Kwa kweli inasikitisha kuona madaktari wanagoma. Ninaelewa kuwa wanadai maslahi bora zaidi na ni kwali wanastahili kupewa. Lakini wagonjwa wanaowategemea wanaumia na wengine wanapotozea maisha.
Nakumbuka miaka ya 90 mwanzo nikiwa mwandishi wa habari Daily News ilitokea mgomo wa madaktari, manesi na wafanyakazi wengine wa afya. Nilipewa 'assignment' ya kwenda Muhimbili kuona hali ilivyo.
Kwa kweli hali ya wagonjwa ilikuwa mbaya nilitoka huko nalia. Niliona maiti za wagonjwa waliokufa kwenye vitanda walivyofia. Wodi fulani kulikuwa na nesi mmoja tu, anahangaika na wagonjwa wote. Nilimhurumia. Wenye pesa waliondoa wagonjwa wao na kuwapelka private.
Hivi hakuna njia nyingine ya watu wenye kazi nyeti kama madaktari kudai maslahi yao?
*************************************************************************
Kutoka ippmedia.comSerikali Yawashukia Madaktari
2008-08-12
Na Mary Edward, PST Dodoma
Serikali imewaagiza madaktari wote waliogoma, kurudi kazini mara moja kama kanuni, taratibu na maadili ya kazi yao inavyowataka la sivyo hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokaidi. Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Aisha Kigoda alitoa agizo hilo kwa niaba ya Waziri wake, Profesa David Mwakyusa mjini hapa jana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dk. Kigoda alisema, wasipofanya hivyo, hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka agizo hilo. Alisema serikali inashughulikia suala la posho, mishahara na malimbikizo kwa viwango vipya kwa watumishi wote wa umma nchini, na malipo hayo yatakapokamilika, kila mtu atapata stahili yake.
Aidha, Dk. Kigoda alitumia fursa hiyo, kuwapa pole wagonjwa na wananchi kwa ujumla, kutokana na usumbufu uliojitokeza. ``Napenda kuwahakikishia wananchi kwamba, huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, zinaendelea kutolewa na madaktari waliopo, ili kuhakikisha kwamba kila mgonjwa anayestahili kupata tiba, anapata matitabu,`` alisisitiza.
Akitoa maelezo ya suala hilo, Dk. Kigoda alisema, madaktari hao wamechukua hatua hiyo kwa ajili ya kudai mishahara mipya pamoja na malimbikizo ya mishahara, baada ya kuwasilisha madai yao kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambaye aliwaeleza kimaandishi kuwa, suala hilo ni la kiserikali, hivyo litashughulikiwa na wizara. ``Aliiarifu wizara na kuomba Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, akutane na viongozi wao, kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wake, Katibu Mkuu alikutana nao Agosti 7 mwaka huu,`` alisema.
Alisema katika kikao hicho, Katibu Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwaeleza kuhusu hali halisi kwamba, serikali inashughulikia malimbikizo ya watumishi wote na itakapokuwa tayari watalipwa. Kuhusu mishahara mipya, Dk. Kigoda alisema, Katibu Mkuu aliagiza wataalamu wa fedha wa wizara na wa hospitali wafanye mahesabu, ili kutambua kiasi kinachohitajika ili kiwasilishwe Wizara ya Fedha na Uchumi, kabla ya Agosti 11 ambayo ndiyo siku ya mwisho kwa waajiri wote, kuwasilisha madai hayo ya malimbikizo ya miashahara.
``Hali hii inatokana na ukweli kwamba, wanalipwa fedha zao kwa utaratibu wa posho na si kwa kupitia Pay Roll za serikali,`` alisema.
Aliongeza ``napenda kusisitiza kwamba, ufafanuzi uliotolewa na juhudi zilizoainishwa na Katibu Mkuu wa viongozi wao, ulikuwa unatosha kuthibitisha dhamira ya serikali ya kuhakikisha kuwa, posho yao inazingatia viwango vipya na stahili yao ya malimbikizo ipo pale pale na itashughulikiwa pamoja na watumishi wengine wote wa serikali.``
Aidha, alisema katika muda wote huo wa majadiliano, viongozi hao hawakuonyesha nia wala dhamira ya kupanga wala kutaka kugoma kama ambavyo wamefanya sasa. ``Kitendo hiki kinakiuka kanuni za kiutumishi, taratibu na sheria zinazohusu migomo katika kazi na maadili ya taaluma ya udaktari,`` alisema.
Lakini wakati naibu Waziri wa Afya akitoa agizo hilo, madaktari hao wasaidizi kwa upande wao, wamekubali kusitisha mgomo huo baada ya serikali kuwaahidi kushughulikia madai yao ndani ya siku saba, anaripoti Lucy Lyatuu. Hayo yalisemwa na Rais wa madaktari hao, Bw. Magesa Paulo, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Alisema jana walikaa katika kikao kilichomjumuisha Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Mkuu wa Taasisi ya Mifupa (MOI), wawakilishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao kwa pamoja walikuwa wakizungumzia madai yao.
Alisema baada ya mazungumzo, walikubaliana kuwalipa madai yao ya mshahara mpya wa serikali wa Julai na Agosti pamoja na malimbikizo yao inayoanzia Januari hadi Juni. Aliongeza kuwa, ndani ya kikao hicho, wawakilishi kutoka serikalini wamewaahidi pia kuwaletea kiwango kamili cha madai yao ifikapo Jumatatu.
Hata hivyo, alisema endapo ahadi hizo zisipotekelezwa katika siku hizo saba, watachukua hatua nyingine ambayo hakuitaja ni ya aina gani. Aidha, alisema anaishangaa serikali kutokuwa na uhakika wa ahadi za kuwalipa licha ya kwamba wamekuwa wakiwaandikia barua kila mara. Kuhusu udaktari kuwa wito na kwamba hawapaswi kugoma ili kutowaathiri wagonjwa, alisema madai ya msingi kwa madaktari ni ya msingi na kwamba hamna wito kama hupati mahitaji ya msingi.
``Bila kula na kushiba nguvu ya kushughulika utaipata wapi,`` alihoji Bw. Magesa. Aliongeza kuwa, kwa kuzingatia misingi hiyo, madaktari watano wasaidizi tayari wameambukizwa virusi vya Ukimwi kutokana na kuwachoma sindano wagonjwa walioathirika.
Alisema kutokana na misingi ya kiubinadamu kupata mahitaji yake, ni hivyohivyo na wao kupewa haki zao ili waweze kutimiza wajibu wao. Alisema asilimia 70 ya huduma za madaktari hospitalini hapo haswa wodini, hutegemea madaktari hao na kwamba kugoma kwao kumeathiri wagonjwa.
Madaktari hao walikuwa wakidai malipo ya mshahara mpya kama ilivyoagizwa katika waraka wa serikali, malimbikizo yanayoanzia Januari hadi Juni pamoja na mapumzikoya siku 28. Mkuu wa Mkoa wa Dares Salaam, Bw. Abbas Kandoro jana alitembelea Hospitalini hapo kwa lengo la kufuatilia hali ya mgomo. Alisema serikali inaanda utaratibu wa kufuatilia madai yao kwani yatajumuishwa pamoja na watumishi wote wa serikali.
1 comment:
umetoa maoni yako madaktari wameyasikia lakini ningependa nikukumbushe kitu kimoja kazi za wito zilikuwepo enzi za ujamaa, hakuna wito kwenye huu ulimwengu wa utandawazi ambapo kila mtu anataka awe na maisha mazuri. ukisema madaktari wawe na wito watoto wao watasoma kwa wito, watakula wito? au mnataka muanze kusema huyu naye eti daktari hata bajaji hana. napenda nikuhakikishie dadangu madaktari ni watu wazuri sana na wanapenda kuwasaidia watu, ingawa sikatai wapo wachache ambao huwaharibia, lakini hao wazuri wanaondolewa molari na viongozi na wanasiasa, wao wanaendelea kusema udaktari ni wito huku wakilipwa vimishahara vidogo kwa nini mtu asijitafutie riziki sehemu nyingine, hata ningekuwa mimi ningefanya hivyo hivyo. cha muhimu tumia kalamu yako ishauri serikali iwalipe vizuri kama wanavyolipana wanasiasa uone ni kiasi gani ufanisi utaongezeka, nadhani umenipata. waonee huruma madaktari kazi wanayofanya ni ya pekee, wanaokoa uhai ambao hauthaminishwi na chochote. kazi njema.
From "Mwanafunzi wa udactari niliye ughaibuni na naogopa hata kurudi nimalizapo masomo"
Post a Comment