Sunday, November 01, 2015

Harufu ya Urais Ilianzia Kahama

Harufu ya Urais ilianzia Kahama

HADI saa nne za asubuhi ya Oktoba 26 mwaka huu, mgombea wa ya urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, alikuwa anatumia ?mifumo na muundo wa kiprotokali? ya chama hicho tawala.

Lakini mfumo huo wa kiprotokali ulibadilika ghafla wakati msafara wake ulipowasili mjini Kahama, mkoani Shinyanga, ukitokea wilayani Chato ambako mgombea huyo alikwenda kupiga kura yake Oktoba 25, Jumapili iliyopita.

Kwa kawaida wakati wa kampeni Dk. Magufuli alitumia gari la CCM na wakati wote alikaa kiti cha mbele na kuhudumiwa kiulinzi na maofisa wa CCM wakisadiwa pia na maofisa protokali wa chama hicho.

Dk. Magufuli na timu yake ya kampeni waliamua kutumia usafiri wa barabara kurudi jijini Dar es Salaam akitokea Chato badala ya usafiri wa ndege uliozoeleka kwa viongozi wengi wa Tanzania.

Msafara huo uliwasili Kahama majira ya nne asubuhi na kusimama katika hoteli moja iliyoko pembezoni mwa barabara kuu ya Kahama-Shinyanga, kwa lengo la ?kuchimba? dawa.

Baada ya mapumziko hayo mafupi yaliyochukua dakika 10 hivi Raia Mwema lilishuhudia maofisa wa CCM na wale wa Idara ya Usalama wakijadiliana na kabla msafara kuendelea, Dk. Magufuli alibadilishiwa gari na ?kukalishwa? kiti cha nyuma, hali iliyoashiria kuwa kuna mabadiliko katika mfumo wa kiprotokali.

Aidha mfumo wa kuendesha magari ulibadilika, kwa tahadhari huku gari la mgombea huyo likiwekwa kati na kuhakikisha kuwa hakuna gari au kitu chochote kitakachohatarisha usalama wake na ule wa msafara mzima.

Wakati viongozi wa mikoa husika ambako msafara ulipita kuanzia Geita, Shinyanga, Tabora na Singida, walitokeza kumpokea wakiongozwa na makamanda wa polisi wa mikoa hiyo.

Moja wa maofisa wa juu wa CCM aliliambia Raia Mwema kuwa wamefikia uamuzi wa kubadilisha mfumo huo na kumkabidhi Dk. Magufuli kwa timu maalumu ya maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, baada ya kupokea maelekezo kutoka ngazi juu.

Tumepokea maelekezo kutoka juu tubadilishe utaratibu na sisi ni wajibu kutekeleza amri,alieleza ofisa huyo bila ya kufafanua zaidi.

Kuna kila dalili kuwa kwa taarifa za matokeo ya awali, ushindi kwa CCM unanukia na tumeongoza katika baadhi ya mikoa na majimbo hivyo jukumu la ulinzi sasa tunaliacha kwa timu maalumu ya watu wa Idara,? alieleza ofisa mwingine.

Msafara wa Dk. Magufuli ulipumzika juzi, Jumatatu, mjini Dodoma na uliendelea na safari ya kurudi Dar es Salaam kwa njia hiyo hiyo ya barabara, kusubiri matokeo ya mwisho ya uchaguzi huo wa kihistoria nchini.


CHANZO - RAIA MWEMA

No comments: