Monday, May 04, 2009

SERIKALI KULIPA FIDIA WALIOATHIRIKA NA MABOMU YA MBAGALA - PINDA

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali imekubali kubeba mzigo wa kulipa fidia fidia kwa wakazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam ambao wamehabiriwa nyumba na mali zao kutokana na mlipuko wa mabomu uliotokea wiki iliyopita.

Akizungumza na wakazi wa Mbagala Kuu, wilayani Temeke alipokwenda kuwapa pole jana jioni (Jumamosi, Mei 2, 2009), Waziri Mkuu aliwataka wanakamati waliopangiwa kufanya kazi ya tathmini ya mali zilizoharibika zikiwemo majumba, mali, misikiti na makanisa na kuikamilisha mapema iwezekenavyo.

Alisema kamati iliyoteuliwa ifanye kazi ya kukagua mali na kufanya tathmini ili Seriklai ione namna na kutoa kufidia ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete ambalo lilitolewa Mei Mosi, 2009.

“Serikali imeshaanza kugharimia gharama za mazishi kwa watu waliokufa katika ajali hii, na itaangalia jinsi ya kuwapa pole wale waliofiwa ili kupunguza makali ya maisha na kuwasaidia waliopata ulemavu kwa matibabu na vifaa,“ alisema Waziri Mkuu.

Alisema kazi iliyo mbele ni kubwa lakini Srikali itajitahidi kuendelea kuwahudumia hadi warejee katika hali zao za awali.

Aliwashukuru watu waliojitolea kwa nafasi mbalimbali ikiwemo wale waliojitosa katima mto Mzinga ili kuopoa maiti za watu waliokufa wakati wakijitahidi kujiokoa kutoka kwenye ajali hiyo.

Waziri Mkuu pia alielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. William Lukuvi juhudi za kuwakimu wahanga ikiwa ni pamoja na kuwapatia magodoro, vyandarua, mablanketi, vyakula na maji ya kunywa.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
DAR ES SALAAM..

JUMAPILI, MEI 3, 2009.

No comments: