Wednesday, December 17, 2008

Filamu na Tamthiliya zinapotosha Waadili

(Pichani l-r Kathy Flewellen, Geri Augusto, naWalter Bgoya 1974)

Nakubaliana nao kabisa. Mnakumbuka miaka ya sabini Mwalimu alipopiga maarufuku mtindo wa 'Jiving' na kuimba nyimbo za kizungu. Alisema kuwa si maadili yetu na pia alitaka tukuze utamaduni wa Tanzania. TV na filamu za nje zilikuwa marufuku. Mnakumbuka kulikuwa na censorship board chini ya Tanzania Film Company.

***************************************************************
Na Beda Msimbe (Lukwangule Entertainment Blog)

TAMTHILIYA zinazoonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, zimeelezwa kuwa ndiyo chanzo cha kuharibu jamii na kusababisha wanajamii wengi kuiga utamaduni wa magharibi badala ya ule wa Tanzania na Afrika.

Hayo yalisemwa na Godfrey Mngereza, kutoka Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA wakati akichangia mada kwenye mkutano wa sita wa Sekta ya Utamaduni, unaoendelea kwenye Hoteli ya Oasis mjini Morogoro.

“Ikifika nyakati za usiku, watoto wetu hasa wasichana wamekuwa wakiangalia tamthiliya ambazo nyingi zinakuwa haziko katika maadili ya Kitanzania, hizi ndizo zinasababisha kuporomoka kwa maadili ya kitanzania.

Mngereza alisema kuwa kuna kila sababu ya televisheni mbalimbali kuonyesha tamthiliya zenye kuonyesha maadili na utamaduni wetu. “Mfano, tunataka kuona televisheni ya taifa, TBC1 inapigania maadili mazuri ya utamaduni, lakini si kuwa mfano mbaya katika ujenzi wa maadili,” alisema.

Alisema pia kuwa vibanda vya mitaani vinavyoonyesha sinema, vimekuwa chanzo cha kumomonyoka kwa maadili kwa kuonyesha filamu za ngono. “Utashangaa watoto hawaendi kulala na utasikia wanakwenda kwenye pilau…wenyewe wanaziita hizi filamu za ngono pilau, sasa huwezi kuelewa, lakini wenyewe wameshazipa jina,” alisema.

Naye mtunzi na mchapishaji wa vitabu, Walter Bgoya alisema kuwa Tanzania imeendelea kuwa jalala la filamu za Kinaijeria hata kama hazina ubora na nyingine hazifundishi.
Alisema wasanii wa Tanzania hawana mbinu wala hawawezi kutengeneza filamu bora ndiyo maana kumekuwa na kumwagika kwa filamu hizo. Hata hivyo, alisema kuwa wasanii wa Tanzania wanatakiwa kujifunza zaidi mbinu za kisasa na kuweza kutengeneza filamu bora.

Bgoya alisema kuwa wasanii wa Tanzania hawataki kusoma na kuongeza wigo wa kujifunza. Hii ni wazi kuwa wanatakiwa kusoma sana ili kuweza kutengeneza mwongozo bora utakaotoa filamu bora.

Akizungumzia utandawazi, Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa Tanzania , BASATA, Ghonche Materego alisema kuwa Watanzania wameathiriwa na utandawazi na sehemu kubwa huendesha utamaduni kwa kuangalia umagharibi.

“Hata wasanii wa bongo fleva, wamekuwa wakifanya kazi zao kwa kuangalia mitindo ya mataifa ya Magharibi, hatuwezi kukwepa utandawazi, utaendelea kuharibu jamii ya wasanii kwa kuiga.

2 comments:

Anonymous said...

JEE HUO UTAMADUNI WA KUFANYA MIKUTANO KATIKA HOTELI ZA KIFAHARI NA KUTUMIA FEDHA ZA WALIPA KODI NI UTAMDUNI WETU? UTAMADUNI WETU NI KUFANYA MIKUTANO CHINI YA MITI YENYE VIVULI SIO KATIKA MAHOTELI.

NA JEE UTAMADUNI WETU NI KUVAA SUTI KWENYE MIKUTANO KAMA HUYO MHESHIMIWA? NADHANI AJITIZAME NA YEYE KWANZA KABLA YA KUONGEA

Anonymous said...

Umegonga mahala pake kabisa anonymous. Kwanza utamaduni wa Kitanzania ni upi huo? Kuendesha mashangingi ya bei mbaya huku hospitali hazina dawa na wataalam? Au kuuza mali za wazalendo kwa bei ya kutupa huku wananchi wenye mali zao wakifa kwa njaa? Hao wanaoharibika kimaadili ni juu yao tatizo ni hao wanaojipa mi-posho mikubwa mikubwa kwa ajili ya kujaddili majungu eti wanaita maadili.