Kutoka gazeti la MWANANCHI:
Hayo ni makubwa! Nani anaumia hapa? Bongo wanavyodharua walimu ni aibu! Ndo maana watu hawataki kuwa walimu.
***************************************************************************
Mkurugenzi awakana walimu 200 Dar, Afisa Elimu mkoa ashangaa
Baadhi ya walimu kati ya 200 ambao mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es salaam amedai kuwa hawatambui hivyo wakatafute nafasi mahali pengine.
Gedius Rwiza na Aika Mushi
MKURUGENZI wa Manispaa ya Kinondoni amewakana zaidi ya walimu 200 waliondamana hadi ofisini kwake kudai fedha za kujikimu ambazo hawajapewa tangu waripoti katika vituo vyao vya kazi mwezi Mei mwaka huu.
Akizungumza baada ya kupokea maandamano hayo, mkurugenzi wa manispaa hiyo, Noel Mahyenga alisema, hahusiki na walimu hao na wala hawatambui kama waajiriwa wa manispaa yake.
"Wanatakiwa kurudi ngazi ya mkoa ili kuangalia sehemu watakapowaweka kwa kuwa manispaa yangu haina upungufu wa walimu, ingawa tatizo hili nalifahamu," alisema mkurugenzi huyo.
Alipotakiwa kutoa maelezo kuhusu mshahara waliolipwa mwezi walioanza kufanya kazi, mkurugenzi huyo alidai kuwa, walilipwa kimakosa na kwamba kama watabahatika kupata sehemu za kwenda, ataongea na wizara ili wakatwe mshahara huo.
"Kulipwa mshahara, barua na mkataba wa kazi si hoja. Katika bajeti yangu sina pesa ya kuwalipa walimu hawa. Warudi mkoani. Kama walipangiwa Kinondoni ni makosa yalifanyika bila kujua. Nina walimu wa kutosha," alisema Mahyenga.
Majibu hayo yaliwasikitisha walimu hao.
"Nashindwa kuelewa tunapoambiwa kwamba sisi siyo waajiriwa wa Manispaa wakati tuna barua za kuripoti kazini na mikataba tunayo, na kama walijua sisi siyo waajiriwa kwa nini tumelipwa mshahara wa mwezi Julai?" alihoji Mwalimu Rehema Macha.
Akizungumzia suala hilo, Afisaelimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makali Bernard alikiri kutokea tatizo hilo na kuongeza kuwa hahusiki.
"Nilishamaliza kazi ya kuwapangia vituo vya kufanyia kazi. Nashangaa kusikia kwamba Manispaa haiwatambui kama watumishi wao," alisema. "Kazi yangu ni kugawa vituo kama ninavyoagizwa na wizara. Hilo ni suala la mkurugenzi wa manispaa ambaye ndiye mwajiri wao."
Walimu hao walisema hali yao kifedha ni mbaya na kwamba fedha walizokuwa nazo zilishaisha siku nyingi, lakini bado wanaendelea kufundisha. Walidai kuwa baadhi yao walikuwa wamepanga vyumba, lakini wamefikia hatua wanaona watashindwa kulipia kodi ya pango, huku baadhi wakiwa wameanza kufukuzwa.
Mwanasheria wa Chama cha Walimu (CWT), Leonard Haule, aliwashauri walimu hao kurudi nyumbani na kwamba ataenda nao kwenye ofisi za manispaa hiyo kujua mustakabali wao.
Rais wa chama hicho, Gratian Mukoba alisema kuwa, hali hii inaonyesha kuwa mgomo wao waliopanga ufanyike Oktoba 15 utakuwa na nguvu.
"Kama wanaona walimu ni lazima waandamane ili wapate haki zao, tutawaonyesha tulivyochoka na usumbufu huo," alisema. "Kama wamefikia kuwakana wafanyakazi wao, hali inasikitisha."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
That is Our Tanzania for You! halafu bado tunashangaa kwamba Elimu yetu iko down na out kabisa!
Post a Comment