Sunday, April 29, 2007

Clip from Bongoland film - Original - Juma and Mukulu

Juma on a date from the original movie Bongoland. See www.kibirafilms.com

Kwa wapenzi wa Bongoland, tazameni scene ya Juma kuonja uchungu wa maisha Marekeni!

Saturday, April 28, 2007

Watalii waharibu Mbuga za Wanyama

(UTANI)

Jamani, jamani, jamani. Inasemekana mtalii kutoka USA alienda kwenye mbuga ya wanyama na backpack mgongoni. Alikuwa kwenye land rover na watalii wengine. Sasa walivyoona simba, waliingiwa na kiwewe na backpack ikaburuzwa kwenye chuma fulani kwenye land rover yao. Kwa bahati mbaya chupa ya shampoo ilianguka mbugani. Shauri ya woga ya kuliwa na hao simba, waliamua kuacha chupa pale pale ilipoanguka.

Watalii waliondoka na gari yao. Sasa simba na utundu wake kaona hiyo chupa, kaanza kulamba lamba maana ilikuwa na ladha ya nazi. Mwisho kaipasua na kulamba shampoo yote. Baada ya wiki moja watalii walirudi na kuona huyo simba wa kiafrika kawa simba wa kizungu (pichani)!

Thursday, April 26, 2007

Muungano

Tanzania Flag (above)
Zanzibar Flag (above)
Tanganyika Flag (above)Miaka 43 iliyopita, siku ya leo, marehemu Mwalimu Nyerere alichanganya udongo kutoka Tanganyika na udongo kutoka Zanzibar kama ishara ya Muungano wa nchi hizo mbili. Nchi iliyounganishwa ukaitwa Jamhuri ya Muungano wa TANZANIA (United Republic of Tanzania).

Kama wewe ni Mzanzibar au Mtanganyika wewe ni MTANZANIA! WaTanzania tunajivunia kwani sisi ni mfano mzuri kwa waafrika wenzetu na dunia.

WaTanzania tumepitia mengi lakini bado tuna Muungano wetu.

Mungu alinde Muungano wetu. Tuendelee kukaa kwa amani. Mungu Ibariki Tanzania!


***************************************************************************
Wafungwa wasemehewa!

Ni mila ya marais kusamehe baadhi ya wafungwa siku ya leo. Taarifa zinasema kuwa Rais Jakaya Kikwete amesamehe wafungwa 4,022.

Katika kuadhimisha miaka 43 ya Muungano, Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,022. Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi leo imesema waliofaidika na msamaha huo ni pamoja na wale wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano ambao hadi jana walikuwa wameshatumikia robo ya kifungo chao.

Kwa habari zaidi nenda: http://www.ippmedia.com/ipp/alasiri/2007/04/26/89258.html

Wednesday, April 25, 2007

Konyagi


Hata Boston, tunakunywa Konyagi! Ni pombe ya aina ya pekee duniani na waTanzania tunaweza kujivunia kuwa na sisi tuna kikali chetu! Inatengenezwa na Tanzania Distillers.

Jana niliamua kustarehe kidogo na kikali. Huwa napenda wine, au bia baridi! Lakini jana nilipata hamu ya Konyagi! Nilivyoenda Bongo mwaka jana nilirudi na kachupa ya Konyagi. Siku moja moja nikitaka kukumbuka 'home' nakunyawaga. Konyagi ni pombe enye ladha ya pekee. Halafu ni clear kuliko hata maji ya kunywa ya hapa Marekani.

Nashangaa haijanywa kinywaji kikuu ng'ambo kama vodka, najua unaweza kununua Uingereza lakini bado sijauona kwenye maduka ya pombe hapa USA. (Wasomaji mnishahishe kama nimekosea) Je, watengenzaji wamefanya international marketing?

Konyagi inatengenezwa na mabibo. Mnakumbuka tulivyokuwa tunaharibu nguo zetu na juisi ya mabibo. Doh! Pale UDSM, kati ya Hall 3 na Hall 2, kuna orchard kubwa kweli ya mikorosho. Tulikuwa tunashinda huko tuna chuma maikorosho, una kula ile bibo enye juisi kibao na korosho unatupa kwenye mfuko. Mfuko ukijaa unachukua kipande cha bati, halafu unatengeneza moto juu! Tia hizo korosho, na kaa mbali maana moshi huo! Nyie korosho zile za kuchuma na kuchoma wenyewe ni tamu.

Basi niwape story. Mara yangu ya kwanza kunywa Konyagi nilikuwa JKT. CO (Commanding Officer) alikuja Officer's Mess na kunipa offa. Nilmshukuru lakini ilibidi nikatae maana nilikuwa sijaozea kunywa pombe.

OHOOO! Si jamaa kanipa amri sijui adhabu ninywe nusu glass straight mbele yake! Niliinywa kama sumu, baada ya hapo nikaenda bweneni kulala hadi asubuhi huko tumbo na kichwa kinaumwa!

Lakini Konyagi kwa kiasi si mbaya hasa ukichanganywa na soda. Msinywe sana maana inalewesha haraka!

Konyagi JUU!

Tuesday, April 24, 2007

Nani atakuwa Juma?


Wikiendi hii huko Minneapolis walifanya auditions kwa ajili ya kumpata atakayeigiza mhusika mkuu kwenye sinema ya Bongoland 2, Juma. Bongoland 2, ni sinema itakayapigwa Tanzania, mwezi Julai. Ni sehemu ya pili ya sinema ile ya Bongoland.
Pictured Front row: Director Josiah Kibira, na auditioners, Honest, Peter & Deus.
Kwa habari na picha zaidi someni :

Monday, April 23, 2007

Maoni ya Wasomaji kuhusu Mgomo wa wanafunzi UDSM

Expelled UDSM students - pic from Michuzi blog

Nimeamua kubandika maoni machache niliopata kwenye blogu kuhusu mgomo wa wanafunzi wa UDSM. Karibuni mtoe maoni yenu.
Na sasa kuna habari kuwa wanalegeza masharti ya wanafunzi kurejea Chuoni. Kwa habari zaidi someni:
**********************************************************************************

Kithuku said...

Hili suala la kugoma kila mara tena kwa sababu zisizo na mantiki tumechoshwa nalo kabisa. Watu wenye matatizo Tanzania ni wengi tu, sio wanafunzi peke yao. Pesa zinazotolewa za huduma za jamii zinapaswa ziwafaidishe wote, si wanafunzi peke yao. Kwa nini wang'ang'anie 100% sponsorship bila kuwafikiria watanzania wengine wanaohitaji fedha hizohizo? Mbona wagonjwa mahospitalini wanachangia gharama za huduma za afya, wao nani atawasaidia kugoma ili watibiwe bure 100%? Kuna matatizo ya njaa, barabara, nishati, makazi, usalama, n.k, yote yanahitaji fedha. Mbona hawa vijana wanakosa uzalendo? Na hata hivyo serikali ilikwisha waahidi wawe na subira, hatua zinapangwa kuboresha hali iliyopo.

Kwa maoni yangu, vijana hawa wamekosa hekima na tena hawana adabu. Huwezi kumlazimisha anayekukopesha akukopeshe hela yote unayohitaji. Kopa kiasi kwake, nyingine jazia kutoka kwa mkopeshaji mwingine au kutoka vyanzo vyako vingine vya mapato. Na la zaidi, ni ukosefu wa nidhamu uliokithiri kumpa Rais wa Nchi ultimatum, ati atoe majibu ndani ya siku mbili! Wewe ni nani? Rais wetu yuko kushughulikia matatizo ya wanafunzi tu? Au hilo lilikuwa na dharura gani hadi likashindikana kusubiri?

Huu ni ulevi wa madaraka ya kitoto, mtu anachaguliwa kuwa rais wa wanafunzi, nafasi ya mwaka 1 tu, basi anajiona naye ni Rais kama Mh Kikwete, anaweza kumtishia hata Rais wa Nchi! Anampa ultimatum! Uchuro kabisa huu! Rais wa wanafunzi ni mwanafunzi, na urais huo unakoma anapokoma uanafunzi. Waelewe hivyo. Waache kuyumbishana wanafunzi kwa kutumia vyeo feki hivyo na kudanganyana ati "solidarity", hakuna solidarity hapo wakati huna cheti! Subiri upate cheti (degree) ndipo utaweza kumsumbua mwajiri wako kwa masharti kwa sababu atakuwa anahitaji utaalam wako. Sasa hivi huna utaalamu wowote unabwabwaja ati "solidarity"! Utaula wa chuya kwa uvivu wa kuchagua!

Nashauri UDSM wachambue vizuri wale waliosababisha fracas hii wapewe adhabu ya kukomesha kabisa. Wakomolewe kabisa hao, wala siwatetei ng'o! Uongozi uwe tu makini wasije wakaumiza wale wasio na hatia.

Kuhusu haya masharti mapya mie naona safi sana, kwanza wameyataka wenyewe hao wanafunzi. Nasema University ikaze uzi, masharti ndio hayo, naunga mkono kabisa na naomba serikali isimamie hilo. Hakuna jipya hapo, kwani hata wagonjwa hospitalini wanalipia gharama, sembuse hao wazima kabisa! Walipe hizo hela. Kama kweli yupo asiyeweza kulipa, abaki kwanza nyumbani tuone wangapi wanaweza tuendelee nao kwa kipindi hiki, tena itasaidia kupunguza fujo. Hao watakaoshindwa kabisa watafutiwe mpango wa kuwasaidia (mfano kama kampeni za michango mbalimbali n.k) na fedha zikishapatikana ndipo waitwe chuoni. Hata watoto wanaopelekwa kutibiwa India, ni fedha zinachangwa kwanza zikishatosha ndipo wanapelekwa. Tufanye hivyo kwenye elimu pia. Pesa mbele, hakuna huduma inayoweza kupatikana bila fedha.
Nasema tu poleni sana lakini mmevuna mlichopanda.
4:52 AM

*************************************************************************************
Maricha said...

Da Chemi,

Hakuna mahala ambapo kuna kazi za kumwaga, hata wale walio soma nje wanalijua hilo. Wanasoma by day na kufanya kazi za ajabu ajabu by nite.

Tumefanya kazi za kubeba mabox, kazi za kuosha vibibi, kazi za kuanmgalila taahira, kazi za kuosha vyomba nk ili mradi hela ya rent na shule ipatikane.

Hawa vijana wakiwa creative wanaweza kufanya kazi, hakuna kazi itayoenda kuwatafuta, hakuna! itabidi wao ndio wazitafute kazi. Nitatoa mifano ya kazi wanazoweza kuzifanya.

1) Wanaweza kuanzisha migahwa ya chakula ya kwao wenyewe. Kama watu wanasoma masomo ya biashara ni kwanini wasianze kupractice? Akina mama ntilie wanatengeza hela ya kutosha wao wanawaangalia tu kazi kugoma kila kukicha.

2) pia wanaweza kufanya kazi kama baa tenda. Inasound vibaya mwanafunzi kuw abaa medi lakini kazi ni kazi.

3) wanaweza kufanya kazi za ukarani na utalishi. Makampuni kibao yanahitaji watu wanaoongea inglish sasa wao si ni wasomi bana kwanini wasichukue kazi izo?

TATIZO
Tatizo nilionalo mimi ni Scheduling, jinsi vyuo vya kwetu vinavyopanga ratiba ni vigumu sana kwa mtu kufanya kazi na kusoma. manake utakuta masomo ni kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa 12 jioni.

Ni nini cha kufanya? Mimi naona Chuo kiamriwe na serikali au owner wake ili kiwe na flexible ya scheduling ya ratiba ya madarsa.

La pili ni lazima masomo yapewe credit ili wanafuinzi wachukue lodi wanayoweza na kwa gharama wanayoweza kuimudu.

NaLa tatu ni vyema chuo kikaanzisha Payment plan ya namna fulani ivi. Yaani hata kama unadaiwa laki nane ni vyema wakuruhusu kuendelea na shule huku ukilipa leo shiling elfu kumi kesho laki cha msingi by the end of the semester wanafunzi wawe wamelipa hela yote.
9:34 PM

Saturday, April 21, 2007

Miss America wa mwaka 1944 afanya tendo la kishujaa mwaka 2007!


Waliomsahau mshindi wa mashindano ya urembo Marekani, Miss America, wa 1944, watamkumbuka na wasiomjua, sasa watamjua.
Bi Venus Ramsey ana miaka 82 sasa. Wakati wa ushindi wake ulikuwa wakati wa vita kuu vya dunia ya pili.

Juzi alivamiwa nyumbani kwake kwenye shamba huko Kentucky. Mwizi alijaribu kuwmibia vifaa vyake vya kulimia shamba. Kwa kutumia 'walker' aliweza kusimama imara na kufyatua risasi na kulipua matairi ya gari ya huyo mwizi.
Kwa habari zaidi ya hiyo tukio someni:


Poleni Wanafunzi wa UDSM lakini....

Students trying to Leave UDSM Main Campus
Ofiice Notice about UDSM Closing
Wanafunzi wa Uuniversity of Dar es Salaam (UDSM), waliofukuzwa majuzi wataruhusiwa kurudi Chuoni lakini kwa masharti:

From Michuzi Blog:

" Taarifa za redio mbao zilizonifikia punde ni kwamba wanafunzi wa udsm waliofukuzwa juzi kwa kugoma kuingia darasani wametakiwa waandike barua ya kujieleza ikiwa imeambatanishwa na 100,000/- ya matibabu pamoja na ada asilimia 40 (kama laki nane hivi) kupitia benki na wawe wamezipeleka barua na risiti za malipo hayo ya benki kwa makamu mkuu wa chuo kati ya aprili 23 hadi mei 4 ili kuweza kufikiriwa kurudi chuo. nafanya juhudi kupata waraka kamili wa masharti yote. "


Nimesoma kwenye ippmedia.com, kuwa wanafunzi waliofukuzwa na wasio na familia DSM, wameishia kuuza vitu vyao kama simu na TV ili wapate hela ya chakula na nauli ya kurudi makwao. Wanasema kuwa wasichana 'wanajiuza' ili wapate mahitaji yao. Ama kweli hali inasikitisha.

Nani aliwachochochea wagome? Je, wako wapi? Nikikumbuka miaka ya nyuma na migomo mingine anayeumia ni mtoto wa mkulima, au mtoto aliyetoka kwenye familia enye kipato kidogo. Watoto wanaotoka familia zinazojiweza wanapelekwa 'abroad' kumaliza masomo yao.

Kuhusu eti zamani watu walisoma bure, lazima niseme si kweli. Kumbuka kuwa kulikuwa na JKT, ilikuwa njia moja ya 'kutoa shukurani' kwa serikali kukusomesha. Pia ilikuwa ukianza kazi unatakwa mshahara kwa muda fulani. Kwa kweli ilikuwa si bure. Pia enzi zile wasomi walikuwa wachache. Je wakiamua kurudisha ule utaratibu wa kusomesha mamia kwa mwaka badala ya maelfu hali itakuaje?

Ni mwaka 2007, na siyo miaka ya 1960's au 1970's na hata 1980's. Na wajue maisha ni magumu duniani pote. Hata hapa USA kama huna full scholarship utafanya kazi mbili tatu, huko unasoma ili kuweza kumudu fees. Wenye wazazi wanaoweza kuwalipia 'full' ni wachache sana ukilinganisha na idadi ya wanafunzi. Wanafunzi wengi wanasoma kwa mchanganyo wa mikopo, grants, scholarships na kazi.

Na kumbuka enzi zile wengi walipelekwa Eastern bloc, yaani Urusi, Poland, Bulgaria, East Germany, Yugoslavia etc. kusoma bure lakini hakuna tena. Dunia umebadilika.

REMEMBER LIFE IS NOT EASY.

Thursday, April 19, 2007

Kibira Films bado wanamtafuta 'Juma'!

Bado actor anatafutwa kwa ajili ya kuigiza kama mhusika mkuu wa sinema ya Bongoland 2!

WHERE IN THE WORLD IS JUMA.....

We cannot find him and this is why this weekend on Saturday April 21, 2007 we are conducting a screen test.A screen test of the would be Juma - the lead actor for the movie...Bongoland II. If you are game and think you can act here is the venue...Holy Trinity Lutheran Church in Minneapolis - the address is 27 EAST 31st Street.

The screen test will start at 10:00 AM. Please check our site for the updates on the outcome.


Kwa habari zaidi bonyeza hapa: BONGOLAND 2

Kwaheri Sanjaya!

American Idol Judges Randy Jackson, Simon Cowell, & Paula Abdul

Kwa wapenzi wa American Idol naomba maoni yenu. Huyu kijana Sanjaya aliwezaje kukaa kwenye American Idol kwa muda wote huo? Jana alivyotolewa nilibakia nashabikia kwa furaha maana hakustahili kufika hadi kuwa namba 7 kati ya waimbaji kumi na wawili bora.

Sanjaya ni shombe wa kihindi kutoka Washington State. Ana miaka 17. Mama yake ni mzungu na baba yake ni mhindi. Ana nywele nyingi nyeusi, na sauti yake ni ndogo na ya kike kike kama ya Michael Jackson. Anaweza kuimba nyimbo za stevie wonder vizuri. Akiimba wasichana wadogo wadogo wanaanza kulia shauri ya kuingiliwa na kiwewe fulani. Watu wanasema baba yake kamfanyia dawa za kihindi maana hana sauti ya kuwa American Idol.

Watu kama Howard Stern na wengine wenye chuki walifanya kampeni za kupata watu wa kumpigia kura ili ashinde. Mungu ni mwema na wameshindwa! Sanjaya katoka jana kwa majonzi. Alivyoambiwa ndo siku yake ya mwisho, alibakia analia kama mtoto mdogo.
Kitu kilichowafanya wasichana wadogo wadogo wampende ni, kutabasamu kwake, nywele nyingi (kila wiki alibadilisha staili ya nywele), na eti ana sura nzuri yaani handsome. Lakini kuimba hawezi. Watu waliokuwa wanaimba vizuri kama Stephanie Edwards, Brandon na Gina Glocksen walitolewa kabla yake.

