Tuesday, September 25, 2007

Waziri wa Ulinzi Prof. Kapuya apata ajali Tabora



UPDATE - Prof. Kapuya na majeruhi wengine wameletwa Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

(Photo kushoto from Michuzi Blog)



Prof. Kapuya apata ajali

2007-09-25 Na Abubakary Mlawa,Jijini

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Profesa Juma Kapuya amepata ajali mbaya na hivi sasa madaktari wanapigana kufa na kupona kuokoa maisha yake.
Katika ajali hiyo, watu watatu wamefariki dunia na wawili kati yao inadaiwa ni mabodigadi wa Profesa Kapuya.

Ajali hiyo mbaya ilitokea jana majira ya saa 1:00 usiku katika kijiji cha Kaliua wilayani Urambo na kulihusisha gari la Profesa Kapuya, ambalo lilipasuka gurudumu la mbele la kulia kabla ya kupinduka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Muhidin Mshihiri, amesema watu hao waliokufa wanasadikiwa kuwa askari wa Jeshi la Wananchi, JWTZ.

Akieleza ajali hiyo, Kamanda Mshihiri ambaye amezungumza na Alasiri kwa njia ya simu leo asubuhi, amesema Waziri Kapuya alikuwa katika ziara ya kulitembelea jimbo la Urambo ambalo yeye ni mbunge wake.

Amesema akiwa umbali mfupi kabla ya kufika nyumbani kwake, ndipo ajali hiyo mbaya ilipotokea.

Hata hivyo, Kamanda Mshihiri amesema bado hajapata majina ya watu waliofariki.

Imeelezwa kuwa wawili wamekufa papo hapo wakati mwingine alifikia hospitali. Kwa mujibu wa Kamanda Mshihiri, mbali na Profesa Kapuya ambaye amejeruhiwa, wengine waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo ni watu wanne, ambao wote walikuwa abiria katika gari la Waziri. Imeelezwa gari hilo lilikuwa na watu wanane wakati linapata ajali.
`Hadi usiku wa jana, Mheshimiwa Waziri (Kapuya) na majeruhi wengine walikuwa wakiendelea na matibabu,` amesema Kamanda Mshihiri.

Hata hivyo, Kamanda Mshihiri amesema wanaendelea kufuatilia ili kuwatambua waliofariki na kujua hali za majeruhi.
`Naelekea hospitali ili kuwatambua waliofariki na pia kujua hali ya Mheshimiwa Waziri ambaye hadi sasa sijafahamu amejeruhiwa kwa kiasi gani,` akasema Kamanda Mshihiri.
Habari zilizolifikia gazeti hili wakati linakwenda mitamboni zinasema kulikuwa na mpango wa kumhamishia Waziri Kapuya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

2 comments:

Anonymous said...

Hizi ajali zimezidi jamani-labda kwa sababu zimeanza kugusa wanasiasa, labda wataanza kufikiria mikakati ya kudhibiti hizi ajali!! Pole sana mzee Kapuya

Anonymous said...

Ninapofurahi mimi ni kuwa,wote waliopata ajali walikuwa katika majimbo yao ya uchaguzi.Sasa kama tatizo ni barabara,baaasi wamejionea wenyewe na wame-experiance.So wakiwa bungeni watajua waongee nini kuliko kila kitu makofi tuu.
Majita