Wednesday, September 12, 2007

Wizi hata kwenye Mazishi

Jamani, sijui ni njaa au nini inafanya watu wawe na roho ngumu hivyo! Watu wanaiba kwenye mazishi. Lakini nishangae nini, maana hata mfiwa mume wa marehemu Amina Chifupa aliibiwa simu kwenye mazishi ya mke wake!

Someni habari hizi kutoka ippmedia.com

***************************************************************
Aliyejaribu kuiba msibani Dar nusra auawe
2007-09-12

Na Job Ndomba, Mikocheni

Kijana mmoja aliyejaribu kuiba mali wakati wa maombolezo ya msiba amekiona chamoto baada ya waombolezaji kumpa kisago kikali kabla ya Polisi kumuokoa. Mtu huyo amenusurika kupata madhara zaidi baada ya waombolezaji wenye hasira kutaka kuendelea kumpa kichapo zaidi baada ya kumnasa akiwa kwenye harakati za kunyofoa vifaa vya gari moja la waombolezaji hao na kuondoka navyo.

Tukio hilo linadaiwa kutokea jana, mishale ya saa 9:30 na saa 10:00 jioni pale kwenye makaburi ya Kinondoni. Inaelezwa kuwa wakati huo, waombolezaji walikuwa wakiendelea na shughuli za kuuzika mwili wa mpendwa wao.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, ni kwamba kibaka huyo akiwa na wenzake wawili, walitinga makaburini hapo wakati waombolozeji hao wakiwa `bize` na shughuli za mazishi.

Akizungumza na Alasiri mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Bw. Peter, amesema watu hao walitinga eneo hilo wakiwa katika taxi yenye namba T 500 AEF. Msimuliaji huyo amesema wakati shughuli za maombezi zikiendelea, wakasikika watu waliokuwa wakiitilia wezi karibu yao.

Akasema muda si mrefu wakawaona vibaka hao waliokuwa wakinyofoa vifaa kadhaa toka katika shangingi la mmoja wa waombolezaji wakaanza kutimua mbio na hapo baadhi ya watu hawakukubali na kuanza kuwatimua.

``Walikuwa zaidi ya wawili? kwa bahati, mmoja akakamtawa na ndipo watu walipoanza kumpa kipigo,`` akasema msimuliaji huyo.

Aidha, ikasimuliwa kuwa muda si mrefu Polisi wakafika eneo hilo na kumuokoa kibaka aliyenaswa ambaye pengine, kama angeendelea kupigwa angeweza kuuawa kwa mawe.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa tayari kibaka huyo alishakuwa taabani kutokana na kipigo alichopewa. Inaelezwa zaidi kuwa baadaye, lilifika `breakdown` na kuivuta teksi waliyokuwa nayo vibaka hao.

Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Jamal Rwambow, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo.

SOURCE: Alasiri

No comments: