Saturday, January 24, 2009

Serikali Yafuta Leseni za Waganga wa Kienyeji

Wadau, nasema WAZIRI PINDA NI SHUJAA!!!!

*******************************************************************
Waziri Mkuu Pionda afuta leseni za waganga wa kienyeji

SERIKALI imetangaza kufuta leseni zote za waganga wa jadi kuanzia jana (Ijumaa Jan. 23, 2009) ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya mauaji ya Albino na Vikongwe nchini.

Amri hiyo ilitangazwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika mkutano wa hadhara mjini Shinyanga jana mwishoni mwa ziara yake ya mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhamasisha mapambano ya Serikali dhidi ya mauaji hayo.

Waziri Mkuu alisema kuwa aliwasiliana na Mwanasheria Mkuu kuhusu uamuzi wa kuchukua hatua hiyo ya kufuta leseni hizo na Mwanasheria Mkuu akasema jambo hilo linawezekana.

"Kuanzia leo leseni zote za waganga wa jadi futa… Mtu yeyote akiendelea na kazi hiyo mfuatilieni," aliwaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakuu wa Halmashauri zote za Jiji, Miji na Wilaya nchini.

Waganga wa jadi wamekuwa wakituhumiwa kuwa ndiyo chimbuko la mauaji hayo kwa vile wao ndiyo hupiga ramli za kuelekeza hivyo.

Katika mikutano na viongozi wa mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Tabora na Shinyanga, wachangiaji wengi waliitaka serikali kufuta leseni hizo. Hata baadhi ya waganga wa jadi waliochangia walikiri.

Waganga wa jadi husajiliwa na kupewa leseni za kufanya kazi zao na Halmashari kwa utaratibu wa kiutawala. Ipo sheria ya mwaka 2002 kuhusu Tiba Asilia na Tiba Mbadala (Traditional and Alterntive Medicine Act), lakini Kanuni za utekelezaji wake zilikuwa hazijatengenezwa.

Waziri Mkuu alisema mganga wa jadi ambaye anaweza kuruhusiwa baadaye ni yule ambaye dawa zake za mitishamba au za asili zitakuwa zimethibitishwa na Kitengo cha Uchunguzi wa Tiba Asili cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwa kweli zinatibu. Mgonjwa naye atatakiwa awe na cheti kutoka hospitali kitakachothitisha maradhi yake na kuwa tiba yake hopitali imeshindikana.

"Waganga hawa ni waongo wakubwa…Siyo lazima kuwa nao. Wangekuwa waganga wa kweli magonjwa mengi yangepungua nchini, lakini magonjwa yapo na sasa wanapiga ramli na kuwa kichocheo cha mauaji.

Mkoa wa Shinyanga unasemekana unaongoza kwa idadi ya waganga wa jadi waliosajiliwa na wako 1,104 na 94 ambao hawakusajiliwa. Wilaya ya Kahama peke yake ina 763.

Waziri Mkuu aliuambia umati uliofurika kwenye uwanja wa Chuo cha Biahshara cha Shinyanga (Shycom) huku akishangiliwa kuwa mapambano dhidi ya mauaji ya Abino ni vita na ndiyo maana anataka ulinzi wa jadi wa Sungusungu urejeshwe kusaidiana na vyombo vya dola kukabiliana na hali hiyo.

Aliwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa kufnya kazi zao kwa ufanisi zaidi na "kujipanga upya na kuteremka hadi ngazi ya chini" kusimamia mapambano dhidi ya mauaji ya Albino na Vikongwe.

"Inapotokea kuwa Albino au Kikongwe anauawa katika eneo fulani, mimi nitamshukia Mkuu wa Mkoa na kumuuliza kwa nini aliacha hali itokee hivyo. Mkuu wa Mkoa naye atamshukia Mkuu wa Wilaya na vivyo hivyo," alisema.

Aliongeza: "Tukijumuika wote kwa pamoja tutashinda vita hii kama tulivyoshinda vita dhidi ya nduli Idi Amin wa Uganda".

Waziri Mkuu pia alisema atamwomba Jaji Mkuu kuwa zile kesi za mauaji ya Albino ambazo ziko tayari zinapangiwa majaji maalum ili zikamilike na hatima yake ijulikane haraka.


Tangu Juni mwaka 2007 mpaka Novemba mwaka 2008 jumla ya Albino 34 wameuawa nchini kwa imani za ushirikina kuwa eti viungo vyao vinasaidia kupata utajiri. Idadi yao kimkoa kwenye mabano ni Mwanza (19) Mara (4) Kigoma (3) Shinyanga (4), Kagera (3) na Mbeya (1). Mwaka huu tayari wameuawa watatu.

Jumla ya vikongwe waliouawa nao kwa kushukiwa wachawi ni 2583 ambapo idadi yao kimkoa kwenye mabano ni Mwanza (696), Shinaynga (522), Tabora (508), Iringa (256), Mbeya (192) Kagera (186), Singida (120) na Rukwa (103).

Ziara ya Waziri Mkuu Pinda katika mikoa ya Kanda ya Ziwa inamalizika leo kwa majumuisho yatakayowahusisha viongozi wa mikoa hiyo. Alianzia Kagera na badaye kutembelea mikoa ya Mwanza, Tabora na Shinyanga. Mkoa wa Mara ulijumuishwa kwa viongozi wake kuhudhuria mkutano wa viongozi Mwanza.
(mwisho)
Imetolewa na:
Ofisi ya Waziri Mkuu,
S.L.P. 3021,
DAR ES SALAAM

*************************************************************
Pinda ataka jino kwa jino
Na Victor Kinambile, Tabora

KATIKA hali ya isiyo ya kawaida, Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana aliwaambia wananchi kuwa wanaoua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja vikongwe ni hawana budi kuuawa kwa kuwa wakisubiri mahakama kuwahukumu, watakuwa wanakosea.

Waziri Pinda, ambaye ameanza ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye lengo la kuhamasisha vita dhidi ya mauaji ya vikongwe na albino, aliutaka Umoja wa Vijana wa CCM kuongoza vita hiyo, akisema lina jeshi zuri.

Mauaji ya albino yamekuwa ni tatizo kubwa nchini na hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Pamoja na serikali kutangaza hatua kadhaa za kupambana na wauaji hao, bado matukio ya kuuawa kwa watu hao wenye ulemavu wa ngozi yamekuwa yakiendelea kuripotiwa, lakini Waziri Pinda ameenda mbali zaidi katika kukabiliana na tatizo hilo alipotaka wauaji hao wauawe badala ya kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Kauli ya Pinda, ambayo inaweka maswali katika suala la utawala bora, imekuja wakati ambao wananchi wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi na kuua vikongwe kutokana na imani za uchawi.

Akihutubia wakati wa kufungua mkutano wa 16 wa Shirikisho la Vyama vya Kuweka na Kukopa (SCCULT) kwenye ukumbi wa Chuo cha Utumishi Umma mkoani hapa, Waziri Pinda alisema iwapo wananchi wataendelea kuwahurumia wauaji hao ambao wanatafuta viungo vya albino wakitegemea mahakama itatenda haki huku nao wakiongeza kasi ya mauaji kwa Watanzania, watakuwa wanakosea.

Hivyo alisema kwamba kuanzia sasa mtu yeyote atakayemuona mtu amemkata shingo au mkono mweziwe basi naye auawe papo hapo hii itakuwa ndiyo dawa kwani vingozi wote tumechoka na mauji hayo.

"Mkimuona mtu akamkata mwingine shingo naye muueni kwani sasa viongozi wote tumechoka... no more, I can't tolerate anymore (imetosha, siwezi kuvumilia tena)," alisema Pinda huku akiwaacha watu midomo wazi.

Aliviomba vyama vya siasa kushirikiana na wananchi kuhakikisha suala hili la mauji linakwisha kwani wauji "tunaishi nao na ni rahisi kulimaliza iwapo tutakuwa kitu kimoja katika kuondoa kashifa hii ambayo imekuwa mbaya kwa nchi yetu".

Aliuagiza Umoja wa Vijana wa CCM kuhakikisha mauaji hayo yanatokomezwa kabisa, akisema kuwa ni jeshi zuri ambalo likiamua kutokomeza kabisa mauaji ya vikongwe na ndugu zetu maalbino inawezekana.

"Umoja wa vijana mna jeshi zuri ambalo naamini mkiamua mnaweza kutokomeza mauaji ya wazee wetu pmoja na ndugu zetu maalbno na kazi hiyo nawaagiza muanze leo msisubri auawe mwingine tena," alisema waziri mkuu.

Baada ya kumalizika kwa mkutano huo, baadhi ya watu wanaoonekana kuwa ni wa "serikali" waliwafuata baadhi ya waandishi wa habari, akisihi suala hilo lisiripotiwe magazetini kwa madai kuwa kauli hiyo ya Waziri Pinda inaweza kusababisha matatizo.

Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia amekuwa mstari wa mbele kupiga vita mauaji hayo, alitofautiana na Waziri Pinda katika moja ya hotuba zake aliposema kuwa adhabu ya kuua haitofautishi muuaji wa albino na muuaji mwingine na kwamba watakaopatikana na hatia ya kuua albino, atakabiliana na adhabu ya kifo kama ilivyo kwa muuaji mwingine.

Waziri Pinda alionekana kukerwa na mauaji ya albino wakati alipopata taarifa kwamba kuna mama mwingine aliuawa usiku wa kuamkia juzi.

"Nimeambiwa kuwa juzi wilayani Sengerema kuna mama mmoja ambaye ni mlemavu wa ngozi amekatwa mkono na wauaji wakaondoka na mkono huo na tayari mama huyo amekufa," alisema Pinda na kusisitiza kushughulikia wauaji hao.

Akitoa takwimu za mauaji ya vikongwe na malbino alisema mwaka 2003 waliuwawa vikongwe 517, mwaka 2004 waliuawa vikongwe 444, mwaka 2005 (494), 2006 (vikongwe 386), mwaka 2007 (vikongwe 526) na albino sita na mwaka 2008 (vikongwe 526 na albino 28).

Alisema tayari mwaka huu wameuawa albino watatu hivyo kufanya albino na vikongwe waliouawa kufikia kuwa jumla 2,900.

Waziri mkuu ameanza ziara ya siku nne kutembelea mikoa ya Shinyanga, Tabora na Mwanza ili kuhamasisha wananchi watokomeze vitendo vya mauaji ya vikongwe na watu weye ulemavu wa ngozi.

1 comment:

Anonymous said...

asante Yesu haya ndo tulikuwa tunayaomba yatokee, ma bado lazma uchawi uteketee kwa jina yesu.