Monday, April 21, 2008

Kifo cha Ditopile


Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete wakimfariji mjane wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Marehemu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri huko nyumbani kwake Upanga. Kulia ni Mariam Ditopile mtoto wa marehemu na nyuma ya Rais ni mtoto wa Rais, Rashid Chodo Kikwete. Aliyesimama karibu na Mama Salma Kikwete ni ndugu wa marehemu ambaye jina lake halikuweza kutambulika mara moja

Maziko ya Mheshimiwa Ditopile ambayo yalikuwa yafanyike Aprili 21,2008 huko Kinyerezi sasa yatafanyika Aprili 22. Jana Aprili 20 maiti yake iliondolewa hospitali ya mkoa wa Morogoro na kupelekwa hospitali ya Jeshi Lugalo kwa hifadhi.Pichani jeneza lenye mwili wa marehemu Ditopile likiingizwa katika gari ya wagonjwa la jeshi kikosi cha Pangawe, Morogoro. Picha nyingine ni Rais Jakaya Kikwete akimpa salamu za pole mke wa Ditopile nyumbani kwake Upanga hapo Aprili 20,2008.


Picha kutoka Lukwangule Blog

Habari Kutoka Michuzi Blog


ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Tabora Kepteni Mstaafu Ukiwaona Ditopile Mzuzuri aliyefariki jana Aprili 20,2008 majira ya saa 3:00 katika Hotel ya Hilux iliyopo Mkoani Morogoro anatarajiwa kuzikwa kesho huko Kinyerezi, pembezoni mwa jiji la Dar, maeneo ya Segerea.
Mamia ya waombolezaji wamefurika nyumbani kwa mareehemu mtaa wa Mindu, Upanga, Dar, kujiunga na familia ya marehemu katika kuomboleza kifo hicho ambacho kimeacha watu wengi midomo wazi.

Marehemu Ditopile alifikia katika hoteli ya Hilux ,Morogoro akitokea Tabora akiwa safarini kuelekea Dar es Salaam kwa mapumziko akiwa ameambatana na mkewe mdogo,Tabia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa hoteli hiyo Joseph Kitambi, Ditopile alifika hotelini hapo Aprili 18, majira ya saa 5:30 usiku,ambapo alipatiwa chumba No.106.

Kitambi alisema Aprili 19,majira ya saa 5:00 usiku watumishi wa hoteli hiyo wakati wakifunga shughuli zao za huduma, Ditopile alikuwa bado hajarudi hotelini kutoka kwenye shughuli zake ambazo amekuwa akizifanya kwa muda wote tangu kufika hotelini hapo.

Akifafanua zaidi Mkurugenzi huyo alisema, Aprili 20 majira ya saa 2:30 asubuhi mkewe Tabia alitoa taarifa ya kuzidiwa kwa mumewe na kuomba msaada ambapo wahudumu walifika katika chumba chake na kumwangalia na kukuta akiwa amelala kwenye kochi,na alionekana kuwa ni mtu asiyejitambua,na kutoa taarifa kwenye hospitali kuu ya Mkoa kwa msaada zaidi.

Mkurugenzi huyo aliiambia habari leo kuwa marehemu alifariki kabla ya kupata kifungua kinywa cha asubuhi ambacho hutolewa na hoteli hiyo kuanzia saa 12:30 asubuhi hadi majira ya saa 4:30.
Alisema kuwa wauguzi wa hospital walifika katika hoteli hiyo,na kumchukua kwenye gari,akionekana kama mtu ambaye ameshafariki,na kumpeleka hospitalini kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alidai kwa kipindi chote ambacho Ditopile amekuwa katika hoteli hiyo,alionekana kuwa ni mtu aliyekuwa akisumbuliwa na maradhi,kutokana na mwili wake kudhoofu na nyuso kutokuwa na uchangamfu.

Aidha alidai kuwa wakati wafanyakazi hao wanautoa mwili wake nje kwa kushirikiana na madaktari waliofika kutoka hospitalini,walikuta mswala wa kuswalia,ambapo mkewe alidai kuwa mumewe aliamka alfajiri na kuswali swala ya asubuhi,kabla ya mauti kumkuta.Baada ya mwili huo kufikishwa hospitalini Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa Dkt.Meshack Masi alisema alipokea taarifa kutoka kwenye uongozi wa hoteli hiyo,iliyoeleza kuwa Ditopile amezidiwa hivyo wanahitaji msaada haraka.

'Kweli tulipokea taarifa hizo…walikuwa wakiomba msaada haraka…na sisi tulituma gari pamoja na wauguzi mara moja kwenda pale Hilux hoteli na kumleta hapa hospitalini'alisema Daktari Masi.

Hata hivyo Dkt.Masi alisema baada ya wauguzi kufika hotelini hapo,na kuuona mwili wake waligundua kuwa ameshafariki na kuubeba mwili wake na kuupeleka hospitalini hapo na kuulaza wodini grade 1, kwa ajili ya kuudhibitisha,kabla ya kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Thobias Andengenye alisema kuwa marehemu alipotoka mkoani Tabora alifika Mkoani Morogoro na kwenda Wilaya ya Mvomero kwa ajili ya kukagua mashamba yake yaliyopo kwenye eneo la Mgongola akiwa na mkewe mdogo Tabia kabla ya kufika Morogoro Mjini ambapo alipata malazi.

Aliongeza kuwa baada ya kukagua mashamba yake marehemu aliondoka Wilayani Mvomero na kuja Morogoro Mjini ambapo alifika majira ya saa 3 usiku na kufikia kwenye hotel ya Hilux iliyopo Mjini hapo kwa ajili ya kupata malazi ambapo alipewa chumba No.106.

Alisema marehemu aliitumia siku ya Aprili 19,kutembelea ndugu na jamaa zake kabla ya kurudi nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam,na kudai kuwa alirudi hotelini hapo majira ya saa 12 jioni,ambapo alitarajia kuondoka Aprili 20 kurudi nyumbani kwake.

Katika ziara ya marehemu ya kutembelea na kusalimiana na ndugu zake,pia alipata wasaa wa kumtembelea Chifu Kingalu Mwana Banzi wa 14 wa kabila la waluguru.

Kwa upande mwingine mdogo wake na Marehemu, Selemani Mzuzuri,alipohojiwa alisema hana lolote la kuzungumza na kueleza kuwa bado ana majonzi mazito ya kifo cha kaka yake,hivyo hataweza kuzungumzia jambo lolote.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Meja Jeneral mstaafu Said Kalembo ambaye alifika hospitali ya mkoa wa Morogoro akizungumza na waandishi wa habari alisema kwamba mwili wa marehemu unatarajiwa kuchukuliwa na gari la jeshi na kusafirishwa kuupeleka kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kwenye hospitali ya Jeshi ya Lugalo iliyopo Dar es salaam.

Marehemu Ditopile, ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, amewahi pia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Lindi na Tabora kabla ya kukabiliwa na kesi ya Mauaji bila kukusudia.

1 comment:

Anonymous said...

Watu huwa tunasahau kuwa duniani ajali hutokea, kama Marehemu Ditto angelijua hiyo siku kuwa hayo yangemkuta asingetoka nje ya nyumba yake. Hivi kuna mtu kweli anaweza kuamka asubuhi akasema leo naenda kumuua dereva wa daladala? Je mna ushahidi wa kilichotokea mpaka mnamhukumu. Laiti mngemjua alikuwa ni mtu wa aina gani msingetoa hayo maneno yenu. Na hata hivyo aliomba kwenda kutibiwa mara kibao lakini alikataliwa kwa kisingizio kuwa atatoroka, sasa kumzuia kwenda kutibiwa kote faida yake ni nini? Mungu ameondosha mzizi wa fitna.

Niliwahi kufanya kazi na marehemu Dittopile sio chini yake lakini nikiwa sehemu nyingine kabisa mahusiano ya kikazi yalitukutanisha na nilijifunza mengi sana kupitia kwake. Hakuwa na kibri wala jeuri pamoja na ukubwa wa cheo chake, alikuwa mkweli na mahali palipokuwa na uonevu alisema hili ni la uonevu. Alinifundisha kuwaamini wananchi wa vijijini na kushauri pesa za miradi kupelekwa moja kwa moja kwa wanakijiji ili kuleta ufanisi na hakuficha alisema wazi pesa hizi zikienda halmashauri hazitawafikia walengwa. Alikataa kusaini mafomu ya LF23 yaliyompa mtu/kampuni haki ya kuchukua ardhi ya wanakijiji bila ushahidi wa wananchi kulipwa fidia ya ardhi, alitetea sana wananchi wa chini kulipwa fidia ya ardhi inayochukuliwa na lazaidi angekuwa na uwezo angozuia ardhi ya wanyonge kuchukuliwa. Aligombana na Lowassa juu ya hili na kuzuia mradi wa kuchuka ardhi za watu masikini wa pwani bila kuwalipa fidia kwa kisingizio cha kupanua dar es salaam. Na mradi huu ulipopita baadae Dittipile alikuwa akiuliza hii ardhi ya huku tu ndio haina thamani mbona watu hawaendi kuchukua ardhi bure huko Arumeru na Kilimanjaro?

Marehemu Dittopile alisimamisha mabasi yanayokwenda hovyo au kupakia abiria mpaka kwenye carrier huko Lindi alivyokuwa Mkuu wa Mkoa ili kuwanusuru wananchi wake na vifo vya kizembe vinavyosababishwa na madereva wazembe na wakorofi.

Hata hiyo ya kesi ya dereva wa dala dala hakutoka nyumbani kwake akasimama barabarani akamshuti driver wa dala dala. Sitaki kuingilia na kusema ilikuwaje lakini kuna siku ukweli utajulikana. Kila mtu ana mwanzo na mwisho wake huo ndio mwisho wake lakini kumbukumbu yangu ya Dittopile nakumbuka mara ya mwisho nilikutana naye anatoka safari ya kikazi huko vijijini anawahi kwenda kuapishwa kuwa Mkuu wa Dodoma. Neno lake lilikuwa endelea na mwendo huo huo kama mradi endeleeni kuwapa wanavijiji pesa za kufanya miradi ya maendeleo wao wenyewe kwa sasa ni ngumu kwao lakini huo ndio uwezeshaji watajifunza na baadae wenyewe wataweza kusimamia miradi yao ya maendeleo wao wenyewe!

Huyo ndiye Dittopile niliyemjua mimi sio yule aliyekuwa akichorwa na vyombo vya habari.

Natoa pole kwa familia ya marehemu kwa msiba mkubwa uliwakuta. Innalillahi wainnaillaihi rajiuna.

Na sie tuliobaki kila siku tukumbuke kuwa Mola ndiye mpangaji wa yote, hujafa hujaumbika hujui hatma yako itakuwaje hata dakika tano zilizoko mbele yako.