuwa na umeme. Ifikapo Juni 2015, idadi hiyo itaongezeka na kuwa milioni 7.4 sawa na asilimia 21. Haya ni mafanikio makubwa kwa wananchi wengi vijijini na mijini kupata umeme katika kipindi kifupi kiasi hiki. Ni mageuzi ya aina yake yatokayotoa mchango muhimu katika kuinua hali za maisha ya Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Tunaanza kuiona nuru ya matumaini kwamba siku si nyingi kutoka sasa, makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya chuma ya Liganga yataweza kutumika kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wa Ludewa. Maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015 kuanza ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe kule Mchuchuma, mtambo wa kufua umeme, ujenzi wa mgodi wa chuma kisichoyeyushwa pale Liganga na ujenzi wa kiwanda cha kuyeyusha chuma.
Natoa pongezi maalum kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wabia wenzao, Kampuni ya Sichuan Hongda ya China kwa hatua iliyofikiwa. Inakadiriwa kuwa miradi hii ikikamilika itatoa ajira 33,000 za moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja.
Ndugu Wananchi;
Mradi mwingine mkubwa wa kimkakati ni ule wa kujenga Eneo Maalumu la Kiuchumi (Special Economic Zone) la Mbegani, Bagamoyo. Kwa mujibu wa mpango kazi wa wabia wa mradi huo yaani Mamlaka ya Kuendeleza Maeneo huru ya Uwekezaji (EPZA), Kampuni ya China Merchants Holdings International na Mfuko wa Uhifadhi wa Akiba ya Mali za Serikali ya Oman (Oman State General Reserve Fund), ujenzi wa bandari na miundombinu mingine itakayowezesha viwanda kujengwa imepangwa kuanza Julai 2015.
Miundombinu ya Usafiri na Uchukuzi
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga barabara za lami na kuimarisha barabara za udongo ili ziweze kupitika wakati wote ziliendelea kote nchini. Huu nao ni mradi mkubwa wa kimkakati. Barabara za lami 19 zenye urefu wa kilometa 1,459 zimekamilika kujengwa mwaka huu katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga, Morogoro, Arusha, Tabora na Shinyanga. Ujenzi unaendelea kwa barabara nyingine 24 katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa, Simiyu, Katavi, Tabora, Mwanza, Dar es Salaam, Kagera na Pwani ambazo wakati wo wote mwaka 2015 zitakamilika. Maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara nyingine nane yanaendelea vizuri sehemu mbalimbali nchini.
Kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara, tumeendelea kufanya kazi ya ujenzi na ukarabati wa barabara za udongo kote nchini. Mwaka huu Mfuko huo umetengewa shilingi bilioni 751.7 ukilinganisha na shilingi bilioni 504.4 mwaka jana. Aidha, mwaka huu tumeweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero. Matumini yetu ni kuwa ujenzi wa daraja hilo na Daraja la Kigamboni utakamilika mwaka 2015. Ujenzi wa Daraja la Malagarasi ulishakamilika mwaka jana, kinachosubiriwa ni sherehe ya uzinduzi.
Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, tunategemea kukamilisha ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya barabara za mabasi yaendayo kasi. Ni matarajio yetu pia kwamba mabasi yataanza kusafirisha abiria katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Halikadhalika, tunategemea katika mwaka 2015 ujenzi utaanza wa barabara zinazozunguka jiji la Dar es Salaam (ring roads), barabara ya Mwenge - Morocco na ile ipitayo juu ya nyingine (flyovers) eneo la TAZARA. Vile vile, daraja jipya la Salenda litaanza kujengwa. Aidha, kivuko cha abiria 300 cha MV Dar es Salaam kitaanza kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam Kaskazini na Ferry mapema mwakani. Hatua zote hizi zinalenga kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Usafiri wa Anga na Reli
Ndugu wananchi;
Jitihada za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati zimeendelea kwa mafanikio. Mwaka huu vichwa vinane vya treni vimekarabatiwa, mabehewa mapya 22 ya abiria na mabehewa 274 ya mzigo yamenunuliwa. Mabehewa hayo yameanza kuwasili nchini kati ya Novemba na Desemba mwaka huu. Kati ya Januari na Mei, 2015 tunatarajia kupokea vichwa vipya vya treni 13. Uboreshaji huu wa huduma za treni unakwenda sambamba na ukarabati wa reli yenyewe, ujenzi wa madaraja na kuimarisha maeneo yaliyo korofi katika reli hiyo.
Kuhusu ujenzi wa reli iliyo pana zaidi (standard guage), yenye uwezo wa kubeba mabehewa mengi na kuwezesha treni kwenda kwa mwendo wa kasi zaidi, juhudi za kutafuta fedha za ujenzi au wabia wa kushirikiana nasi kujenga zinaendelea. Wakati huo huo, tunaendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya reli ya TAZARA ili mambo yaende vizuri. Tutashirikiana kwa karibu na wabia wenzetu wa Zambia. Bahati nzuri Serikali ya China iko tayari kuunga mkono juhudi zetu za kufufua reli ya TAZARA.
Usafiri wa Anga
Ndugu Wananchi;
Sekta ya usafiri wa anga imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi ya abiria wanaowasili na kutoka katika viwanja vyetu vya ndege nchini imeongezeka kutoka abiria milioni 2.5 mwaka 2013 hadi abiria milioni 3.5 kufikia Septemba, 2014. Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi za nje zimeongezeka kutoka 274 Januari, 2013 hadi 295 kufikia Septemba, 2014. Hili ni ongezeko la asilimia 8. Safari za ndege ndani ya nchi nazo zimeongezeka kutoka safari 230,458 mwaka 2013 hadi safari 241,922 mwaka 2014. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 39. Maongezeko haya ni kielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii na biashara nchini zimeendelea kukua.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa Jengo la 3 (Terminal 3) la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea vizuri. Jengo hilo litakapokamilika mwakani, litakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa abiria milioni 8 kwa mwaka. Aidha, ukarabati wa Jengo la 2 (Terminal 2) utafanyika ili liweze kutoa huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na ujenzi huo, Wakala wa Viwanja vya Ndege wameendelea kukarabati na kuboresha viwanja vya ndege vya KIA, Mwanza, Songwe, Bukoba, Tabora na Kigoma. Tunatarajia ukarabati wa viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga kuanza mapema mwaka 2015.
Elimu
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupiga hatua za kuridhisha katika kuboresha elimu nchini. Tumefanikiwa kupunguza tatizo la upungufu wa maabara, vitabu na walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeajiri walimu 36,339 kati ya 81,562 wanaohitajika. Tumebakiwa na upungufu wa walimu 45,223 yaani 26,946 wa shule za msingi na 18,277 wa shule za sekondari hususan wa masomo ya sayansi. Hivi sasa hatuna tatizo la walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari.
Mwaka huu tumeanza mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya Diploma ya Ualimu kwa masomo ya sayansi na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo jumla ya wanafunzi 5,602 wa masomo hayo wamedahiliwa. Mpango huu utatuwezesha kupunguza pengo kubwa tulilonalo la walimu wa sayansi katika muda mfupi zaidi.
Ujenzi wa Maabara
Ndugu wananchi;
Ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari za Kata 3,463 umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa zijengwe maabara 10,389 ilipofika Novemba, 2014. Taarifa kutoka TAMISEMI zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 29, 2014, maabara 4,207 sawa na asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688 sawa na asilimia 54.8 zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na maabara 494 sawa na asilimia 4. zilikuwa katika hatua za awali za ujenzi.
Ndugu Wananchi;
Natoa pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini pamoja na wananchi, kwa jitihada kubwa iliyofanyika. Kwa kutambua jitihada hizo, nimeongeza miezi sita zaidi kwa wale ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo wafanye hivyo. Sikusudii kuongeza tena muda baada ya hapo. Naomba watumie kipindi hicho kitumike kutafuta vifaa vya maabara. Serikali itasaidia upatikanaji wa watunza maabara (laboratory technicians) ambao tumeanza programu kubwa ya mafunzo yao na mahitaji mengine ya maabara.
Ununuzi wa Vitabu
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya kufundishia katika shule za msingi na sekondari. Tumekuwa tunanunua vitabu kwa kutumia Bajeti ya Serikali na misaada kutoka kwa marafiki zetu wa maendeleo. Kwa mfano, Serikali ya Marekani imetupatia vitabu milioni 2.5 vya masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari. Ongezeko hili la vitabu linashusha uwiano uliopo sasa wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili. Lengo letu ni kila mtoto kuwa na kitabu chake kwa kila somo ifikapo mwaka 2016.
Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Ndugu wananchi;
Mafanikio mengine tuliyopata mwaka huu ni kukamilika kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Hii ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya elimu nchini hakuna badala yake. Sera mpya inalenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa za elimu iliyo bora na inayolinga na wakati tulionao. Jambo jipya sana na la kihistoria katika Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa ada katika elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule za msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari. Kwa mujibu wa maelezo hayo ya Sera, nimekwishatoa maagizo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango kuanza kutafakari namna jambo hilo litakavyotekelezwa.
Afya
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2014 jitihada za kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na mlipuko wa homa ya dengue iliyowapata watu 1,039 na kusababisha vifo vya watu 3 kati yao. Kwa upande wa maradhi ya ebola tumejiandaa vya kutosha kutambua watu wenye maradhi hayo wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege vya kimataifa na vituo vyote vya mpakani. Aidha, tumejipanga vyema kuwahudumia wagonjwa wa maradhi hayo iwapo watatokea.
Mwaka huu pia, Madaktari wetu watano wamekwenda Liberia kusaidiana na ndugu zetu wa huko katika kukabiliana na ugonjwa wa ebola. Madaktari wetu hao wako salama na wanaendelea vizuri kutoa huduma. Madaktari hao watakaporejea nchini watakuwa hazina kubwa ya taifa katika kupanga mipango ya kukabiliana na ugonjwa huu hatari. Hali kadhalika, watakuwa viongozi wa wengine katika kutibu wagonjwa wa maradhi ya ebola iwapo watatokea nchini.
Ndugu Wananchi;
Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri watumishi wa sekta ya afya 8,345 ambao kati yao kuna madaktari 244, madaktari bingwa 75, wauguzi 2,555 na wataalamu wa kada nyingine za afya 5,471. Mwaka huu pia tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 7,956 katika mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi 9,730. Kwa ongezeko hilo, sasa tumefikia asilimia 97 ya lengo letu la kudahili wanafunzi 10,000 ifikapo mwaka 2017.
Jitihada zetu za kuongeza fursa za mafunzo kwa Madaktari, Wauguzi na wataalamu wengine wa afya zina muelekeo mzuri. Ujenzi wa hospitali ya kufundishia pale Mloganzila unaendelea vizuri na hospitali ya kufundishia ya Chuo Kikuu cha Dodoma umekamilika. Ni matarajio yangu kuwa wakati wo wote mwakani ujenzi wa kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila utaanza. Ujenzi huo ukikamilika Chuo kikuu cha Muhimbili kitaweza kudahili wanafunzi 12,000 kutoka wanafunzi 2,500 wa sasa jambo ambalo litafanya upungufu wa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wa Afya kupata jawabu la uhakika. Tumeendelea kufanya mambo mengine ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba za ubongo na mishipa ambalo limekamilika pale Muhimbili, sasa tunahangaikia kupata vifaa.
Maji
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu wa 2014 tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuwapatia wananchi maji safi na salama mijini na vijijini. Kwa ajili hiyo miradi 498 ya maji vijijini imekamilika na miradi 740 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine 378 ipo katika maandalizi ya ujenzi kuanza. Ni matarajio yetu kwamba katika mwaka ujao wa 2015, miradi mingine 731 itatekelezwa na vituo 25,790 vya kuchota maji vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza kuwafikia asilimia 71 ya wananchi wanaopata maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 58 ya sasa. Kwa ajili hiyo, tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la kuwapatia watu maji asilimia 65 ya Watanzania waishio vijijini ifikapo 2015. Ombi langu kwa ndugu zetu wa Hazina waiangalie sekta hii ya maji kwa ukaribu zaidi na wawapatie fedha kwa wakati.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga Same Mkomazi pamoja na miji na vijiji vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015. Fedha zimekwishapatikana na Mkandarasi wa Awamu ya Kwanza ameshapatikana. Makandarasi wa Awamu ya Pili na Tatu watapatikana muda si mrefu kutoka sasa. Hii pia itahusu kupata Mkandarasi wa mradi wa maji wa mji wa Orkesment.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu miradi ya kuipatia maji miji kadhaa nchini ilikamilika na tatizo la upungufu wa maji litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ipo miji kadhaa ambayo miradi imefikia hatua ya juu na kwamba wakati wowote mwakani itakamilika. Jiji la Dar es Salaam lipo katika kundi hili. Kazi ya upanuzi wa miradi ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa msaada wa Serikali ya Marekani na mkopo kutoka Serikali ya India imefikia hatua nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Mwaka ujao pia visima virefu vya Kimbiji na Kipera vitachimbwa na Bwawa la Kidunda litaanza kujengwa.
Serikali ya India pia imekubali kutupatia mkopo wa Dola za Marekani milioni 268.2 kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji miji ya Tabora, Nzega na Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa kujumuisha miji ya Sikonge na Urambo katika mradi huo utaangaliwa.
Bunge na Mahakama
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2014, mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea kutekeleza vyema majukumu yao. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza kuendesha shughuli zake kama ilivyopangwa pamoja na kulazimika kugawana Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum la Katiba. Bunge limefanya mikutano mitatu, Miswada 17 ya Sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza, Sheria tano na maazimio saba yalipitishwa. Maswali ya msingi 569 na ya nyongeza 1,541yaliulizwa na kujibiwa. Aidha, sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow nalo lilijadiliwa na kutolewa maazimio. Tumeshaanza kuchukua hatua kuhusu maazimio hayo na bado tunaendelea.
Napenda kuitumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wabunge wetu kwa kutekeleza vizuri wajibu wao wa Kutunga Sheria na kusimamia Serikali. Nawasihi waendelee na msimamo huo mwema na chanya kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mahakama napenda kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa ya kupunguza mrundikano wa mashauri katika Mahakama za ngazi zote. Wahenga wamesema mcheza kwao hutunzwa. Hatuna budi kutoa pongezi maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kwa uongozi wake mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wamejiwekea malengo ya kusikiliza na kutoa hukumu kwa mashauri yasiyopungua 200 kwa mwaka kila mmoja wao.
Habari njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea vizuri. Mashauri 870 yalisikilizwa na kuamuliwa kwenye Mahakama ya Rufani, mashauri 11,334 kwenye Mahakama Kuu, mashauri 8,715 kwenye Mahakama ya Mahakimu Wakazi na Mashauri 25,683 katika Mahakama za Wilaya. Aidha, mkakati wa kupeleka timu ya Majaji wa Mahakama Kuu kwa wakati mmoja kwenye maeneo yenye mashauri mengi kama ilivyofanyika Kigoma, Shinyanga na Tabora umesaidia sana kupunguza mrundikano wa mashauri ya siku nyingi. Haijawahi kutokea mashauri mengi kiasi hicho kusikilizwa na kumalizwa katika historia ya Mahakama nchini.
Ndugu Wananchi;
Mkakati huu mpya umeleta matumaini mapya kwamba tatizo la kuchelewesha kwa mashauri ambalo lilidhaniwa kuwa ni tatizo sugu sasa limeanza kupatiwa ufumbuzi. Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote natoa shukrani na pongezi nyingi kwa Jaji Mkuu, Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wa ngazi zote kwa kazi nzuri waifanyayo.
Hali kadhalika, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama na watendaji wote wa Mahakama kwa kazi nzuri waifanyayo ya kuwawezesha Majaji na Mahakimu kutimiza ipasavyo majukumu yao. Hakika utendaji Mahakamani umebadilika na kuwa bora zaidi. Mimi naahidi kuendelea kusaidia Mahakama kwa kuwahimiza ndugu zetu wa Hazina kutoa kwa wakati pesa zilizotengwa katika bajeti.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yameendelea bila ya ajizi. Katika mwaka huu wa 2014 TAKUKURU wamepokea taarifa 237 na wamekamilisha uchunguzi wa mashauri 545. Watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni 428. Mashauri yaliyomalizika ni 205, kati ya hayo 125 watuhumiwa waliachiliwa na 80 walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Mwaka huu wa 2014 mali na fedha taslimu zenye thamani ya shilingi bilioni 38.96 zimeokolewa. Katika kuimarisha Taasisi hiyo kiutendaji, maafisa wapya 394 wameajiriwa.
Sherehe za Miaka 50 ya Muungano
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu wa 2014 tuliadhimisha miaka 50 ya Muungano wa nchi zetu mbili yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kwa heshima inayostahili. Maadhimisho yalifikia kilele tarehe 26 Aprili, 2014 na zilifanyika sherehe nchini kote na sherehe hizo zilifana sana. Ni ukweli usiopingika kuwa kwa Muungano wetu kuweza kudumu kwa nusu karne ukiwa bado imara na unazidi kustawi ni mafanikio makubwa. Matumaini kwa siku za usoni ni mazuri. Naamini Muungano wetu utaimarika zaidi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwani yale mambo yenye kuleta matatizo hivi sasa yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Miaka 50 ya JWTZ
Ndugu Wananchi;
Wakati nchi inasherehekea miaka 50 ya Muungano, baadhi ya vyombo na taasisi muhimu kitaifa zilifanya hivyo hivyo. Miongoni mwa walioadhimisha nusu karne ya kuundwa kwake ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kama mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe 1 Septemba, 1964. Jeshi letu liliadhimisha siku yao hiyo kwa kufanya zoezi kubwa la kivita lililoanza Kibaha mkoani Pwani na kumalizikia Monduli Mkoani Arusha.
Nilibahatika kushuhudia siku ya mwisho ya zoezi hilo. Nilifurahishwa sana na kiwango cha utayari kivita cha Jeshi letu. Wanajeshi wetu walionesha weledi wa hali ya juu, umahiri mkubwa, ujasiri, ukakamavu na uvumilivu wa aina yake wakati wa kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu ya uwanja wa medani za vita. Niliwapongeza siku ile na narudia tena leo kuwapongeza. Niliyoyaona yamenihakikishia mimi na Watanzania wote kuwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liko imara kulinda mipaka ya nchi yetu na kuhakikisha usalama wa taifa letu na watu wake. Jeshi letu bado ni lile tunalolijua sisi sote, lakini limezidi lile lililomngoa mvamizi Dikteta Iddi Amin wa Uganda, tena limezidi kwa mbali.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu pia tumeshuhudia kukamilika kwa zoezi muhimu la kuandika Katiba Inayopendekezwa. Kama tujuavyo sote, mchakato uliozaa Katiba Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo lilikamilisha kazi yake kwa salama siku mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba, 2014 ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho. Mimi na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein tulikabidhiwa nakala za Katiba Inayopendekezwa tarehe 8 Oktoba, 2014. Nimeshatimiza wajibu wangu wa kuchapisha katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni kuwa tarehe 30 Aprili, 2015. Nimeshatoa maagizo kwa Tume ya Uchaguzi kufanya matayarisho husika ya kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika.
Ndugu Wananchi;
Moja ya mambo muhimu ambayo Tume ya Uchaguzi inafanya kwa sasa ni kuandikisha wapiga kura katika Daftari la Mpiga Kura. Tume imeamua kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Register. Uandikishaji wa majaribio umefanyika katika baadhi ya Kata katika Majimbo ya Mlele, Kawe na Kilombero. Matatizo yaliyojitokeza yatasaidia kuboresha mfumo huo kabla ya uandikishaji wa watu wote wenye sifa stahiki kuanza.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuwafahamisha Watanzania wenzangu wote kuwa mfumo mpya unatengeneza Daftari Jipya la Mpiga Kura ingawaje lugha inayotumika ni uboreshaji wa Daftari la sasa. Uboreshaji huu wa Daftari la Mpiga Kura ni tofauti na ule tuliouzoea ambapo walikuwa wanaandikishwa wapiga kura wapya na wale waliopoteza vitambulisho vyao. Safari hii wanaandikishwa wote wapya na wa zamani na wote watapata vitambulisho vipya. Hivyo basi, sisi wenye vitambulisho vya kupiga kura vya zamani tusifanye ajizi, tujitokeze kujiandikisha wakati ukifika.
Jambo la pili ni kwamba, Daftari la Mpiga Kura linalotayarishwa siyo kwa ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa peke yake, daftari hilo hilo litatumika pia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo basi, kujiandikisha ni jambo muhimu sana. Usipofanya hivyo siyo tu utajinyima fursa ya kushiriki kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa bali pia utakosa fursa ya kuchagua Rais wako, Mbunge wako na Diwani wako. Katu usikubali yakukose hayo.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo tarehe 14 Desemba, 2014 na 20 Desemba, 2014 ulifanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Uchaguzi umekwisha na viongozi wamekwishapatikana. Sasa ni wajibu wa viongozi hao kufanya kazi waliyoiomba. Kwa walioendesha uchaguzi ni wakati mzuri wa kufanya tathmini ili wapate mafunzo yatokanayo na uchaguzi huo. Kwa TAMISEMI na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, lengo liwe ni kuona namna ya kuimarisha mazuri na kusahihisha makosa na matatizo yaliyojitokeza. Kwa walinzi wa amani watambue matatizo ya kiusalama yaliyotokea na kuona namna ya kutengeneza mikakati ya kuzuia matatizo ya namna hiyo yasijitokeze tena. Hatma ya yote, shabaha yetu ni kutaka kufanya vizuri zaidi katika chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa na kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni zamu yetu kwa mujibu wa mzunguko wa uongozi wa Jumuiya yetu kati ya nchi wanachama. Ni dhamana kubwa na kwamba wenzetu wa Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze katika kutekeleza malengo na madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa katika Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika, tunategemewa kuongoza katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya vikao vya Jumuiya. Hii inahusu maamuzi yaliyokwishafanywa kabla yetu ambayo utekelezaji wake unaendelea na uamuzi mpya utakaofanywa katika kipindi cha uongozi wetu.
Kwa niaba ya Watanzania wote napenda kuwashukuru ndugu zetu wa Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda kwa kutuamini. Napenda kuahidi kuwa hatutawaangusha. Sisi Watanzania tutafanya kila tuwezalo kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa manufaa ya Jumuiya yenyewe, nchi zetu na wananchi wa Afrika Mashariki. Tutajitahidi kuwa wabunifu kwa nia ya kuona utangamano unakua na kustawi kwa kasi na kuzaa matunda ya maendeleo tunayoyatarajia sote. Matunda tuliyoyatarajia tulipoamua kuanzisha Jumuiya hii na matunda tuliyoyapata tulipoamua kwa hiari yetu kujiunga nayo kuwa wanachama.
SADC, AU NA UN
Ndugu Wananchi;
Kuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, tunaahidi kuendelea kuwa wanachama waaminifu na kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mashirika haya ya kikanda na kimataifa. Kwa upande wa SADC tutaendelea kushiriki katika utekelezaji wa mikakati na mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ile ya kisiasa na kiusalama kama ilivyoainishwa katika RISDP (Regional Indicative Strategic Development Plan) na SIPO (SADC Strategic Indicative Plan for the Organ). Kwa ajili hiyo Tanzania, itaendelea kutoa mchango wake katika kukuza utangamano wa kiuchumi katika SADC na kusaidia kuimarisha uhusiano mwema na usalama miongoni mwa nchi wanachama wa SADC. Hii ni pamoja na kusaidia katika kutatua migogoro ya kisiasa na kusalama kati ya nchi wanachama.
Kwa upande wa Umoja wa Afrika tutaendelea kutekeleza maamuzi ya vikao na taasisi mbalimbali za Umoja huo. Daima tutakuwa wanachama waaminifu wa Umoja wa Afrika na kuchangia katika uimarishaji wake. Kuhusu Umoja wa Mataifa tutaendelea kutimiza wajibu wetu kama wanachama wa Umoja huo wa kimataifa ulio adhimu na muhimu kwetu na dunia nzima. Tutaendelea kushiriki katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunao wanajeshi wetu katika majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan na Lebanon. Tuko tayari wakati wote kuchangia zaidi iwapo Umoja wa Mataifa watatutaka tufanye hivyo.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Namaliza hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa kuiunga mkono Serikali yetu na kwa mchango wenu uliowezesha nchi yetu kupata mafanikio haya makubwa tunayojivunia katika mwaka 2014. Tumeweza kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu mengi. Umoja wetu na mshikamano wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza mwaka 2015 kwa matumaini makubwa. Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya kuendelea kuliimarisha zaidi taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo huenda ukawa na changamoto na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka huu. Uelewa wetu, umoja wetu, mshikamano wetu na moyo wetu wa uzalendo ndivyo vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. Mimi nina imani kubwa kwa uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa nzuri ya nchi yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na utulivu. Tumeweza mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na miaka ijayo. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka mpya.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza.
Rais Jakaya Kikwete

Wednesday, July 03, 2013

Idi Amin Speech to Queen Elizabeth the II

 
 
Uganda Dictator General Idi Amin Dada called himself Conqueror of the British Empire
IDD AMIN SPEECH TO THE QUEEN

"My majesty Mr. Queen Sir, horrible ministers and members of parliament, invented Guests, ladies under gentlemen. I hereby thank you completely…..Mr. Queen, sir; and also what he has done for me and my fellow Uganda who come with me.

We have really eaten very much. And we are fed up completely:And also very thanks to you keenly open up from all windows: so that those plenty climates can come into lunch. But before I go back to my country with a plane from the Entebbe airport of London I wish to invitation you Mr. Queen, to become home to Uganda so that we can also revenge on you .

You will eat a full cow:and also feel up your stomach and walk with difficult because of full stomach completely. Even when you want to rest at night; I will make sure that you sleep on top of me in the top up stairs of my mansion completely so that you can enjoy all the gravity of fresh air.

"But now am sorry because I have to tell you that I have made a shortcall on you only. But next time I shall make a long call on you to last the whole moon completely. Thank you very much to allow me to undress you completely before these extinguished ladies undergentlemen sir.

Lastly but not list, I ask the band to play our international anthem of the republic of Uganda and also the British international anthem..Your majesty sir, I thank you from the bottom of my heart and from thebottoms of all the people of Uganda .

With this few words I thank you Sir.

