Wednesday, April 23, 2008

Tuzo za filamu za Vinara zaiva!

PRESS RELEASE FROM ONE GAME:

Tuzo za filamu za Vinara zaiva!

Zoezi la ukusanyaji wa filamu zitakazoshiriki katika kinyang'anyiro cha Tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania lilimalizika rasmi Ijumaa iliyopita ya Aprili 18, 2008 ikiwa ni hatua ya kwanza kabla ya kufanyika kwa onesho la utoaji wa tuzo hizo.

Akiongea nasi mratibu wa tuzo hizo zinazotolewa na kampuni ya One Game Promotions ya jijini Dar es Salaam, Khadija Khalili alisema kuwa, wamefanikiwa kupokea filamu zipatazo sabini na mbili kwa ajili ya kushiriki katika tuzo hizo kwa mwaka 2007/08.

"Zoezi la ukusanyaji wa filamu lilifanyika kwa wiki kadhaa, ambapo watayarishaji wa filamu walitakiwa kuchukua fomu katika vituo vilivyopangwa na kuzirejesha katika ofisi za Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) pamoja na nakala za filamu zao," akasema.

Akaelezea zaidi kuwa, kukamilika kwa hatua hiyo ya ukusanyaji wa filamu hizo, ndio mwanzo wa hatua nyingine katika kuelekea kupatikana kwa wasanii watakaofanikiwa kutwaa tuzo hizo kwa mwaka huu.

Bi Khalili akaongeza, baada ya kupokelewa kwa filamu hizo, jopo la majaji litazipitia na kuibuka na majina matano katika kila 'kategori' na baadaye kusubiri hadi siku ya onesho la kutolewa kwa tuzo hizo kwa ajili ya kutambua atakayeibuka na tuzo kwa kila 'kategori'.

"Siku hiyo zitatolewa tuzo ishirini pamoja na tuzo ya heshima kwa msanii aliyetoa mchango mkubwa kwa sanaa hiyo nchini, hivyo tutakuwa na 'kategori' kumi na tisa zitakazokuwa na majina matano-matano, ambapo mmoja wao atatwaa tuzo," akafafanua.

Tuzo zinazowaniwa ni Filamu Bora ya Mwaka, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora Mwaka wa Kike, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kike, Mwongozaji Bora wa Filamu wa Mwaka na Mchekeshaji Bora wa Mwaka.
Nyingine ni Mwandishi Bora wa Filamu, Mtunzi Bora wa Filamu, Filamu Bora ya Kutisha, Muigizaji Mwandamizi Bora Kike, Muigizaji Bora Mwandamizi wa Kiume, Adui Bora wa Filamu, Mhariri bora wa Filamu na Tuzo ya Heshima.

Wadhamini wakuu wa tuzo za Vinara ni Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Ndovu Special Malt pamoja na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC). Onesho la tuzo hizo linatarajiwa kufanyika Mei 30 mwaka huu.

No comments: