Tuesday, April 25, 2006

Miaka baada ya Tukio kaniomba Msamaha!

Nilipokuwa Jeshi ya Kujenga Taifa (JKT) karibu nibakwe na afande Fulani (jina nahifadhi). Lazima niseme kuwa katika kipindi hicho wanaume wengi waliona makambi ya JKT kama ‘buffet’ ya wasichana. Si maafande wa jeshi tu, bali hata viongozi wa serikali walikuwa wanapitia makambi ya JKT kula tani yao!

Mimi nilikuwa Masange JKT, Tabora. Wakati huo huyo jamaa alikuwa ni Kepiteni wa JKT. Nadhani alidhania kwa vile yeye ni kepiteni basi alikuwa na haki ya kutembea na yeyote aliyemtaka. Kwangu aligonga ukuta! Bila shaka alikuwa hajawahi ‘kunyimwa’ mpaka siku hiyo alipokutana na mimi.

Miaka baada ya tukio nikiwa nafanya kazi Daily News mara nyingi nilikuwa napishana naye Posta Mpya. Basi ananisemesha, na mimi namnunia halafu napita zangu kimya bila kumjibu kwa hasira. Siku moja kanisimamisha kaniambia, "Chemi, naomba msamaha, nisemahe tafadhali, kweli nilikukosea!” Aliongeza kuwa miaka mingi imepita hivyo sina sababu ya kuwa na hasira naye! Na mimi nilimjibu, “Mshenzi sana wewe!” nikaenda zangu.

Ikapita kama mwaka nyingine. Jamaa anaendelea kunisalimia kila nikimpita njiani na mimi kwa uchungu bado nikashindwa kusema kitu. Basi nikafikiria alichoniambia Posta Mpya. Lakini nilona kama jambo hilo linamsumbua. Na nikasema kama Bwana Yesu aliweza kusamehe watu kwa madhambi yao kwa nini mimi nisimsamehe. Basi baada ya hapo ikiwa nikimwona na akinisalimia naitika na naendelea zangu na nikaona kidogo hata yeye alikuwa na raha. Lakini bado najiuliza kama kitendo chake kilimsumbua miaka na miaka kama ilivyonisumbua mimi.

Unauliza ilikuaje mpaka nikajikuta kwenye situation ya kubakwa. Au mnasema nilitaka mwenyewe. Ngoja niwaelezee ilivyokuwa. Nilikuwa mhudumu Officer’s Mess, mpishi na msafishaji. Huyo jamaa alikuwa ni mgeni kutoka Makao Makuu ya JKT Dar es Salaam. Kwa kweli sikutaka kufanya kazi pale Mess lakini tulichaguliwa special na Matron, mimi kwa vile niijua kupika vyakula mbalimbali hasa za kizungu. Lakini uzuri wa hiyo kazi ni kuwa uanambulia mabaki ya vyakula (leftovers), na mara nyingine kulikuwa hakuna.

Basi huyo Afande alikaa kambini wiki kadhaa. Katika kumhudumia tukawa tunaongea na mimi nikawa namheshimu kama kaka vile. Wala sikusikia mapenzi yoyote kwake. Basi jioni fulani, kanialika chumbani kwake kunywa soda na biskuti na kwa Maongezi zaidi. Sasa kama ulienda jeshi unajua njaa kali unayokuwa nayo. Nikaenda, kanikaribisha vizuri, nilipewa soda na tukawa tunaongea. Basi nikaona mwenzangu anabadilika ghafla! Mara ananikumbatia kwa nguvu, na kunibusu na mengine. Nikajaribu kuaga lakini jamaa hakuniachia. Baada ya ku-plead naye aniachie, kaniachia. Kaomba msamaha na kaniomba niendelee kukaa nimalize hizo soda alizoninulia. Kama mjinga nikamwamini, nikakaa nakunywa hizo soda. Tukaendelea na Maongezi, kukaa kidogo huyo kanirukia, najaribu kusimama huyo, kanivuta na kuniangusha kitandani! Mimi saa hizo nikawa naogopa kabisa nia yake!

Kaniambia eti, “ukipiga makelele najua nitasema nini! Nyamaza! Huna sababu ya kunikatalia!” LOH! Kanizaba na kibao! Nikamwuliza kwa nini anaifanyia hivyo, na mimi nilikuwa namwona kama kaka yangu!

Hapo sasa ikaniingia. Nabakwa! Loh! Nilimpiga mangumi na mateke lakini jamaa alikuwa na nguvu huyo kachana chupi yangu! Baada ya hapo, jamaa kashika miguu yangu huko anafoka kwa sauti kama vile anatoa amri “panua miguu! PANUA MIGUU!” Huko katoa ume wake uliyosimama kwenye suruali! Basi kuona sipanui jamaa kaongeza makofi na kafanikiwa kupanua miguu yangu! Kuona kafanikiwa kupanua huyo kajaribu kupenya. Ilipogusa kwangu nilipiga kelele cha kufa! Nikasema, “Nakuufaaaa!” Heh! Ghafla jamaa kaniachia kaniambia niende. Alisema, “Nimeigusa na ume wangu, unatosha!” Nenda zako! Na ukimwambia mtu najua nitasema nini!”

Loh nilikimbia bwenini na giza lile la Masange huko nalia. Wenzangu wananiuliza vipi, nikashindwa niseme nini! Kwanza niliona haya! Fikiria, niliona haya (shame)!

Kesho yake nikaenda dispensary na kujiandikisha mgonjwa. Sikwenda kazini Officer's Mess bali nililala bwenini. Siku iliyofuatia huyo Afande mshenzi kapita bwenini kwetu kaulizia hali yangu, na mimi huko natetemeka kwa woga nikashindwa niseme nini. Alininunulia Orange squash na biskuti na kuzileta bwenini. Sitasahau alivyonitazama! Ilikuwa kama vile anapanga jinsi gani atanipata.

Baada ya hapo alimwopoa msichana mwingine na huyo alimkubali kabisa. Akawa analala kabisa huko Officer’s Mess. Hakuna anayemsumbua wakijua ni bibi wa Afisa. Basi, siku za yule jamaa kukaa kambini zikaisha, na yule binti alienda naye Tabora mjini kwa siku kadhaa. Halafu jamaa karudi zake DSM. Yule binti karudi zake kambini! Kumbe alienda bila pass. Alidhania kwa vile yuko na mkubwa hana haja ya pass. Na yule Afande ndo kaondoka kimoja! Maafande waliobakia wacha wamtese huyo binti alivyorudi kambini! Walimtesa kwa Extra drill na mengine mpaka ikabidi Military Police waombe wakuu wamsamehe la sivyo atakufa. Raha yake iliishia kwa suluba! Sijui yule binti alidhania jamaa atamwoa! Kwa nini alimkubali yule mshenzi. Anyway, kila mtu na vyake. Alivyotoka kwenye suluba tulimwuguza! Siku haizkupita na mimi nilitolewa kazi Officer’s Mess na kupelekwa kwenye kikosi cha Ujenzi na lazima nisema hapo nilifurahi sana.

Basi miaka ilipita. Mimi nilikuwa mwandishi wa habari Daily News, tena nilijenga jina. Sasa nikawa napishana na yule jamaa huko kapandishwa cheo na yuko JWTZ. Jamaa anajaribu kunisalimia na mimi napita zangu kimya, namnunia kabisa. Nilimwona mshenzi, mnyama, na kila kitu kibaya ndo ilikuwa yeye! Angefanikiwa kuingiza na kunimwagia uchafu wake ningejiona mchafu mpaka leo! Miaka kama 20 imepita sasa na bado nina uchungu naye.

Jamani nyie wanaume nawaambia kubaka kinaathari zake kwa wanawake. Unataka raha ya dakika na unamwachia mwenzio na uchungu wa maisha! Wengine mpaka wanakuwa wagonjwa wa akili.

Kwa nini nimeamua kuzungumzia kubakwa kwangu hapa, ni kwa sababu naona wasichana wengi wanabakwa, halafu wanaamua kunyamaza kimya. Kisa wakienda polisi na hospitali wanahofia kuambiwa ni Malaya au walitaka wenyewe! Hata mwamanke mwenzako anaweza kukufokea kuwa ulitaka mwenyewe.

Tanzania, wanaume walikuwa na usemi wao kuhusu wanawake na ngono. Walisema eti ukimwomba mwanamke halafu akijibu ndiyo, manake ndiyo atafanya. Akisema labda, manake atafanya, akisema hapana, manake hapana. Lakini jamani tendo si inakuwa tamu kama wote mmekubali? Na kama angefanikiwa kuingiza si angeniumiza sana!

Wengine wanasema ningemshitaki. Je, ningemshitaki ingekuaje? Kwanza jeshini mimi ningepewa Extra Drill mpaka niumie au kufungwa jela ya jeshi iliyojaa maji na mbu kusudi niteswe. Kumbuka ilikuwa Tanzania na yule alikuwa ni Kepiteni wakati huo na mimi nilikuwa Private. Hakuna ambaye angekuwa tayari kunisikia zaidi ya wenzangu maPrivate, na yeye alijua hivyo. SHENZI TAIPU!

Monday, April 10, 2006

Umeona Phat Girlz?





Kama hamjaenda kuona sinema mpya, Phat Girlz, nawashauri mkaione. Mchezaji mkuu wa hiyo sinema ni mwigizaji na mcheshi, Mo’nique. Nilienda kuiona wiki iliyopita na kwa kweli nilifurahi sana kuona hiyo sinema na hasa zile scene zilizohusu Afrika na mila za Nigeria. Sehemu ya picha ilipigwa Lagos, Nigeria. Hii sinema ilitungwa na kuwa directed na dada Nngest Likke ambaye ana asili ya Eithiopia.

Wahusika wakuu katika filamu hiyo ni Jazmin Biltmore, rafiki yake Stacey, ambaye naye ni menene kiasi, halafu binamu yake Jazmin, Mia. Huyo Mia ni mwembamba, hana matako na anajiona mzuri mno kwa vile yuko shepu hiyo ambayo Hollywood insema ni nzuri. Ila ku-maintain hiyo shepu anaishi kwa kula karoti, lettuce na maji tu.

Sinema inanza na Dada Jazmin akiwa ndotoni. Wanaume wazuri wazuri wanamtaka kimapenzi. Baadaye tunagundua kuwa ni siku nyingi tangu aonje penzi. Jazmin anatamani sana aweze kuvaa nguo saizi 5. Lakini kama alivyo anavaa saizi 20+. Ana kula vidonge vya kupunguza unene kama pipi lakini hazimsaidii. Anafanya kazi na rafiki yake Stacey kwenye duka la kuuza nguo, inaitwa Bloomfeld’s.
Basi wanalalamika kuhusu jinsi hakuna nguo nzuri dukani kwa ajili ya wanene. Nguo zenyewe ni mbaya mbaya, hazipendezi, au kumfanya aliyevaa apendeze. Na Jazmin ana kipaji cha Designing, na ndoto yake ni kuwa na line ya nguo zinazopendeza kwa ajili ya wanene.

Basi siku moja anaingia kwenye mashindano ya kupata safari kwenda kwenye Spa/Hotel Palm Springs. Kwa bahati nzuri Jazmin anashinda. Yeye, Stacey na Mia wanaenda kustarehe kwa wiki moja kwenye hiyo Spa. Kufika huko wanakuta kila kitu kiko kwa ajili ya wembamba, hata zile massage tables, na robes. Basi Jazmin akiingia kwenye Spa, hao wembamba wanatoka kuonyesha hasira na unene wake.

Wanaenda kwenye Bwawa la kuogelea. Basi Mia kavaa bikini yake anajiona kapendeza kweli kweli. Yuko karibu uchi na bikini enyewe ni kama lithong. Kuna baba mweusi anaogelea, na Mia anamtamani kweli kweli. Na yule baba anatazama tazama walipo akina Jazmin, basi Mia anadhania lazima anamtazama yeye kwa vile ndo mwembamba kati yao. Yule baba anatoka kwenye maji na kuelekea kwa akina Jazmin. Jamaa ni mzuri kweli halafu mwili wake fiti. Mia anajua kuwa anamfuata yeye, basi yule baba anawasalimia na anamw-ignore Mia. Hawezi kutoa macho yake kwa Jazmin. Jazmin mwenyewe anapumbazwa maana hawezi kuamini kinachotokea. Anakosa maneno ya kusema. Yule baba ni Dr. Tunde, na kumbe yuko Palm Springs na wenzake kutoka Nigeria kwa ajili ya Mkutano wa madaktari.

Marafiki wawili wanamfuata Tunde kwa akina dada hao. Hapo inachekesha maana wanaongea kikwao huko wakimgombania Stacey. Hakuna anayemtaka Mia kwa vile ni mwembamba mno. Wanamwita kibiriti. Jioni wote wanaenda kwenye party ya waNigeria na yule Daktari aliyemwambulia Mia anaona haya na kuwaambia waNigeria wenzake kuwa ni mgonjwa wake. Na yule ambaye amempata Stacey anamsifia, mpaka Stacey anaondoa haya aliokuwa nayo. Basi Stacey akishavua haya loh, anaelekea kama anajaribu kulipiza siku alizokaa bila kupata penzi.

Basi hiyo scene ya Party utafurahi, maana wanaonyesha vyakula vya KiNigeria. Ugali wao ndo 'fufu' kuna samaki ya kukaanga, nyama choma, mboga za majani. Party inafanana na Party tunazofanya za waBongo. Halafu kwenye scene hiyo wameweka ule wimbo wa Kasongo. Cheki Jazmin na Tunde wanavyocheza. Jazmin na Tunde wanakuja kupendana lakini Jazmin anakuwa na wasiwasi kuwa haiwezi kuwa kweli. Yeye anaamini kabisa kuwa mwanaume mzuri hawezi kumpenda kwa sababu ni mnene. Mpaka Jazmin anamwaidi Tunde kuwa atakuwa saizi 5. Tunde anampa ukweli anamwambia kuwa hata siku moja hata kuwa saizi 5 kwa hiyo akubali hivyo.

Basi Mambo yanaenda vizuri mpaka hapo Jazmin anapojidhalilisha akishikwa na wivu. Kwa haya, Jazmin anakimbia na wenzake wanarudi kwao. Jazmin anajifungia chumbani siku kadhaa na anakuwa kama kachanganikiwa akili. Lakini anaamka na kuanza kujiamini. Ndo hapo anafanikiwa kupata line ya Nguo za akina mama wanene inayoitwa Thick Madame na kutajirika. Lakini bado anammisi Tunde, ndo anapanda ndege na rafiki zake na wanakwenda Lagos kumtafuta.

Sitaki kusema zaidi maana nataka muone wenyewe. Kuna vichekesho vingi katika hii sinema, na pia uta huzunika na jinsi jamii ya Marekani inavyowafanya watu kutokujithamini kwa ajili ya unene. Hii sinema ni nzuri maana inafundisha kuwa watu wajipende kama walivyo. Inasikitisha kuwa ilichukua wageni kutoka Afrika kuwafanya Jazmin na Stacey wajue kuwa ni watu wa maana duniani.

Jamii ya Marekani imejenga utamaduni ya kuchukia unene wote, yaani wanataka kila mtu awe mwembamba jambo ambalo haiwezekani. Watu wananjinyima chakula mpaka kupata utapiamlo. Hali inasikitisha. Pia unaona matangazo ya Gym, Vidonge vya diet, vifaa vya kufanyia mazeozi nyumbani, vyakula visivyo na mafuta, na mengine. Lakini ukicheki vizuri yote ni biashara. Je kuchukia unene ni matokeo ya ubepari, maana ukiangalia picha zilizopigwa Marekani katika miaka iliyopita utaona wakina mama wamejaa jaa, na waliitwa warembo. Cheki Marilyn Monroe, na Jayne Mansfield, lakini leo hii wangeitwa wanene. Hii wembamba mpaka mtu anabakia mifupa na ngozi si hali ya kawaida na wala hawapendezi na hawana raha.

Jambo lingine, wenye chuki na wanene na weusi wameipiga sana vita hii sinema. Wanaipigia kura mbaya bila kuiona. Inasikitisha. Nimesoma sehemu kadha watu wakitukana weusi, matako yao makubwa na mengine. Site ya Fox Searchlight ambao ni Distributor wa hii sinema walifuta Message Board ya Phat Girlz, maana ulijaa chuki dhidi ya weusi utadhania ilikuwa website ya wale wabaguzi wa rangi KKK. Bado kuna ubaguzi Marekani.

Nawakaribisha mcheki Blog yangu ya Kimombo http://chemiche.blogspot.com/ nimeandika zaidi hapo.

Thursday, April 06, 2006

Kwa Heri Mandisa!

Dada Mandisa kawa VOTED OFF on April 5, 2006. Mbele ya umati wa wapenzi wa American Idol, Mandisa mwenye sauti nzuri kuliko wanawake wote katika mashindano ya Season 5 katolewa kwa vile hakupata kura za kutosha. Mimi nimekasirika kweli, sijui kama nitakuwa na moyo wa kuangalia tena!

WaMarekani walisema kuwa ana sauti nyororo lakini hawezi kuwa American Idol kwa sababu ni mnene mwenye mizinga ya hips na matako!

Wengine wansema eti alivaa nguo mbaya na ana mikono minene! Jamani Kama hufanani na Paris Hilton watu hawaridhiki!

Naamini kuwa Mandisa atakuwa SUPERSTAR, na American Idol ndo ilikuwa mwanzo tu!