Picha aliyepiga dada yake, Shyamali, akiwa uchi huko anapiga gitaa ilimsaidia pia. Shyamali aliwahi kufanya kazi kwenye restaurant ya Hooters. Alitolewa zamani wakati walivyobakia waimbaji 48.
Bora hakushinda maana kuendelea kuwepo kwake ungehatarisha maisha yake, maana nchi hii kuna vichaa. Angepigwa risasi na mtu mwenye chuki eti kawa nini Sanjaya anaharibu show.

Na leo naamini kuwa producers wa American Idol wanapumua vizuri. Maana Sanjaya angeshinda ingekuwa mwisho wa American Idol maana ushindi wake ungehibitisha kuwa American idol siyo kamchagua anayejua kuimba, bali anayependwa na watu.

Lakini huo si mwisho wa Sanjaya. Kwa vile kapendwa sana lazima tutamwona kwenye matangazo ya TV, au akiigiza kwenye sinema za mateenager.

Wednesday, April 18, 2007

Mauji Chuo Kikuu cha Virginia Tech


Sura ya Muaji Cho Seung-Hui

Poleni waKorea wote. Sasa asante Cho Seung-Hui, itakuwa vigumu wapate visa za kuja kusoma Marekani bila kuchambuliwa kila kitu toka walichofanya toka wazaliwe mpaka wanakunya saa ngapi.

WaMarekani waoga sana na wabaguzi sana na sasa wamepata kisingizio cha kunyanyasa waKorea wote Marekani. Msisahau kabla ya 9/11 jinsi waarabu walivyokuwa wanathaminiwa Marekani shauri ya pesa zao.

Kama hamjasikia, vituko na visa vya kijana, Cho Seung-Hui, mwenye miaka 23, na mwanafunzi aliyekuwa anasoma Chuo Kikuu cha Virginia Tech nitawasimulia kwa ufupi. Siku ya jumatatu akili zilimruka na aliua wanafunzi na walimu wa chuoni hapo. Watu 32, walioamka na kufanya shughuli zao kama kawaida siku hiyo walipoteza maisha yao.

Cha ajabu, watu walijua kuwa huyo jamaa ni mwendawazimu siku nyingi. Hata mwalimu wake alienda polisi kumshitaki kuwa ana wasiwasi naye. Lakini polisi hawakufanya kitu.
Na wote tunajua mweusi angekuwa na vituko kama vyake, angefukuzwa shule zamani. Cho alikuwa anadika michezo ya kuigiza na mashairi zenye plots za kutisha kama kubaka, kuua, na kujiua.

Nani asiyejue kuwa waMarekani wanasema kuwa hao wenye asili ya Asia wana akili sana. Na si ajabu ndo maana huyo Bwana John Markell, alimwuzia bastola bila maswali mengi. Alisema, “he looked like a clean cut College student”, yaani alionekana hana matatizo. Je, kijana mweusi anayesoma Chuo Kikuu angeweza kununua bastola kwenye duka lake kwa urahisi hivyo? Na leo asubuhi nilikuwa nabishana na bosi wangu kuhusu hiyo swala, nikamwambia, huyo Markell asingeniuzia mimi mwanamke mweusi hiyo bastola, lazima angetafuta kisingizio cha kutokuniuzia maana sionekani kama clean cut college student au clean cut period.

Kati ya hao waliouliwa siku ya jumatatu kulikuwa na weusi kadhaa. Mmoja ni Ryan Clark, aliyekuwa na akili sana na kusoma Major tatu (haya nyie wazungu mnaosema kuwa weusi hawana akili). http://www.wrdw.com/news/headlines/7071667.html

Na jambo lingine kinachoniudhi. Wansema kuwa haya ndo mauaji makuu yaliyowahi kutokea nchini Marekani. Wamekosea, au wansema hivyo kwa vile weusi siyo watu kwao. Miaka ya nyuma huko Florida (1923) walikuwa mamia ya weusi, na mauaji ya weusi yalitokea Arkansas (1919) na Oklahoma (1921) pia.

Karibuni mtoe maoni yenu.

Saturday, April 14, 2007

Marudio - Acheni Ushamba

Hii ni kati ya posts zangu za mwanzo:

Tuesday, October 18, 2005

Acheni Ushamba! Jamani, jamani, jamani! Siku hizi nikiona vijana waBongo hapa mitaani Boston nakimbia! Hao vijana siyo wale wa miaka ya nyuma waliokuwa tayari kufanya kazi mbili/tatu ili waweze kuishi vizuri na kupeleka zawadi nyumbani. Hapana vijana wa siku hizi wanataka vya dezo!

Wamekuja Marekani wakidhania maisha USA ni kama vile kwenye video za Rap. Hapana vijana, maisha siyo hivyo kabisa. Hapa USA kama hukuja na hela zako basi uwe tayari kuchapa hizo kazi mbili/tatu, utafanikiwa! Lakini kinacho niudhi hasa ni hao vijana wanaoenda madukani na kuiba, yaani shoplifting! Yaani mtu anaingia dukani anasomba vitu, tia ma-cap kichwani halafu wanatoka nje ya duka. Wanakamatwa halafu unaombwa uwawekee dhamana! Si waliiba wao wacha wakome huko jela! Tena jela za Boston ni nzuri kuliko kupelekwa Keko! Nasema hao vijana ni washamba maana ukiwauliza kwa nini waliiba, watasema, “Oh, sikujua kama wananiona!” Hawakuoni???? Heh!

Mjue mkifika kwenye mall tena parking lot, mnaanza kuchgunguzwa na makamera yaliofichawa kila mahala isipokuwa chooni! Yale mapambo na magololi yanayoing’inia si urembo tu, bali ni masecurity camera. Hivyo huwezi kusema, “Oh sikuiba!” huko store detective anakutolea kanda ya video ambacho wewe ndo star!

Wanaona kwa vile mlango huko wazi hakuna security, au watu wengi basi ni free for all. Kitu kingine hao vijana,utasikia wanaongea, sijui vitu gani, wakidhania English! Wanajaribu kuiga ma-slang wanaosikia kwenye movies. Nyie! Watu hawaongei hivyo!

Ukitaka kazi ya maana ujfinze kuongea English! Yaani inatisha maana huwezi hata kuelewa ansemaje na Slang zake zenye Bongo accent! Na acheni kuvaa kama gangsta! Kwanza ukikosea rangi utapigwa risasi na ma-gang au utasumbuliwa na polisi wakidhania wewe ni gang banga!

Na poleni vijana ambao wanashuka kwenye ndege wakidhania wanaenda kuishi kwenye nyumba inayofanana na ya P. Diddy, lakini wanakuta wanaenda kubanana watu 10 kwenye chumba kimoja.

Na kuna wengine wanafanya uhalifu kama kuingia kwenye biashara haramu ili wapate pesa za haraka. Sijui ni kwa kuwa hawajui au hawajali,lakini wanhatarish maisha yao na za familia na marafiki zao!

Ngoja niishie hapa ...maana!

Bongoland 2


(Photos courtesy of Muhidini Michuzi)

Naona Kibira Films International inasonga mbele na maandalizi ya kupiga picha ya Bongoland 2, Tanzania mwezi Julai. Wasanii nchini Tanzania wanatoka kwa wingi kujaribu kupata nafasi ya kuigiza katika hiyo sinema. Katika picha za juu, ni baadhi ya wasanii waliotokea kwenye Casting Call.
Sinema itakuwa sehemu ya pili kuhusu maisha ya Juma Pondamali, ambaye katika sinema ya Bongoland, alishindwa na maisha ya Marekani. Hatimaye aliamua kurudi zake Tanzania, tena baada ya waBongo wenzake kumchangia nauli ya tiketi. Je, alivyorudi maisha yake yalikuaje?
Kibira Films, inaongozwa na Bwana Josiah Kibira, wa Minneapolis, Minnesota. Kampuni hiyo ilitengenza sinema ya Tusamehe. Mimi naigiza katika sinema hiyo kama Mama Kurusumu.

Wednesday, April 11, 2007

Sinema ya ROOTS
Tangu jumapili TVOne, wamekuwa wakionyesha sinema kabambe ya ROOTS. Hiyo sinema ilionyeshwa kwa mara ya kwanza mwaka 1977 na kuingia katika vitabu vya historia kwa watazamaji wengi. Zaidi ya watu 130 milioni nchini Marekani walitazama.

Nasifia sana hiyo sinema maana inakumbusha watu na hasa waMarekani weusi kuwa wametoka mbali. Inaonyesha kuwa waafrika walikuwa na utamaduni na mzungu alijaribu kuifuta kwa kuzuia watumwa kutoongea lugha zao, kuchukua majina ya kizungu, na walizuiliwa kufanya kitu chochote cha kiaafrika. Katika Roots unamsikia binti Fanta, akisema mimi nimesahau kila kitu cha Afrika, nia yangu niishi. Na utasikia watumwa waliozaliwa Marekani wanavyowakashifu watumwa waliotoka Afrika. Watumwa wanajiona bora kuliko wale waafrika.
Roots ilitungwa na marehemu Alex Haley. Inahusu historia ya familia yake na inaanzia kijiji huko Gambia, na kuzaliwa kwa Kunta Kinte. Kunta anakamtawa na kuletwa Marekani. Ukiona walivyokuwa wanasafirisha weusi utalia. Huko nakumbuka dada moja mmarekani mweusi kaniambia eti kafurahi kuwa mababu zake waliletwa kama watumwa kutoka Marekani maana ana maisha bora na hashindi njaa. Pia inasikitisha ukiona Kunta Kitne kafungwa cheni shingoni na wanam-pat kichwani kama mbwa!
Huko mashuleni Marekani ni lazima vijana watazame sinema ya Schindler's List kusudi waelewe wayehudi walivyouliwa na Hitler wakati wa vita kuu ya pili ya dunia. Sasa kwa nini isiwe lazima watazame ROOTS kusudi waelewe history ya mwafrika Marekani na mateso waliopata.
Ukitazama Roots, pia utaweza kuelewa vizuri zaidi matatizo yanayowakabili wamarekani weusi kwa sasa. Matatizo mengi yanatokana na historia yao ya utumwa. Na kwa maoni yangu wengi bado wana mawazo ya kitumwa.
Leo wataonyesha tena TVone sehemu ya nne. Itatoka kwenye DVD May 22.
Karibuni mtoe maoni yenu.

Tuesday, April 10, 2007

Awatukana eti ni Malaya wenye nywele za kipilipili!

Captain wa Timu ya Rutgers, Essence Carson, akiongea na waandishi wa habari leo 4/10/07.

Mbaguzi Don Imus

Ubaguzi hauishi Marekani. Wiki iliyopita kuna huyo mtangazaji maarufu wa Marekani, Donald Imus, kasema eti wasichana wanaocheza basketball kwenye timu ya Chuo Kikuu cha Rutgers ni nappy headed hos (malaya wenye nywele za kipilipili). Alikuwa anaongea na meneja wake kwenye hicho kipindi na walizidi kusema wamejaa matatoo na pia wamekaa kidumedume. Kisa timu ya Chuo Kikuu cha Tennessee iliwashinda katika mashindano ya Basketball ya wanawake.

Mazungumzo enyewe ni hayo:

Imus started the firestorm after the Rutgers team, which includes eight black women, lost the NCAA women's championship game to Tennessee. He was speaking with producer Bernard McGuirk and said "that's some rough girls from Rutgers. Man, they got tattoos . . ."

"Some hardcore hos," McGuirk said.

"That's some nappy-headed hos there, I'm going to tell you that," Imus said.
Pia walisema kuwa eti hiyo timu ya Rutgers inafanana na timu wa wanaume ya NBA, The Toronto Raptors!"

Jana alikutana na Reverend Al Sharpton kuomba msamaha lakini Sharpton alikasirika baada ya Imus kusema, "You People!" (Nyinyi watu weusi). Na Reverend Jesse Jackson naye amekasirika ana anataka Imus afukuzwe kazi. Jackson kasema hiyo siyo 'Slip of the Lip' (Utelezi wa ulimi).

Lakini kwa hapa Marekani kusema kuwa mtu mweusi ana nywele za kipilipili ni tusi kubwa mno! Hii inatokana na asili ya utumwa Marekani. Pia nywele za kilipili inahusishswa na watu wesui hasa weusi tii. Na kama unataka kuelewa kwe undani zaidi ni kuwa hapa USA, unavyozidi kwa weusi ndo unavyoshushwa kwenye hadhi ya ubinadamu. Insikitisha! Weusi wenyewe wanadharau weusi na hasa weusi tii. Unasikia, "You Too black" yaani wewe ni mweusi mno. Ama kweli Imus, kachokoza watu.

Haya mambo ya nywele ni mjadala mkubwa maana utasikia weusi wanasema, yulekichwa chake kimejaa 'naps' (Kipilipili), na yule ana good hair (nywele nzuri), zimekaa kizunguzungu. Biashara ya ku-perm na ku-relz nywele kusudi zinyoke kama mzungu imeshamiri duniani. Hata Bongo watu hawaridhiki na nywele waliozaliwa nayo, unatukuta watu wanakimbilia saluni kupata 'relaxer'.

Na huyo Captain wa timu leo kaonekana na nywele ambazo zimetiwa Relaxer! Zimenyoka kabisa. Ningemheshimu zaidi kama angetoka na Afro. Ni kama vile wanaona haya kuwa na nywele za kiafrika.

Tangu enzi za utumwa hapa Marekani wanasema kama una hata tone moja ya damu nyeusi basi wewe ni mweusi. Unakuta watu ambao ungedhania ni wazungu lakini la, ni weusi! Na kama umetazama ile sinema ya School Daze ya Spike Lee, utaona mgogoro kati ya wanafunzi weusi. Weupe wanajiona bora kuliko wale ambao ni weusi zaidi.

Haya sasa Imus amesimamishwa kutangaza redioni kwa kipindi cha wiki mbili. Watu wanataka afukuzwe maana wanasema kuwa si mara yake ya kwanza kuongea mambo ya kibaguzi. Siku zijazo tutasikia hii 'issue' inaishia wapi.

Kwa habari zaidi mnaweza kusoma hii tukio:Tuesday, April 03, 2007

TAMWA

Bila shaka mmesikia majina kama Fatma Alloo, Leila Sheikh, Edda Sanga, Maria Shaba, Pili Mtambalike, Wema Kalokola (marehemu), na Ananilea Nkya. Hao ni kati ya waanzalishi wa chama cha waandishi wa habari wanawake nchini Tanzania, TAMWA. Na mimi ni mmoja wa waanzalishi wa TAMWA (Tanzania Media Women's Association).

Tulitoka mbali maana mwanzoni tulipata pingamizi nyingi kutoka kwa wanawake na wanaume. Tulitukanwa na kuitwa majina ya ajabu kama, 'frustrated women, na malesbo'. Hivi sasa wanaume wakisikia jina la TAMWA wanatetemeka. TAMWA imefanya mengi kutetea haki za akina mama nchini Tanzania na inaendelea kwa nguvu! Tulianzisha kwa ajili ya kusaidia akina mama waliokuwa waandishi wa habari lakini ilikuwa mpaka kutetetea haki za akina mama Tanzania.

TAMWA Oyee!

Hii picha ilipigwa mwaka 1992. Tulikuwa kwenye safari Zanzibar na wageni wetu kutoka vyama vya akina mama mbalimbali barani Afrika. Mimi niko kushoto kabisa na miwani! Pia wamo Edda Sanga (3rd from left, Maria Shaba 5th from left, Halima Shariff 2nd from right). Wengine ni wageni kutoka nje.
Ndo baada ya hii safari iliyofana ilitokea kasheshe kubwa kutokana na picha fulani aliyopiga Muhidini Michuzi, na kuwekwa kwenye front page ya gazeti ya Daily News mpaka ilibidi viongozi wa TAMWA warudi Zanzibar kuomba radhi. Picha eneyewe ilipigwa kwenye shughuli ya mpendwa somo na kungwi mkuu wa Tanzania, Bi Kidude.
Kwa habari zaidi kuhusu TAMWA someni:

Afungwa Marekani kwa kutokuvaa Mask! Anaumwa Kifua Kikuu!


Jamani, leo nimeshutushwa na habari ya Mrusi kufungwa jela tangu mwezi Julai mwaka jana kwa ajili ya kutokuvaa mask hadharani. Jamaa amefungwa huko Pheonix, Arizona. Anaitwa Robert Daniels, na ana miaka 27. Anaumwa ugonjwa hatari wa kifua kikuu (Tuberculosis au TB). Kisa cha kumfunga ni kuwa anaumwa aina ya TB inaitwa XDR-TB. Wanasema kuwa ni drug resistant na haitibiki.

Mahakama ya huko Phoenix, inasema kuwa ilibidi Daniels afungwe kwe vile akikataa kuvaa mask (kizuio kwenye mdomo na pua), akitoka nje na kuwa na watu wengine. Walisema kuwa ana nia mbaya ya kutaka kuambukiza watu huo ugonjwa wa TB kwa maksudi.

Habari zinasema kuwa haijulikani atafungwa mpaka lini na huenda atafungwa mpaka anafia huko jela. Baada ya kusoma hivyo nikasema ni kweli wana haki ya kumfunga hasa kama hiyo TB haina tiba. Wakubwa wanasema kuwa kama watu wengine watapatikana na huo ugonjwa itabidi nao wafungwe.

Wataalam wa afya wanasema kuwa kama mtu anaumwa HIVAIDS (UKIMWI) na akipata huo ugonjwa atakufa siku 25 tu, baada ya kuambukizwa. DUH!

Na walivyo na woga na huo ugonjwa jamaa haruhusiwi kuoga kwenye shower. Anatumia wipes (vifutio). Hana TV, simu wala redio. Anasema kuwa maisha yake huko jela ni mabaya kuliko ya mtu alifungwa kwa kosa la jinai.

Chumba chake kina ventilation ya peke yake na filters za chumba zinachomwa moto, na watu waliojifunika kama vile astronauts! Ama kweli waMarekani hawataki huo ugonjwa usambae na siwalaumu.

Mnasemaje wapendwa wasomaji?

Kwa habari zaidi ya kufungwa kwa Robert Daniels mnawaeza kusoma: