Press Release kutoka One Game:
Majaji tuzo za Vinara kuanza kazi leo!
Na Mwandishi Wetu
Jopo la majaji wa Tuzo za Vinara wa filamu nchini (Vinara Film Award) leo Jumamosi ya Mei 3, 2008 linatarajiwa kuanza rasmi kazi ya kuziangalia filamu za Kitanzania zinazowania tuzo hizo kabla ya kuzitolea maamuzi.
Mratibu wa One Game Promotion inayoaandaa utolewaji wa tuzo hizo, Khadija Khalili amesema kuwa, majaji hao watatanguliwa na semina ya siku moja kabla ya kuanza zoezi la kuziangalia filamu hizo chini ya usimamizi wa maafisa wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Jopo hilo linaloundwa na wataalamu wa mambo ya filamu nchini wanakutana leo katika hoteli ya Regency ya Mikocheni jijini Dar es Salaam na kuendelea na kazi hiyo kwa siku kadhaa kabla ya kuibuka na majina ya filamu na wasanii walioingia katika makundi ya kuwania tuzo hizo.
"Kikubwa ni kwamba jopo la majaji linategemea kukutana Jumamosi ya Mei 3 (leo) katika hoteli ya Regency Mikocheni kwa ajili ya semina na kuanza kazi ya kuzipitia filamu zilizowasilishwa kwa ajili ya kuwania tuzo za Vinara," alisema Khalili.
Vipengele vinavyoangaliwa ni Filamu Bora ya Mwaka, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kike, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kike, Muongozaji Sinema Bora wa Mwaka, Mchekeshaji Bora wa Mwaka, Mwandishi Bora wa Filamu na Mtunzi Bora wa Filamu.
Vingine ni Filamu Bora ya Kutisha, Muigizaji Mwandamizi Bora wa kike), Muigizaji Bora Mwandamizi wa Kiume, Adui Bora kwenye Filamu, Wimbo Bora wa Mwaka (Sound Track), Mhariri Bora wa Filamu ambao wote watapata tuzo. Pia itatolewa tuzo ya heshima kwa wale waliotoa mchango wao kukuza sanaa nchini.
Wiki iliyopita, Khalili alisema kuwa, zaidi ya filamu sabini zimeingizwa na watengenezaji wa filamu nchini kuwania tuzo hizo.
Filamu zinazowania tuzo hizo ni zile zilizokamilika kutengenezwa Januari 2007 mpaka Machi 31, 2008.
Tuzo hizo zitakazotolewa Mei 30, zimedhaminiwa na Tanzania Breweries Limited (TBL) kupitia bia ya Ndovu Special Malt, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Global Publishers.
Saturday, May 03, 2008
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment