Saturday, December 30, 2006

Heri ya Mwaka Mpya!


Ninawatakia heri ya mwaka mpya! Mbarikiwe wote katika mwaka mpya 2007! Nashukuru Mungu kuwa wote tumefika na nawaombea wote uzima na mafanikio mema katika huu mwaka mpya. Naomba pia tuwe pamoja mingi mingi zijazo, Inshallah!

Pia nawaoba msherekee mwaka mpya kwa amani na usalama kwani kipindi hiki kuna kuwa na ajali nyingi shauri ya ulevi.

HAPPY NEW YEAR!

Tuesday, December 26, 2006

Marehemu James BrownREST IN PEACE JAMES BROWN

1933 - 2006

Jamani nilisikitika kusikia habari ya kifo cha Godfather of Soul, James Brown! Alifariki jana asubuhi, Krismasi, akiwa anaumwa Pneumonia. Lakini jamani Ijumaa mbona alionekana mzima, ana-sign autographs na kutoa zawadi za Krismasi kwa watoto!

Ukweli, mimi ni mmoja wa washabiki wake wakuu. Yaani kila nikisimikia animba 'funk' lazima niinuke na kucheza! Nyimbo zake, 'Say it Loud, I'm Black and Proud!', 'Hot Pants, 'Sex Machine', Get Up, na zingine nyingi haziwezi kusahaulika. Sasa kwa vile ni marehemu bei ya CD's zake zitaongezeka bei.

Nisiseme habari ya jinsi nilivyokuwa nashangalia akicheza na kutia madoido ya 'splits'! Nina mpaka mDoli wa James Brown, una bonyeza mahala na anaanza kucheza na kuimba ule waimbo wake wa 'I Feel Good!' (Najisikia vizuri). Tangu mdogo yaani miaka minne hivi nakumbuka kucheza na kupiga kelele kila nikisikia anaimba, eti najaribu kumwiga!

Mungu amlaze mahali pema mbinguni. Amen.


Saturday, December 23, 2006

Nawatakia Krimasi Njema!


Wapendwa Wasomaji, ninachukua nafasi hii kuwatakia wote Krismasi Njema! Japo ni sikukuu ya kusherekea kwa kupeana zawadi, kula mlo mzuri na wa fahari, kukutana na familia na marafiki, kunywa pombe etc., tusisahau kuwa ni siku ya kukumbuka kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

Napenda sana kipindi hiki Marekani, maana watu wanakuwa na roho nzuri na kusalimiana na watu ambao kawaida wasingewasalimia. Pia watu wanatoa misaada mingi kwa wasiojiweza na maskini kwa vile wameingiliwa na 'Christmas Spirit'. Hata bosi mwenye roho mbaya anaweza kuwa na roho nzuri japo kwa siku moja!

Wengine wataenda kwenye mikesha kanisani, wengine wataenda kwenye party, wengine watalala na kupumzika, wengine hawatasherekea kabisa hasa wasio waKristo.

Bila kujali dini, ninawatakia wote Krismasi Njema, na mapumziko mema.

Mungu Awabariki Wote!

Friday, December 15, 2006

Niliuliwa na Mzungu mwenye Hasira (Aftershock:Beyond the Civil War)
Jamani msishangae sana. Huu ni mguu wangu! Na bado niko hai. Nilikuwa naigiza katika sinema ya 'Aftershock:Beyond the Civil War' kama Field Hand. Hao field Hands walikuwa ni watumwa walioachiwa huru lakini bado walikuwa wanaishi katika hali ya kitumwa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe (Civil War) 1865. Wakati wa filiming tulikuwa peku kwenye matope! Sinema ilipigwa mwezi wa sita na wa saba hapa Massachusetts.

Hiyo make-up ya damu feki ilipakwa kwenye mguu baada ya kulala chini! Nakumbuka Director David Padrusch anamwambia make-up lady, ongeza, ongeza damu haitoshi! Ai! Walinipaka mwili mzima. Niliona kinyaa maana hiyo damu feki inaonekana kama damu kweli. Na usoni pia nilipakwa madamu na majeraha, ilikuwa tuonekana kama tumepigwa risasi nyingi. Ni kwamba weusi wengi waliuliwa na wazungu wenye hasira baada ya hiyo vita.

Sinema ya Aftershock itaonyeshwa History Channel, Saturday December 30, 3:00PM (Eastern).

Cheki website yao kwa maelezo zaidi.

http://www.history.com/shows.do?episodeId=203497&action=detail

Pia unaweza kusoma habari zaidi ya experience yangu kwenye seti ya Aftershock hapa:

http://chemiche.blogspot.com/2006_06_01_chemiche_archive.html

Unaweza kuona Trailer kwenye You Tube.

Thursday, December 14, 2006

Kariakoo = Carrier Corps

Hapo zamani za kale kabla ya magari, lori, petroli, basikeli, wazungu walitegemea binadamu na wanyama kubeba mizigo yao. Hao waafrika walioajiriwa waliona sifa kubwa kufanya kazi na mzungu na kulipwa.

Hao wabebaji wlaikuwa wanaitwa Carrier Corps, na baada ya 'kuswahililize' ndo ikawa jina la Kariakoo tunaoijua leo.

Kabla ya hao wa kulipwa waafrika walilazimshwa kubeba hiyo mizigo wakiwa kama watumwa. Historia ya mwafrika jamani.

Jamani cheki hiyo mizigo ilivyo mizito halafu fikiria unabeba kuanzia Dar hadi Mwanza, na wakati huo hakuna barabara. Lazima mizigo ilipotea, hasa kama mtu anaanguka nayo kutoka mlimani. Mtu unatembea nayo unatazama mbele huko nyoka anakuuma! Na, kama wabebabaji walikufa njiani nani alibeba mzigo wake?

Kama mmewahi kuona sinema za Tarzan na zingine zilizohusu Afrika, utaona mzungu alivyobebwa kwenye kiti na waafrika huko ana wabebabaji mizigo yake. Tena waafrika wakionekana wavivu wanachapwa kama punda! Ama kweli tumetoka mbali.

Wednesday, December 13, 2006

Nilitolewa Ushamba Dar - Text Messaging


Haya nimezungumza habari ya watu wengi kuwa na cell phone Dar. Sasa kuna hiyo kitu 'text messaging'. Naona ndo mawasiliano ya bei rahisi kuliko voice call. Kila mtu anajua kutuma text message, isipokuwa mimi!

Niliazima simu ya mama yangu. Watu walikuwa wananitumia text message. Doh, niliweza kuzisoma, lakini nilishindwa kutuma jibu! Niliona aibu kweli. Dada moja kanipigia na kusema, 'Nilivyona hujajibu niijua hujui kutumia texting!"

Ni kweli nilikuwa najibu watu kwa kuwapigia simu na of course ni ghali. Japo nina cell phone miaka mingi na nimeona hiyo text feature, huwa nasoma message na kuinua phone na kupiga kama inabidi nijibu. Nimeona vijana na watoto wadogo wanajua kutumia lakini haikuniingia kuwa nami nitumie. Na mara nyingi kwenye TV utasikia, send a Text message to halafu wanakupa namba. Lakini hata siku moja sijajaribu! Jamani USHAMBA! Ni kama vile compyuta. Mtu unaona lakini unaogopa kutumia! Ukianza kutumia unasema, Kumbe ni rahisi hivyo!

Sasa nimerudi Boston, na natazama cell phone yangu. Na ndo nimekuwa na-explore jinsi ya kutumia hiyo text message. Nimeanza kupatia. Lakini naomba mnieleza jinsi ya kuweka space kati ya maneno! Kwa sasa naweka period kati ya maneno.

Kumbe ni simple na mawasiliano rahisi. Nimeanza kupenda text messaging. Ushamba wa text messaging umenitoka.

Thursday, December 07, 2006

Dar es Salaam kuna Joto!


Jamani Dar kuna joto! Loh! Unapigwa nayo ukishuka tu kwenye ndege. Siku mbili za mwanzo nilivyokuwa huko niliona joto kweli. Ni kweli kuwa Novemba/Desemba joto unazidi Dar, lakini kwa kweli nilikipata. Kwa siku nilikuwa na kunywa maji mengi kweli, na vinywaji vingine. Jamani nilitoka jasho zile siku za mwanzo.

Halafu mara nyingi umeme ulikatika kwa hiyo feni na Air Conditioning hazifanyi kazi, kwa hiyo unaendelea kuchemka. Unakwenda ofisini mwa mtu halafu unabakia kujipepea na gazeti shauri ya joto. Asubuhi, umeme ulikuwa unakatika saa 12 kamili. Basi unaamka kwa sababu feni chumbani unazimika na joto unaanza kuzidi. Hata hivyo siku zilivyopita nilianza kuzoea joto.

Haya nilivyondoka nilianza kusikia baridi kwenye ndege. Nilitamani ningebaki Bongo nifaidi joto. Na kufika Boston nilikaribishwa na snow (theluji)! Unatoka kwenye joto kuingia kwenye snow.

Basi nimerudi Boston na ka-tan. Nilikuwa navaa sleveless Dar, basi unaona kabisa mikono umekuwa Dark. Sehemu zilizokuwa zimefunikwa zilikuwa light. Wazungu kazini waliniuliza kama nimepata 'sunburn'. Nikawaambia hapana ni tan, na sisi weusi tunapata tan pia. Lakini wacha nifaidi hiyo Vitamin E ya jua, maana kipindi hiki cha winter jua unaliona tu. Mambo ya kukaa nje na mwili kuganda shauri ya baridi hatutaki.

Monday, December 04, 2006

Aftershock itaonyeshwa History Channel 12/19 and 12/20/06


Habari zenu wapendwa wasomaji. Ile sinema ya 'Aftershock: Beyond the Civil War' itaonyeshwa kwenye History Channel, siku ya jumanne 12/19/06 saa mbili usiku (8:00pm Eastern) na pia itaonyeshwa tena 12/20/06 saa sita usiku (12:00am Eastern midnight). Mimi naigiza humo kama mfanyakazi wa mzungu mbaguzi mno mwenye uchungu shauri ya Confederates kushindwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe Marekani miaka ya 1860's.

Kwa habari zaidi soma hapa:

http://www.history.com/schedule.do

Pia nimewahi kuandika kwa kirefu kuhusu hiyo sinema hapa:

http://swahilitime.blogspot.com/2006_06_01_swahilitime_archive.html

Thursday, November 30, 2006

Kila Mtu ana cell Phone Dar

Jamani, mawasiliano ya simu ni rahisi sana Dar. Cell phone nyingi, makampuni yanashindana kupata wateja, phone cards zinauzwa kila mahala, tena bei si mbaya hata shilingi 500/- unapata! Watu wengi wanazo! Mbona cell phone USA ni ghali sana, tena ukiweka kwenye credit kadi ndo unalaguliwa kabisa! USA wanaweza kujifunza kutoka Bongo!

Lakini jamani barabara mbovu sana Dar, tena sana! MAVUMBI!

Baadaye!

Sunday, November 26, 2006

Diary from Dar es Salaam

Haya, ni siku yangu ya tano Dar. Malalamiko yangu makuu ni:

Ukosefu wa umeme
Barabara mbovu
Maji shida
Mbu!

Nimetafunwa na mbu! Na nimetumia mosquito repellent. Labda wamekuwa sugu. Lakini wamekunywa damu ya Boston!

Niko Mbezi kwenye cafe iliyoko barabarani kabisa. Kwa kweli computer zao ni safi sana, kuliko cafe iliyoko karibu na nyumbani. Wale wana computer nzee na slow.

Vumbi na michanga!

Lakini jana nilikuwa kwenye sherehe ya arusi. Jamani kuna catering companies siku hizi! Juzi nilikuwa kwenye Graduation party, ilikuwa kama arusi Ama kweli Tanzania kumekuwa Party Culture!

Friday, November 24, 2006

Niko Bongo!

Habari zenu wasomaji wapendwa. Niko Bongo Dar es Salaam. Nimetua juzi, kwa kweli ni joto sana lakini naona naanza kuzoea. Nimefurahi kufika nyumbani baada ya muda mrefu. Leo nimeenda mjini na kwa bahati nimegongana na watu wengi tu ambao nilikuwa nawafahamu. Naweza kuwa natembea halafu nasikia 'Che-Mponda!' Na cheki ni mtu nilimfahamu toka zamani.

Sasa jamani ile jengo la Daily News la zamani wanaifanyia nini? Naona Maktaba wamekarabati kwa nje. Maji ya kunywa ya chupa na phone cards ziko kila mahala, mawasiliano ni rahisi. Lakini barabara nyingi mbovu, na traffic jams ni mbaya! Yaani kutoka mjini kwenda Mbezi Beach ni two hours!

Nimepapenda Slipway! Ice Cream yako safi na ile Mashua Bar pale Beachfront safi sana. Halafu kuna ATM's kila mahala siku izi hakuna kwenda benki kusimama kwenye foleni ndefu. Nimshangaa kuona kuna hata Casino pale karibu na Greek Cub ya zamani karibu na Red Cross. Bongo kumeendelea hata hii internet nayo tumia ni nzuri sana na up to date!

Jamani nisiendelee maana umeme shida!

Mengine baadaye!

Thursday, November 16, 2006

Huyu ni Emmitt Smith na patna wake, Cheryl Burke wlioshinda mashindano ya 'Dancing with the Stars' jana. Alishinda baada ya watazamaji wengi kumpigia kura kama vile American Idol. Kila wiki wachezaji walipunguzwa mpaka kupata wachezaji bora.

Emmitt ni mcheza football na pia bonge la baba, lakini alishangaza watazamaji kwa 'moves' zake ambazo usingeweza kutegemea mtu na mwili kama wake kufanya.

Wacha wazungu wanune lakini weusi wamejaliwa na 'rhythm'! Kucheza iko katika damu yetu!

Navyosikia wanaume wengi sasa wanachukua Dance Lessons! Haya sasa Dancing ni' in' kwa wanaume!

Monday, November 13, 2006

Massachusetts yapata Gavana mweusi! (Ni wa pili katika Historia ya Marekani)Wiki iliyopita siku ya tarehe saba Novemba, 2006, ilitokea jambo la kihistoria hapa Massachusetts, Marekani. Ni Gavana mweusi wa pili tu katika historia ya Marekani. (Wa kwanza alikuwa Douglas Wilder wa Virginia mwaka 1990). Wingi wa wapiga kura walimchagua mtu mweusi kuwa Gavana! Na walimpigia kura kwa wingi mpaka mpinzani wake ilibidi akubali kuwa kashindwa vibaya mno!
Aliyechaguliwa kuwa Gavana mpya wa Massachusetts ni, Deval Patrick ambaye yuko kwenye chama cha Democrats. Bwana Patrick alizaliwa na kukulia ghetto ya Chicago. Bahati nzuri alikuwa na kipaji kimasomo na alifanikiwa kusoma Milton Academy kwa scholarship na Harvard University. Kwa habari zake zaidi unaweza kusoma hapa.

Mpinzani wake alikuwa bibi mmoja wa kizungu, Kerry Healey. Huyo mama ni tajiri na alikuwa Naibu Gavana wa Bwana Mitt Romney ambaye ni Gavana wa sasa na hashindi hapa Massachusetts. Si uwongo kuwa mwaka 2002, Romney alidanganya watu wa Massachusetts na kusema kuwa hawanii uraisi, kumbe kama Republicans wenzake ni mwongo mkubwa. Anagombea urais mwaka 2008! Na alimchagua Healey asiyekuwa na sifa za siasa zaidi ya kuwa tajiri kuwa Lieutenant wake.

Wakati wa kampeni ya Healey hivi majuzi, Romney alimtupa pia na wala hakumsaidia. Lakini niachane na mambo ya Romney maana nitasema mengi juu yake akigombea uraisi. Na si mazuri.

Healey aliishia kuchukiwa vibaya na watu. Hata Republicans wenzake walimgeuka na kumtupa. Huyo mama alikuwa na kampeni chafu na ya kibaguzi. Tangazo lake la mwisho kwenye TV ilikuwa na mzungu dume aki-jog kwenye eneo la wazungu huko tukimsikia mawazo yake. Yaani alisema mabaya mpaka tulisema alichoacha kusema ni kuwa hataki kuongozwa na Gavana mweusi.

Na pia alikuwa na tangazo la mbakaji mweusi ambaye Deval alimsaidia akiwa akifanya kazi ya mwendesha mashitaka. Heh! Jamaa si alikuwa anafanya yake. Na Healey alidiriki kutuma watu nyumbani kwa Patrick na Naibu wake Tim Murray kufanya maandamano wakiwa wamevaa nguo za wafungwa. Bahati yake mbaya mtoto wa Tim Murray mwenye miaka 12 alikuwa nyumbani peke yake akijiandaa kwenda shule. Waliishia kumtisha mtoto! Watu walimgeuka, na wakasema huyo mama hafai kabisa. Kaishia kuonekana kama mtu mwenye roho mbaya ajabu. Pia sikumwona akifanya kampeni kwenye maeneo ya weusi au waspanish. Walimwonyesha kwenye TV akiwa kwenye barbecue eti kwenye nyumba za wananchi wa kawaida. Doh, mbona nyumba zenyewe zilikuwa za wazungu tena nyumba za fahari.

Patrick wakati huo alikataa kabisa kufanya kampeni chafu dhidi ya mwenzake na alishinda. Tena kwa kura nyingi mpaka Democrats nchi nzima wanamtazama kwa mshangao na wanataka kujifunza kutoka kwake.

Januari, ndo Gavana Patrick ataanza kazi yake rasmi na naamini kuwa atakuwa Gavana mzuri maana ukiwa mweusi ni lazima ufanye kazi mara nne ya mzungu kusudi uonekane kama unafanya kazi.

Mengine, Democrats watawala sasa, walifanikiwa kunyakua Congress na Senate! Raisi Bush alie tu! Udikteta wake umekwisha! Watu wameamka sasa. Na wanasema kuwa Bush alikuwa Mnyonge kweli kweli siku ya uchaguzi baada ya kuona Republicans wanaangushwa vibaya! Watu wanasema Republicans waliangushwa katika ‘Tsunami’ ya kura! Na kweli ilikuwa tsunami na watu walimpiga kura kwa wingi mpaka sehemu nyingi walishiwa kura.

Ama kweli Demokrasia inafanya kazi Marekani.

Saturday, November 11, 2006

Anaomba Urafiki wa Kalamu

Huyu kijana (kulia) ni Corey Brown. Ana miaka 27. Ni mtoto wa rafiki yangu Queenae Mulvihill aliyeko Los Angeles. Kama mnakumbuka, Queenae ni mtunzi wa ile sinema Maangamizi. Kwenye hii picha Corey yuko na binamu yake.

Timu ya Maangamizi walivyokuwa Bagamoyo mwaka 1994, walikuwa na Corey. Alikuwa teenager wakati huu. Huenda kuna wanaomkumbuka.

Kwa sasa, Corey amefungwa gerezani huko California, na anatarajia kutoka baada ya miezi kumi na mbili. Kosa lake ni kughushi cheki ya dola mia ($100). Ameniandikia kuniomba kama naweza kumsaidia kutafuta marafiki wa kalamu. Anapenda sana Afrika na Ulaya.

Kama unataka kumwandikia au kumtumia post card kumsalimia anwani yake ni:

Mr. Corey Brown
coc#T-73384
Dorm 5 - Bunk 8
1150 East Ash Street
Shafter, California 93263

Asanteni

Monday, October 30, 2006

Wacheza sinema wanatafutwa kwa ajili ya Bongoland 2!

Kwa walio na ndoto ya kuigiza katika sinema, hii ni nafasi yako. Samahani lakini sitatafsiri posti na ni kimombo.

Ni hivi Josiah Kibira aliyetengeneza sinema za Bongoland na Tusamehe yuko mbioni kutengeneza sinema nyingine. Sinema hiyo ni Bongoland 2, na itapigwa Tanzania mwakani.

Casting Call ni hii hapa chini
:


SWAHILI SPEAKING ACTOR WANTED

By, Josiah Kibira

Kibira Films International is currently looking actors for its upcoming project to be filmed next year in Tanzania - July 1st - July 31, 2007 This new movie is a sequel to the movie Bongoland which was produced in 2003 by Kibira Films. Bongoland was/is a drama about different challenges that immigrants face once they arrive in the foreign land. It dealt with issues of immigration papers, employment, school and relationships. The main characters asked - "would you rather be a well fed slave or a hungry freeman"? He asked this while contemplating whether to keep chasing the ever elusive American dream or go back to his native land.

The sequel is a continuation of that drama following the main character Juma to see if his dreams for a better life were fulfilled after he decided to go back to his native Bongoland. The working title for the movie is "Bongoland II - There Is No Place Like Home."

Here are the qualifications for the post:

[1.] Be a male actor. [2.] Fluent Swahili speaker.[ 3.] Some film or stage acting - not necessary but would be helpful. [4.] Have seen the movie "Bongoland" [5.] Currently living in the United States [6.] Have legal status to travel in and out of USA. [ 7.] Willing to work on a deferred payment contract. [8.] Ability to get along with people.

Additional Perks for the role:

[1.] Free round trip ticket to Tanzania. [2.] All accommodations provided while in Dar. [3.] Daily stipend while on the set. [4.] Possibility of earning a role in Kibira Films future projects. [5.] Exposure to Film festivals in USA, Europe and Africa. [6.] Screen testing in Minneapolis, MN if selected or being considered. [7.] Possible career move.

For consideration:

[1.] Send a headshot. [2.] Your resume OR. [3.] An essay of why you think you should be considered for the role. [4.] Any tapes, DVD, vocals showing your acting abilities - In actual production i.e. play, movie (if you have it)

[5.] Send to: Kibira Films International 2860 Zanzibar Lane North Plymouth, MN 55447

[6.] Email - info@kibirafilms.com Thanks and Good Luck.

More information about Kibira Films - www.kibirafilms.com

Phone #: Office: (612)-291-2719; Mobile: (763)-229-2495

Saturday, October 28, 2006

Washindi wa 2006 ni Cardinals!


Ukikaa Marekani lazima utasikia habari ya mchezo BASEBALL! Zamani sikuwa na habari na huo mchezo na wala sikuujali lakini siku hizi mimi nimekuwa mshabaki! Kila mji Marekani una timu yake. Miji mikuu ina timu kubwa na wachezaji wanalipwa donge nono. Naona kama watu wana mapenzi na Baseball zaidi ya watu wanavyokuwa na mapenzi ya mpira wa miguu Tanzania.

Jana jioni timu kutoka St. Louis, Missouri iitwayo, Cardinals, walishinda timu kutoka Detroit, Michigan iitwayo, Tigers. Cardinals ni aina ya ndege na Tiger ni aina ya paka kubwa, sasa ungetemea Tigers washinde. Lakini Cardinals walinyakuwa ushindi wa World Series, yaani kuwa timu bora ya baseball ya mwaka 2006. Hongera kwao.

Ukweli nilikuwa nashabikia Tigers. Sijui kwa nini, lakini napenda sana wakicheza kwenye uwanja wao Detroit. Kila wakipata bao (score), na kukanyaga Homeplate basi unasikia mlio wa Tiger halafu macho ya sanamu ya Tiger wao yana waka na kucheza cheza! Kama wangefanikiwa kushinda World series sijui huyo Tiger wao angefanyeje.

Safari ya wacheza baseball ni ndefu kila mwaka. Wanaanza msimu wao April na kucheza na timu mbalimbali na kupunguzwa mpaka wanapata timu bora kwenye mchezo wa World Series. Tofauti na michezo mingine kama Football, wachezaji wa baseball wanacheza karibu kila siku na siku zingine hata game mbili kwa siku! Na kuna washabiki ambao hawakosi hata game moja ya timu wao.

Baseball ni mchezo uliyoanza marekani. Zamani weusi walibaguliwa na hawakurusiwa kucheza japo kwenye timu za weusi tupu. Miaka ya 1950's walianza kuruhusu weusi kucheza. Siku hizi kuna wachezaji wengi kutoka nchi za Amerika ya Kusini kama Dominican Republic, Cuba na Colombia. Na pia waJapani na waChina wapo. Wacehzaji wa kizungu katika Major Leagues wamekuwa wachache lakini bado watu wanashabikia.

Watoto wadogo wanacheza kwenye timu za Little League. Uwongo mbaya game zingine ni kama vile game za wakubwa Major Leagues. Watoto na wazazi wa wachezaji wanakuwa tayari kushikana masharti. Mwaka huu kocha wa timu fulani ya Little League alifungwa jela baada ya kumlipa mtoto wa miaka minane kumpiga na kumjeruhi mtoto mwingine kwenye timu yake na mpira kwa vile aliona kama yule mtoto atafanya washindwe.

Navyoona mchezo ni mgumu na lazima uwe na roho kuucheza maana ukipigwa na kale kampira (baseball) utaumia! Mchezaji anajitahidi kuupiga mpira unaoenda spidi kali mno na kamti (bat). Kusudi watu wasivunje mikono wakiudaka wanavaa gloves maalum. Batter ambaye ni zamu yake kujaribu kuupiga anavaa kofia kubwa na ngumu kichwani maana ukipgwa nayo unaweza kufa. Hapa Boston kwenye timu yetu, Red Sox, kuna jamaa, Matt Clement ambaye ni fundi wa kutupa mpira (pitcher) kapigwa kichwani na mpira mwaka jana na hajawa mzima tokea hapo!

Hapa Boston, timu yetu ni Red Sox na walishinda World Series, mwaka 2004. Japo ni timu ya mji wetu mimi siwapendi sana. Ni ghali mno kwenda kwenye game zao halafu tiketi zinauzwa magendo mpaka dola $3,000! Kukaa bleacher ni dola $70 na huoni kitu bila kuwa na binoculaurs!Waachie wenyewe tutazama kwenye TV! Au nitaenda Baltimore na New York kuangalia game huko maana tiketi ni dola $40 tu.

Haya nawaachia nafasi mtoe stori zenu za baseball.

Thursday, October 26, 2006

David Banda MadonnaHuyo mtoto mweusi ni mtoto wa miezi kumi na tatu, David Banda ambaye baada ya miezi kumi na nane atakuwa mtoto wa mwimbaji maarufu Madonna na mume wake, Guy Ritchie. David yuko Uingereza sasa na familia yake mpya.

Juu, ni picha ya Madonna na watoto wake wote, chini ni picha ya David na baba yake mpya Guy Ritchie. Yaani wiki mbili tu, mtoto kanawiri na kuonekana mwenye furaha!

Madonna alimpata David kutoka kwenye nyumba ya watoto yatima huko Malawi. Mama yake alikufa katika uzazi na pia wakubwa zake walifariki shauri ya malaria. Baba yake mzazi Yohane Banda, alishindwa kumtunza mwanae na kumpeleka huko kwa watoto yatima. Baba yake anasema ni bora amchukuea maana angebakia Malawi angekufa.

Huyo mtoto atalelewa katika nyumba ya fahari na atakuwa na mahitaji yake yote na atasoma digrii zote anazotaka kusoma. Pia mama yake Madonna lazima atamwachia mamilioni ya dola za kurithi. Si uwongo kulelewa katika familia ni tofauti na kulelewa kwenye nyumba ya yatima.

David Banda kazaliwa katika umaskini, lakini leo anaishi katika utajiri. Na lazima kuna watu wanamwonea wivu!

Monday, October 09, 2006

Leo ni Sikukuu ya Columbus Marekani

Leo ni sikukuu ya Columbus hapa Marekani. Ni siku ya kusherekea aliyegundua Marekani, Bwana Christopher Columbus. Columbus alitua Marekani na meli zake tatu mwaka 1492. Kuna nyimbo kadhaa za kumsifia na utasikia watoto wanaimba, "Columbus sailed the Ocean blue in 1492!"

Columbus alikuwa ni mwitalia aliyepewa pesa na malkia na mfalme wa Spain kugundua nchi kadhaa duniani. Kwanza enzi hizo wazungu walidhani kuwa dunia iko fleti na ukienda mbali utaanguka na kuishia motoni. Columbus alisema dunia ni mviringo. Alivyochukua meli zake na wakawa wanaenda, wanaenda, wafanyakazi wake kwenye meli waliokuwa na hofu kubwa kuwa meli yao itafika mwisho wa dunia, wataanguka na kufa wote. Walipanga hata kumpindua Columbus na hata kumwua na kurudi huko Spain. Lakini Columbua alifanikiwa kuwatuliza na hatimaye walifika Marekani. Ukweli alligundua Marekani kwa bahati tu, maana nia yake ilikuwa afike India. Alivyofika alishangaa kuwa hauko kama alivyofikiria na ndo kajua kagundua sehemu nyingine ndo kapaita West Indies. Ukweli Columbus hakufika Marekani tunayojua leo, bali alifika visiwa vya Bahamas. Lakini alifungua mlango kwa ajili ya wazungu kuja kwa wingi huko walivyojua kuna ardhi huko upande wa pile wa bahari!

Ajabu, utadhania kuwa kulikuwa hakuna watu Marekani kabla ya Columbus kufika. Watu walikuwepo. Hao wenyeji waliteswa na kunyanyaswa na hao wazungu. Waliuliwa na kuibiwa mali zao na kufanywa watumwa. Hao wazungu waliwaletea magonjwa, kama surua, na mafua na kaswende na wenyeji walikufa kwa wingi.

Watu unaowaona Marekani leo ni mchanganyiko wa watu kutoka kila pande ya dunia. Wako wa kila rangi, kila, kabila na kila dini. Uzuri Marekani wanasema kuwa kuna 'melting pot' yaani watu wanayeyushwa na kuwa moja. Na huko serikali ya Marekani inataka kufunga milango wahamiaji waache kuja. Wanasahau kuwa hii ardhi ilinyang'anywa kutoka kwa wenyeji waliokuwepo. Maangamizi ya wenyeji wa Marekani ilikuwa ni ya hali ya juu.

Kwa kweli kuna mengi ya kusema, lakini kwangu mimi sioni kama huyo Coulumbus ni shujaa.

Wednesday, October 04, 2006

Ngoma ya 'Tap'Najifunza kucheza ngoma ya Tap Dance. Hii picha nilipiga baada ya Show niliyofanya na Studio yetu hivi karibuni.

Tap Dance ni ngoma inayochezwa ukiwa umevaa viatu maalum vyenye vyuma chini. Kuna kuwa na chuma mbele na nyingine nyuma kwenye kisigino. Unacheza heel-toe, heel-toe na kila kikigonga chini kinaitwa tap. Na hivyo viatu vinatoa sauti kama muziki ukiweza kuvimudu.

Tap Dance ulianzishwa na waMarekani weusi na baadaye kudakwa na wazungu. Miaka ya nyuma watu wengi sana Marekani walijua kucheza lakini siku hizi 'interest' nayo inafifia. Watoto walikuwa wanacheza tangia wadogo. Marehemu Gregory Hines alijitahidi sana kufufua. Bila shaka mmeona watu wanacheza kwenye sinema kadhaa hasa zile sinema za zamani na musicals.

Kwa kweli inahitaji kazi na mazoezi na moyo. Ukiona wakina Savion Glover wanacheza ujue wamejifunza miaka na miaka. Ajabu ni mchezo wa mahesabu, maana lazima uwe na taps kadhaa katika sehemu ndogo ya muziki na zifuate muundo maalum. Huwa inategemea na muziki unayaotumia. Kwa sasa vijana wengi wanapenda Jazz Tap na Hoofing. Hizo staili kidogo una uhuru wa kwenda nje ya muundo wa ku-tap kwa mahesabu.

Kuna mama fulani marehemu sasa alikuwa anaitwa Ann Miller, alikuwa anaweza kupiga tap zaidi ya 500 kwa dakika moja. Ndo mwenye rekodi ya kutap haraka. Wandugu sitafika huko! Sitini kwa dakika moja ni kazi.

Si ajabu unauliza sababu iliyonifanya nianze kujifunza. Ni hivi, nilienda kwenye audition ya show fulani na kuulizwa na nina dance experience. Nikasema najua kucheza ngoma za East Africa. Wao walisema wanataka watu wanaojua ngoma za hapa USA kama ballet na tap. Basi ikabidi ninunue viatu na nitafute darasa! Mwanzo ulikuwa mgumu lakini sasa sioni kitu cha ajabu sana. Na naona raha kuwa naweza kucheza wimbo mpaka mwisho bila kukosea. Na next time nafanya audition wakisema wanataka nicheze dance niko tayari kuwa 'tapia'!

Kama uko Marekani au Ulaya bila shaka kuna studio karibu na wewe inayofundisha tap dance.

Saturday, September 30, 2006

TUUNGEJUA!!!!

Mwaka juzi mimi na rafiki yangu Alina tulikuwa tunaongea habari za kuweka pesa za kuishi na za kutosha tukiwa tumestaafu kazi. Miezi mitatu baada ya hayo maongezi Alina alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya mapafu. Siku hiyo tuyliyovyo kuwa tunaongea hakujua kuwa anaumwa. Kazini kwangu kuna mama fulani alienda lunch, hakurudi maana alipata massive heart attack na kufa barabarani kwenye sidewalk. Kijana mwingine aliaga kuwa tutaona wiki ijayo lakini alipata ajali ya gari na kufa kesho yake.

Mnafahamu wimbo wa maiti? “Nimekufa leo, kesho ni zamu yako!” Ukweli, watu wanakufa kila siku. Wengine wanakufa shauri ya uzee, wengine kwa ajali, wengine kwa kuuliwa na binadamu wenzao au wanyama wa porini, wengine kwa ugonjwa. Hakuna mtu anayajua atakufaje. Nadhani watu wangejua wangekaa kwa woga, wangeshinda wanalia na kutetemeka ovyo.

Nadhani ni vizuri kuwa sisi bindamu hatujui siku ambayo tumepangiwa kifo. Fikiria kama tungejua. Dunia ingekuaje?

Tuseme fulani anajua kuwa atakufa leo jioni saa mbili usiku. Basi ingekuwa hekaheka kuomba kupiga simu kwa watu na kuomba msamaha kwa watu aliyowakosea. Au angesema mi nakufa kleo ngoja nilipize kisasi kwa kumwua fulani na fulani. Mtu angeenda kuichoma moto nyumba ya mtu akijua kuwa hata akifungwa jela siku yake ya kufa ni karibu. Mtu asingehangaika na shule akisema haina faida maana atakufa siku fulani hivyo hiyo shule haitamsaidia na anapoteza muda. Asingeenda kazini, maana angesema nakufa siku fulani ngoja nifanye shughuli zangu binafsi.

Haya tuseme fulani anajua kuwa atakufa wiki ijayo Ijumaa saa tatu asubuhi. Basi anamaliza pesa kwenye credit card kwa kula laifu, na kuachia familia yake madeni tele. Huko anafanya ngono ovyo bila kujali magonjwa wala nini. Huenda angekunywa pombe kupita kiasi na kumaliza siku zake akiwa kwenye coma hospitalini! Wengine wangeenda kutapeli watu wakijua kuwa kifo kiko karibu hivyo hawana shida.

Wengine wangejua siku yao, basi ndo wangemaliza vitu walivyoanza halafu hawakumaliza kama vile kuandika vitabu, kushona gauni, wangemaliza kujenga nyumba zao, wangekazania kumpachika mtu mimba, wangeenda kwao kuona wazee na ndugu zao ambao hawajaona miaka mingi. Mtu angekaa na watoto wakae anawaambia kuwa anawapenda badala ya kushinda baa anakunywa pombe. Wangekuwa kanisani, miskitini, temple na sehemu zingine za dini wakitubu madhambi zao. Mtu kwenye foleni angeomba apishwe maana ni karibu saa yake ya kufa. Kwa kweli kama watu wangejua siku yao ya kufa ingekuwa pilika pilika.

Mungu aliumba kila kitu na sababu. Kwa kweli tunapita tu katika hii dunia. Mabibi na mababu zetu walitangulia na vizazi vijavyo vinafuata. Na ni maksudi alituumba kusudi tusijue siku ya kuondoka duniani. Hivyo kaeni mfikirie je, ningejua nitakufa lini ningefanya nini.

Friday, September 22, 2006

Tanzanian Model Tausi Likokola - International StarHuenda mmesikia jina la Tausi Likokola. Tausi ni model wakiTanzania anayejulikana kimataifa. Amekuwa kwenye maonyesho ya Urembo ya Gucci, Christian Dior, Tommy Hilfinger, Issey Miyake, na Escada. Mambo yake si mchezo. Huenda amepishana na Naomi Campbell na Tyra Banks kwenye Catwalk (jukwaa inayotumika kwenye maonyesho ya urembo).

Zaidi ya kazi za urembo Tausi amekuwa akifanya kazi ya kusaidia wagonjwa wa UKIMWI kupitia NGO yake iitwayo Tausi AIDS FUND . Aliaanzisha baada ya ndugu na marafiki wengi kuaathirika na huo ugonjwa hatari.

Akina Dada watapenda site yake. Anatoa tips za urembo kama kutunza ngozi, nywele, vyakula bora na mengine. Pia ametunga vitabu na kuna muhtasari za vitabu vyake.

Website ya Dada Tausi Likokola:

http://www.tausidreams.com

Ama kweli WaTanzania tunaweza kujivunia kuwa nasi tuko kwenye jukwaa la fesheni ya kimataifa. Hongera Tausi, mfano wako ni wa kuigwa.

Saturday, September 09, 2006

Cynthia Masasi - The Original Tanzanian Pin-Up Girl

Nilipokuwa nasoma Tabora Girls niliwahi kumwambia clasasmate wangu kuwa naona kawa, "Popular " sana. Nilisema hivyo kwa vile niliona kila mtu anampenda kuanzia wasichana wa O level na walimu wavulana wa shule zingine. Basi kusema hivyo aliona kama nimemtukana. Kwa kweli nilisema hivyo kwa nia ya kumsifia na siyo nia ya kumkashifu. Na aliona mbaya mapaka tunamaliza Form 6.

Sasa nasema kuwa Cynthia Masasi amekuwa ‘pin-up’ kwa nia ya kumsifia na siyo kumkashifu. Na sijui kama nimekosea kusema kuwa dada Cynthia Masasi ni pin-up girl wa kwanza Mtanzania. (Site yake ni http://www.cynthiamasasi.com) Kwa sasa anaishi Atlanta, Georgia, USA.

Ngoja niwaeleze maana ya ‘pin-up’ girl. Ni mrembo anayekuwa kwenye poster au calendar na mara nyingi mrembo anakuwa kavaa nguo ya kuogelea, mara nyingi bikini. Picha inaitwa pin-up kwa vile unakuwa chomekwa ukutani. Akina Marilyn Monroe na, Jayne Kennedy (mweusi), walikuwa pin-up girls. Na enzi zao nadhani wanajeshi wengi, vijana wa shule waliweka picha zao ukutani na kwenye locker. Na kila wiki gazeti la ‘Jet’ inatoa pin-up girl wa wiki. Wanawake wengi hawakubali iwekwe kwenye sebule zao. Wanaume ndo watakuwa wanunuzi wakuu. Lakini ndo swimsuit kalenda zilivyo. Unazikuta mfano kwenye maklabu ya wanaume, barbershop, vyuoni kwenye bweni za wavulana.

Kama hamjasikia, Cynthia anatoa kalenda enye picha zake akiwa amevaa swimsuit. Kila mwezi na picha yake. Nimesikiliza interview Cynthia aliyofanya na Kaka Deus Gunza wa Pod Radio Butiama huko Columbus, Ohio.

Cynthia anasema alikuwa na copy 5,000 za kalenda yake na zimeisha. Imebidi agize zingine. Nasema ‘Hongera ‘kwa kupendwa hivyo! Kwanza hapa Marekani model wangapi watauza kalenda nyingi hivyo kama si Supermodel au wana-promote kitu kama pombe na sigara.
Modelling una sehemu nyingi mfano kuna runway model, catalog model, store model, kalenda model. Nampongeza Cynthia kwa kuingia katika fani ya modelling, tena ana model akiwa amevaa bikini. Umezua maneno kwa vile watu wanahushisha na umalaya. Kwa mila na desturi za kiTanzania naweza kusema kavunja miiko maana tumefundishwa kujifunika . Lakini nikiona bikini na picha za wanawake huko Swaziland, tena wanaacha matiti na matako nje, nasema bora ya hiyo bikini. Kwa Marekani si wengi wanaweza kuwa na mwili wa model. Na hao supermodel wanajishindisha njaa na kujikondesha mno.

Kwa wapenzi wa rap na MTV, Cynthia ametokea kwenye music video za Nelie, Bow Wow, na Ludacris akiwa kama mcheza densi. Anasema amekuwa kwenye video 15. Kwa mashindano yaliyoko kapiga hatua, maana kwenye audition wanatokea mamia ya wasichana. Kuchaguliwa wakati mwingine ni kama bahati nasibu. Huenda kuna siku tutamwona kwenye fashion show ya Boateng.

Kwa binti zetu wa kiTanzania nasema, fanyeni kama moyo wenu unavyowatuma. Na kama umebarikiwa na mwili wa kuwa model, na unapenda fania hiyo fuatilia. Si lazima uwe swimsuit model, tunaweza kukuona kwenye mafashion show. Nani atakuwa 'pin-up' girl ijayo?

Cynthia atakuwa na Calendar party Chicago, Illinois, September 30th. Atazindua Calendar yake ya 2007.

Monday, September 04, 2006

Crocodile Hunter Steve Irwin Kafa


Loh! Leo asubuhi nimeamka nakufungua TV na kuona habari kuwa Steve Irwin au kwa jina lingine Crocodile Hunter (mlinda mamba) kafa. Wanasema kauliwa na samaki aina ya Sting Ray. Hicho kichomi chake chenye sumu kilimchoma kwenye moyo.

Nilisikitika sana kuwa kafa lakini huko najiuliza je ansingekuwa anacheza na wanyama hatari si angekuwa bado yu hai? Siku zote nilisema ngoja tutasikia kuwa kaumwa na nyoka na kafa. Hata siku moja sikudhania kuwa hatima yake ingekuwa samaki Sting Ray.

Nilipokuwa nakaa Chuo Kikuu cha Dar es Salaaam, jirani yetu mzungu akawa anatulaumu kwa kuua majoka. Na kama kulikuwa na nyoka nyumbani kwake, analazimisha houseboy wake amkamate na kumpelea idara ya Zoology pale UDSM. Mzungu mwenyewe alikuwa mshenzi, anamfuata na gari yake kuhakikisha kuwa anampeleka kweli!

Ilikuwa sisi wengine tukiona nyoka, tunatafuta fimbo, mawe na kuua! Kwanza ukiumwa na huyo nyoka, kutakuwa na dawa kweli dispensary ya kukukutibu. Au unaweza kuchelewa kupata usafiri wa kwenda hospitalini na kufa. Na mara nyingi tulisikia mtu kafa kwa kuumwa na nyoka, hivyo kwa nini tusiwaue! Ua au uliwe!

Lakini wazungu sijui wakoje, wakiona mnyama hatari wanataka awe pet. Lakini mnyama pori ni mnyama pori tu! Mnakumbuka yule tiger alivyomtafuna Roy, huko Las Vegas kwenye Seigfried & Roy Show. Yule tiger alifugwa nao taokea azaliwe. Je, mnakumbuka yule kijana wa kizungu mwenye miaka 17 aliyekufa baada ya kuumwa na pet kifutu (viper) wake huko Kenya? Alikuwa anafuga majoka wa kila aina nyumbani kwake, macobra, chatu, nk. na alishumwa nao, lakini huyo kifutu ndo kamwuma na kumwua.

Haya nirudi kwa marehemu Steve Irwin. Ilikuwa wakati mwingine nikitazama show zake nasema anajiona mungu wa wanyama na hawatadhuru. Utamwona yuko Afrika anakamata black mamba na cobra mwenye hasira. Mara anacheza ma mamba mkubwa kweli kweli huko kashika mtoto wake, tena mdogo mwenye umri miezi michache tu. Tena anamtembeza mbele ya mamba kama kitoweo vile. Halafu alidiriki kusema, alijua kuwa mamba hawezi kumdhuru mwanae. Bora angesema ilikuwa bahati mamba hakumdhuru.

Na leo tunasikia alikuwa anaogelea na sting rays huko Australia kwa ajili ya show yake, ndo alikuwa anaogelea juu ya sting ray na stingray kanyanyua kichomi chake na kumchoma kifuani kwenye moyo! Naona huyo sting ray alikuwa si rafiki yake, au alichoka naye.

Mungu amlaze kaka Steve Irwin mahali pema mbinguni. Amen. Na kifo chake iwe fundisho kwa wengine, mnayama pori ni mnyama pori.

Thursday, August 24, 2006

Kajambanani?

Kila siku asubuhi nikiamka nafungua TV kuangalia taarifa ya habari kwenye Fox 25. Kuna mzungu mwanaume mnene ndo anchor wa Beacon Hill studio (Dowtown Boston) na anapendwa na wengi, anaitwa VB. Na huko kwneye studio yao Dedham kunakuwa na akina Dada Anquenette (mweusi), Gene Levanchy na Kim Carrigan. Leo nikafungua na nikasikia sauti ya ajabu. VB kajamba tena kwa sauti. Nikajiuliza kama VB kaweka microphone matakoni kusudi tumsikie. Nikasema sijui kala nini jioni yake. Kwanza nikamwonea huruma maana najua hawezi kuamka kukimbia chooni mpaka break ikaja. Bora yuko nje maana studio utajaa harufu ya mishuzi. Basi kila baada ya sekunde chache anaachia. Nikasema huyo mzungu kala maharagwe na hajayazoea nini! Cha kushangaza kawa anaongea bila kujali kitu.

Kukaa kidogo huko kwenye studio kuu, anchor Gene Levanchy naye kajamba. Kim Carrigan kamtazama kwa dharau kubwa na kushika pua lake. Gene na VB wakamwuliza kama yeye hajambi na kawa kama kasirika kuuliza hivyo. Kim kajifanya hayumo kwenye mambo ya kujamba. Basi kwenye break aliamka kwenye kiti halafu tukasikia mjambo pwaaaach. Tukasikia kila mtu studio anacheka. Kumbe wenzake walimwekea ‘Whoopee cushion’ (Kimpira kinachotoa mlio kama mtu kajamba). Ukikalia inatoa mlio kama vila mtu kajamba. Kima katoka haraka uso mwekendu!

Basi ndo VB kaelezea kisa cha yeye kuwa anajamba jamba. Kumbe kwenye magazeti waliandika habari ya intern huko White House kusema kuwa rais Bush anapenda kujamba ofisini. Heh! Rais mzima anjamba! Tena mbele za watu. Lakini kwa nini watu washangae, ni bindamu na vayakula anavyopenda ni vya kiMexico ma nacho, refried beans, na maburrito na bia. Lazima zitafanya tumbo ijae gesi. Sijui kama yuko na Rais mgeni kutoka nchi nyingine anaachia mishuzi. Tumekwisha jua kuwa anapataga ashki.

Haya sasa fikiria uko kwenye basi au subway (treni). Watu wanajamba huko hasa kama umejaa, tena vile vya kimya kimya vya kuniuka hasa! Bora hizo zenye milio mikubwa. Cha kuchekesha mtu anabanwa gesi, anaachia kimya kimya inanuka halafu watu wanalalamika na huyo aliyetoa analamika. Huwezi kujua nani kajamba.

Wazungu wengine hawana haya, wanajamba, halafu wanasema, “Oh Excuse me” Utajibu kweli? Kama unamjua labda utasema, “You’re excused”. Wamarekeni weui wana usemi, “You smelt it, you dealt it!” (Umesikia ushuzi hivyo wewe ndo umejamba), Ukiwa na weusi ni bora kunyamaza na ubane pua.

Na hapa Marekani watu wanatajirika kwa kuuza vidonge vya kuzuia watu kujamba. Phazyme, Beano, Papaya pills, vina soko kubwa.

Kabla sijamaliza lazima nikumbuke Bongo na usafiri wa treni Third Class Bongo (Central Line). Watu walikuwa wanabanana safari ndefu, watu wana jamba jamba, na huwezi kuwalaumu maana choo hakuingiliki na inabidi usubiri mpaka treni isimame kwenye kituo halafu ushuke haraka na kujisaidia pembeni. Basi Thedi ikapewa jina, KAJAMBANANI! Unasafiri daraja gani, Nasafiri, KAJAMBANANI bwana hela sina ya First!

Lakini baada ya maajabu niliyoona leo nangojea kusikia kama kutakuwa na Official Fart Day! Siku ya kujamba. Kumbe kujamba ni sifa, wazungu bwana!

Wednesday, August 23, 2006

Kusogoa Chooni


Jamani Marekani watu maofisini wananishangaza sana. Kuna mtindo wa watu kusogoa na kupiga gumzo chooni. Tena kwa muda mrefu.

Yaani mtu anajisaidia, huko mwenzake yuko nje anamsemesha. Au unaingia chooni na kukuta watu wamepiga kambi kwenye masinki ya kunawia mikono na kupiga soga, huko watu wanajisadia kwenye stalls. Wanasikia mtu anakojoa, hao wanaongea bila kujali. Kwa kweli nashangaa sana. Labda mtu akiwa anajisaidia haja kubwa ndo wakimbie kwa ajili ya mishuzi.

Kwa kweli Restrooms/Bathrooms za Marekani maofisini ni safi sana, yaani unakuta toilet bowl cheupe kama vile bado kipya. Zinasafishwa mara kwa mara kwa siku. Nakumbuka Mbongo fulani aliwahi kusema vyoo vingine visafi mpaka unaweza kula huko, (mhhh sijui, mimi siwezi kula huko)! Usafi chooni ni muhimu sana hapa, na hao wanaosafisha wakizembea wanashutukia kazi hawana wanaletwa wengine. Lakini bado sijaona kama chooni ni sehemu ya kupiga gumzo.

Unaingia kwenye stall (kichumba chenye choo), mwenzako yuko nje kaona unaingia anaanza kupiga mastori. Aisei umesikia, hivi na hivi, je, unaonaje hivi na vile. Kwa kweli naona mkojo unataka kwa shida huko unajisaidia, huko unajaribu kuongea.

Lakini kuna kitu niligundua. Kisheria Marekani, mwajiri anarushisiwa kuweka recording devices kila mahala ofisini na Mfanyakazi asijue. Wanaweza kuwa na makamera na ma-audio device na usijue. Ila ni mwiko kuweka hizo devices chooni! Je, ni sababu ya watu kupiga gumzo chooni kwa vile wanajua hawawezi kunaswa kwa ajili ya kupoteza muda kazini.

Mnaonaje kuhusu suala hii?

Monday, August 21, 2006

Idi Amin Hajambo?Sisi waTanzania hatutasahau ushenzi wa aliyekuwa Dikteta wa Uganda marehemu Idi Amin Dada. Lazima yuko motoni kwa mauaji aliyofanya akiwa kiongozi wa nchi hiyo. Lakini alivamia nchi yetu Tanzania na kusema eti Kagera ni sehemu ya Uganda. Ndipo Mwalimu Nyerere kaja juu na kutuma Jeshi la Wananchi na Mgambo kumtoa nduli Idi Amin! Na hatutasahau ile miezi kumi na nane ya shida baada ya hapo ambayo karibu iwe miaka kumi na nane ya shida. Enzi za kukosa sabuni, sukari, na vyakula na bidhaa mbali mbali madukani na sokoni! Lakini asante Nyerere huyo kichaa kafukuzwa Uganda maana maiti zilikuwa zinajaa Ziwa Victoria mpaka watu walikataa kula samaki kutoka pale!

Leo nimepata habari kuwa kuna sinema itatoka mwezi ujao (Septemba) kuhusu Dikteta Idi Amin wa Uganda. Sinema hiyo inaitwa, ‘The Last King of Scotland’.

Sinema ilipigwa Uganda na mcheza sinema maarufu hapa Marekani, Forrest Whittaker, ndiye anaigiza kama Idi Amin. Mcheza sinema mrembo, Kerry Washington anaigiza kama mmoja wa wake za Amin. Sinema hiyo inasubiriwa kwa hamu na wengi na tayari wanazungumzia habari za ma Oscar kwa ajili ya Forrest Whittaker na Kerry Washington.

Uzuri sinema ilipigwa Uganda kwa ruksa ya Rais Yoweri Museveni. Alitoa msamaha ya kodi mbali mbali kwa ajili ya watengeneza sinema waliokuwa na bajeti ndogo ya kutengeneza hiyo filamu. La sivyo wasingweza kuitengeneza. Alikubali kuwa hatimaye sinema hiyo inaweza kusaidia kuongeza utalii Uganda.

‘The Last King of Sctoland’ inatoka tarehe 26 Septemba. Kwa habari zaidi someni hapa.

Bonyeza hapa kuona Trailer ya sinema: THE LAST KING OF SCOTLAND

Monday, August 14, 2006

Kitabu kuhusu Utengenezaji wa filamu Maangamizi


Bi Queenae Mulvihill ametoa kitabu kuhusu sinema Maangamizi the Ancient One. Hiyo sinema ilipigwa Bagamoyo, Kilimanjaro na Morogoro kati ya 1994 na 1997. Mimi niliigiza kwenye hiyo sinema kama Nurse Malika. Sinema hiyo ilikuwa ni ya kwanza kutoka Tanzania kuwa katika mashindano ya Academy Awards Hollywood yaani Oscars.

Kwa kweli kuna mengi yalitokea na yalitendeka. Kulikuwa na majonzi mengi, ukosefu wa fedha, ugomzi, hasira, vifo, ahadi za uongo, wizi na mengine. Pia hao akina Mulvihill bado wanadaiwa karibu $150,000 kutokana na hiyo sinema. Lakini sinema ilitoka. Jamani kutengeza sinema siyo rahisi. Kinahitaji utaalamu, uvumilivu na pesa!

Kitabu kinaitwa 'Warriors: Spritually engaged - The Making of Maangamizi the Ancient One.'

Linki ya kitabu ni hii....

http://calendars.lulu.com/content/265217

Kitabu kina ukurasa 379. Siku nyingi sijasoma kitabu kizuri lakini wikiendi hii niliacha kila kitu na kukisoma. Kilikuwa kizuri na sijui nilipenda kwa vile nafahamu watu wengi waliotajwa mle, au vipi, lakini ni kizuri. Dada Queenae ana kipaji cha kuandika and amedika kutoka moyoni na anaongea kwa uwazi na bila aibu. Mambo yaliyoomo ni karibu kuvunjika kwa ndoa yake na mapenzi. Moyo wangu ulijaa huzuni, majonzi na raha nilivyosoma.

TWO THUMBS UP!

Kwa habari zaidi kuhusu sinema ya Maangamizi bonyeza hapa...

http://www.grisgrisfilms.com/

Wednesday, August 09, 2006

Meli ya M.V. LiembaKuna sinema ambayo itatoka hivi karibuni kuhusu meli ya MV Liemba. Hiyo meli iko Ziwa Tanganyika. Nilishangaa sana kusikia kuwa baada ya miaka yote hii bado inafanya kazi. Yaani imefanya kazi karibu miaka 100!

Kumbe ndo meli iliyotumika kwenye sinema ya The African Queen. Kwa hiyo wacheza sinema wa enzi zile Humphrey Bogart na Katherine Hepburn walipanda.

Kwa habari zaidi someni hapa:

http://www.liemba.org/

Mimi sijawahi kufika Ziwa Tanganyika. Kama umewahi kusafiri na hiyo meli tupeni story basi.

Thursday, August 03, 2006

Wapenzi na Wivu

Mara nyingi tunasikia habari ya mtu kumpiga mpenzi wake kwa ajili ya wivu. Mwanamke kasalimiwa na mwanaume mwingine, kibao! Mwanamke anapiga simu nyumbani kumwulizia mume wa mtu, mke anampiga na sufuria na mengine. Lakini wakati mwingine wivu unazidi mpaka watu wanafanya maajabu.

Nimesikitika sana kusikia habari ya jamaa kujinyonga Gesti huko Tandika eti kwa vile mpenzi wake wa miaka 19 alikuwa na wapenzi wengi. Kitu gani kilimwingia marehemu Said Libonge mpaka kaamua kumchoma mpenzi wake kisu na yeye mwenyewe kujinyonga. Ni wivu au ugonjwa wa akili?

Mimi sikuwepo bali nimesoma tu hiyo habari ya kusikitisha. (Soma Hapa) Na huyo dada lazima atajiuliza mara mbili tatu kabla ya kuingia gesti na mwanaume au kuwa na mpenzi mwingine.

Lakini nikikumbuka vituko wanavyofanya wapenzi kwa jina la wivu, nasikitika na nacheka. Haya tuchukue kesi ya mama fulani aliyemkuta mume wake yuko kwenye shughuli ndani ya gari eneo ya Mbuyuni Dar es Salaam miaka ya tisini. Yule mama alidai kuwa alifungua mlango wa gari kamkuta mume wake yuko juu ya howara wake anapampu na alidai kuwa mambo yao yalikolea kiasi kuwa alikuwa anampiga mume wake aliyekuwa ameshusha suruali matakoni na hakusikia kitu. Kwanza mtu wa kawaida angebakia anashangaa mdomo wazi, au angekimbia kwa aibu. Lakini hapa huyo mama na wivu zake kaweza kufungua mlango wa gari na kuanza kumpiga mtu shughulini.

Haya nakumbuka kisa cha mama mwingine miaka ya themanini. Mume wake alienda na howara wake kwenye gesti Manzese. Yule mama alijua yuko chumba gani. Kitanda kilikuwa chini ya dirisha. Basi yule mama alikesha pale kwenye dirisha na walipoanza mambo yao, yule mama kafungua dirisha na kuwamwagia chupa ya tindi kali. Kwa vile walikuwa uchi wote waliungua vibaya! Wivu jamani!

Nilivyokuwa nasoma Tabora Girls kuna dada fulani aliuliwa na mume wake. Sitamsahau yule dada. Alikuwa anakaa National Housing na mume wake, ndoa yao bado changa. Dada mwenyewe alikuwa mzuri kweli kweli. Mume wake alikuwa ni mwanajeshi mwenye cheo cha Kepiteni. Alikuwa mwembamba mwenye kipara. Kuna wenzangu walimuwa wanamvizia yule baba. Basi kuna siku yule baba alishikwa na wivu, kamfunga kamba mke wake na kumtia matambara mdomoni mwake kusudi asiweze kupiga kelele. Wanasema kuwa yule baba alimpiga raundi ya kwanza, kampiga raundi ya pili, kampiga raundi ya tatu mpaka yule dada kafa. Eti kapusuliwa bandama! Kisa cha kumpiga mke wake mpaka kafa kilikuwa eti alimwona anaongea na mwanume mwingine. Yule baba alihukumiwa kifo.

Niendelee? Kuna visa vingi, vya watu kuua au kuumiza wapenzi wao kwa jina la wivu.

Mimi mwenyewe nimeshikwa na wivu mara kadhaa lakini siyo kiasi cha kuua au kumwumiza mtu! Niwasimulimie kisa kimoja. Kuna jamaa nilikuwa nampenda sana. Lakini yeye hakunijali wala nini zaidi ya kusalimiana. Basi kuna siku nilimwona anakwenda kwenye deti mjini DSM na dada fulani! DUH! Nilijikuta naona kizunguzungu, Siwezi kusema, hasira zimejaa na nikaanza kulia! Watu waliniuliza nalia nini, nikashindwa kusema! Baadaye nikasema basi Mungu hakupanga niwe naye. Yaani nikikumbuka nacheka.

