Tuesday, January 16, 2007

Ndoto inaweza kutokea Kweli!




Mimi nimewahi kuota kuwa natuzwa Oscar. Nilivyoamka ilibidi nicheke. Nikasema haiwezekani nituzwe hiyo Oscar, kwanza weusi huwa hawatuzwi, na pili nani atanipa nafasi ya kuigiza kwenye sinema itakayonipa nafasi hiyo.

Lakini jana nimeamini kuwa ndoto huwa inaweza kutokea kweli. Baada ya kuona, Jennifer Hudson, kashinda Golden Globe Award kama Best Supporting Actress. Ijumaa alishinda Critics Choice Awards na sasa watu wanasema anastahili Oscar. Mwaka jana saa hizi nani alitegemea kuwa leo, Jennifer angekuwa Superstar? Ni sinema yake ya kwanza kuigiza, na pia mwaka 2004, alishindwa kwenye mashindano ya American Idol….kama utakumbuka Fantasia Barrino alishinda mwaka ule. Jaji Simon Cowell, alimwambia kuwa hata fika mbali na uimbaji. Kwa kweli nilisikitika sana siku hiyo alivyotolewa kwena AI, maana nilijua Jennifer ana kipaji.

Mungu ni mwema. Akifunga dirisha anafungua mlango. Jennifer kapata nafasi ya kuwa kwenye sinema ya Dreamgirls. Jennifer alichaguliwa kutoka kwenye waigizaji 781 waliofanya audition. Kama hujaiona Dreamgirls nakushauri ukaione. Nilienda kuiona juzi na kwa kweli ni sinema nzuri mno, yaani mno. Sijawahi kuona sinema nzuri kiasi hicho miaka mingi, tena waigizaji wakuu ni weusi. Na waMarekani wametokea kuipenda hiyo sinema. Soundtrack ya sinema ni namba one sasa hivi! Na kila mtu anamsifia Jennifer Hudson na kuigiza na kuimba kwake.

Kwa ufupi, Jennifer anaigiza kama Effie White, ambaye ni mwimbaji mkuu wa Kikundi cha The Dreams. Meneja wa Kikundi (Jamie Foxx) anamshusha na kumweka, Deena Jones, (Beyonce) kuwa mwimbaji mkuu kwa vile ni mzuri wa sura kuliko Effie. Effie anatupwa na kikundi cha chake na anasota na maisha. Sitaki kuwaeleza mengi lakini kuna mapenzi mle. Beyonce naye aliteuliwa kwa ajili ya tuzo ya Best Actress, lakini hakupata.

Eddie Murphy anaigiza kama James ‘Thunder’ Early, ambaye ni mwimbaji mwenye staili ya pekee ya kuimba. Anatokea kupendana na moja wa hao Dreams. Naye alituzwa Golden Globe kama Best Supporting actor. Kama hamkuona show, walivyomtangaza mshindi, alionekana kuwa na mshangao. Sishangai maana alishateuliwa mara kadhaa kwa ajili ya sinema kana The Nutty Professor, na hajashinda hata siku moja. Na huko kwenye Oscars ndo hawajamjua kabisa.

Kwa hiyo ndoto huwa zinatokea kweli. Jennifer Hudson, ametuonyesha kuwa inawezakana.

Tuesday, January 09, 2007

Oprah ajenga shule ya kifahari ya Wasichana Afrika Kusini

Bila shaka mmesikia habari ya Oprah Winfrey kufungua shule ya wasichana huko Afrika Kusini. Shule enyewe inaitwa ‘The Oprah Winfrey Leadership Academy’. Kwa kweli nampongeza kwa kitendo chake cha kukumbuka Afrika na kusaidia wasichana huko. Wanafunzi waliochaguliwa wanatoka kwenye familia zenye kipato cha chini. Na walichaguliwa kutoka kwa maelfu ya wasichana walioomba nafasi ya kuingia huko.

Oprah alijenga shule hiyo kwa gharama ya dola za kimarekani $40 milioni. Kwa sasa ina wanafunzi 145. Bila shaka tutasikia waliosoma hapo watapata mafanikio mazuri kimasomo na kwenda kusoma vyuo vikuu maarufu duniani kama Harvard, Stanford, Cambridge, Oxford etc.

Shule enyewe ni ya kifahari hasa. Hata wanaosoma shule za Ivy League na ma Prep school duniani wanaweza kuwaonea wivu has wasichana. Nikisema ni ya kifahari, nina maana ni ya kifahari hasa. Oprah mwenyewe ni bilionea na kazoea maisha ya kifahari na alitaka hao wasichana wajue ufahari manake nini. Mfano, shule ina saloni kwa ajili ya kutengeneza wasichana nywele, wanalalia mashuka enye nyuzi 200 count (Duh…kama wanalala hoteli ya Waldorf Astoria) sahani zilichaguliwa na Oprah na si ajabu sahani moja ina gharama ya dola mia, ina theatre za ndani na nje, ina ma fireplace tele (Afrika unahitaji fireplace ya nini?) na mengine mengi. Walimu wameletwa kutoka nchi za nje.

Je, wakirudi majumbani mwao kwa ajili ya likizo wataishi namna gani? Si wamezoea ufahari. Si uwongo kuna watu ambao baada ya kukosa maisha ya kifahari waliozoea, walirukwa na akili na wengine kujiua. Natumaini Oprah ana mpango wa kuhakikiisha hao wasichana wanaendelea kuishi maisha ya kifahari wakimaliza masomo yao.

Lakini najiuliza kama hizo pesa katumia vizuri kweli? Nakubali kuwa ni hela yake na anaweza kufanya anachoaka nazo. Lakini jamani hiyo hela ingeweza kusomesha maelfu ya wasichana huko Afrika Kusini na Afrika kwa ujumla. Kuna faida gani ya mtu kula chakula kwenye sahani enye thamani ya dola mia, wakati huko nyumbani kwake huenda hakuna chakula. Pia watoto wengi Afrika wanashindwa kusoma vizuri shauri ya kukosa mlo wa kutosha. Na kisa cha kulalia shuka enye 200 thread count wakati huko majumbani mwao wanashukuru kuwa na sehemu safi ya kulala. Au wanalala wane kwenye Kitanda kimoja. Kuhusu hiyo saloni si bora wangekuwa wanasukana wenyewe kwa wenyewe, ili wajue sanaa ya kutengeneza nywele.

Samahani lakini navyoona kuna watoto Afrika ambao wangeshukuru kuwa na unifomu na viatu vya kuvaa kwenda shule. Wangeshukuru kuwa na vitabu, na madaftari. Wangeshukuru kama wanakuwa na uhakika wakulipwa ada ya shule, na kuwa na njia ya kufika shule bila bugudha, kama vile school buses. Yaani hiyo dola milioni $40 zingeweza kutumiwa kujenga hata shule kumi bora Afrika na kusaidia wengi zaidi.Hayo ni maoni yangu tu. Wapendwa wasomaji, mnaonaje?

Saturday, January 06, 2007

Hongera Dada Asha Rose Mtengeti-Migiro



Nachukua nafasi hii kumpongeza Dada Asha Rose Mtengeti-Migiro, kwa kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (United Nations). Kwa kweli ni jambo sisi WaTanzania lazima tujivunie.

Namfahamu Dada Asha Rose, tangu alivyokuwa anasoma UDSM. Mimi wakati huo bado nilikuwa nasoma Secondary School. Kwa kweli huwezi kujua Mungu amempangia mtu nini. Nikikumbuka enzi zile, yaani tusingeweza kutegemea kuwa atakuwa kiongozi anayeheshimika dunia nzima. Alikuwa hana makuu. Lakini miaka ilivyoenda tuliona alivyoonyesha meno kuwa anaweza kuongoza na kuongoza vizuri.

Pia kuteuliwa kwake unaonyesha jinsi Tanzania inavyoheshimika duniani. Hatujawa na migogoro mingi ya kisiasa kama nchi zingine barani Afrika. Na nasikia ilikuwa kila mkutano wa kimataifa akienda anapata washabiki kwa uongozi wake mzuri. Watu wengine wamekuwa wakishangaa alipataje kuteuliwa katika nafasi nzito hivyo. Nawambia ameteuliwa kwa sababu ameonyesha watu wengi Tanzania na nje ya Tanzania kuwa ni mtu mzuri mwenye moyo na kipaji cha uongozi.

Jambo lingine ni kuwa mwanamke kutoka Third World amekababidhiwa uongozi mzito. Lazima Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bwana Ban Ki-Moon, kamwona Dada Asha Rose ni mwanamke jasiri atakayeweza hiyo kazi.

Dada Asha Rose amekuwa ni mfano mzuri kwa wasichana wote wa Tanzania na Afrika kwa ujumla!

Akina Mama Oyee!

Wednesday, January 03, 2007

Poleni Wafiwa


Kwanza naomba mnisamehe kwa kuongea kuhusu kifo. Najua si jambo la kufurahisha.

Leo nimekwenda kwenda 'Wake' (kilio) ya Mama Anastazia Rupia. Alifariki hapa Boston siku chache kabla ya Krismasi. Alikuwa amekuja kwenye mahafali ya mwanae, Septemba na kwa bahati mbaya alianza kuumwa muda mfupi baada ya hapo.

Kwa kweli waBongo walitokea wengi kuwafariji wenzao waliofiwa na mama yao. Mchungaji mzungu alisoma misa mzuri sana. Watu walikuwa na majonzi hasa mtoto wa marehemu John Rupia, alivyosimulia habari ya maisha ya mama yake na alivyougua. Alivyomaliza naye, John alianza kulia ndo hapo chumba chote tuliishia kulia.

Maiti anawasili Dar Jumamosi na ndege ya SwissAir, naomba muwepokea vyema huko. Poleni.

Lakini jamani ukweli uchungu wa kufiwa unaujua wewe uliyofiwa. Hata tukikupa pole ngapi, marehemu ni marehemu, hatarudi. Watu wataenda zao kwenye shughuli zao na wewe mfiwa utabakia na majonzi yako.

Watu wengi wanajua uchungu wa kufiwa na mtu wa karibu. Nilivyofiwa na mume wangu wa kwanza, mwaka 1995 hata sikumbuki nilifikaje Tanzania. Nilikuwa nasoma hapa Boston, nikapata taarifa, nikakatiwa tiketi na nikashutukiwa niko Dar uwanja wa ndege na wafanyakazi pale walinipa pole na kuniuliza kama nina mtu wa kunipokea. Ile safari yaani ilikuwa kama vile ndoto mbaya na niseme miezi kadhaa baada ya kufiwa si kuwa mzima maana nilijisikia kama sijui niko wapi. Wakati mwingine nilikuwa najiona kama niko kwenye wingu, mara naona mwili mzito kutembea shida. Mungu alinisaidia kipindi kile. Amini usiamini, miaka zaidi ya kumi imepita na bado nina omboleza ila siku hadi siku uchungu unapungua. Unapungua lakini haushi kabisa.

Lakini sisi tuliyobaki inabidi tuendelee kuishi na kujenga maisha yetu na kusimulia kwa wanaetu kuhusu ndugu zao waliowatangulia hapa dunia.

Kwa kila mtu aliyefiwa na ndugu au rafiki yake nasema, pole. Poleni wafiwa wote popote mlipo, na Mungu awape nguvu katika kipindi hiki kigumu. AMEN.

Saturday, December 30, 2006

Heri ya Mwaka Mpya!


Ninawatakia heri ya mwaka mpya! Mbarikiwe wote katika mwaka mpya 2007! Nashukuru Mungu kuwa wote tumefika na nawaombea wote uzima na mafanikio mema katika huu mwaka mpya. Naomba pia tuwe pamoja mingi mingi zijazo, Inshallah!

Pia nawaoba msherekee mwaka mpya kwa amani na usalama kwani kipindi hiki kuna kuwa na ajali nyingi shauri ya ulevi.

HAPPY NEW YEAR!

Tuesday, December 26, 2006

Marehemu James Brown







REST IN PEACE JAMES BROWN

1933 - 2006

Jamani nilisikitika kusikia habari ya kifo cha Godfather of Soul, James Brown! Alifariki jana asubuhi, Krismasi, akiwa anaumwa Pneumonia. Lakini jamani Ijumaa mbona alionekana mzima, ana-sign autographs na kutoa zawadi za Krismasi kwa watoto!

Ukweli, mimi ni mmoja wa washabiki wake wakuu. Yaani kila nikisimikia animba 'funk' lazima niinuke na kucheza! Nyimbo zake, 'Say it Loud, I'm Black and Proud!', 'Hot Pants, 'Sex Machine', Get Up, na zingine nyingi haziwezi kusahaulika. Sasa kwa vile ni marehemu bei ya CD's zake zitaongezeka bei.

Nisiseme habari ya jinsi nilivyokuwa nashangalia akicheza na kutia madoido ya 'splits'! Nina mpaka mDoli wa James Brown, una bonyeza mahala na anaanza kucheza na kuimba ule waimbo wake wa 'I Feel Good!' (Najisikia vizuri). Tangu mdogo yaani miaka minne hivi nakumbuka kucheza na kupiga kelele kila nikisikia anaimba, eti najaribu kumwiga!

Mungu amlaze mahali pema mbinguni. Amen.


Saturday, December 23, 2006

Nawatakia Krimasi Njema!


Wapendwa Wasomaji, ninachukua nafasi hii kuwatakia wote Krismasi Njema! Japo ni sikukuu ya kusherekea kwa kupeana zawadi, kula mlo mzuri na wa fahari, kukutana na familia na marafiki, kunywa pombe etc., tusisahau kuwa ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Napenda sana kipindi hiki Marekani, maana watu wanakuwa na roho nzuri na kusalimiana na watu ambao kawaida wasingewasalimia. Pia watu wanatoa misaada mingi kwa wasiojiweza na maskini kwa vile wameingiliwa na 'Christmas Spirit'. Hata bosi mwenye roho mbaya anaweza kuwa na roho nzuri japo kwa siku moja!

