Wednesday, March 18, 2009

Ubakaji na mauji ya watoto wadogo huko Iringa!

Jamani, hivi huko Iringa kuna nini? Kuna habari kuwa watoto wadogo yaani chini ya miaka sita wanabakwa huko! Sasa huo ni mchezo gani? Najua Afrika Kusini watu wanabaka hao watoto wakidhani eti watapona UKIMWI! Na nashangaa baba zima anataka nini na mtoto mdogo hivyo. Kama hao wahalifu watakamatwa napendekeza wakatwe ume/bolo zao mara moja! Tena mbele ya umati!

********************************************************************

Kutoka Lukwangule Blog:

VITENDO vya ubakaji vimeanza kushamiri mkoani hapa, huku matukio ya hivi karibuni yakionesha wanaokumbwa na sakata hilo wakiwa ni watoto wa kike wenye umri chini ya miaka sita.

Katika matukio mawili yaliyotokea ndani ya wiki tatu, mtoto mmoja amekufa baada ya kufanyiwa unyama huo huku mwingine akiendelea kutibiwa katika hospitali ya Mkoa wa Iringa. Tukio lililopelekea mmoja wa watoto hao kufa lilitokea juzi, baada ya mtoto huyo (jina linahifadhiwa) kubakwa na watu wasiojulikana hadi mauti yake yalipomfika na hatimaye kutupwa kwenye bonde dogo la mlima Tagamenda uliopo mita 600 kutoka stendi ndogo ya mabasi ya mikoani ya Ipogolo ya Iringa mjini.

Polisi waliokuwepo kwenye eneo hilo walifanikiwa kuutoa mwili wa mtoto huyo mwenye miaka mitano kutoka katika bonde hilo lenye miti mingi yenye miba akiwa hana nguo na amelowa damu sehemu zake za siri, huku umati mkubwa wa watu waliokuwepo wakiangua kilio kwa uchungu.

Polisi hao wakiongozana na baadhi ya ndugu wa mtoto huyo waliukimbiza mwili huo katika hospitali ya mkoa wa Iringa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na wakati tukienda mitamboni ulikuwa umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk Oscar Gabone alisema katika tukio lingine lililohusisha mtoto mwingine wa miaka mitano kubakwa kwamba lilitokea Februari 22 katika milima ya Gangilonga mjini Iringa aliyepokelewa hospitalini hapo Februari 23.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Jamila Mashaka alisema kwa uchungu kwamba siku ya tukio, mtoto wake na wenzake walikuwa wakicheza nje ya nyumba yao baada ya kujipatia chakula cha jioni.

“Ilikuwa majira ya saa moja jioni, baada ya kupata chakula cha jioni mwanangu huyu na wenzake wakawa wanacheza nje, hata hivyo dada yake alikuja chumbani kwangu baadaye akiniambia kwamba mdogo wake haonekani,” alisema.

Alisema jitihada za kumtafuta katika maeneo wanayoishi na kwa marafiki zake aliokuwa akicheza nao hazikuzaa matunda na ndipo ilipofika saa 4.30 usiku wa siku ya tukio walipkwenda kutoa taarifa Polisi.

“Kesho yake saa 4.30 asubuhi nililetewa taarifa kwamba kuna mtoto yuko hospitali ya mkoa, na nilipokwenda kumtazama nikabaini kwamba ni wa kwangu. Nawashukuru madaktari wanaomuhudumia kwasababu hivi sasa anaendelea vizuri,” alisema.

habari hii kwa hisani ya Frank wa HabariLeo Iringa

No comments: