Saturday, June 30, 2007

Shairi - Amina Hayupo Tena

Amina Chifupa aliwatembelea waginjwa hospitali ya Amana, Ilala, Dar es Salaam
(Photo from Jiachie (Michuzi Jr.) Blog)


Amina Hayupo Tena

Imetungwa na Fahdili Mtanga

Nasikia radioni, Amina hayupo tena,
Ninashindwa kuamini, umetutoka Amina,
Amina wetu jamani, Amina wetu Amina,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Mola wetu tusikie, twaja kwako Maulana,
Amina tumlilie, mbunge wetu vijana,
Faraja utupatie, usiku hata mchana,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina mbunge wetu, tuliyekupenda sana,
Uliyeonesha utu, kwa wazee na vijana,
Uliyekuwa mwenzetu, tena bila ya hiyana,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina ulitujali, tukakupenda kwa sana,
Juhudi zako za kweli, zilikubalika sana,
Mola wetu mfadhili, lini tutamwona tena?
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Umetuacha jamani, twakulilia Amina,
Ni vigumu kuamini, kuwa hatukwoni tena,
Majonzi yetu moyoni, mbona ni makubwa sana,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Twashindwa kuelezea, jinsi inavyotuuma,
Ni vigumu kuzowea, kupoteza kitu chema,
Wewe ulijitolea, ukweli ukausema,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina bado kijana, umetuacha mapema,
Ndoto zako nyingi sana, ukaamua kusoma,
Kwa marefu na mapana, uiongeze hekima,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina muongeaji, waongea kwa hekima,
Wewe mshereheshaji, Amina ukawa mama,
Amina mpiganaji, vita sasa waitema,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Amina tulikupenda, ukawa rafiki mwema,
Ona sasa umekwenda, kwa heri hujaisema,
Mauti yamekutenda, basi uende salama,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Pole wanafamilia, pole Tanzania nzima,
Sote tunakulilia, utakumbukwa daima,
Wewe umetangulia, nasi twaja tuko nyuma,
Mola umlaze pema, rafiki yetu Amina.

Mola akupumzishe, peponi mahala pema,
Nasi tukajikumbushe, dunia siyo salama,
Mola wetu tuepushe, na hicho chako kiyama,
MOLA UMLAZE PEMA, RAFIKI YETU AMINA.


Fadhili Mtanga,
http://www.fadhilimshairi.blogspot.com/
Dar es Salaam.

4 comments:

ombui said...

Ni sikitiko kumpoteza Amina Chifupa. Natumai wabunge na wanaharakati waliopo wataendeleza kazi nzuri aliyofanya au miradi aliyoanzisha.

Chemi Che-Mponda said...

Sijui kama wataendeleza. Ukifa umekufa watu wanakusahau. Hapa USA unakuta mtu akifa, watu wanaanzisha mfano scholarships zenye jina la marehemu. Lakini yaani acha tu, bado ni vidumu kuamini kuwa Amina Chifupa ametutoka.

Fadhy Mtanga said...

ni mshumaa uliozimika ghafla.hakuna aliye tayari kuchukua kiberiti na kuuwasha mshumaa mwingine.
sina hakika sana kama patatokea Amina mwingine. inauma sana kwa sababu ni vigumu mno kumsahau Amina.
Amina alikuwa Amina kweli.
tumnamwomba Mungu amlaze mahali pema peponi.Amina.

Chemi Che-Mponda said...

Inanisikitisha kuona kuwa wanahabari wanaendeleza kuandika maneneo ambayo siyo mazuri juu ya Amina. Nafikiri ni uungwana kumwacha dada huyu apumzike kama Mwinyezi Mungu alivyoamua apumzike. Mwacheni apumzike jamani
Matt