Saturday, November 22, 2008

Tarzan wa Bongo


Mnakumbuka ile hadithi ya Tarzan ya kijana wa kizungu aliyelelewa na wanyama kwenye pori Afrika? Naona huyo kijana Baraka ni Tarzan wa kweli. Vyombo vya habari vya nje vikipata hii habari mtasikia hata Hollywood wanatengeneza sinema juu yake.

*********************************************************************




Mtoto amlilia nyani aliyemlea

2008-11-22
Na Godfrey Monyo


Kijana Baraka Bahati Rose (11) aliyelelewa na nyani porini kwa miaka zaidi ya mitano anamlilia `mama yake` huyo mlezi na akasema kuwa heri asingeuawa.

Alisema nyani huyo aliyemlea ndiye anayempenda zaidi na hakukuwa na haja ya kuuawa.

Bahati alikuwa akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam ilipomtembea kwa lengo la kujua namna anavyoishi.

Alisema hakumbuki wala hajui alifikaje huko msituni ila anajua kuwa kulikuwa na mnyama mkubwa aliyekuwa akimtunza na kumlinda katika majanga yote yaliyokuwa yakitokea msituni kule.

Bahati alisema anakumbuka wakati askari wa wanyamapori walipokuwa wakijaribu kumchukua katika mikono ya nyani huyo alipigwa risasi mguuni jambo ambalo lilimsababishia maumivu makubwa.

Mtoto huyo alisema angependa siku moja kuwa daktari ama polisi na angependa kusoma kama wanavyosoma watoto wengine.

``Nataka kuwa polisi au daktari kama walivyo watu wengine,`` alisema mtoto huyo huku akishika shika vitu na mara nyingine akitaka kukaa chini kana kwamba anataka kuanza kuruka ruka kama nyani.

Mtoto huyo hata hivyo haonekani kama akili zake zimeshakuwa sawa kutokana na uwezo wake mdogo wa kujua mambo ukilinganisha na watoto wengine wenye umri wake.

Aidha, mtoto huyo anazungumza kwa shida kama wanavyofanya watoto wanapoanza kujifunza kuzungumza.

Pia, lafudhi na mpangilio wa maneno ya Kiswahili anayozungumza yana mapungufu mengi.

Naye mama mlezi wa mtoto huyo, Rose Mbwambo, ambaye ndiye aliyekubali kumtunza na kuja naye Dar es Salaam akitokea Shinyanga, alisema imani yake ndiyo iliyomsukuma kumsaidia mtoto huyo.

Alisema kuwa wapo watu wengi wanaoguswa na tatizo la mtoto huyo, lakini wanaogopa kumsaidia.

``Mimi nilipoelezwa namna mtoto huyu anavyopata shida na jinsi alivyookotwa niliamua kumchukua na kuja naye ili apate msaada kwa wasamaria wema wengine,`` alisema mama huyo.

Kuhusu mtoto huyo, alisema kama akichukia hukunja uso na kuwa na sura kama ya nyani kabisa, sio mwoga na anajiamini kupita kiasi.

Aidha, alisema kuwa mtoto huyo ni mbunifu wa mambo mbalimbali na kila akiona kitu lazima ahakikishe anakichunguza hadi akijue.

Nipashe ilipowasiliana na Katibu Tawala Wilaya ya Bukombe mkoani Shinyanga, Michael Nhende, alithibitisha mtoto huyo kuokotwa msituni na alikuwa akiishi na nyani huyo.

Alisema katika eneo la mbuga ya Usanga alipookotwa mtoto huyo hakuna mtu ambaye hajui habari ya Bahati na wala sio habari ya kutunga.

Mtoto huyo aliokolewa kutoka katika mbuga hiyo mwaka 2005 na kupelekwa katika Hospitali ya Ushirombo.

SOURCE: Nipashe

No comments: