Friday, January 23, 2009

Wimbi la Ajali za Mabasi Bongo!

Hivi jamani, chanzo cha hizi ajali hizi ni nini? Barabara mbovu, uendeshaji mbaya, mabasi mabovu? Ni nini? Yaani katika mwezi tu, mamia ya watu wamekufa huko Tanzania!

***************************************************************************

Kutoka ippmedia.com

Ajali zaondoa uvumilivu wa Kikwete

2009-01-23
Na Mwandishi Wetu

Rais Jakaya Kikwete, amesema serikali haiwezi kuvumilia kutokea kwa ajali za barabarani zinazosababisha vifo na upotevu wa mali, wakati mamlaka zenye kusimamia usalama katika eneo hilo zipo.

Katika salaamu za rambirambi alizozitoa jana kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima, kufuatia ajali ya juzi iliyosababisha vifo vya watu 16 na wengine kadhaa kujeruhiwa, Rais alisema ni lazima juhudi zifanywe kupunguza ajali hizo kama si kuzikomesha kabisa.

Ajali hiyo ilihusisha basi la abiria, Toyota Double Coaster liitwalo Mapenzi ya Mungu na lori, ilitokea katika eneo la daraja la mto Nduruma, nje kidogo ya mji wa Arusha.

``Hatuwezi kuendelea kuvumilia kutokea kwa ajali hizi, wakati mamlaka zenye dhamana ya kusimamia sheria ya usalama barabarani zipo,`` Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, imemkariri Rais Kikwete akionya.

``Tufanye jitihada zilizo ndani ya uwezo wetu, kupunguza kwa kiwango kikubwa na ikiwezekana kukomesha kabisa ajali hizi za barabarani ambazo
katika kipindi kifupi tangu kuanza kwa mwaka mpya, zimepoteza maisha ya wenzetu wengi,`` alisema.

Rais Kikwete, alisema ajali mfululizo zinazotokea nchini, hazina budi kuwekewa mikakati madhubuti ya kudhibitiwa, kutokana na mamlaka husika kuwa na uwezo huo.

Katika salam zake hizo, Rais Kikwete, alitoa pole kwa majeruhi na kusema: ``Ninatambua maumivu makali mnayoyapata hivi sasa...Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu.``

Tangu mwaka huu uanze ajali nyingine mbaya mbili za mabasi zimetokea kanda ya kaskazini, moja mkoani Tanga na nyingine mkoani Kilimanjaro. Ya Kilimanjaro iliua wanandugu 11 waliokuwa wanatoka kwenye sherehe ya ubarikio Hai na ya Tanga iliua watu 28.

Pia kuna ajali nyingine ya basi lililokuwa likisafiri kutoka Dodoma kwenda Manyara iliyoua watatu katika mwezi huu.

SOURCE: Nipashe

1 comment:

Anonymous said...

Kafara hizo hamjui uchaguzi ni mwakani?