Wengine wataenda kwenye mikesha kanisani, wengine wataenda kwenye party, wengine watalala na kupumzika, wengine hawatasherekea kabisa hasa wasio waKristo.

Bila kujali dini, ninawatakia wote Krismasi Njema, na mapumziko mema.

Mungu Awabariki Wote!

Friday, December 15, 2006

Niliuliwa na Mzungu mwenye Hasira (Aftershock:Beyond the Civil War)




Jamani msishangae sana. Huu ni mguu wangu! Na bado niko hai. Nilikuwa naigiza katika sinema ya 'Aftershock:Beyond the Civil War' kama Field Hand. Hao field Hands walikuwa ni watumwa walioachiwa huru lakini bado walikuwa wanaishi katika hali ya kitumwa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe (Civil War) 1865. Wakati wa filiming tulikuwa peku kwenye matope! Sinema ilipigwa mwezi wa sita na wa saba hapa Massachusetts.

Hiyo make-up ya damu feki ilipakwa kwenye mguu baada ya kulala chini! Nakumbuka Director David Padrusch anamwambia make-up lady, ongeza, ongeza damu haitoshi! Ai! Walinipaka mwili mzima. Niliona kinyaa maana hiyo damu feki inaonekana kama damu kweli. Na usoni pia nilipakwa madamu na majeraha, ilikuwa tuonekana kama tumepigwa risasi nyingi. Ni kwamba weusi wengi waliuliwa na wazungu wenye hasira baada ya hiyo vita.

Sinema ya Aftershock itaonyeshwa History Channel, Saturday December 30, 3:00PM (Eastern).

Cheki website yao kwa maelezo zaidi.

http://www.history.com/shows.do?episodeId=203497&action=detail

Pia unaweza kusoma habari zaidi ya experience yangu kwenye seti ya Aftershock hapa:

http://chemiche.blogspot.com/2006_06_01_chemiche_archive.html

Unaweza kuona Trailer kwenye You Tube.

Thursday, December 14, 2006

Kariakoo = Carrier Corps





Hapo zamani za kale kabla ya magari, lori, petroli, basikeli, wazungu walitegemea binadamu na wanyama kubeba mizigo yao. Hao waafrika walioajiriwa waliona sifa kubwa kufanya kazi na mzungu na kulipwa.

Hao wabebaji wlaikuwa wanaitwa Carrier Corps, na baada ya 'kuswahililize' ndo ikawa jina la Kariakoo tunaoijua leo.

Kabla ya hao wa kulipwa waafrika walilazimshwa kubeba hiyo mizigo wakiwa kama watumwa. Historia ya mwafrika jamani.

Jamani cheki hiyo mizigo ilivyo mizito halafu fikiria unabeba kuanzia Dar hadi Mwanza, na wakati huo hakuna barabara. Lazima mizigo ilipotea, hasa kama mtu anaanguka nayo kutoka mlimani. Mtu unatembea nayo unatazama mbele huko nyoka anakuuma! Na, kama wabebabaji walikufa njiani nani alibeba mzigo wake?

Kama mmewahi kuona sinema za Tarzan na zingine zilizohusu Afrika, utaona mzungu alivyobebwa kwenye kiti na waafrika huko ana wabebabaji mizigo yake. Tena waafrika wakionekana wavivu wanachapwa kama punda! Ama kweli tumetoka mbali.

Wednesday, December 13, 2006

Nilitolewa Ushamba Dar - Text Messaging


Haya nimezungumza habari ya watu wengi kuwa na cell phone Dar. Sasa kuna hiyo kitu 'text messaging'. Naona ndo mawasiliano ya bei rahisi kuliko voice call. Kila mtu anajua kutuma text message, isipokuwa mimi!

Niliazima simu ya mama yangu. Watu walikuwa wananitumia text message. Doh, niliweza kuzisoma, lakini nilishindwa kutuma jibu! Niliona aibu kweli. Dada moja kanipigia na kusema, 'Nilivyona hujajibu niijua hujui kutumia texting!"

Ni kweli nilikuwa najibu watu kwa kuwapigia simu na of course ni ghali. Japo nina cell phone miaka mingi na nimeona hiyo text feature, huwa nasoma message na kuinua phone na kupiga kama inabidi nijibu. Nimeona vijana na watoto wadogo wanajua kutumia lakini haikuniingia kuwa nami nitumie. Na mara nyingi kwenye TV utasikia, send a Text message to halafu wanakupa namba. Lakini hata siku moja sijajaribu! Jamani USHAMBA! Ni kama vile compyuta. Mtu unaona lakini unaogopa kutumia! Ukianza kutumia unasema, Kumbe ni rahisi hivyo!

Sasa nimerudi Boston, na natazama cell phone yangu. Na ndo nimekuwa na-explore jinsi ya kutumia hiyo text message. Nimeanza kupatia. Lakini naomba mnieleza jinsi ya kuweka space kati ya maneno! Kwa sasa naweka period kati ya maneno.

Kumbe ni simple na mawasiliano rahisi. Nimeanza kupenda text messaging. Ushamba wa text messaging umenitoka.

Thursday, December 07, 2006

Dar es Salaam kuna Joto!


Jamani Dar kuna joto! Loh! Unapigwa nayo ukishuka tu kwenye ndege. Siku mbili za mwanzo nilivyokuwa huko niliona joto kweli. Ni kweli kuwa Novemba/Desemba joto unazidi Dar, lakini kwa kweli nilikipata. Kwa siku nilikuwa na kunywa maji mengi kweli, na vinywaji vingine. Jamani nilitoka jasho zile siku za mwanzo.

Halafu mara nyingi umeme ulikatika kwa hiyo feni na Air Conditioning hazifanyi kazi, kwa hiyo unaendelea kuchemka. Unakwenda ofisini mwa mtu halafu unabakia kujipepea na gazeti shauri ya joto. Asubuhi, umeme ulikuwa unakatika saa 12 kamili. Basi unaamka kwa sababu feni chumbani unazimika na joto unaanza kuzidi. Hata hivyo siku zilivyopita nilianza kuzoea joto.

Haya nilivyondoka nilianza kusikia baridi kwenye ndege. Nilitamani ningebaki Bongo nifaidi joto. Na kufika Boston nilikaribishwa na snow (theluji)! Unatoka kwenye joto kuingia kwenye snow.

Basi nimerudi Boston na ka-tan. Nilikuwa navaa sleveless Dar, basi unaona kabisa mikono umekuwa Dark. Sehemu zilizokuwa zimefunikwa zilikuwa light. Wazungu kazini waliniuliza kama nimepata 'sunburn'. Nikawaambia hapana ni tan, na sisi weusi tunapata tan pia. Lakini wacha nifaidi hiyo Vitamin E ya jua, maana kipindi hiki cha winter jua unaliona tu. Mambo ya kukaa nje na mwili kuganda shauri ya baridi hatutaki.

Monday, December 04, 2006

Aftershock itaonyeshwa History Channel 12/19 and 12/20/06


Habari zenu wapendwa wasomaji. Ile sinema ya 'Aftershock: Beyond the Civil War' itaonyeshwa kwenye History Channel, siku ya jumanne 12/19/06 saa mbili usiku (8:00pm Eastern) na pia itaonyeshwa tena 12/20/06 saa sita usiku (12:00am Eastern midnight). Mimi naigiza humo kama mfanyakazi wa mzungu mbaguzi mno mwenye uchungu shauri ya Confederates kushindwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe Marekani miaka ya 1860's.

Kwa habari zaidi soma hapa:

http://www.history.com/schedule.do

Pia nimewahi kuandika kwa kirefu kuhusu hiyo sinema hapa:

http://swahilitime.blogspot.com/2006_06_01_swahilitime_archive.html

Thursday, November 30, 2006

Kila Mtu ana cell Phone Dar

Jamani, mawasiliano ya simu ni rahisi sana Dar. Cell phone nyingi, makampuni yanashindana kupata wateja, phone cards zinauzwa kila mahala, tena bei si mbaya hata shilingi 500/- unapata! Watu wengi wanazo! Mbona cell phone USA ni ghali sana, tena ukiweka kwenye credit kadi ndo unalaguliwa kabisa! USA wanaweza kujifunza kutoka Bongo!

Lakini jamani barabara mbovu sana Dar, tena sana! MAVUMBI!

Baadaye!

Sunday, November 26, 2006

Diary from Dar es Salaam

Haya, ni siku yangu ya tano Dar. Malalamiko yangu makuu ni:

Ukosefu wa umeme
Barabara mbovu
Maji shida
Mbu!

Nimetafunwa na mbu! Na nimetumia mosquito repellent. Labda wamekuwa sugu. Lakini wamekunywa damu ya Boston!

Niko Mbezi kwenye cafe iliyoko barabarani kabisa. Kwa kweli computer zao ni safi sana, kuliko cafe iliyoko karibu na nyumbani. Wale wana computer nzee na slow.

Vumbi na michanga!

Lakini jana nilikuwa kwenye sherehe ya arusi. Jamani kuna catering companies siku hizi! Juzi nilikuwa kwenye Graduation party, ilikuwa kama arusi Ama kweli Tanzania kumekuwa Party Culture!

Friday, November 24, 2006

Niko Bongo!

Habari zenu wasomaji wapendwa. Niko Bongo Dar es Salaam. Nimetua juzi, kwa kweli ni joto sana lakini naona naanza kuzoea. Nimefurahi kufika nyumbani baada ya muda mrefu. Leo nimeenda mjini na kwa bahati nimegongana na watu wengi tu ambao nilikuwa nawafahamu. Naweza kuwa natembea halafu nasikia 'Che-Mponda!' Na cheki ni mtu nilimfahamu toka zamani.

Sasa jamani ile jengo la Daily News la zamani wanaifanyia nini? Naona Maktaba wamekarabati kwa nje. Maji ya kunywa ya chupa na phone cards ziko kila mahala, mawasiliano ni rahisi. Lakini barabara nyingi mbovu, na traffic jams ni mbaya! Yaani kutoka mjini kwenda Mbezi Beach ni two hours!

Nimepapenda Slipway! Ice Cream yako safi na ile Mashua Bar pale Beachfront safi sana. Halafu kuna ATM's kila mahala siku izi hakuna kwenda benki kusimama kwenye foleni ndefu. Nimshangaa kuona kuna hata Casino pale karibu na Greek Cub ya zamani karibu na Red Cross. Bongo kumeendelea hata hii internet nayo tumia ni nzuri sana na up to date!

Jamani nisiendelee maana umeme shida!

Mengine baadaye!

Thursday, November 16, 2006

Huyu ni Emmitt Smith na patna wake, Cheryl Burke wlioshinda mashindano ya 'Dancing with the Stars' jana. Alishinda baada ya watazamaji wengi kumpigia kura kama vile American Idol. Kila wiki wachezaji walipunguzwa mpaka kupata wachezaji bora.

Emmitt ni mcheza football na pia bonge la baba, lakini alishangaza watazamaji kwa 'moves' zake ambazo usingeweza kutegemea mtu na mwili kama wake kufanya.

Wacha wazungu wanune lakini weusi wamejaliwa na 'rhythm'! Kucheza iko katika damu yetu!

Navyosikia wanaume wengi sasa wanachukua Dance Lessons! Haya sasa Dancing ni' in' kwa wanaume!

Monday, November 13, 2006

Massachusetts yapata Gavana mweusi! (Ni wa pili katika Historia ya Marekani)



Wiki iliyopita siku ya tarehe saba Novemba, 2006, ilitokea jambo la kihistoria hapa Massachusetts, Marekani. Ni Gavana mweusi wa pili tu katika historia ya Marekani. (Wa kwanza alikuwa Douglas Wilder wa Virginia mwaka 1990). Wingi wa wapiga kura walimchagua mtu mweusi kuwa Gavana! Na walimpigia kura kwa wingi mpaka mpinzani wake ilibidi akubali kuwa kashindwa vibaya mno!
Aliyechaguliwa kuwa Gavana mpya wa Massachusetts ni, Deval Patrick ambaye yuko kwenye chama cha Democrats. Bwana Patrick alizaliwa na kukulia ghetto ya Chicago. Bahati nzuri alikuwa na kipaji kimasomo na alifanikiwa kusoma Milton Academy kwa scholarship na Harvard University. Kwa habari zake zaidi unaweza kusoma hapa.

Mpinzani wake alikuwa bibi mmoja wa kizungu, Kerry Healey. Huyo mama ni tajiri na alikuwa Naibu Gavana wa Bwana Mitt Romney ambaye ni Gavana wa sasa na hashindi hapa Massachusetts. Si uwongo kuwa mwaka 2002, Romney alidanganya watu wa Massachusetts na kusema kuwa hawanii uraisi, kumbe kama Republicans wenzake ni mwongo mkubwa. Anagombea urais mwaka 2008! Na alimchagua Healey asiyekuwa na sifa za siasa zaidi ya kuwa tajiri kuwa Lieutenant wake.

Wakati wa kampeni ya Healey hivi majuzi, Romney alimtupa pia na wala hakumsaidia. Lakini niachane na mambo ya Romney maana nitasema mengi juu yake akigombea uraisi. Na si mazuri.

Healey aliishia kuchukiwa vibaya na watu. Hata Republicans wenzake walimgeuka na kumtupa. Huyo mama alikuwa na kampeni chafu na ya kibaguzi. Tangazo lake la mwisho kwenye TV ilikuwa na mzungu dume aki-jog kwenye eneo la wazungu huko tukimsikia mawazo yake. Yaani alisema mabaya mpaka tulisema alichoacha kusema ni kuwa hataki kuongozwa na Gavana mweusi.

Na pia alikuwa na tangazo la mbakaji mweusi ambaye Deval alimsaidia akiwa akifanya kazi ya mwendesha mashitaka. Heh! Jamaa si alikuwa anafanya yake. Na Healey alidiriki kutuma watu nyumbani kwa Patrick na Naibu wake Tim Murray kufanya maandamano wakiwa wamevaa nguo za wafungwa. Bahati yake mbaya mtoto wa Tim Murray mwenye miaka 12 alikuwa nyumbani peke yake akijiandaa kwenda shule. Waliishia kumtisha mtoto! Watu walimgeuka, na wakasema huyo mama hafai kabisa. Kaishia kuonekana kama mtu mwenye roho mbaya ajabu. Pia sikumwona akifanya kampeni kwenye maeneo ya weusi au waspanish. Walimwonyesha kwenye TV akiwa kwenye barbecue eti kwenye nyumba za wananchi wa kawaida. Doh, mbona nyumba zenyewe zilikuwa za wazungu tena nyumba za fahari.

Patrick wakati huo alikataa kabisa kufanya kampeni chafu dhidi ya mwenzake na alishinda. Tena kwa kura nyingi mpaka Democrats nchi nzima wanamtazama kwa mshangao na wanataka kujifunza kutoka kwake.

Januari, ndo Gavana Patrick ataanza kazi yake rasmi na naamini kuwa atakuwa Gavana mzuri maana ukiwa mweusi ni lazima ufanye kazi mara nne ya mzungu kusudi uonekane kama unafanya kazi.

Mengine, Democrats watawala sasa, walifanikiwa kunyakua Congress na Senate! Raisi Bush alie tu! Udikteta wake umekwisha! Watu wameamka sasa. Na wanasema kuwa Bush alikuwa Mnyonge kweli kweli siku ya uchaguzi baada ya kuona Republicans wanaangushwa vibaya! Watu wanasema Republicans waliangushwa katika ‘Tsunami’ ya kura! Na kweli ilikuwa tsunami na watu walimpiga kura kwa wingi mpaka sehemu nyingi walishiwa kura.

Ama kweli Demokrasia inafanya kazi Marekani.

Saturday, November 11, 2006

Anaomba Urafiki wa Kalamu

Huyu kijana (kulia) ni Corey Brown. Ana miaka 27. Ni mtoto wa rafiki yangu Queenae Mulvihill aliyeko Los Angeles. Kama mnakumbuka, Queenae ni mtunzi wa ile sinema Maangamizi. Kwenye hii picha Corey yuko na binamu yake.

Timu ya Maangamizi walivyokuwa Bagamoyo mwaka 1994, walikuwa na Corey. Alikuwa teenager wakati huu. Huenda kuna wanaomkumbuka.

Kwa sasa, Corey amefungwa gerezani huko California, na anatarajia kutoka baada ya miezi kumi na mbili. Kosa lake ni kughushi cheki ya dola mia ($100). Ameniandikia kuniomba kama naweza kumsaidia kutafuta marafiki wa kalamu. Anapenda sana Afrika na Ulaya.

Kama unataka kumwandikia au kumtumia post card kumsalimia anwani yake ni:

Mr. Corey Brown
coc#T-73384
Dorm 5 - Bunk 8
1150 East Ash Street
Shafter, California 93263

Asanteni

Monday, October 30, 2006

Wacheza sinema wanatafutwa kwa ajili ya Bongoland 2!

Kwa walio na ndoto ya kuigiza katika sinema, hii ni nafasi yako. Samahani lakini sitatafsiri posti na ni kimombo.

Ni hivi Josiah Kibira aliyetengeneza sinema za Bongoland na Tusamehe yuko mbioni kutengeneza sinema nyingine. Sinema hiyo ni Bongoland 2, na itapigwa Tanzania mwakani.

Casting Call ni hii hapa chini
:


SWAHILI SPEAKING ACTOR WANTED

By, Josiah Kibira

Kibira Films International is currently looking actors for its upcoming project to be filmed next year in Tanzania - July 1st - July 31, 2007 This new movie is a sequel to the movie Bongoland which was produced in 2003 by Kibira Films. Bongoland was/is a drama about different challenges that immigrants face once they arrive in the foreign land. It dealt with issues of immigration papers, employment, school and relationships. The main characters asked - "would you rather be a well fed slave or a hungry freeman"? He asked this while contemplating whether to keep chasing the ever elusive American dream or go back to his native land.

The sequel is a continuation of that drama following the main character Juma to see if his dreams for a better life were fulfilled after he decided to go back to his native Bongoland. The working title for the movie is "Bongoland II - There Is No Place Like Home."

Here are the qualifications for the post:

[1.] Be a male actor. [2.] Fluent Swahili speaker.[ 3.] Some film or stage acting - not necessary but would be helpful. [4.] Have seen the movie "Bongoland" [5.] Currently living in the United States [6.] Have legal status to travel in and out of USA. [ 7.] Willing to work on a deferred payment contract. [8.] Ability to get along with people.

Additional Perks for the role:

[1.] Free round trip ticket to Tanzania. [2.] All accommodations provided while in Dar. [3.] Daily stipend while on the set. [4.] Possibility of earning a role in Kibira Films future projects. [5.] Exposure to Film festivals in USA, Europe and Africa. [6.] Screen testing in Minneapolis, MN if selected or being considered. [7.] Possible career move.

For consideration:

[1.] Send a headshot. [2.] Your resume OR. [3.] An essay of why you think you should be considered for the role. [4.] Any tapes, DVD, vocals showing your acting abilities - In actual production i.e. play, movie (if you have it)

[5.] Send to: Kibira Films International 2860 Zanzibar Lane North Plymouth, MN 55447

[6.] Email - info@kibirafilms.com Thanks and Good Luck.

More information about Kibira Films - www.kibirafilms.com

Phone #: Office: (612)-291-2719; Mobile: (763)-229-2495

Saturday, October 28, 2006

Washindi wa 2006 ni Cardinals!


Ukikaa Marekani lazima utasikia habari ya mchezo BASEBALL! Zamani sikuwa na habari na huo mchezo na wala sikuujali lakini siku hizi mimi nimekuwa mshabaki! Kila mji Marekani una timu yake. Miji mikuu ina timu kubwa na wachezaji wanalipwa donge nono. Naona kama watu wana mapenzi na Baseball zaidi ya watu wanavyokuwa na mapenzi ya mpira wa miguu Tanzania.

Jana jioni timu kutoka St. Louis, Missouri iitwayo, Cardinals, walishinda timu kutoka Detroit, Michigan iitwayo, Tigers. Cardinals ni aina ya ndege na Tiger ni aina ya paka kubwa, sasa ungetemea Tigers washinde. Lakini Cardinals walinyakuwa ushindi wa World Series, yaani kuwa timu bora ya baseball ya mwaka 2006. Hongera kwao.

Ukweli nilikuwa nashabikia Tigers. Sijui kwa nini, lakini napenda sana wakicheza kwenye uwanja wao Detroit. Kila wakipata bao (score), na kukanyaga Homeplate basi unasikia mlio wa Tiger halafu macho ya sanamu ya Tiger wao yana waka na kucheza cheza! Kama wangefanikiwa kushinda World series sijui huyo Tiger wao angefanyeje.

Safari ya wacheza baseball ni ndefu kila mwaka. Wanaanza msimu wao April na kucheza na timu mbalimbali na kupunguzwa mpaka wanapata timu bora kwenye mchezo wa World Series. Tofauti na michezo mingine kama Football, wachezaji wa baseball wanacheza karibu kila siku na siku zingine hata game mbili kwa siku! Na kuna washabiki ambao hawakosi hata game moja ya timu wao.

Baseball ni mchezo uliyoanza marekani. Zamani weusi walibaguliwa na hawakurusiwa kucheza japo kwenye timu za weusi tupu. Miaka ya 1950's walianza kuruhusu weusi kucheza. Siku hizi kuna wachezaji wengi kutoka nchi za Amerika ya Kusini kama Dominican Republic, Cuba na Colombia. Na pia waJapani na waChina wapo. Wacehzaji wa kizungu katika Major Leagues wamekuwa wachache lakini bado watu wanashabikia.

Watoto wadogo wanacheza kwenye timu za Little League. Uwongo mbaya game zingine ni kama vile game za wakubwa Major Leagues. Watoto na wazazi wa wachezaji wanakuwa tayari kushikana masharti. Mwaka huu kocha wa timu fulani ya Little League alifungwa jela baada ya kumlipa mtoto wa miaka minane kumpiga na kumjeruhi mtoto mwingine kwenye timu yake na mpira kwa vile aliona kama yule mtoto atafanya washindwe.

Navyoona mchezo ni mgumu na lazima uwe na roho kuucheza maana ukipigwa na kale kampira (baseball) utaumia! Mchezaji anajitahidi kuupiga mpira unaoenda spidi kali mno na kamti (bat). Kusudi watu wasivunje mikono wakiudaka wanavaa gloves maalum. Batter ambaye ni zamu yake kujaribu kuupiga anavaa kofia kubwa na ngumu kichwani maana ukipgwa nayo unaweza kufa. Hapa Boston kwenye timu yetu, Red Sox, kuna jamaa, Matt Clement ambaye ni fundi wa kutupa mpira (pitcher) kapigwa kichwani na mpira mwaka jana na hajawa mzima tokea hapo!

Hapa Boston, timu yetu ni Red Sox na walishinda World Series, mwaka 2004. Japo ni timu ya mji wetu mimi siwapendi sana. Ni ghali mno kwenda kwenye game zao halafu tiketi zinauzwa magendo mpaka dola $3,000! Kukaa bleacher ni dola $70 na huoni kitu bila kuwa na binoculaurs!Waachie wenyewe tutazama kwenye TV! Au nitaenda Baltimore na New York kuangalia game huko maana tiketi ni dola $40 tu.

Haya nawaachia nafasi mtoe stori zenu za baseball.