Monday, September 22, 2008
Skandali nyingine Bank of Tanzania (BoT)
Kutoka kwa Mzee wa Sumo (Mpoki Bukuku) Blog:
" Hii ni kutoana nishaji jamani na ukiukwaji haki za wanawake yaani wengine wameamua kutoa wigi la urembo kujikinga na fedheha! Sijui wengine walikuwa na swaum? " - Mpoki Bukuku akizungumzia picha alizopiga.
TUHUMA za kuwepo kwa upendeleo wa watoto wa vigogo kwenye ajira za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zimesimamisha kizimbani wafanyakazi wanane ambao wameshtakiwa kwa kosa la kughushi vyeti.
Tuhuma dhidi ya watoto 16 wa vigogo ziliibuka wakati kashfa ya wizi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), ikiwa imeshamiri kiasi cha kusababisha aliyekuwa gavana, Daud Ballali kusitishwa mkataba wake na kufanyika kwa mabadiliko kadhaa kwenye uongozi wa chombo hicho nyeti cha fedha.
Na Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, aliahidi kuzishughulikia tuhuma hizo wakati huo baada ya tuhuma hizo kushikiwa bango.
Jana, wafanyakazi wanane wa BoT, baadhi yao wakiwa wamejifunika nyuso kwa nguo na nywele za bandia, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakishtakiwa kwa tuhuma za kughushi vyeti na kutoa hati za uongo.
Wafanyakazi hao, wengi wao wakiwa wanawake, ni Justina J Mungai, ambaye imeelezwa kuwa ni mtoto wa Joseph Mungai, ambaye amewahi kushika wizara tofauti ikiwemo ya elimu, Christina G Ntemi, Siamini Eddie Kombakono, Janeth John Mahenge, Beatha Constantine Massawe, Jacquiline David Juma, Philimina Philibert Mutagurwa na Amina Mohamed Mwinchumu.
Wafanyakazi hao walifikishwa katika mahakama hiyo saa 4.00 asubuhi na kusomewa shtaka mbele ya Hakimu Neema Chusi. Wakili wa serikali, Edgar Luoga, akisaidiana na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Abubakar Msangi, ndio walioongoza mashtaka hayo.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri wao, ambaye ni BoT.
Washtakiwa Mungai, Massawe na Mwinchumu, wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2001, wakati Ntemi, Kombakono, Mahenge na Mutagurwa wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2002. Wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa BoT hati za uongo, wakionyesha kuwa vimetolewa na Baraza la Mitihani la Taifa, wakati si kweli.
Ilidaiwa kuwa, Mutagurwa alighushi cheti hicho mwaka 2000.
Labels:
Bank of Tanzania,
Daudi Balali,
EPA,
Kisutu Court,
Mpoki Bukuku
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
4 comments:
Wanaona haya! Waficha nyuso zao mbaya na roho zao za kutu!
Huyo ambaye hajaficha uso hana hatia! SHE IS NOT GUILTY!
Ni kweli. Kwa nini hao wameficha uso. Pia huyo ana maana gani kuvua wigi anadhani watu hawatamtambua na nywele za kusuka?
Wanawaonea tu ao akina dada, kosa lao kubwa ni kutafuta chakula cha watoto wao au vijisenti vya kujikimu. mbona wanaofoji vyeti vya Phd tunawajua wangine ni wabunge na hatujaskia wamechukuliwa hatua za kisheria?
Kuna maprofesa wangapi wameshalalmikiwa chuo kikuu cha Mzumbe? Je Dr Kamala na Dr Chimba walipatia wapi udakatari wao? mbona hatujaskia Ma dr hao na wa aina hiyo wamechukuliwa hatua? achilia mbali kupelekwa mahakamani?
Wezi wa EPA na mafisadi wa richimondi mbona wao hatua waliochukuliwa ni kuundiwa tume tu hakuna zaidi ya hapo???
Post a Comment