Saturday, January 21, 2006

Kukosa Nguvu za Kiume si Mwisho wa Dunia!

Jamani, jamani, jamani, kuna jirani yangu kafa hivi majuzi. Alikuwa ni baba wa makamu, mmarekani mweusi. Alikuwa mcheshi na ilikuwa kila tukionana lazima tusalimiane. Mara ananinunulia kahawa halafu tunakaa namsimulia kuhusu Afrika. Yule baba, alionekana mzima na mwenye afya fiti kabisa. Nilibakia kushangaa kusikia kafa na si kwa ajali. Mke wake alifariki mwaka juzi, lakini miezi ya karibuni alikuwa anaonekana mwenye furaha kwa vile alipata mpenzi, dada mwenye miaka 25 hivi.

Story niliyoskia ni hivi: Kumbe jamaa alikuwa na matatizo ya moyo. Alifia kitandani akiwa kwenye shughuli ya kufanya tendo la ndoa na mpenzi wake. Tena wanasema alifariki mara alipofikia kilele cha tendo. Navyosikia ilikuwa ni ‘massive heart attack’. Kama ni massive bila shaka na utamu wa shughuli hakujua kuwa yuko hatarini. Nasikia huyo mpenzi wake alipiga sana makelele majirani walipigia simu polisi 911 kwa vile walidhania wameingiliwa na majambazi. Wanasema baba wa watu kamwangukia yule dada na kafa macho wazi.

Lakini bado nilikuwa nashangaa maana kama nilivyosema awali, jamaa alionekana kuwa na afya. Kumbe jamaa alikuwa mtumizi wa Viagra, yaani vile vidonge vya kuongeza uume, na kumpa mwanaume uweza wa kufanya tendo la ndoa. Ndugu zake wanalamika kweli, maana hakuzipata kwa prescription ya daktari, alizaiagiza kwenye mtandao (internet). Kwa kumwangalia alivyofiti nisingefikiria kuwa ana matatizo ya nguvu za kiume. Kumbe mtazame mtu, matatizo yake anayajua mwenyewe na daktari wake.

Nikawa najiuliza kama jamaa alijua ana matatizo ya moyo, kwa nini alitumia Viagra. Maana hata tangaza kwenye TV na magazeti wanaonyo kuwa kabla ya kutumia. Halafu pia wanaonya kuwa mwanaume anaweza kupofuka kama anatumia. Lakini wanaume bado wanazitumia! Na siku hizi dawa za kuongeza nguvu za kiume ziko nyingi kuna Ciallis, Levitra, Yohimbine na mengine. Hizo dawa zina side effects kama kuumwa kichwa, kuharisha, pua kuziba, macho mekundu, tumbo kuumwa na mengine mengi. Pamoja na side effects bado zina soko kubwa. Na zikipigwa marufuku nina amini kuwa watu watatajirika kwa kuzifanyia magendo.

Kwa kweli wanaume wako tayari kufa kama wakishindwa kufanya tendo la ndoa. Nashindwa kuelewa sababu. Yaani tendo la ndoa ni tamu kiasi hicho au wanahofia kuwa kwa vile hawa ‘function’ tena ndo basi si wanaume? Mtu anakuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa ajili ya kufanya tendo la ndoa. Mwanaume anaambiwa anaweza kupofuka akitumia hiyo dawa lakini bado yuko tayari kuchukua risk. Halafu mwanaume akiitwa ‘hanithi’ yuko tayari kupigana au kuua. Sijui bila kusimamisha anajiona si mtu tena…sielewi kabisa!

Nikawa najadiili na marafiki zangu juzi na tulikubaliana kuwa wanaume wako tayari kuchukua ‘risks’ kuliko wanawake. Yaani mwanaume anaweza kufanya tendo la ndoa hata akijua kuwa kuna hatari ya mwenzake kuwa na ugonjwa wa zinaa na ataambukizwa. Bongo, walikuwa wanasema eti, ‘Ajali Kazini’! Hiyo ajali inaweza kukuua! Sijui hiyo ume ikisimama ndo basi tena, akili zote zinahamia hapo. Nauliza tena, tendo la ndoa ni tamu kiasi kwamba mko tayari kuhatarisha maisha yenu? Kukosa nguvu za kiume zi mwisho wa dunia jamani. Bado tunawahitaji!

Lakini nikirudi kwa marehemu jirani yangu, uwongo mbaya, alikuwa anatabasamu ndani ya jeneza lake!

Tuesday, January 03, 2006

Tupende Urembo Asili

Baada ya kuandika kuhusu matako makubwa, na kusoma feedback yenu, nimeona niongee kuhusu mashindano ya urembo. Asante kaka Ndesanjo kwa kunichokoza!

Hivi karibuni Miss Tanzania 2005, Bi Nancy Sumary alienda kwenye mashindano ya Miss World na kafanikiwa kutwaa taji la Miss Africa. Kwa kweli lazima nimpongeze maana toka mashindano ya Miss Tanzania ifufuliwe miaka ya 90, hakuna Mtanzania aliyefanikiwa kuingia katika raundi za fainali na hata kutwaa taji lolote. Kwa kweli Tanzania imepata sifa kubwa katika dunia ya mashindano ya U-Miss. Pia Tanzania imepata sifa kuwa ina wanawake wazuri, lakini nauliza ni uzuri wa aina gani? Maana sioni kama ni uzuri unayafuata maadili ya kiafrika bali ni uzuri wa kizungu!

Nikitazama picha na kanda za video za Miss Ilala, Miss Kinondoni, Miss Utalii, na mashindano mbalimbali za u-Miss huko Tanzania nashangaa nachoona. Kwa kweli naona wasichana weusi wakijaribu kuiga wazungu! Wengine wanapaka make-ups usoni ambazo zimetengezwa kwa ajili ya wazungu wakati make-up za weusi zipo. Yaani ni vichekesho mpaka wengine wanaonekana vituko. Najua hapo niatambiwa nawaonea wivu lakini si kweli na naomba mnisikilize kabla ya kunipa hukumu.

Kwanza tutazame hao wanaopelekwa na nchi zao katika mashindano hayo. Ukiangalia walio kwenye Miss World na Miss Universe, washindi wote wana hulka (characteristics) za kizungu. Tutazame waafrika wanaoenda, cheki nywele zao, zinafanana na wazungu, yaani zimenyoka kabisa. Na kama tunavyojua, sisi wenye asili ya Afrika nywele zetu ni za kipilipili. Hawa wanaweka dawa au weave! Wanaficha nywele zao za asili, sijui wanazionea haya. Je, wanaona haya kusuka nywele zao au kuonyesha mtindo wa nywele enye asili ya Afrika?

Haya, tutazame shepu zao, wote ni wembamba, hakuna mnene, hata hips za maana hawana. Na kama ana matako ni kiasi, sio ile boxi, wowowo, yokohama inayopendwa Africa. Yaani wanafanya mazeoezi eti kusudi wapunguze matako yao. Na hao weusi kutoka Marekani na Ulaya wanafanya liposuction na surgery kupunguza matako yao asili, eti iwe ya kizungu fleti. Huko Afrika tunasema mtu mwembamba ana shida, hana raha, mgonjwa, lakini mzungu anasema ni uzuri. Na sisi tunaiga! Basi unakuta akina dada hata Tanzania, “Oh nafanya diet!” Kheh! Kisa anataka kufanana na mtu amliyemwona kwenye gazeti. Hawajui kuwa hizo picha zinafanyiwa editing na air brushing. Kwa hiyo dada zetu wanashinda njaa kusudi wawe wembamba! Hawajui kuwa hao wanaofanikiwa kwenda kwenye u-Miss, wanajitapisha, na kujinyima chakula kusudi wasinenepe, na ukweli hawana raha.

Haya tuangalie wanavyotembea na kuongea…wanaongea na kutembea kizungu! Jamani na hata macho hawasahau, maana wanatia contact lenses zenye rangi ya bluu na kijani kusudi wawe na macho ya kizungu! Doh! Matokeo ni kuwa hao siyo watu tena bali na madoli.

Na kuhusu rangi ya ngozi, ni lazima niulize, je, umewahi kuona mshindi mweusi tii? Hao weusi wanaofanikiwa wengi ni weupe. Basi hao dada zetu wanajichibua na madawa ya ajabu. Ubaya ni kuwa usoni wanaonekana weupe lakini miili yao bado rangi yao ya asili. Mwisho wanakuwa na rangi mbili. Halafu wengine baadaye wanajikuta wana kansa ya ngozi shauri ya dawa hizo za kujichibua.

Ubaya ni kuwa kama nchi ya kiafrika inataka kushinda mashindano kama Miss World, Miss Universe ni lazima mtu wao awe Mdoli wa kizungu. Mfano, miaka mingi Nigeria walikuwa wanapeleka mrembo wao ambaye alikuwa mrembo Nigeria lakini mbaya kwa wazungu. Mwaka 2001, waliamua kumpeleka Mdoli wa kizungu, yaani dada fulani, mwembamba, futi sita na kashinda. Na tazama kesi ya aliyeshinda Miss Universe 1996, Miss Venezuela, Bi Alicia Machado…baada ya kashinda, alinenepa kweli! Yaani aliongezeka kama kilo 20! Basi majaji wakasema watamvua taji lake kama hatapungua! Dada wa watu alilia na kusema kachoka kashinda njaa!

Na tuanganlie hatima ya hao wanaoabudu hiyo standard ya kizungu na kuwa wembamba. Wanapambana na magonjwa kama Osteoperosis, yaani ugonjwa wa mifupa kuvunjika kwa urahisi, utapialmlo, na magonjwa wa akili. Ndiyo, mtu ambaye kila saa anawaza kujikondesha na kuwa hatapendwa kama si mwembamba ana ugonjwa wa akili. Je, madaktari huko Tanzania wako tayari kutibu hayo magonjwa wa kisasa?

Mashindano ya U-Miss yataendelea kuwepo, na dada zetu wataendelea kutaka kushindana na kufanana na madoli wa kizungu. Bahati mbaya ndo dunia ya leo. Lakini napendekeza tuwe na mashindano ya Miss Bantu, Miss Tanzania asili pia. Mashindano hayo yawe na nia ya kusifia uzuri asili wa mwanamke wa kiafrika. Tusisahau tulikotoka. Na hao wazungu wakiona tunajipenda basi wao wataanza kuheshimu maadili zetu.