Wednesday, April 30, 2008

Utamu wa Tunda la Kuiba

Wadau nimekuta haya mashairi JAMBO FORUMS. Yanafurahisha kweli.

*****************************************************************
Jamvini najikongoja,

Cheichei kwa pamoja,

Heko mlotoa hoja

'Sauti ya Shamba'

kwa kuleta hii hoja,

Naye 'Mwangwi wa Handaki' kajibu moja kwa moja,

Kaomba tumalizie Waridi chake kioja,

Nami nabinya vitufe kujibu hoja kwa hoja,

Tunda la kuiba tamu!


Tulia na utulize moyo wako,

Punguza kilio chako,

Kwani si wewe peke yako,

Hata wa pembeni yako,

Tuna kilema ka'chako,

Tunda la kuiba tamu!


Ingawaje nina tunda langu,

Lindani shambani mwangu,

Naliona kama nungunungu,

Linachoma kwa uchungu,

Nachelea la mwenzangu,

Nauona ulimwengu,

Si wangu ni wa wenzangu,

Nidokoe tunda tamu!


Tunda limenishangaza,

Kwa unono lapendeza,

Kwa deko lanipumbaza,

Lina ngozi yateleza,

Na macho yakulegeza,

Udenda nikachuruza,

Jino nikatumbukiza,

Tunda nikalibinyiza,

Jamani la kuiba tamu!


La kuiba tamu tunda,

Hiyo ndiyo yake inda,

Lau upepo ukipinda,

Akakufuma mlinda,

Tendo baya takutenda,

Kwa machozi utaenda,

Nenda ewe mwana kwenda,

Hapo tamu huwa chungu!


Wahenga wajisemea,

Yana tabu mazoea,

Tunda 'kishalizoea,

Sasa lishakupotea,

Tena umelikimbia,

Masikini la kuiba tamu!


Yana tabu mazoea,

Mengine 'takodolea,

Kwani tamu 'mekolea,'

Talinyemelea pea,

Kidole talinyoshea,

Nono tajichagulia,

Mate tajidondoshea,

Utamu jamani tamu,

unda la kuiba tamu!

Litabaki kuwa tamu!!!


By Palloma (Binti wa Kitanga)


***********************************************

Mzee Mwanakijiji Ajibu:


Tulia mwana nipange, majibu yangu niseme,

Tulia bila mawenge, hoja zangu mzisome,

Tulia miye nilonge, hili tunde nisiteme,

Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!


Tulia nikuambie, uzuri wa tunda lile,

Tulia nisimulie, tunda hilo ni la kale,

Tulie nihabarie, na wewe hilo ukale,

Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!


Tulia mwenye kuhoji, Bwana Bushiri kapanda,

Tulia la mwenye mji, hakuliacha kuvunda,

Tulia yeye mpaji, kalitunza hilo tunda,

Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!


Tulia mimi nakiri, sikuingia gharama,

Tulia akisafiri, najinoma huku nyuma,

Tulia alfajiri, hadi wanapoadhama,

Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!


Tulia kama mlevi, ndivyo ninavyosambua,

Tulia kama mvuvi, tunda ninalichambua,

Tulia silete gomvi, utamu nimeng'amua,

Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!


Tulia hata samadi, wa kijiji sikuweka,

Tulia si ukaidi, mwenyewe naneemeka,

Tulia silipi kodi, la bure nalitamka,

Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!


Tulia mwana nitame, kaditamati nafika,

Tulia msiniseme, ati nimeghafirika,

Tulia kisu kichume, na mchuzi kumwagika,

Tunda lile la jirani, hilo halina gharama!


Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Shamba)

2 comments:

Anonymous said...

KWA MTAJI HUU UKIMWI HAUTAKAA UISHE KAMWE NDIO MAANA SIKU HIZI MAMBO YA KUCHUKILIANA MKE NA MUME YAMEKUWA KAMA KITU CHA KAWAIDA LAKINI NI UKOSEFU MKUBWA WA MAADILI. NATAFSIRI MASHAIRI HAYA KWA MTAZAMO WA MAHUSIANO YA KIJAMII!

Anonymous said...

tatizo wenye ndoa wakishazoeana huwa hakuna manjonjo ya kimapenzi tena zaidi ya kulea watoto hivyo mtu akitoka nje anapata vitu adimu ambavyo amevimiss kwa muda mrefu!