Nilipoanza Form One 1977, nauli ilikuwa sumni (senti hamsini) kwa mwanafunzi. Tena hata wikiendi na jioni uliweza kulipa sumni, mradi una kitambulisho. Mnakumbuka mabasi ya UDA? Basi kila mwezi tulikuwa tunaenda Kurasini Depot ya UDA kununua 'monthly pass' nadhani ilikuwa kama shilingi 20/-! Walifuta pass hizo 1979.
Nilivyomaliza mwaka 1980, nauli ilikuwa shilingi 1/-. 1984 nikiwa nafanya kazi Daily News mabasi binafsi yaliingia. Nauli ulikuwa shilingi 5/- (dala) Ndo jina daladala. Tuliona hiyo dala nyingi lakini ulikuwa usafiri mzuri kuliko wa UDA. Miaka imeenda na sasa nauli ni shs. 500/- (one way). )Of course miaka ya 70 hiyo dola ilikuwa eight shillings to the dollar. Kwa sasa ni 1 dollar -1,200/-.)
Sasa jamani, matatizo ni yale yale, Mtu unapata mshahara lakini haitoshi hizo bili za mwezi. Na siki hizi kila kitu ni kulipia, shule, hospitali. Watu wanakoma ingawa serikali ilipandisha kima cha chini mwaka jana. Mambo ni yale yale maana hata wakati ule mshahara ulikuwa hautoshi. Miradi ndo ziliokoa watu, kuku, ice cream.
Nimeona wanafunzi wamechachamaa huko Dar Leo. Lakini jamani, Bongo kuna mabadiliko. Enzi za Mwalimu mnadhani watu wangeweza kuandamana hivi hivi na mabango?! Watu fulani wangezolewa halafu ungewaona wanarudi 'kiiimya" hawana neno tena. Nyie wengine mngeshulikiwa vizuri na FFU. Ndo tulikuwa tunsema, "kamchape class".
Serikali itazame upya hi suala la nauli. Dar mji mkubwa, watu kutembea miendo si mchezo. Na familia enye watoto wengi wanaosoma si ni balaa kwao!
Miaka mingi tumekuwa tunasema 'Tunataka hali bora ya maisha kwa kila MTanzania'. Sijui hali itakuwa bora lini.
*******************************************************************************
Nauli Mpya ni Kilio
2008-08-01
Na Sharon Sauwa, Jijini
Hatimaye kile kiama cha nauli mpya kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kimeanza leo asubuhi na kuwatoa chozi abiria kibao hasa wale akina kwangu pakavu tia mchuzi.
Alasiri ilipovinjari maeneo kadhaa ya Jiji imeshuhudia abiria kadhaa wakiwalilia makonda wa mabasi kuwaruhusu japo kwa leo kulipa nauli ya zamani kwa kile walichodai kuwa hawakuwa na pesa zaidi.
``We vipi, mlishatangaziwa kwamba nauli mpya inaanza leo...kama huna mia nne yangu, anza...dereva ondoa gari, hakuna kichwa hapa`` konda mmoja wa basi la kutoka Mbezi-Mwenge alisikika akimwambia abiria aliyekuwa akimlilia apokee nauli ya zamani. Kutokana na kupanda kwa nauli, baadhi ya abiria walionekana wakitembea kwa mguu huku wengine wakitokwa na majasho kutokana na kupiga kwata umbali mrefu.
``Tangu saa 11:30, niko njiani. Mshahara wenyewe ndio huo...nikitoa kodi ya nyumba, chakula, ada ya watoto, umeme, nauli hii ya Sh. 600 kwa kila ruti nitaipata wapi? Nimeona nianze mapema kabisa kutembea,`` mwanamama mmoja aliyekuwa akitokea Boko kwenda Mwenge ameliambia Alasiri.
Kwa upande wa wanafunzi, wengi walionekana wakiwa wamejazana vituoni kutokana na makonda kuwazuia kupanda mabasi hadi waonyeshe nauli yao mpya. ``Tulidandia malori la sivyo tusingekwenda shule kabisa,`` denti mmoja kutoka Tabata anayesoma maeneo ya Mbezi amesema.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usafiri, Nchi Kavu na Majini, SUMATRA, nauli mpya ilitakiwa kuanza kutumika leo ambapo watu wazima wanatakiwa kulipa Sh. 300 kwa safari fupi ambazo hazizidi kilomita kumi wakati wale wa umbali wa kilomita kumi na tano wanatakiwa kulipa nauli ya Sh. 400 na wale wa kilomita 25, nauli yao ni Sh. 500.
Kwa upande wa ruti za kulala usingizi, yaani zile za umbali wa kilomita 30, wanatakiwa kulipa nauli ya Sh. 600 wakati wanafunzi nauli yao imepanda kutoka Sh. 50 hadi Sh. 100. Habari zilizotufikia wakati tukienda mitamboni zinasema kuwa wanafunzi wa shule mbalimbali Jijijini Dar es Salaam wameitisha mgomo mkubwa kupinga nauli mpya za daladala.
Imedaiwa kuwa wametinga ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro kumweleza tatizo hilo.
Friday, August 01, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Hii nauli mpya inaumiza si mchezo. Bei ya viatu imepanda maana ndo magari sasa.
Post a Comment