Thursday, March 14, 2013

Rais Kikwete Afungua Rasmi Jengo la Kitivo Cha Sayansi MUM

HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA UFUNGUZI RASMI WA JENGO LA KITIVO CHA SAYANSI KATIKA CHUO KIKUU CHA WAISLAMU CHA MOROGORO (MUM),


TAREHE 14 MACHI, 2013, MOROGORO

Mzee Kitwana Suleiman Kondo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF);
Mheshimiwa Joel Bendera, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;
Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro;
Profesa Hamza Mustafa Njozi, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro;
Viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na Jumuiya mliohudhuria;

Wageni waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Niruhusuni niungane na wenzangu walionitangulia kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kukutana hapa. Nakushukuru sana Mama Mwantumu Malale, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro na viongozi wenzako kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii adhimu ya ufunguzi wa jengo la Kitivo cha Sayansi katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro. Mmenipa heshima kubwa ya kuwa sehemu ya historia ya Chuo hiki. Kwa kweli, nimefarijika sana kuona Chuo chetu kinazidi kupata mafanikio ya kutia moyo hasa ukizingatia ukweli kwamba kina muda mfupi tu tangu kuanzishwa kwake.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Natoa pongezi nyingi kwako, Makamu Mkuu wa Chuo na wale wote walioshiriki kubuni wazo la kuwa na jengo la Kitivo cha Sayansi na kufanikisha ujenzi wake. Juhudi zao na moyo wao wa kupenda maendeleo ndio umetufanya sisi kujumuika hapa leo kushuhudia mafanikio haya. Hakika ni jambo la kujivunia. Pia, nawapongeza sana Wajenzi na Mhandisi Mshauri kwa kazi nzuri waliyofanya ya ujenzi wa jengo hili. Sote tunaliona jengo lilivyojengwa vizuri na kwa namna yake linapendezesha mandhari ya Chuo.

Kwa namna ya pekee napenda kwa niaba yenu nitoe shukrani zangu za moyoni kwa taasisi ya Al-Barakah kwa kufadhili ujenzi wa jengo hili. Asanteni sana kwa ukarimu wenu na upendo mkubwa mliouonesha kwa nchi yetu na watu wake. Naomba taasisi nyingine na watu binafsi waige mfano huu mzuri wa kusaidia miradi mbalimbali inayonufaisha jamii. Tukumbuke ule msemo wa wahenga kuwa “kutoa ni moyo, usambe si utajiri”.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Mabibi na Mabwana;

Kwa miaka mingi madhehebu ya dini na mashirika ya dini yamekuwa washirika muhimu sana wa Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Yamekuwa yanajihusisha na kutoa huduma kwa jamii kama vile afya, elimu na nyinginezo. Kwa ajili hiyo watu wengi sana nchini wamenufaika na wanaendelea kunufaika na huduma zinazotolewa na mashirika ya dini.

Kwa miaka mingi mashirika na taasisi za madhehebu ya dini ya Kikristo ndiyo yaliyokuwa yakionekana kutoa huduma hizo. Kwa upande wa Waislamu, ukiacha Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan, mchango umekuwa mdogo sana. Ni jambo la faraja kubwa kuona Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF) ikionyesha njia. Kwa kumiliki na kuendesha Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro kwa ufanisi, MDF inatoa mchango muhimu katika kuendeleza elimu ya juu na maendeleo nchini. Idadi kubwa ya wanafunzi waliofuzu masomo yao na waliopo katika Chuo hiki tangu kilipoanzishwa mwaka 2005 ni ushahidi tosha wa kazi nzuri inayofanywa na MDF. Hongereni sana. Tunawaombea kwa Mola mpate mafanikio makubwa zaidi miaka ya usoni kwa upande wa elimu na huduma nyingine muhimu.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Katika kipindi cha miaka saba sasa, Serikali yetu imeongeza sana uwekezaji katika upanuzi wa elimu tangu ya awali hadi elimu ya juu. Tumeamua kufanya hivyo kwa sababu vijana wengi waliokuwa wanastahili kupata elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu ya juu walikuwa hawapati. Tanzania ni kubwa kuliko Kenya na Uganda kwa eneo na idadi ya watu lakini ndiyo tuliokuwa na idadi ndogo ya wanafunzi kwa ngazi zote hizo. Kwa mfano, mwaka 2005 idadi ya wanafunzi waliokuwa Chuo Kikuu nchini Kenya ilikuwa 108,407, Uganda 88,360 na kwa baadhi ya nchi za SADC kama vile Afrika Kusini idadi hiyo ilikuwa 717,973. Wakati wenzetu wakiwa na idadi hiyo, sisi tulikuwa na wanafunzi 40,719 tu katika vyuo vikuu nchini. Hali ilikuwa hivyo pia kwa elimu ya sekondari. Kenya ilikuwa na wanafunzi 925,341, Uganda 619,519 na Afrika Kusini 4,186,882 wakati Tanzania ilikuwa na wanafunzi 524,325 tu waliokuwa katika shule za sekondari.

Tuliona hali hii haikubaliki hivyo tukaamua hatuwezi kuiacha iendelee. Tukaamua kudhibiti. Tukachukua hatua tulizochukua za kupanua elimu katika ngazi zote. Matokeo ya uamuzi huo ni kwamba vijana wanaopata fursa ya kupata elimu katika ngazi zote wamekuwa wengi kuliko wakati mwingine wo wote katika historia ya nchi yetu, tumewafikia na kuwapita majirani zetu. Kazi kubwa tunayoendelea nayo sasa ni kuwekeza katika kuimarisha ubora wa elimu waipatayo vijana wetu kwa kuongeza walimu, vifaa vya kufundishia, vitabu na huduma nyinginezo. Inshallah hata kwa dhamira yetu, hii njema Mola atatuwezesha. Mwanzo mgumu lakini hatma itakuwa nzuri.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kufuatia juhudi hizo, idadi ya wanafunzi waliopo kwenye vyuo vikuu nchini imeongezeka sana, kutoka wanafunzi 40,719 mwaka 2005 hadi wanafunzi 166,484 mwaka 2012. Kwa upande wa sekondari mwaka 2011 tulikuwa na wanafunzi milioni 1.79 na wenzetu wa Kenya walikuwa na wanafunzi milioni 1.77. Haya ni mafanikio makubwa.

Serikali itaendelea kuwekeza kwenye upanuzi wa fursa za elimu na ubora wake. Hata hivyo ushiriki wa wadau wengine kuunga mkono juhudi za serikali ni jambo muhimu sana. Tumeweka mazingira mazuri kwa wadau hao kufanya hivyo na mafanikio yanaonekana wazi. Kama nilivyokwishasema awali, mashirika ya dini yamekuwa wadau wa kutumainiwa na mchango wao uko wazi. Unajieleza wenyewe. Kwa mfano, katika vyuo vikuu 49 vilivyopo nchini, vinavyomilikiwa na umma ni 14 tu. Vyuo vikuu 24 vinamilikiwa na mashirika ya dini na 11 na sekta binafsi.





Ndugu Mkuu wa Chuo;

Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa na muhimu unaotolewa na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na mashirika ya dini na sekta binafsi. Ninyi mmekuwa washirika wazuri na wa uhakika katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya elimu katika nchi yetu. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nanyi ili kuwawezesha vijana na Watanzania wengi zaidi waweze kupata elimu. Uamuzi wa kufanya utaratibu wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu uhusishe wanafunzi wa vyuo visivyokuwa vya umma ni moja ya mambo mengi muhimu yanayofanywa na Serikali kuthibitisha usemi wangu huo.

Tulipoingia madarakani mwaka 2005 tulifanya mambo mawili muhimu kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Kwanza uamuzi kwamba, mikopo itolewe kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma na vile visivyokuwa vya serikali. Kabla ya hapo ilihusu vyuo vya umma pekee. Pili kwamba, kila mwaka tuongeze fedha zinazotengwa kwa ajili ya Mfuko huo ili idadi ya wanafunzi wanaonufaika iongezeke. Tulikuta Mfuko ukiwa na shillingi billioni 56.1 unanufaisha wanafunzi 16,345 mwaka 2005. Tukaongeza kila mwaka na katika mwaka huu wa fedha (2012/13) tumetenga shillingi bilioni 345 zinazowanufaisha wanafunzi 98,772.

Tutaendelea kuongeza fedha katika Mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi wanufaike na hata ifikie siku moja tuweze kuwakopesha wote bila ya kujali sifa ya uwezo wa wazazi au walezi kulipa ada. Kwa kasi tuliyonayo na kwa jinsi tunavyozidi kufanikiwa katika kukusanya mapato ya serikali, naamini miaka michache ijayo tunaweza kufikia lengo hilo. Nawasihi Bodi ya Mikopo iwekeze katika kuimarisha uwezo wa kuwafuatilia waliokopeshwa kulipa mikopo waliyopewa. Matamanio yangu ni kuwa fedha zilizotolewa zizunguke ili tupunguze kiasi kinachotolewa na bajeti ya serikali kila mwaka.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Mabibi na Mabwana;

Niruhusuni nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Mkuu wa Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo, Wahadhiri na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu hiki kwa kazi kubwa na nzuri muifanyayo ya kuendeleza na kuboresha Chuo. Tumeshuhudia ujenzi wa jengo nililolifungua leo. Tumeona mafanikio kwa upande wa ongezeko la idadi ya wanafunzi, walimu, wafanyakazi na fani zinazofundishwa katika kipindi hiki kifupi cha uhai wa Chuo hiki.

Nimefurahishwa na kufarijika sana kusikia kuwa ubora wa elimu inayotolewa hapa chuoni ni jambo linalopewa kipaumbele cha kwanza. Jambo hili ni muhimu sana kulisisitiza kwani tunataka wahitimu wa Chuo hiki wafanane na wahitimu wa Chuo chochote kizuri nchini na hata duniani. Ningependa kuona wahitimu wa Chuo hiki wanagombewa katika soko la ajira. Hili ni jambo linalowezekana. Kinachotakiwa ni uamuzi wa Baraza na Seneti kuwa iwe hivyo na kuchukua hatua zipasazo. Sina shaka kuwa mnaweza kufanya hivyo. Hakika mnaweza, na sote kwa umoja wetu tunaweza.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Nimefurahi sana, pia, kusikia kuwa Chuo kinatoa mafunzo ya ualimu. Bila ya shaka mnaelewa kwa nini nafurahi. Tuna uhaba mkubwa wa walimu nchini hivyo Chuo cho chote kinachotoa mafunzo ya ualimu hunifurahisha. Endeleeni kuimarisha mafunzo hayo ili Chuo chenu kitambulike na kukubalika nchini kwa sifa ya kutoa walimu wazuri. Walimu wa kutoka Chuo hiki wawe wale wanaojua vyema masomo wanayofundisha, mahiri kufundisha na waadilifu. Naomba pia mtoe kipaumbele cha juu kwa mafunzo ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati. Mkifanya hivyo, mtakuwa mnatoa mchango mkubwa katika jitihada za kupunguza uhaba wa walimu wa masomo hayo nchini. Naamini kitendo cha kuzindua Jengo la Kitivo cha Sayansi, kilichofanyika muda mfupi uliopita kinatoa matumaini ya Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro kuchangia katika jitihada za kupunguza pengo la walimu wa sayansi nchini.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Nimewasikia mkieleza kwa ufasaha changamoto kubwa na ndogo ambazo Chuo inakabiliana nazo. Nawapongeza kwa dhati, wewe na viongozi wenzako kwa ubunifu wenu na hatua mnazochukua kuzikabili changamoto hizo. Nawaahidi msaada na ushirikiano wangu na wa serikali kwa yale yaliyoko kwenye uwezo wangu na wa serikali katika kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zinazowakabili.

Nawapongeza kwa uamuzi wenu wa kutafuta vyuo vikuu rafiki vilivyoko katika nchi mbalimbali duniani mnavyoweza kushirikiana navyo. Endeleeni kufanya hivyo kwani vyuo vikuu vingi duniani hufanya hivyo. Hamtakuwa wa kwanza na wala hamtakuwa mnafanya jambo la kustaajabisha. Mnaweza, mkipenda, kuwaomba Mabalozi wetu waliopo katika nchi mbalimbali duniani wawasaidie. Ni wajibu wao kufanya hivyo kwani kusaidia kusukuma maendeleo ya hapa nchini kutoka huko waliko ndilo jukumu lao la msingi. Vile vile, nimefurahishwa na mipango yenu ya baadaye ya kuwa na matawi katika mikoa mbalimbali nchini. Hongereni kwa uamuzi wenu wa busara. Lazima Chuo kitanuke kwa maana ya kuwa kikubwa zaidi, makao makuu na kwa kuwa na vyuo vishiriki na shule au vitivo sehemu mbalimbali nchini.

Ndugu Mkuu wa Chuo;

Kazi iliyo mbele yenu ni kubwa, hivyo ni vyema kuweka mikakati mizuri na mipango thabiti ya utekelezaji na ufuatiliaji wa dhamira yenu hiyo njema. Rai yangu kwenu ni kuwaomba muwe wabunifu zaidi hasa katika kutafuta vyanzo vingine vya mapato vitakavyosaidia Chuo kujiendesha bila kutegemea ada peke yake. Chuo kiangalie uwezekano wa kufanya shughuli zitakazowaingizia mapato kama vile kufanya shughuli za kutoa ushauri. Pia muangalie uwezekano wa kuwekeza wenyewe kwenye miradi ya kiuchumi au kwa kushirikiana na wawekezaji katika baadhi ya maeneo.

Kuhusu nafasi mbili za ufadhili nilizopewa na Chuo kikuu cha Tun Abdul Razak cha Malaysia, nitafuatilia kujua kilichoendelea na kinachoendelea. Je, nafasi hizo bado zipo? Zikiwepo, nitawasiliana na wahusika waangalie uwezekano wa kuwapeni. Kama zimeshagawiwa basi tusubiri safari ijayo. Kwa masuala ya ardhi na maombi mengine nimeyasikia, yaleteni tuangalie namna ya kusaidiana.

Ndugu Makamu Mkuu wa Chuo, na

Wafanyakazi wote wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;

Napenda kuwakumbusha kuwa mnayo dhamana kubwa na wajibu mkubwa na wa kihistoria. Ule ukweli kwamba ni mara ya kwanza kwa Taasisi ya Waislamu wazawa kuwa na Chuo Kikuu inawapeni wajibu maalum wa kuhakikisha Chuo kinafanikiwa. Ni mtihani na changamoto ya aina yake kuthibitisha kuwa Waislamu nao wanaweza kuwa na Chuo kizuri na chenye kutoa elimu ya ubora wa hali ya juu. Kwa sababu hiyo hamna budi kuhakikisha kuwa mna mipango mizuri ya kujenga Chuo cha hadhi na ubora wa hali ya juu. Ihakikishwe kuwa mipango hiyo inatekelezwa kwa ukamilifu.

Aidha jumuiya yote inao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, maarifa na weledi ili dhima hiyo ya Chuo iweze kutimizwa kwa ukamilifu. Timizeni wajibu wenu ipasavyo ili jina la Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro likue haraka. Sifa yake isambae na kuvuma kote nchini. Chuo kifanye vizuri ili wanafunzi waone fahari kuwa wahitimu wa Chuo hiki. Chuo ambacho, wazazi wapende kuleta vijana wao kuja kusoma hapa. Kwa jinsi Mkuu wa Chuo alivyoeleza, mimi nina imani mnaweza, fanyeni kweli.





Ndugu Wanafunzi wa Chuo cha Waislamu cha Morogoro;

Naomba wote muone fahari ya kuwa wanafunzi katika Chuo cha kihistoria hapa nchini. Nawasihi mjitume kwa kadri ya uwezo na vipaji mlivyopewa na Mwenyezi Mungu mfanikishe kile kilichowaleta. Jifunzeni kwa bidii mfaulu vizuri ili mkihitimu muwe kielelezo kizuri cha mafanikio na ubora wa Chuo Kikuu Cha Waislamu cha Morogoro. Muwe Mabalozi na kioo cha ufanisi wa Chuo hiki. Nawasihi mjiepushe na mambo yatakayowapunguzia muda au kuwaondoa katika shughuli ya msingi iliyowaleta hapa ya kujifunza mpate digrii katika fani mliyochagua mwenyewe kuisomea. Vishawishi ni vingi na wapo watu wengi wanaopanga kuwashawishi mtumie muda wenu adhimu kufanya wanayoyataka wao ambayo mkishiriki huwatoa kwenye malengo na kutekeleza yao. Mambo ya dunia ya nje ya Chuo ni mengi huna budi kutambua lipi ufanye na lipi usifanye na kwa wakati gani!

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu ni mtu mzima, si mtoto. Lazima ujue kuwa unawajibika kwa kila unaloamua na kutenda. Amua kuwajibika vizuri. Fikiri kabla ya kutenda, changanua lipi ni lipi kabla ya kufanya uamuzi wa kile unachotaka kufanya. Wakati wote uongozwe na busara na hekima na siyo jazba na ushabiki wa matakwa ya kundi. Kama ni jema fanya na kama si jema usifanye. Kwanza tambua wewe ni nani na uko hapa kwa ajili gani. Lazima ujue kuwa hatma ya yote uko peke yako. Utafaulu au kufeli wewe. Utapata shahada wewe na si mtu mwingine. Hakuna ubia wa kufaulu au kufeli au kiwango cha kufaulu. It will always remain personal. Katika masomo unanufaika wewe. Shirikiana na wengi lakini usisahau kujali maslahi yako. Maslahi ya wengi yasiyojumuisha yako, yahoji vizuri kabla ya kuamua kushiriki au kufanya. Vinginevyo labda kama umeamua kujitoa muhanga, uwe shujaa. Hata kwa hilo, sijui utakuwa shujaa wa nani.

Mabibi na Mabwana;

Kabla ya kumaliza napenda kutambua na kumshukuru Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa na viongozi wa MDF kwa juhudi zao za pamoja zilizowezesha Chuo hiki kuwepo. Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru wananchi wanaokizunguka Chuo kwa ujirani mwema na wakazi wa Morogoro kwa ujumla kwa kukipokea vizuri na kuishi na wanajumuiya wa Chuo hiki kwa upendo mkubwa. Naomba muendelee na moyo na ushirikiano huo.

Baada ya kusema hayo, nawashukuru sana kwa kunialika. Nawatakia kila la heri na mafanikio tele.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Tuesday, February 05, 2013

Ujumbe Kutoka Kwa Rais Obama Kwa WaKenya



Rais Obama katoa ujumbe mzito kwa WaKenya na waafrika kwa ujumla!

Friday, February 01, 2013

Hotuba ya Rais Kikwete Kwa Wananchi Mwisho wa Mwezi Januari 2013

Rais Jakaya Kikwete
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenye
Rehema, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuzungumza kwa mara
nyingine kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri wa mawasiliano baina ya
Rais na wananchi wa Tanzania kila mwisho wa mwezi.  Siku ya leo
nitazungumzia safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia.  Pia
nitazungumzia ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara
kuja Dar es Salaam.

Safari za Kikazi Nje ya Nchi


Ndugu Wananchi;
        Safari yangu ya Ufaransa, Uswizi na Ethiopia ilikuwa na
manufaa makubwa kwa nchi yetu.  Nchini Ufaransa licha ya kuimarisha
uhusiano wa kirafiki baina ya nchi zetu, tumepata wawekezaji wengi
wakubwa wenye nia thabiti ya kuja kuwekeza hapa nchini.  Pia
tumekubaliana kuanza mazungumzo ya kuwa na mpango mwingine wa
ushirikiano.  Mpango wetu wa sasa ulioanza mwaka 2006 uliisha mwaka
2010.  Mpango ule ulitusaidia sana kuboresha huduma za maji katika
miji ya Utete mkoani Pwani na Mpwapwa mkoani Dodoma.

        Katika mkutano wa Kongamano la Uchumi wa Dunia uliofanyika
Davos, Uswizi, tumehakikishiwa ushirikiano katika kuendeleza juhudi
zetu za kuleta mapinduzi ya kijani ili tujihakikishie usalama wa
chakula na kupunguza umaskini vijijini na kukuza uchumi wa nchi yetu.
Aidha, tulipata bahati ya kushirikishwa katika mjadala wa kuanzishwa
kwa programu kubwa ya kuzisaidia nchi za Afrika kutatua matatizo ya
upatikanaji wa umeme.  Naamini programu hiyo ikitekelezwa na wakubwa
kuheshimu kauli na ahadi zao itakuwa msaada mkubwa kwa maendeleo ya
nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ndugu Wananchi;
        Nchini Ethiopia tulishiriki katika mkutano wa Wakuu wa Nchi
na Serikali wa Umoja wa Afrika na katika kikao cha African Peer Review
Mechanism (APRM) ambapo taarifa ya tathmini ya utawala bora ya
Tanzania na Zambia iliyofanywa na APRM ilijadiliwa.  Kwa jumla hatuna
mahali tuliponyooshewa kidole kuwa tunafanya vibaya.  Tumepongezwa
katika mambo mengi na tumepewa ushauri kwa baadhi ya maeneo waliyoona
hatuna budi kuyaboresha.  Nilipata nafasi ya kusema ambayo niliitumia
kufafanua baadhi ya mambo yaliyokuwamo kwenye taarifa.  Niliwashukuru
na kuahidi kuufanyia kazi ushauri uliotolewa.  Tathmini ya nchi yetu
ilipitishwa kwa kauli moja.

Vurugu za Kupinga Gesi Kusafirishwa Kutoka Mtwara

Ndugu wananchi;
Kama mtakavyokumbuka tarehe 8 Novemba, 2012 kule Kinyerezi, Wilaya ya
Ilala hapa Dar es Salaam, niliweka jiwe la msingi la ujenzi wa bomba
la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es
Salaam.  Karibu na mwishoni mwa Desemba, 2012 kukafanyika maandamano
mjini Mtwara kupinga ujenzi wa bomba hilo.  Katika
maandamano yale na baadaye kwenye kauli za wanasiasa na wanaharakati
yakatolewa madai kuwa gesi hiyo itumike kwa maendeleo ya Mtwara na
kwamba yale yanayotakiwa kufanyika Dar es Salaam yafanyike Mtwara.
Pia, zilitolewa shutuma nyingine dhidi ya Serikali eti kuwa kwa miaka
mingi imewasahau na haiwajali wananchi wa Mikoa ya Kusini na ujenzi wa
bomba hilo ni muendelezo wa hayo. Kauli mbalimbali za wanasiasa na
wanaharakati ni kama vile ziliongeza mafuta kwenye kaa la moto na
kuuchochea mpaka kukatokea matukio yaliyotusikitisha na kutshtua
sote.  Baadhi ya ndugu zetu wamepoteza maisha na mali za watu na
Serikali kuharibiwa.

Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya kuaga mwaka 2012 na kuukaribisha mwaka 2013,
tarehe 31 Desemba, 2012, nililisemea jambo hili.  Leo mwezi mmoja
baadae, napenda kusisitiza mambo mawili.  Kwanza kwamba, si kweli kuwa
Serikali inapuuza Mikoa ya Kusini.  Na pili, kwamba kujenga bomba la
kuipeleka gesi Dar es Salaam hakuinyimi Mikoa ya Mtwara na Lindi fursa
ya kunufaika na gesi iliyopo Mtwara.

Ndugu Wananchi;
        Serikali imefanya, inafanya na ina mipango ya kufanya mambo
mengi mazuri kwa ajili ya kuleta maendeleo katika Mikoa ya Mtwara na
Lindi.  Ipo mipango ya kuboresha miundombinu, huduma za kiuchumi na
kijamii pamoja na kukuza uchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda
vikubwa na vidogo.  Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya uongozi wa Rais
Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilijenga daraja katika Mto Rufiji
maarufu kama Daraja la Mkapa.  Hii ilikuwa ni hatua kubwa ya awali
katika safari ya kutatua matatizo ya usafiri ya Mikoa ya Kusini.
Serikali ninayoiongoza mie iliachiwa kazi ya kukamilisha ujenzi wa
barabara za lami kufikia darajani na kuunanisha Mkoa wa Mtwara na Mkoa
wa Ruvuma.  Kazi hiyo, tumeitekeleza vizuri na sasa tunakaribia
kuimaliza.  Tulikamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Mnazi-Mmoja
hadi Nangurukuru.  Mwaka 2009 tukaanza ujenzi wa barabara ya kilomita
56kutoka Somanga hadi Ndundu (darajani).  Ujenzi wakilometa 36 za
mwanzo ulienda vizuri.  Bahati mbaya ujenzi wa kilomieta 20 za mwisho
umechelewa sana kwa sababu ya mmiliki wa kampuni iliyokabidhiwa
kufanya kazi hiyo kufariki.  Kwa sababu hiyo, kampuni ilipata
mtikisiko kiasi na kusababisha kazi kutotekelezwa kwa kasi
tuliyoitarajia.  Sasa mambo yametengemaa na kazi inaendelea kwa kasi
nzuri.  Matumaini yetu ni kuwa ifikapo mwezi Desemba, 2013 kazi hiyo
itakuwa imekamilika.

Hali kadhalika, Rais Mstaafu, Mzee Benjamin Mkapa alituachia jukumu la
kumaliza ujenzi wa Daraja la Umoja katika mto Ruvuma na ujenzi wa
barabara ya lami kuanzia Mikoa ya Mtwara na Ruvuma.  Tumelikamilisha
Daraja hilo na ujenzi wa barabara ya lami kutoka Masasi hadi Mangaka
umekamilika.  Mchakato wa kujenga barabara ya kwenda Songea na kwenda
Darajani umefikia  mahala pazuri.  Tenda ya ujenzi wa barabara kutoka
Tunduru hadi Mangaka mpaka Darajani imeshatangazwa.  Kama mambo
yataenda sawa miezi mitatu ijayo mjenzi atapatikana.  Wakati huo huo
ujenzi wa barabara kutoka Namtumbo hadi Songea – Mbinga na Namtumbo –
Tunduru unaendelea.  Hivyo basi, kwa barabara ya “Mtwara Corridor”
kazi iliyobaki ni kutoka Mbinga kwenda Mbambabay ambayo tutaifanya
wenyewe kama tulivyofanya kwa Mnazi Mmoja – Nangurukuru na Somanga –
Ndudu na Daraja la Umoja.

Ndugu Wananchi;
Ipo pia mipango ya kuipanua na kuijenga upya bandari ya Mtwara ili
iweze kuhudumia mahitaji ya utafutaji na uchimbaji wa gesi baharini,
kuhudumia na kuvifanyia matengenezo vyombo vinavyotumika katika
utafiti, uchimbaji na uendelezaji wa gesi.  Pia iweze kuhudumia
shughuli za kiuchumi zitakazotokana na uchumi wa gesi pamoja na
zilizopo sasa.  Nilipozungumza na makampuni ya utafutaji gesi pale
Mtwara tarehe 25 Julai, 2011 waliomba nikubali bandari ya Mtwara iwe
mahali pa kuhudumia vyombo vyote vinavyofanya shughuli ya utafutaji na
uchimbaji wa gesi na mafuta katika pwani ya Afrika ya Bahari Kuu ya
Hindi.  Pia waliomba kuwa sehemu hiyo ya bandari iwe bandari huru.
Niliwakubalia bila ya kusita na tayari eneo la hekta 110 zimeshatengwa
na kutangazwa rasmi kuwa bandari huru.  Vile vile waliomba wapewe
sehemu ya bandari ya sasa kuendeshea shughuli na eneo la kujenga kituo
cha mitambo ya kuchakata gesi na kusafirisha nje.

Ndugu Wananchi;
Baada ya kuzungumza na makampuni ya utafutaji gesi na mafuta na
kuelezwa mahitaji yao nilibaini kuwa bandari ya Mtwara inahitaji
kupanuliwa na kujengwa upya.  Bahati nzuri viongozi wa Mamlaka ya
Bandari walikuwepo na walinihakikishia kuwa watafanya hivyo.

Tayari eneo la bandari limeongezwa kutoka hekta 70.68 hadi 2,693.68.
Eneo la bandari huru limeshatengwa hivyo hivyo na eneo la kampuni ya
Dangote na makampuni ya gesi yaliyopo.  Aidha, mchakato wa kupanua
bandari iliyopo, kujenga gati mpya na kuendelea na ujenzi hadi maeneo
ya Msanga Mkuu ipo katika hatua mbalimbali za matayarisho na
utekelezaji.

Ndugu Wananchi;
        Kwa upande wa Mkoa wa Lindi mipango ya kupanua na kuijenga
upya bandari ya Lindi imefikia hatua nzuri.  Naibu Waziri wa Uchukuzi,
Mhe. Dkt. Charles Tizeba alithibitisha hayo tarehe 1 Desemba, 2012
nilipotembelea bandari hiyo wakati wa ziara yangu ya Mkoa wa Lindi ya
tarehe 1 mpaka 5 Desemba, 2012.  Hali kadhalika mipango ya kujenga
bandari ya Kilwa iko mbioni.  Tena kwa upande wa Mkoa wa Lindi moja ya
makampuni yaliyogundua gesi baharini wameamua kujenga bandari na kituo
cha kuchakata na kusarifisha gesi nje ya mkoa huo kama ilivyo kwa
Mtwara.  Naambiwa wametambua maeneo matatu, kilichobakia ni kuamua
mojawapo ili ujenzi uanze.

Ndugu Wananchi;
        Nilipotoka bandari ya Mtwara, siku ile nilitembelea Chuo cha
VETA na kuzungumza na viongozi wa VETA taifa na wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi kuhusu kuwa na mitaala ya kutoa mafunzo mahsusi
yanayohitajika na sekta ya gesi na mafuta.  Nilisisitiza kwamba
tuwapatie vijana wetu mafunzo yatakayowawezsha kuajiriwa na makampuni
ya gesi na yale yatakayokuwa yanatoa huduma kwa makampuni hayo.
Nilisema tusipofanya hivyo, makampuni hayo yataajiri watu kutoka nje
na hatutakuwa na sababu ya kuwalaumu wala kulalamika.

Nafurahi kwamba agizo langu hilo limefanyiwa kazi ipasavyo.  Hivi sasa
katika chuo cha VETA Mtwara mafunzo hayo yanatolewa.  Kampuni ya
PetroBrass ya Brazil inaendesha mafunzo ya sekta ya gesi kwa vijana 25
kutoka mkoani Mtwara.  Aidha, chuo cha VETA kwa kushirikiana na
Kampuni ya Gesi ya Uingereza (British Gas) na Volunteers Service
Overseas ya Uingereza, kinatekeleza programu ya miaka mitatu iitwayo
Enhancing Employerbility Through Vocational Training.  Programu hii
inalenga  kutoa kozi zitakazowafanya wahitimu kuweza kuajiriwa katika
sekta ya gesi.  Programu hii ilifunguliwa na Makamu wa Rais,
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, tarehe 26 Novemba, 2012.

Ndugu Wananchi;
Chini ya programu hii, walimu wa masomo yanayohusiana na gesi
wanaongezewa ujuzi ili waweze kufikia viwango vya kimataifa.  Vile
vile, Wizara ya Nishati na Madini imetoa upendeleo maalum wa
kudhaminiwanafunzi 50 kutoka mkoa wa Mtwara kusoma chuoni hapo ambao
tayari wameshahitimu mafunzo ya msingi ya uunganishaji vyuma
viwandani.  Mchakato wa kuwapatawanafunzi 50 kwa ajili ya mafunzo kama
hayo kutoka mkoa wa Lindi unaendelea.  Nimeambiwa mpaka wameshawapata
vijana 25 bado 25.

        Hali kadhalika, Wizara ya Nishati na Madini inadhamini
wanafunzi 10 kupata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambako kozi
za mafuta na gesi zinatolewa.  Kipaumbele kwa udhamini huu unatolewa
kwa wanafunzi wa mikoa ya Mtwara na Lindi wenye sifa za kudahiliwa
katika mafunzo haya.  Wamepatikana watatu.  Wataalamu hawa na wengine
wa fani mbalimbali za gesi na mafuta watafundishwa kwa kiwango cha
shahada ya kwanza na baadae uzamili na uzamivu ili nchi yetu
ijitosheleze kwa wataalamu wa sekta hii.

Kupanga Mji wa Mtwara

Ndugu Wananchi;
        Baada ya kutembelea bandari ya Mtwara na Chuo cha VETA,
nilikaa na kuzungumza na viongozi wa Serikali na Manispaa ya Mtwara.
Katika mazungumzo yangu nao niliwasisitizia umuhimu wa kuwa na mpango
kabambe wa kuendeleza mji wa Mtwara – (Mtwara Masterplan) Mpango ambao
utawezesha kujengwa mji mkubwa wa kisasa unaokidhi mahitaji ya mji wa
uchumi wa gesi.  Niliwataka wahakikishe kuwa kuna maeneo ya viwanda,
biashara, makazi, mahoteli, huduma za afya, elimu, mapumziko na
burudani, viwanja vya michezo na kadhalika.  Kazi ya kutayarisha
Masterplan hiyo imeanza na Manispaa ya Mtwara inashirikiana na Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Makazi.
Kwa upande wa uwekezaji nafahamu kuwa mpaka sasa makampuni 51
yameonyesha nia ya kuwekeza Mtwara katika viwanda, hoteli, shughuli za
uchukuzi na huduma hasa kwa sekta ya gesi.  Wanachosubiri ni kutengewa
maeneo ya kujenga, waanze.  Hivyo kukamilika mapema kwa Masterplan ya
mji wa Mtwara kutasaidia kuongeza kasi ya uwekezaji huu kufanyika.
Viwanda hivi vyote vitasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Mtwara na
Watanzania kwa jumla.  Nimeambiwa kwa mfano, wakati wa ujenzi wa
kiwanda cha saruji watu zaidi ya 7,000 wataajiriwa.

Ndugu Wananchi;
        Kabla hata ya ugunduzi wa gesi iliyoko baharini, tulikuwa na
mipango ya kutumia gesi ya Msimbati (Mnazi Bay) kwa ajili ya kuzalisha
umeme, kuzalisha mbolea na kutumika katika kiwanda cha saruji.  Kwa
upande wa umeme kulikuwa na mpango wa kujenga mtambo wa kuzalisha
Megawati 300 kwa kushirikiana na mwekezaji binafsi.  Bahati mbaya
wakati wa matatizo ya kifedha ya dunia mwaka 2009 mwekezaji huyo
akashindwa kupata mkopo, hivyo mradi ukasimama kutekelezwa.  Haukufa
wala haukuhamishiwa Dar es Salaam au Bagamoyo kama ambavyo imekuwa
inapotoshwa kwa makusudi.  Mradi huo bado upo, tena mpango wa sasa ni
kujenga Megawati 600zitumike Mtwara na zingine kuziingiza kwenye gridi
ya taifa kupitia Songea.

NduguWananchi;
Kwa upande wa kiwanda cha mbolea, wawekezaji wengi wameshajitokeza
tangu mwaka 2008 mpaka sasa.  Mchakato umefanyika wa kuchambua
wawekezaji wenye sifa na kutambuliwa.  Mambo mawili yamechelewesha
utekelezaji kuanza.  Jambo la kwanza ni wawekezaji na kampuni ya
Artumas iliyokuwa mbia na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(T.P.D.C) wakati ule, kushindwa kukubaliana nao juu ya bei ya kuwauzia
gesi.  Wawekezaji walitaka bei ya gesi ipunguzwe, lakini kampuni ya
Artumas na T.P.D.C. hawakuwa tayari kupunguza zaidi ya kiasi
walichopunguza, ambacho wawekezaji bado waliona hailipi kwa kuzalisha
mbolea.

Sababu ya pili ni matatizo ya kifedha yaliyoikumba kampuni ya Artumas
katika kipindi hicho.  Kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na
mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/2009 kampuni ya Artumas
iliathirika na kulazimika kuuza hisa zake kwa wawekezaji wengine.
Katika kipindi hicho ilichopitia kampuni, mazungumzo na uwekezaji wa
kiwanda cha mbolea hayakuweza kupewa kipaumbele.  Mtazamo wa sasa wa
wabia wapya na T.P.D.C. ni kuwa wao wenyewe sasa wawekeze katika
ujenzi wa kiwanda cha mbolea. Serikali imekubali rai yao hiyo na
wanaendelea na matayarisho.

Ndugu Wananchi;
        Kwa upande wa kiwanda cha Saruji kitakachojengwa na kampuni
ya Dangote ucheleweshaji ulikuwa kwa sababu mbili.  Kwanza, kampuni ya
Dangote iliomba eneo zaidi ya ililokuwa imeomba na kupewa.  Hoja yao
ilikuwa kwamba eneo la ziada walilokuwa wanaliomba ndilo lenye
malighafi nyingi na bora kwa utengenezaji wa saruji.  Hivyo, waliamua
kusubiri mpaka watakapopewa eneo hilo.

Bahati mbaya eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na mtu mwingine na
alikuwa na hati miliki nalo.  Halmashauri ya Mtwara iliomba Serikali
eneo hilo litwaliwe na baadaye ipewe kampuni ya Dangote. Serikali
ilikubali.  Hata hivyo, mchakato ulichukua muda na hata pale
ulipokamilika mwenye eneo aliupinga uamuzi wa Serikali Mahakamani.
Kesi ilichukua muda kusikilizwa na kumalizika.  Bahati nzuri Serikali
ikashinda na mara baada ya uamuzi wa Mahakama ndipo kampuni ya Dangote
ikamilikishwa eneo hilo.

Kampuni nayo ilichukua muda kuanza.  Hivi sasa, timu yake ipo kwenye
eneo na mradi uko tayari kuanza kutekelezwa.  Niliambiwa kuwa katika
magari yaliyopigwa mawe katika fujo za Mtwara ni pamoja na lile la
mradi huu.  Huo ndiyo ukweli kuhusu ujenzi wa kiwanda cha saruji cha
Dangote.  Madai kuwa kiwanda hicho kimehamishiwa Bagamoyo si ya
kweli.  Ni uzushi wa makusudi wa watu wenye nia mbaya na Serikali.
Huwezi kudai kuwa mtetezi wa wananchi wa Mtwara kwa hoja za uongo na
kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa.

Ndugu Wananchi;
        Ujenzi wa bomba la gesi ndiyo uliozua mzozo wote huu.
Zilijengwa hisia kuwa gesi yote inapelekwa Dar es Salaam na kwamba
Mtwara itakosa gesi na maendeleo yatayotokana na gesi hiyo.  Na,
wengine wakasema gesi inapalekwa Bagamoyo ili kuzidisha chumvi na
kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali kwamba Rais anapeleka
gesi kwao. Kwanza, Kinyerezi iko Ilala na siyo Bagamoyo.  Pili, ukweli
ni kwamba pale Mtwara kuna gesi nyingi ya kutosheleza mahitaji ya
Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na kubaki.  Gesi itakayoletwa Dar es
Salaam niasilimia 16 tu ya gesi yote iliyoko Mtwara kwa miaka ishirini
ijayo.  Hivyo asilimia 84 ya gesi itabaki Mtwara kwa ajili ya kuuzwa
nje ya nchi na kupelekwa kwingineko nchini.

        Kwa sababu hiyo, ndugu zetu wa Mtwara hawana sababu ya kuwa
na wasiwasi. Ipo gesi ya kutosha kwa mahitaji ya sasa na ya miaka
mingi ijayo.  Viwanda vinavyotumia gesi kama mali ghafi na vile
vinavyohitaji gesi kama nishati vyote vitapata gesi ya kutosha.  Kwa
upande wa uzalishaji umeme hali kadhalika ipo gesi ya kutosha
kuzalisha umeme mwingi zaidi.  Hivi sasa tunacho kituo kinachozalisha
umeme wa megawati 15 unaotumika Mtwara, Lindi, Tandahimba, Newala,
Masasi, Nachingwea, Ruangwa, na Mtama. Bado umeme huo hautumiki wote
hivi sasa.

Ndugu Wananchi;
        Nayaeleza yote haya kuwathibitishia wananchi wa Mtwara kuwa
tunawathamini sana na kuwajali.  Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuwapuuza
na kuwatupa mkono wananchi wa Mikoa ya Kusini.  Aidha, sitakuwa tayari
kuwaruhusu watu au mtu ye yote Serikalini kuwapuuza wananchi wa Mikoa
ya Kusini au mkoa wo wote hapa nchini.  Hiyo haitakuwa sawa.
Nilishasema siku za nyuma na napenda kurudia tena leo kuwa kwangu mimi
hakuna mkoa ulio bora kuliko mwingine.  Ni kutokana na msimamo wangu
huo ndiyo maana tumeelekeza nguvu na rasilimali nyingi za Serikali
katika mikoa iliyokuwa inadaiwa kuwa imesahauliwa.  Kazi ya ujenzi wa
barabara za lami iliyofanyika na inayoendelea kufanyika katika mikoa
ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera inajieleza yenyewe.
Mipango ya kuboresha Kiwanja cha Ndege cha Mtwara kufikia hadhi ya
kimataifa na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Lindi na Kilwa ni
ushahidi mwingine kati ya mambo mengi tunayoweza kuyataja.

Ndugu Wananchi;
        Haya niliyoyasema ni sehemu ndogo tu ya yale yaliyofafanuliwa
na kuelezwa kwa kina na Mawaziri na Wakuu wa Idara husika  za Serikali
na Mashirika  ya Umma pale Mtwara katika mkutano wa Waziri Mkuu na
viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa na wazee wa Mkoa wa Mtwara
tarehe 29 Januari, 2013.

Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Waziri Mkuu,
Mheshimiwa Mizengo Pinda, kwa kazi kubwa na nzuri aliyoifanya kule
Mtwara.  Uvumilivu wake, usikivu wake na utulivu wake vimesaidia sana
kulivusha taifa katika moja ya mitihani mikubwa ambayo ingeikuta nchi
yetu tangu Uhuru.  Nawapongeza Mawaziri na Wakuu wa Mashirika ya Umma
na Idara za Serikali kwa mchango wao muhimu walioutoa, uliosaidia
kufafanua masuala ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri.  Kwa wao
nawasisitiza na kuwakumbusha wajibu wao wa kuelimisha jamii kuhusu
shughuli wazifanyazo.  Wakifanya hivyo mara kwa mara migongano
haitakuwepo na wapotoshaji hawatapata nafasi.

Ndugu Wananchi;
        Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru viongozi wa
Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya dini, viongozi wa jamii,
wazee, wana-Mtwara na makundi mbalimbali ya jamii, kwa muda waliotumia
kuzungumza na Waziri Mkuu na kuwasikiliza wasaidizi wake wakifafanua
masuala mbalimbali.  Uvumilivu wao na uelewa wao ndivyo vilivyosaidia
kurejesha hali kuwa ya kawaida.  Nawaomba nao sasa, wote kwa pamoja
washirikiane na Serikali kuelimisha umma kuhusu ukweli wa mambo.  Pia
watumie nafasi hiyo kutahadharisha jamii na kuwataka watu kuwa
waangalifu na kupima maneno wanayoambiwa na watu.  Wajiepushe na
maneno au vitendo vinavyofarakanisha, kuchonganisha na kupandikiza
chuki dhidi ya watu au Serikali. Waambieni kuwa ghasia hukimbiza
wawekezaji kwani wakipata hofu kuwa hali ya amani na usalama ni ya
mashaka, watatoka kwenda kuwekeza kwingine.  Vyema iwe hapa hapa
nchini, lakini wanaweza kwenda nchi nyingine na sisi kupoteza kabisa.

Ndugu Wananchi;
        Nawapa pole wananchi wa Mtwara na Masasi kwa usumbufu
walioupata kutokana na ghasia zilizofanywa.  Nawapa pole waliofiwa na
kujeruhiwa.  Nawapa pole waliopoteza au kuharibiwa mali zao.  Kwa
kweli inasikitisha na kufadhaisha kuona watu wanafanya vitendo vya
kuua, kuchoma moto nyumba za watu na majengo ya Serikali pamoja na ,
kuharibu na kuiba mali za watu.  Huu ni uhalifu ambao hauna maelezo na
haukubaliki.  Tunaviachia vyombo husika vya dola na sheria kutimiza
wajibu wao.  Kwa waliohusika iwe fundisho kwao na kwa wengineo
kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu wengine siku zijazo.  Sasa
wameachwa pekee yao wakati wenzao wako huru na kufaidi maisha

Ndugu Wananchi;
Hili sakata la bomba la gesi limefika mahali pazuri.  Yaliyopita si
ndwele tugange yajayo.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni Sana kwa Kunisikiliza!


Source: http://www.wavuti.com/4/post/2013/02/hotuba-ya-rais-kikwete-ya-mwisho-wa-mwezi-wa-januari-2013.html#ixzz2JkbkOTwJ

Wednesday, November 12, 2008

Hotoba ya Mwalimu Nyeyere

Asante sana Da Subi kwa hii:

****************************************

Karibu kumsikiliza Mwalimu J.K Nyerere katika hotuba aliyoitoa sikuya Jumanne, Machi 14, 1995 katika iliyokuwa hoteli ya Kilimanjaro.

Hotuba ya Mwl. J.K Nyerere siku ya Jumanne Machi 14, 1995 (sehemu ya1/3)

Subi