Tuesday, August 26, 2008

Kongamano la CUF

CUF waandaa kongamano la ukosefu wa uongozi na hatma ya Tanzania

Chama Cha Wananchi
Office of The Secretary General
P.O. Box 10979
Dar Es Salaam, Tanzania
www.cuftz.info
www.hakinaumma.wordpress.blog

TAREHE: 26/08/2008

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU: KONGAMANO LA KITAIFA KUJADILI
UKOSEFU WA UONGOZI NA HATIMA YA TANZANIA

Imetolewa na Mbaralah Maharagande,
Mkurugenzi Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma.

Nchi yetu inapita katika moja ya kipindi kigumu katika historia yake tokea ilipopata Uhuru mwaka 1961. Hali ya uchumi ni ngumu sana huku gharama za maisha zikipanda kwa kasi ya ajabu chini ya falsafa ya ari, nguvu, na kasi mpya. Tofauti za kipato na kiwango cha maisha kati ya matajiri wachache na walalahoi walio wengi inazidi kuongezeka. Migomo ya wafanyakazi na wanafunzi imekuwa ni jambo la kawaida hivi sasa.

Nyufa katika Muungano wetu zinazidi kukua na hata kutishia uhai wa Muungano wenyewe. Migawanyiko ya kidini inaonekana kuzidi kujikita. Mpasuko wa Kisiasa Zanzibar umeshindwa kupatiwa jibu huku uchaguzi mkuu wa 2010 ukiwa unakaribia. Serikali inaonekana kuzidiwa nguvu katika mapambano dhidi ya ufisadi na sasa mafisadi wanaonekana kutamba. Taifa linakwenda bila ya Dira wala Mwelekeo unaoeleweka. Wananchi wanaonekana kukata tamaa.

Matatizo haya kwa kiasi kikubwa yanaonekana kusababishwa na ukosefu wa uongozi thabiti, makini na adilifu. Hii si hali nzuri na tusipokuwa makini Taifa litayumba sana. Wazalendo wakweli wa Tanzania hawapaswi kukaa kimya na kusubiri matokeo ambayo kwa vyovyote vile hayawezi kuwa mazuri.

The Civic United Front (Chama Cha Wananchi-CUF) kikiwa chama makini kikuu cha upinzani nchini, kinachotegemewa na Watanzania walio wengi, kimeandaa kongamano maalum kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali hii ya ukosefu wa uongozi na athari zake kwa hatima ya Tanzania. Kongamano hilo litafanyika siku ya Alhamis, tarehe 28 Agosti, 2008, kuanzia saa 3.30 asubuhi katika ukumbi wa Diamond Jubilee, mjini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba, atawasilisha mada kuhusu UKOSEFU WA UONGOZI NA HATIMA YA TANZANIA na baadaye washiriki watapata nafasi ya kuichambua mada hiyo na kutoa maoni na mtazamo wao.

CUF imewaalika watu mbali mbali kushiriki katika kongamano hilo wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, taasisi za kiraia na kijamii, viongozi wa kidini, wasomi na wataalamu, maofisa wa kibalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

HAKI SAWA KWA WOTE
Mbaralah Maharagande,
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma.

0773 062 577

No comments: