Kwa Kfiupi:
DENI LA TAIFA
1. Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa limeongezeka kwa
kasi kubwa sana, hali ambayo inatishia ustawi wa taifa kama halitasimamiwa kwa
umakini na haraka. Hotuba ya Waziri wa Fedha inaonesha kwamba
hadi kufikia Machi 2014, Deni la
Taifa lilifikia shilingi trilioni 30.563 ikilinganishwa na shilingi trilioni
23.674 la Machi 2013. Hili ni ongezeko la takribani trilioni 7 ambayo ni sawa
na ongezeko la asilimia 29 kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.
2. Mheshimiwa Spika, hili ongezeko la mikopo ya
takribani shilingi trilioni 7 kwa mwaka mmoja tu, halijawahi kutokea katika
historia ya nchi yetu. Ongezeko hili la takribani trilioni 7 ni sawa na bajeti
nzima (full budget) ya mwaka 2008/9 ambayo ilikuwa ni shilingi trilioni 6.839.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2008/9 ni miaka mitano tu iliyopita. Ukopaji wa namna hii unatishia uchumi na usalama wa nchi.
3. Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa ripoti za Benki Kuu na hotuba za bajeti za miaka iliyopita za
Mawaziri wa Fedha, deni la Taifa limeongezeka kwa kasi kutoka shilingi trilioni
9.3 mwaka 2007/8 hadi shilingi trilioni 30.6 mwaka 2013/14. Hii ni wazi kuwa
deni liliongezeka kwa kiasi cha shilingi trilioni 21.3. Serikali imelipa
shilingi trilioni 4 na kufanya fedha zilizokopwa kuwa jumla ya shilingi
trilioni 25.3 katika kipindi hicho cha miaka saba tu. Huu ni ukopaji hatarishi
kwa uchumi wa taifa letu.
4. Mheshimiwa Spika, licha ya deni hili kuwa hatarishi kwa uchumi
wa Taifa, Serikali bado inatajaria kuongeza deni hilo kwa kukopa shilingi
trilioni 4.3 kama ilivyoainishwa katika bajeti ya mwaka 2014/15.
5.
Mheshimiwa Spika,
Serikali imeonesha kushindwa
kulipa deni hilo kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato, badala yake imekuwa
ikikopa ili kulipa deni. Mfano hotuba ya bajeti ya mwaka 2014/15 imeonesha
kuwa katika shilingi trilioni 1.8
zilizokopwa katika soko la ndani, zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zilitumika
kulipa madeni ya hati fungani wakati shilingi trilioni 0.69 tu ziliwekwa kwenye
miradi ya maendeleo. Hiki ni kiashiria
cha karibu sana kwa serikali kufilisika. Kukopa mikopo ya kibiashara yenye
riba kubwa ili kulipa mikopo yenye riba ndogo au kwa uendeshaji wa
kawaida wa serikali au taasisi zake ni kiashiria cha kutosha kuainisha maamuzi
yasiyo na uelewa wa kawaida sana wa utawala na usimamizi wa fedha. (basic business and economic sense). Mikopo
ya kibiashara hutafutwa kwa matumizi ya uwekezaji wenye lengo la uzalishaji.
6. Mheshimiwa Spika, katika uchumi unaokuwa kwa
wastani wa asilimia kati 6.5 na 7 kwa mwaka, ni vigumu sana kuweza kulipa deni
la Taifa linalokua kwa wastani wa asilimia kati ya 15 na 30 kwa mwaka. Bila
kuwa na vyanzo vipya vya mapato au
kusamehewa deni hili itakuwa vigumu sana kuweza kulipa deni hilo kikamilifu.
Hii ni kwa sababu uwiano wa ukuaji wa uchumi hauendani na kasi ya ukuaji wa
deni hata kidogo. Pamoja na upungufu wote huu, Serikali imeendelea kujitapa
kuwa inakopesheka, na hivyo kuashiria kutokuwepo na hofu yeyote ya kukopa huku
holela.
7.
Mheshimiwa Spika,
kinachosikitisha zaidi ni kuwa
sehemu kubwa ya mikopo hii inakopwa
katika soko la ndani. Hali hii imekuwa ikileta ushindani mkubwa kwa wananchi na
wajasiriamali wanaotaka kukopa ili kukuza mitaji. Hali hii hufanya riba za
mabenki kushindwa kushuka na hivyo kuwaathiri wakopaji na uchumi wa nchi kwa
ujumla. Kwa maneno mengine, serikali imekuwa inazuia wajasiriamali wasikope kwa
riba za bei nafuu, hivyo kufanya baadhi ya wanaokopa kwa riba zilizopo, ambazo
ni kubwa kufilisiwa. Hali hii hurudisha biashara nyuma na inainyima serikali
fursa ya kukuza uchumi na kukusanya mapato zaidi.
8. Mheshimiwa Spika, mataifa mengi duniani yanakopa na yana madeni makubwa.
Suala la msingi la kutofautisha nchi
moja na nyingine ni kasi ya kukua kwa deni husika na matumizi ya mkopo
huo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inauliza na kutaka majibu kutoka kwa
Serikali matumizi ya fedha zilizokopwa na nchi yetu ndani ya miaka 7 ni yapi na
yameleta maendeleo kiasi gani kwa Taifa ( value for money).
No comments:
Post a Comment