TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
JK:
Vyama vingi vimepanua wigo wa kisiasa
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mfumo wa
vyama vingi vya siasa ni mzuri, umeleta matumaini kwa kupanua wigo na kufungua
zaidi uwanja wa kisiasa pamoja na kuiwajibisha Serikali.
Hata hivyo, Rais
Kikwete amesema kuwa ili mfumo huo uboreshwe zaidi na uweze kuimarisha misingi
mikuu ya maendeleo ni lazima uendeshwa kwa watu kufuata sheria na wala siyo
kuingiza matumizi ya nguvu ambayo yanaweza kuvuruga nchi.
Rais Kikwete ambaye
pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama aliyasema hayo jana,
Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara (Lecture) kuhusu Usalama wa
taifa – The Security of a Nation- kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi - National Defence College (NDC) Kunduchi,
mjini Dar Es Salaam.
Rais Kikwete alikuwa
anajibu swali la mwanafunzi wa kozi ya pili kwenye chuo hicho kutoka Kenya
ambaye alitaka kujua jinsi gani vyama vingi vya siasa vinavyoathiri umoja wa
kitaifa na kuibadilishaTanzania kufuatia miaka zaidi ya 30 ya Tanzania kuwa
nchi yenye kuleta matumaini kwa nchi nyingine za Afrika na Waafrika.
Rais kikwete alisema:
“Vyama vingi ni vizuri. Mfumo wa vyama vingi unaleta matumaini kwa kupanua wigo
wa kisiasa ambao haukuwa mpana kiasi hicho huko nyuma. Sasa mtu anaweza kuamua
kujiunga na chama chochote cha siasa anachokipenda yeye.”
Aliongeza rais
Kikwete: “Ni mfumo ambao unaiwajibisha Serikali. Ni mfumo mzuri kwa upanuzi wa
demokrasia. Sasa watu wanaweza hata kuamua kupunguza bajeti ya safari za Rais
nje ya nchi. Wanadhani kuwa Rais anaweza kufanikiwa zaidi na Tanzania kupita
hatua za maendeleo haraka zaidi kama Rais atabakia amejifungia ndani ya nchi.”
Rais Kikwete alizidi
kujibu swali hilo: “Jambo la maana ni kwamba tunahitaji aina mbali mbali ya
mawazo. Mawazo ya namna hiyo hayaathiri demokrasia. Mawazo ya namna hiyo
yanasaidia hata chama changu kuimarika zaidi.”
Hata hivyo, Rais
Kikwete amesema kuwa mfumo huo utavurugika endapo baadhi ya watu wataendekeza
matumizi ya nguvu na hoja za nguvu badala ya kupambana kwa hoja na nguvu ya
hoja.
“Wasiwasi wangu ni
kuingiza matumizi ya nguvu katika ujenzi wa demokrasia. Ni makosa kwa watu
kukimbilia kutumia nguvu baada ya kushindwa kwenye hoja. Na hili halivumiliki
na likitokea basi Serikali itaingilia kati kudumisha amani.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR
ES SALAAM
21 Juni, 2014
No comments:
Post a Comment