SEMA USIOGOPE SEMA! Yaliyosemwa na Mheshimwa Augustino Ramadhani ni mazito!
************************************************************************
Kutoka ippmedia.Com
Jaji Mkuu apasua bomu
2008-10-17
Na Simon Mhina
Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, ametoboa siri ya ufisadi unaokua kila kukicha nchini kwamba unatokana na uchaguzi.
Ameonya kama rushwa kwenye uchaguzi haitadhibitiwa basi ufisadi ambao umekithiri kila eneo utaendelea kuitafuna nchi.
Alisema rushwa na ufisadi katika nchi ni sawa na watoto mapacha, na mama yao ni uchaguzi.
Jaji Mkuu alisema hayo jana wakati akitoa mada katika kongamano la siku mbili la kujadili rushwa katika siasa na ugharimiaji wa shughuli za kisiasa katika vyama.
Katika hutuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Msajili wa Mahakama Kuu, Ferdinand Wambali, Jaji Mkuu alisisitiza kuwa bila kudhibiti rushwa kwenye uchaguzi, uovu huo utaendelea hata katika vyombo vya kutunga sheria na vile vya utoaji haki kama mahakama.
``Ukimpitisha mgombea kwa misingi ya rushwa, ujue kiongozi huyo ndiye utakayekutana naye mbele ya safari katika kukuhudumia. Mtu aliyetokana na rushwa kwake ni vigumu kukemea rushwa hata kama imemzunguka,`` alisema.
Naye Jaji Kiongozi Mstaafu, Amir Manento, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, alisema umefika wakati sasa kumpa nafasi Rais kuteua mawaziri nje ya wabunge kwa kuwa wengi wao wamepata nafasi hizo kwa kutoa rushwa.
Alisema wabunge ambao huingia bungeni kwa njia ya rushwa, wanapoteuliwa kuwa mawaziri hutumia fursa hiyo kurudisha fadhila kwa wale waliowakopesha takrima.
Alionya kwamba hakuna mfadhili yeyote ambaye anaweza kutoa fedha zake bure bila kuwa na lengo ya kupata faida baadaye.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alisema chanzo cha rushwa, ufisadi na aina zote za ubadhirifu wa mali ya umma, ambavyo vimeshamiri nchini vinatokana na viongozi kuingia madarakani kwa njia ya rushwa.
Aidha, alisema bila kukomesha rushwa katika uchaguzi, itakuwa vigumu kukomesha ufisadi nchini, kwa vile viongozi wengi wameogolea katika rushwa hadi kufikia katika ngazi walizo nazo.
Kutokana na sababu hizo, Warioba aliona kwamba ni vigumu kwa viongozi waliochaguliwa kwa rushwa kuweza kupambana na janga hilo.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Tasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) lilianza jana jijini Dar es Salaam na linamalizika leo.
Jaji Warioba alisema hivi sasa Tanzania inaelekea kubaya kwani rushwa inaonekana kukubalika kabisa kuwa moja ya kigezo cha kumpima mgombea.
``Hivi sasa hata kama utahubiri sera nzuri kiasi gani, hata kama mgombea anayo sifa kubwa kiasi gani, hawezi kupita bila kutoa rushwa, hizi ni dalili mbaya,``alisema.
Jaji Warioba alisema kutokana na rushwa kushamiri, hivi sasa kampeni za mgombea kuomba kuteuliwa na chama chake zimekuwa nzito kuliko kampeni za ujumla za kiserikali.
Alisema hata baada ya sheria ya takrima kufutwa bado wagombea wamekwa wakibuni mbinu mbalimbali za kugawa rushwa.
Warioba alipinga vikali madai kwamba umasikini wa wananchi ndio unasababisha rushwa kushamiri.
Alisema kwa maoni yake, rushwa inashamirishwa nchini na matajiri pamoja na viongozi ambao tayari wanazo pesa.
Alisema hata hapa nchini, miaka ya nyuma watu walikuwa masikini wa kutupwa, lakini hapakuwa na rushwa katika uchaguzi.
``Kwa hiyo si kweli kwamba umasikini ndio unasababisha rushwa katika uchaguzi, wanaosababisha rushwa na kuwafundisha watu waamini katika rushwa ni viongozi na matajiri,`` alisema.
Jaji warioba alisema kunatokea matatizo makubwa wakati wa upigaji kura, kwani imebainika kwamba baadhi ya wasimamizi, wanapokea rushwa ili `kuvizima` vyama ambavyo hawavipendi.
Alisema japokuwa wagombea huwaamini sana mawakala, lakini sio siri kwamba mawakala hao pia hutumiwa kuwahujumu baada ya kupewa rushwa.
Alionya kuwa kutunga sheria nyingi za kuzuia rushwa hakusaidii kama jamii yenyewe haijaamua kupinga suala hilo.
Vilevile, alisema daftari la kudumu la wapiga kura kimsingi sio mwarobaini wa matatizo ya uchaguzi nchini, kwani linaweza kuchezewa ili kuharibu kumbukumbu sahihi.
Kuhusu mapato ya vyama, Warioba alisema kunahitajika uwazi kwa wale wanaofadhili vyama, ili kuviepusha vyama hivyo visigeuke kuwa vibaraka.
Mathalan, alisema kuna uwezekano mkubwa wa viongozi kugeuka vibaraka wa mafisadi kama waliingia madarakani kwa kufadhiliwa kwa njia za rushwa.
Alionya kuwa si sahihi kutoa ruzuku kwa vyama vyenye wabunge pekee, na kutaka utafutwe taratibu wa kuvipatia vyama vyote ruzuku ili kuweka uwiano.
Vilevile, alisema si sahihi kuvifuta vyama vitakavyokosa kura kabisa, badala yake ameshauri viachwe kwani huenda kuna siku wananchi wakavihitaji.
``Kanu kilikuwa chama kikubwa sana, lakini sasa ni kidogo na vile vidogo sasa vimekuwa vikubwa, hivyo tusifute chama eti kwa vile ni kidogo au hakikubaliki, kuna siku kitakubalika,`` alisema.
Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) akichangia katika kongamano hilo alisema kwamba ufisadi nchini unashamiri kutokana na matajiri na wanasiasa kuendeleza tabia hiyo na wala si umaskini kama wengi wanavyopotosha.
Dk. Emmanuel Makaidi, Mwenyekiti wa National Legue for Democracy (NLD) alisema kwamba serikali ilifuta sheria ya takrima ambayo ilikuwa uchochoro wa kutoa rushwa, lakini inataka kuirudisha kwa njia nyingine ambayo ni mfuko wa jimbo.
Pia alisema daftari la wapigakura linapaswa kuhakikiwa mara kwa mara kuepusha chama kimoja kutumia watendaji kufuta au kuongeza majina kwa manufaa ya chama chao.
SOURCE: Nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Hakuna lolote la maana hapo. Ni hadithi tu - paukwa pakawa!
Ufisadi sasa umekuwa wimbo wa taifa na "Jaji Mkuu" hajachukua hatua yoyote katika kuhakikisha haki inatendeka kwa kushughulikia wanaofilisi nchi. Jaji Mkuu kuendeleza longolongo haisaidii. Cha muhimu ni yeye kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake.
Post a Comment