Mnasemaje kuhusu wapenzi na wivu?

Thursday, July 20, 2006

Rais Bush Apata Ashki Mkutanoni!

Jamani, watu Marekani wamekuwa wakisema kuwa Rais Bush ana utaira fulani wa akili. Kama watu walikuwa hawaamini, nadhani sasa wanaamini.

Wiki hii Rais Bush yuko Urusi kwenye mkutano wa G-8 Summit, na marais na viongozi wa nchi kadhaa. Kiongozi pekee wa kike hapo ni waziri mkuu wa Ujerumani, Bi Angela Merkel. Basi Bush ailiingia kwenye ukumbi wa mkutano, sijui kaingiliwa na kitu gani, huyo anaanza kumpapasa mabega. Na yule mama kamfukuza haraka haraka! Kwa kweli hapa Marekani hiyo initwa unyanyasaji wa kijinsia (sexual harassment), na mtu anaweza kufukuzwa kazi kwa ajili hiyo. Je, Rais Clinton angefanya hivuo watu wangesema awe impeached (avuliwe urais)! Maana kaibisha taifa la Marekani.

Na kabla ya hiyo tukio ya kumpapasa alitukana alivyokuwa anaongea na Waziri Mkuu wa Uingereza, bwana Tony Blair. Alitamka neno 'shyt' akiongea kuhusu waarabu! Jamani kumsikia rais wa Marakeni akitukana ni maajabu na sijui kama imekwishawahi kutokea. Labda tuseme asante teknolojia dunia nzima inaweza kujua vituko vya Rais wa Marekani.

Watu wanasema ndo matokeo ya Bush kutokuwa na 'handlers' wake, akina Cheney, baba yake na Bi Condoleeza Rice. Na ndo matekeo ya kuongea bila scripts!

Ione clip hapa:
http://www.youtube.com/watch?v=q0tEQhaK4VM&search=bush%20back%20rub

Monday, July 17, 2006

Hongera Miss F.A.T. 2006! Ana Boxi huyo!Tanisha Malone & Mo'nique

Natoa pongezi kwa Bi Tanisha Malone wa Newark, New Jersey. Yeye alifanikiwa kutwaa taji la Miss F.A.T 2006, (Fabulous and Thick)! Ukimwona utadhania kazaliwa Afrika. Ni mweusi halafu ana matako makubwa sana! Yaani kabarikiwa hasa hata Miss Bantu wa Bongo ataona wivu! Na najua angekata mitaa Bongo eksidenti zingetokea maana midume ingebakia kumtamzama kwa mshangao. Nilikuwa nacheki comments kwenye neti, nyingi zinazungumzia matako yake yalivyo makubwa, ( big azs)! Juu mdogo lakini chini... midume mtabaki mnahema ovyo!

Kazi anayofanya huwezi kuamini, ni mortuary attendant! Lakini anaongea vizuri na kwa kweli alivyokuwa anatembea anavutia. Kwenye mashindano ya Lingerie (Nguo za ndani) alivaa two piece (Kama bikini)! Nyie mapaja hayo! Shepu kama kibuyu. alisimulia kuhusu jinisi alivyokuwa mdogo alivyoungua na maji ya moto na ikabidi akae hospitali mwaka mzima. Ona makovu kwenye bega na mikono. Lakini kwenye pageant hakuona haya, aliyaonyesha makovu yake bila wasiwasi.

Natafuta full picha yake nibandike. Lakini unaweza kusoma habari za ushindi wake hapo:

http://oxygen.com/specials/monique/tanisha_malone.aspx

WEBSITE YAKE NI: http://www.tanishamalone.com

Friday, July 14, 2006

Sinema ya Gone baby Gone

Mcheza sinema maarufu, Ben Affleck (aliyetaka kumwoa J Lo) yupo hapa Boston anatengeneza sinema inaitwa Gone Baby Gone. Mimi nilibahatika kuwa extra kwenye hiyo sinema. Kama watatumia footage waliyopiga nitakuwa kwenye scene wahusika wakuu wakila chakula kwenye restaurant ya Ghetto. Ilipigwa kwenye restaurant ya Silver Slipper. Insemekana wenye hiyo retaurant walipewa donge nono kwa matumizi ya hapo, eti $100,000! Sijui kama ni kweli. Najua ilibidi wafunge siku nzima, na restaurant enyewe ni ndogo.

Nilibahatika kupiga picha na mcheza sinema maarufu, Ed Harris, alikuwa kwenye sinema kama Radio, Nixon, The Firm, Apollo 13, A Beautiful Mind, na zingine nyingi tu! Ed alikuwa mungwana kweli, alipita kasalimiana na kila extra na kutuuliza majina na kwenye seti akawa anatuita kwa jina. Ben Affleck hajatusemesha hata neno moja. Wengine walisema eti kwa vile tulikuwa weusi, maana huwa anasamlimiana na extras wazungu. Lakini hatukujali tulifanys kazi na tumelipwa!

Pia tulikuwa na John Ashton. Kama mmeona sinema ya Beverly Hills Cop ni yule polisi aliyekuwa na roho mbaya kwa Eddie Murphy.

Cheki walivyogeuza Roxbury kuwa Hollywood set. Hapo ni corner ya Washington St. karibu na Dudley station karibu na kituo cha polisi.

Tuesday, July 11, 2006

Minjemba walikoma Boston!

Ninacheka! Na bado nacheka! Loh! Nimeanguka kwenye kiti, niko kwenye sakafu! Bado nacheka! Mbavu zinauma Jamani, nisaidie! Uwwwwiiiii!

Ni hivi, juzi nilienda kwenye klabu fulani Downtown Boston na rafiki yangu (dada Mmarekani mweusi). Ni msanii mwenzangu na tuliamua kufanya ‘Girls Night Out!” Tulikaa mezani na vinywaji vyetu na sahani ya buffalo wings (mabawa ya kuku enye pilipili). Karibu na sisi kulikuwa na wanaume wawili kutoka Tanzania tena ndo siku yao ya tatu hapa Marekani. Mimi siwajui na wao hawakunijua. Walikuwa wanaongea Kiswahili. Mimi nilijikausha tu, sikutaka wajue naelewa wanasema nini. Nikamwambia rafiki yangu kuwa hao wanaume ni wageni kutoka Tanzania. Aliniomba nimwintroduce kwao na mimi nakakubali ila baadaye kidogo.

Basi, hao minjemba, walikuwa wanasuka mipango ya kuopoa mademu wa kizungu hapo klabuni. Na kutokana na walivyokuwa wanaongea lazima walisuka mpango wa kuonja wazungu kutokea Bongo. Walikuwa wanamcheki kila dada hapo klabuni, mara huyo mbaya, yule mbaya, yule mwembamba, yule hana matako, matiti madogo, yule mzuri kidogo, huyo vile. Wakawa wanajadili watupe offa au la (hatukupata), lakini mmoja kasema nia yao ni kutoka hapo na wazungu. Wakawa wanacheki nani yuko na nani, na wakajadili jinsi ya kuwatongoza. Nikamwambia rafiki yangu walikuwa wanasema nini, tukawa tunacheka.

Basi, kwenye meza karibu na mimi kulikuwa na akina dada wawili wa kizungu, wazuri kweli kweli. Si kawaida yangu kusifia wazungu, lakini hao walikuwa ni wazuri, walijremba vizuri, walivaa vizuri, nywele ndefu zimechanwa vizuri mno, yaani ukiwaona unasema ni ‘perfect’. Tukasema lazima ni models. Walikuwa wamekaa wenyewe wanatazama mambo hapo klabuni. Naona hao minjemba ikawaona. Basi, walikunywa vinywaji vyao kusudi wapate moyo ya kuwa-approach.

Wimbo ukapigwa, na hakuna mzungu aliyewaomba densi, basi wale wakamka na kuwaomba densi. Wale akina dada, bila kusita walikubali. Ungeona nyuso za hao minjemba walivyokuwa na furaha. Wakacheza densi ya kwanza, wakacheza ya pili, mwisho wale akina dada walihamia kwenye meza ya hao minjemba.

Wakati huo watu klabuni wanawatazama, wengine walikuwa wanacheka. Na mimi nikawacheki vizuri. Nikasikiliza maongezi ya hao akina dada. Halafu nikacheki mikono yako, duh, mikubwa! Ikaniingia! DAH! Kumbe si akina dada hao ni midume! Ni ma transvestite! Sasa nikabakia nawatazama wa waBongo kwa mashangao! Nikasema hao akina kaka hawajui wameopoa akina nani, maana usoni walionekana kuwa na furaha kama vile wameshinda bahati nasibu! Na huyo rafiki yangu kaniambia tujiandae kwa ajili ya sinema ya bure.

Nilitaka kuondoka kuelekea kwenda nyumbani, lakini nikamua kukaa maana nilitaka kujua itaishia vipi. Wale akina kaka wakaanza kuwaambia, wako Boston kwenye business, na wako Hoteli fulani. Wakawa wanawaambia habari za Tanzania na kuwa ingekuwa vizuri siku moja wawatembelee huko. Wana majumba ya fahari, na watawapeleka mbuga za wanyama. Mwisho wakawakaribisha hotelini kwao kusudi wapate vinywaji zaidi. Pia walikuwa na zawadi kutoka Tanzania ambazo walitaka kuwapa. Nilishangaa, wale wawili wakasema, “Okaaay!” Basi wakaamka wakasema wanaenda restroom, kujipodoa halafu watarudi.

Walivyoinuka kwenda huko na mimi nikaona ni chensi ya kuwaonya. Rafiki yangu kaniambia nisiwaonye. Lakini nikasema bora niwaonye maana wakifika hoteli na wakikuta si wanawake inaweza kuwa balaa. Nikaamka na kwenda kwenye meza ya hao minjemba, nikawasalimia kwanza kizungu. “Hey guys, how are you?”

Wakajibu, “We are good” Nikasema kwa kiswahili, “Nafurahi kusikia hivyo!” Wakanitazama kwa mshangao, “Heh, Dada Mbongo wewe?”

Asante Pina Colada ulimi ukawa unateleza...nikajibu, “Mimi Mbongo ndiyo. Na nyie kama kaka zangu, nimeona niwaulize, mtawafanya, au mtafanywa?” Wale akina kaka wakajibu, “Heh, nini tena!’ Nikajua kuwa bado hawajajua wako na akina nani.

Nikawambia, “Hamjui kuwa hao akina dada wakizungu mliyonao ni akina kaka! Shauri zenu!” Ungeona nyuso zao, yaani ilikuwa “Kodak Moment!” Bahati mbaya camera niliacha nyumbani. Mmoja kaanza kuongea kwa kigugumizi, Yaa yaa nii, ni wa se se senge!” Nikajibu, “Naam!”

Ungeona ile minjemba ilivyoshikwa na wasiwasi. Mmoja kumwambia mwenzako, “We Bwana si nilikuambia wazuri mno hao na kwa nini wazungu wenzao hawakuwataka!” Waliinuka haraka, na mimi nilitia ndogo ndogo na kurudi mezani kwangu kwa rafiki yangu. Nikamweleza ilivyokuwa naye akawa anacheka kwa sauti mpaka watu klabuni wanatutazama. Rafiki yangu kasema wakome kutaka wazungu. Wale akina kaka wakatoka haraka, haraka klabuni kabla wale trans wamerudi kutoka restroom.

Wale trans wakarudi na kukuta minjemba wamekimbia! Walirudi kwenye ile meza yao ya awali. Wakaonekana na huzuni kidogo. Nikaona watu wengine wanacheka cheka nadhani walijua ilitokea nini. Na sisi tulitoka klabuni na ile minjemba sijui ilipotelea wapi! Naona walikodi teksi kwenda hotelini kwao.

Siku tatu zimepita, na mimi kila nikikumbuka nacheka. Jamani, hapa Marekani wakati mwingine huwezi kujua nani mwanaume, nani mwanamke. Wanawake wengine wanavaa kidume, wanatembea kidume, utadhani wanaume, na pia kuna wanaume kama hao wanapenda kuwa kama wanawake, tena ni wazuri kuliko wanawake.

Kwa hiyo, muangalie mnataka kuopoa nani. Najiuliza, je, wangefika huko hotelini sijui nani angekunjwa, maana na wale minjemba walikuwa wamekunywa hasa. Wangeenda huko hotelini na kukuta wako sawa nao, ingekuaje?!!

Mbavu sina jamani.

Saturday, June 24, 2006

Ni Summer sasa, usije ukapofuka!

Hivi sasa ni kipindi cha joto hapa Marekani, yaani Summer. Joto linavayozidi na nguo watu wanazovaa zinapungua. Wengine wanatembea nusu uchi au karibu uchi kabisa kwa vile eti joto. Wangeonja ule joto wa Tanzania, sijui wangejionaje. Labda wangetembea uchi kabisa! Wanaume wanatembea bila sharti, na wanawake wanatembea na vikaptura na viblausi kama sidiria.

Cha ajabu basi wanatembea barabarani na vinguo vyao bila aibu. Sawa ni mila ya siku hizi kuvaa nguo viduchu hivyo lakini nimeona vituko na lazima niwasimulie.
Juzi nilikuwa Roxbury, yaani ghetto ya Boston. Basi kapita mama fulani mmarekani mweusi, mtu mzima kwa mtazamo wangu labda miaka 50 na zaidi. Alikuwa amevaa kibukta na kablausi. Halafu kanyoa kipara. Uso wake ulikuwa mchanganyiko wa uso wa yule Mwimbaji Seal na yule mgombea wa Uganda Kizza! Yaani alikuwa na uso mbaya! Halafu mapaja na mikono yake ilikuwa imejaa cellulite, nyama zinacheza ovyo akitembea! DUH, alikuwa kama kinyago. Basi anatembea barabarani na watu unaona kabisa wanaona kinyaa. Hivi alijiona mzuri? Angesikia watu walivyokuwa wanamsema, bora angejifunika.

Haya mtaani kwetu Cambridge niliona mzungu mwanamke, huenda ana miaka 60. Basi naye katia kaptura, na blausi isiyo na mikono. Nguo alizovaa hazikuwa mbaya, lakini mama mwenye alikuwa na kitambi, matiti makubwa na hakuvaa sidiria, kwa hiyo akitembea matiti yana ruka hapa na pale. Hiyo blausi haikuwa na mikono na hakunyoa mavuzi kwapani, hivyo nywele zilikuwa zinaing’ingia karibu zifike kwenye kiuno chake! Alikuwa kama katuni! Naye anatembea bila kujali!

Usifikirie kuwa nasema wazee tu. Kuna ma tineja kibao wanavaa hizo vikaptura na visidiria na kujiona wazuri kabisa. Wengine wanapendeza lakini wengine wanaonekana vituko, hasa hao wasio na shepu na wanavaa nguo saizi ndogo wakati wanahitaji saizi kubwa! Hiyo ni kwa sababu hapa Marekani watu wana ugonjwa wa kutaka kuwa wembamba wakati milli yao haitaki. Pia wakienda dukani wananunua nguo eti saizi 8 wakati wanahitaji saizi 12! Basi sababu hizo nguo ndogo manyama yanaing’inginia! Unakuta visichana vidogo vidogo wana manyama nyama lakini kusudi wawe ‘fashionable’ wanavaa hivi vinguo! Hao ambao unawaona kwenye Rap video ni wazuri na wamechaguliwa kutoka kwenye mamia ya wasichana. Lakini hao wanajaribu kuwaiga na kuvaa kama wao kwa kweli! DUH, wanatisha.

Hivi mila ya summer ni kuwa mradi umefunika nyeti zako basi uko sawa? Nimesikia watu wengi, wazungu na weusi, wakilalamika kuhusu jinsi wasichana wasivyojiheshimu na kutembea nusu uchi. Kumbe watu wanajali!

Swali lingine, mbona sioni wanaume wakivaa vinguo nguo?

Haya tungojee baridi uanze tena watu wajifunika na masweta na makoti!

* Nyongeza - Jana nilimwona mama fulani naye katia fola! Huyo ana miaka 35 hivi, ni Mmarekani mweusi, ngozi yake kama ya chui, kuanzia kichwani, hadi miguuni, sijui ni ugonjwa gani! Ni mwembamba na isingekuwa huo ugonjwa wa ngozi angekuwa mzuri, na ana matako makubwa. Basi gauni kavaa shifti, fupi, ina bana anatembea anajiona mzuri! Nguo ilipanda kwenye matako basi ndo mapaja yanaonekana zaidi nayo yako kama ngozi ya chui. DOH! Anatembea na watu wanamwangalia kwa mshangao! Angekuwa Bongo tungemtupia khanga ajifunike!

Tuesday, June 13, 2006

Usicheze na Wanyama Marekani!

Duniani kuna mambo! Marekani usicheze na wanyama, wakati mwingine wanakuwa na haki kuliko bindamu.

Leo hii jamaa fulani, Christopher Guay (mzungu), kafikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa kuua ndege aina ya seagull (wale wa baharini) mjini Boston. Alisema kuwa alimwua kwa vile alikuwa anamsumbua akiwa kazini. Kazi ya Guay ni kuosha madirisha kwenye maghorofa! Lazima mmewaona wanainginia na makamba yao! Kazi hatari hiyo! Na hao seagulls wanakuwa wengi mjini japo bahari ni karibu maana wanatafuta chakula.

Ni hivi kuna mtu kwenye hiyo jengo alimwona na kapiga picha ya tukio. Yule aliyepiga picha kaipeleka kwenye MSPCA (Chama cha Kutetea Haki za Wanyama) nao wakaita polisi. Siku haijaisha Guay kufungwa jela na kufukuzwa kazi. Anaweza kufungwa gerezani miaka mitano!

Cha kushangaza zaidi ni kuwa hiyo habari imeandikwa kwenye kila gazeti, na iko kwenye kila TV stesheni mpaka CNN. Wakati mwingine mtu anaweza kuuawa na habari isiandikwe kwenye gazeti na msione kwenye TV hasa kama marehemu alikuwa ni mweusi.

- Kuna Mfanyakazi mwenzangu mzungu ambaye mbwa wake anaumwa. Jana alitumia nusu siku kwenda kumpeleka hospitali ya wanayama. Leo hakuja kabisa eti anamwuguza. Nisinge jali lakini hapa napofanya kazi kuna mwenzangu MKenya mwenye mtoto mdogo. Mtoto akiugua na inabidi ampeleke hospitalini ni maneno. Mtoto wa mzungu akiumwa wanamwambia atumie muda wowote anaohitaji!

- Nilipokuwa nafanyia zamani mwenzetu alifiwa na paka wake. Wiki mbili nzima anakuja kazini anakaa kwenye deski yake na kulia! Watu walimnunulia makadi, maua na lanchi lakini wapi! Hakufarajika kabisa! Utadhani kafiwa na mtu!

-Kuna MBongo mwenzetu hapa New England alikuwa anafuga mbuzi nyumbani kwake kwa ajili ya kula. Kuna siku majirani zake waliita polisi kwa vile mbuzi moja alitoroka. Polisi waliamua kwenda kufanya ‘search’ nyumbani kwake. Kufika basement wakaona ngozi za mbuzi ambao walichinjwa na kuliwa zamani! Alifungwa jela eti kwa kosa la jinai! Baadaye, baada ya kupata wakili mashitaka yalipunguzwa! Ubaya zaidi walitaka kumnyang’anya watoto wake waliesema eti kama mbuzi anawatesa eti, hao watoto hawako salama!

Hebu mchangie story zenu za wanyama hapa USA!

Sunday, June 11, 2006

Tumefufuka!Hapa Tumemaliza shoot ya scene yetu kwenye Aftershock! Kwenye scene weusi tuliuawa (massacre)! Tulipakwa madamu feki laini ukiona utadhani ni madamu ya kweli!

Tuliambiwa tulale chini halafu mtu wa make-up alipita na lichupa ya damu! Halafu wakati wa 'take' tuliambiwa "HOLD YOUR BREATH" yaani usipumue! Ilikuwa ni kazi!

Thursday, June 08, 2006

Aftershock - Sinema kuhusu Unyanyasaji wa WeusiScene from Aftershock

Habari zenu wapendwa wasomaji? Leo nawajulisha kuhusu sinema inaitwa Aftershock. Film iko sponosred na History Channel na itaonyeshwa kwenye History Channel. Niliwajulisha kuwa nilifanya audition kupata nafasi ya kuigiza kwenye hiyo sinema. Sikupata pati niliyofanyia audition lakini nilipata part nyingine.


Basi juzi nilienda kwenye filming huko Sutton, Massachusetts. Ni kama maili 50 kutoka Boston. Eneo enyewe ni shamba kabisa. Yaani niliposhuka kwenye gari nilifurahi kuona miti mingi, majani, sungura, kuku wanatembea wanavyotaka! Upepo ulikuwa freshi kabisa safi mno! Ama kweli kukaa mjini kunachosha.

Haya kufika kwenye seti ya film, walikuwa wameweka matenti. Moja ya chakula, moja ya make-up, nyingine ya vifaa. Gereji ya nyumba iligeuzwa 'wardobe' (nguo). Nilenda sign-in halafu moja kwa moja nilipelekwa wardrobe kuvalishwa costume. Role yangu ni 'farm hand ' yaani ni 1867 Utumwa umeisha lakini weusi wanaajiriwa kwa hela ndogo sana, na bado kuteswa na kuuliwa ovyo. Walinivalisha sketi nyeusi ndefu, apron, sharti ya dume! Sikuvaa viatu. Baada ya hapo nikaenda make-up. Kwenda huko walinipaka make-up ya uchafu! Kwa kweli ukiona picha zangu kwenye hiyo seti mini na wenzangu ni wachafu kweli kweli! Tulikuwa wachafu mpaka watu walituogopa! Tulikuwa wachafu maana tulikuwa tunalima shamba, na ilikuwa na matope shauri ya mvua! Udongo ulikuwa umejaa wadudu na minyoo wale wakubwa wakubwa (earthworms).

Halafu kulikuwa na farasi mkubwa kweli kweli! Alikuwa anaitwa Barney! Basi alikuwa anapita karibu sana kwangu lakini ali-behave. Tukaanza kuwa marafiki mpaka hapo walipoanza kufyatua marisasi na kaanza kushutuka! Ikabidi wamwondoe kwenye seti. Kaanza kutoka mapovu mdomoni kwa woga!

Niliumwa na mdudu kwenye mguu walimeta EMT (paramedic)! Fikiria walikujwa na huduma ya 911 hapo hapo! EMT’s wawili walikuwa assigned kule kwa shoot yote, pamoja na zimamoto na polisi!

Nitawajulisha zaidi...

Saturday, June 03, 2006

Historia ya weusi Marekani

Hii picha ya watoto haikupigwa Afrika! Ilipigwa Marekani 1867!

Tazama picha ya huyo mzungu (1933)! Fikiria alikuwa na haki ya kubaka mwanamke yeyote mweusi hata mtoto mdogo!

Sisi weusi tunadhani tunashida hapa Marekani. Kwa kweli tunayo lakini miaka ya nyuma ilikuwa balaa! Ubaguzi wa rangi ulikithiri zaidi ya ilivyokuwa Afrika Kusini enzi za apartheid. Nimekuwa nikifanya utafiti na habari nazo soma zinasikitisha na kutia kinyaa kabisa! Weusi waliteswa na waliuliwa ovyo ovyo! Ubaya sheria zilikuwepo za kuwalinda lakini wazungu wengi hawakujali maana walifundishwa kuwa mtu mweusi ni sawa na mnyama! Mapaka walidiriki kusema kuwa watu weusi hawasikii maumivu kama wazungu! Balaa! Basi walikuwa wanapigwa na whips kama ng'ombe na kubakia na makovu ya ajabu mwilini! Wengi wao waliopigwa hivyo walikufa!

Nilijua kuwa weusi walikuwa ni watumwa Marekani na ilitokea vita vya wenyewe kwa wenyewe (Civil War) na Rais Lincoln alisema kuwa watumwa wawe huru. Lakini baada ya hapo wazungu walijitahidi sana kurudisha weusi katika hali sawa na utumwa. Mpaka ikatokea Civil Rights movement miaka ya 1960's ndo weusi kidogo wanaonja usawa Marekani.
Weusi walikuwa na benki yao! Wazungu kuona ina pesa nyingi, walianza kugawa pesa zao kwa mikopo ovyo kwa wazungu. Benki ilikufa na pesa za weusi zilipotea. Shule na makanisa ya wesui zilichomwa moto. Miji ya weusi zilichomwa moto, Florida, Oklahoma, Arkansas na sehemu zingine! Mweusi aliweza kuliwa kwa kumtazama mzungu mwanamke au kumsemesha. Mweusi aliweza kuliwa kama mzungu akimwona anamjibu kijanja (uppity). Mweusi aliweza kuliwa kwa kutokumpisha mzungu kwenye sidewalk! Mweusi aliyejaribu kuunganisha wenzake wachukue hatua dhidi ya mateso anauliwa kwa kudaiwa ni mchochezi (troublemaker)!
Wazungu waliuwa wanawake na watoto na wazee bila kujali! Mwanamke mwenye mimba aliuliwa halafu alipasuliwa mbele za watu na mtoto kutoelewa tumboni! Mwanaume alikatwa uume (nyeti) wake! Wakati mwingine wazungu walikuwa wanafanya pikniki kabisa siku za kuua weusi! Wanamtafuta wa kumyonga hadharani, huko wazungu wanakula chakula chao na kuseherekea! Na hata hiyo kupasua wanawake wenye mimba ilitokea kwenye hizo pikniki!
Baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, wazungu hawakuwa na wafanyakazi wa kulima shmba zao. Basi waliajiri weusi kulima mashamba yao kwa pesa kidogo sana. Siku ya kuja kuchukua malipo walifukuzwa kama wanyama! Basi weusi wengi walikufa kwa njaa shauri ya kutokuwa na pesa za kununua chakula japo walizifanyia kazi!
Kuna vituko vingine vilitokea dhidi ya weusi na hatasijagusia vizuri! Na kumbuka kwa kila mweusi aliyefika akiwa hai kutoka Afrika, Waafrika wanne walikufa! Utumwa ilikuwa maangamizi ya weusi!

Weusi waliteswa. Ubaya ni kuwa unaona vijana weusi Marekani leo, wengi hawajui jinsi mababu zao walivyoteswa. Hawafundishwi shuleni. Wangejua sidhani kama wangekuwa wanaishi kwa ajili ya mabling bling na kutokujali masomo kama wanavyofanya leo!

Thursday, May 25, 2006

Taylor Hicks Ashinda American Idol 2006


Taylor Hicks, mwenye mvi na kakitambi kashinda American Idol 2006! Katharine MacPhee aliyefika mbali kwa ajili ya uzuri wake kawa wa pili. Kwa kweli Katharine sikumwona kama ana cha zaidi ila nilimwona kama 'clone' wa waimbaji waimbaji wengine. Taylor ni Taylor, mtu wa aina yake.

Safari ya Taylor mpaka kuwa mshindi ni ndefu. Kwanza Jaji Simon Cowell, hakumtaka. Waliompitisha kwenda Hollywood kwenye mashindano ni majaji Paula Abdul na Randy Jackson.
Kwenye audition Simon alimdhalisha kwa kumwambia unaonekana Mzee, unataka nini hapa.
Lakini lazima niseme kuwa siku zote Taylor alikuwa na heshima kwa wote. Pia hakuficha kuwa ni mpenzi wa muziki wa weusi hasa Ray Charles na Stevie Wonder. Wapenzi wake wanajiita Soul Patrol, na kila akiimba lazima awataje. Utasikia, Soul Patrol, Soul Patrol. Lakini nilijua kuwa anpendwa hasa nilipoona watoto wadogo wanavaa mawigi enye mvi kumwiga na kuona wanamwiga kwenye show ya vichekesho, Saturday Night Live.

Kama mliangalia show jana lazima mlifurahia. Mandisa na Paris walikuwepo pamoja na wenzao waliokuwa katika waimbaji kumi bora mwaka huu. Sijawahi kuona show ya kumaaliza season kama show ya jana. Paris alimba na Al Jarreau, Taylor alimba na Toni Braxton, Elliott alimba na Mary J. Blige, wote kumi bora waliimba na Dionne Warwick! Halafu kwa kumalizia Prince kaimba!

Namtakia mafanikio mema katika uimbaji na pia huu mwaka anayokaa kama American Idol. Kama hakujua utajiri, ataujua sasa.

Nangojea kwa hamu kuona nani atashinda American Idol 2007.

Monday, May 22, 2006

Barbaro Anusurika Kugeuzwa Gundi!

Nadhani kuna wengine hapa mnashangaa naandika kuhusu nini. Ngoja niwaeleze.

Barbaro ni farasi aliyeshinda mashindano ya Kentucky Derby hivi karibuni. Kentucky Derby ni mashindano inayofanyika kila mwaka kwa ajili ya mafarasi. Ni kama Olympiki ya farasi. Watazamaji wanavaa nguo kama vile wanakwenda kwenye arusi au kula chakula White House na MaRais. Hao farasi wana majina yao. Na wenye farasi wanatumia mapesa chungu nzima kumlea na kumfunza kukimbia kwenye mashindano. Ni sifa kubwa kuwa na farasi kwenye haya mashindano. Huwa nangojea kwa hamu Kentucky Derby kusudi nione jinsi hao mafarasi wanavyotembezwa kabla na baada ya shindano. Wanapendeza kweli hasa wakifanya miondoko (trots) yao.

Kama unajua mafarasi gani ni wazuri unaweza kutajirika maana wanawafanyia ‘betting’ (kama kamari, bahati nasibu). Ukicheza combo inayoshinda kwa dola 5 unaweza kutoka na dola zaidi ya 40,000. Halafu mashindano hayo yanakuwa sinema kabisa maana utaona watu wanvyofurahia wakishinda na wanavyolia wakishindwa. Mwaka juzi mzee wa kizungu aliyeonekana mahututi lakini alienda akiwa kwenye kiti cha wagonjwa (wheelchair) alivua Oxygen mask yake na kuanza kurukaruka farasi wake ‘Smarty Jones’ alivyoshinda. Mbona watazamaji walianza kuwa na wasiwasi kuwa atafia hapo kwenye track!

Sasa wiki mbili tu zilizopita Barbaro alishinda Kentucky Derby. Juzi maskini ya Mungu, kavunjika mguu wake vibaya akiwa kwenye mashindano ya Preakness. Loh! Watu walianguka kilio kama vile mtu kafa. Ni hivi, kwa kawaida farasi akivunjika mguu anauliwa mara moja kusudi asiteseke. Na walitakiwa wampeleke pembeni wampige risasi. Halafu nzoga ya farasi inatumika kutengeneza gundi, lakini bila shaka anagezikwa kwa heshima zote za farasi mshindi. Lakini hawakumwua. Badala yake ilitokea gari la wagonjwa (ambulance). Na walimpeleka kwenye hospitali ya wanyama wakubwa. Farasi kama umemona live ni mnyama mkubwa sana. Huko hospitalini walimpiga ma X-ray na kugundua kuwa mguu wake umevunjika vipande vipande. Basi walimfanyia upasuaji na kujaribu kutengeneza huo mguu. Upasuaji huo ulichukua muda wa masaa manane. Alivyotoka, Barbaro kaamka na kutafuta chakula na mabibi pamoja na kuwa na lizinga la POP mguuni. Cha kuchekesha watu walipeleka maua, kadi, mabango yakumtakia afya njema na apone. Huyo mtalaamu wa upasuaji wa wanyama lazima atatafutwa sana na kutengeneza kibunda kwa vile alimfanyia upasuaji mshindi wa Kentucky Derby.

Na nilisahau kuwaeleza, baada ya Barbaro kuumia, mshindi wa Preakness, Bernardini ,hakupata sifa kamili. Macho yote yakawa kwenye hali ya Barbaro. Sasa hali ya Barbaro ni habari kubwa kuliko ushindi wa Bernardini.

Haya sasa Barbaro akipona na akiweza kuishi, hatakuwa anakimbia tena. Kazi yake itakuwa ni kupanda mbegu tu! Watu watakuwa wanalipwa kusudi farasi zao majike yapate nafasi ya kupandwa mbegu na Barbaro aliyeshinda Kentucky Derby 2006!

Najua kuna wanaume lazima wanamwonea wivu! Wanafikiria kazi yake pekee ya kupanda mbegu! Haya tungojee kuona mwakani dunia ya mafarasi itakuwa na drama gani.

Friday, May 19, 2006

Wanaoigiza wabaguzi kwenye sinema si wabaguzi kweli!

Watumwa Marekani 1864


Sijui kama umewahi kuona sinema za Roots na Amistad. Hizo sinema zinahusiana na utumwa Marekani. Zilivyotengenezwa nasikia wazungu waigizaji walikuwa wanaowaombea radhi wachezaji wenzao weusi kwa vile ilibidi watukanwe na wateswe kwenye scene. Nasikia mpaka ikabidi watumie crew weusi kufungwa wachezaji weusi pingu kwa ajili ya hizo scenes kwenye films. Halafu baadaye wakawa wanasema, “I’m so sorry, but that’s not me, I’m just acting!” (yaani samahani, siyo mimi naigiza tu). Wiki hii na mimi nilionja hali hiyo.

Nilienda kwenye audition ya sinema (documentary) inayotengenezwa kwa ajili ya History Channel. Hiyo Sinema itahusu kipindi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Marekani (Civil War) iliyotokea 1861-1865 na kuangamiza mikoa ya kusini mwa nchi. Hicho kipindi kinaitwa Reconstruction (Kujenga upya).

Nikitazama vijana weusi hapa Marekani najiuliza kama wanajua historia yao na mababu zao walitokea wapi. Kwa kweli waliteswa sana na kuishi maisha iliyojaa woga na wasiwasi. Ingekuwa mimi ningesema kila mtu anayesoma shule ya msingi Marekani lazima atazame ile sinema ya Roots. Asante Civil Rights vijana weusi leo wanasoma shule na wazungu, wanakaa na wazungu, na kuingia kwenye restaurants na wazungu, pia wanaweza kwenda kwenye maduka na wazungu. Lakini wengi wa hao vijana hawajui kuwa si miaka mingi iliyopita mtu mweusi hakuwa na haki Marekani. Walikuwa wanauliwa ovyo na wazungu na hakuna aliyejali. Na hao MaKKK (Ku Klux Klan) walikuwa wanaua weusi ovyo, wakiona mweusi ana nyumba nzuri, shule, wanaichoma moto!. Basi hiyo Sinema niliyofanya audition itahusu MaKKK na jinsi walivyofanya komesha maendeleo ya weusi katika enzi za Reconstruction.

Audition enyewe ilifanyika Arlington, Massachusetts, mji ambayo si mbali na Boston. Nilipanda basi na kufika huko mapema tu. Na nawaambia Mungu ni mwema, maana siku ya kwanza waliponiita niliandika anwani walionipa. Nikapoteza ile karatasi na ikabidi nipige simu kuomba anwani tena. Kumbe ile anwani ya kwanza ilikuwa na kosa. Alisema Park St. kumbe ni Park Avenue sehemu tofauti kabisa. Na watu walipotea na wengine hawakuweza kufika kwenye auditions. Lakini nilifika bila taabu!

Nilipofika kulikuwa na mtu ndani, wanamaudition. Sikuweza kumwona lakini nilimsikia akiongea ‘lines’ kwa nguvu na kuaminika kabisa. Jinsi anayochukia weusi na yuko tayari kuwaua. Jamani msishangae maana ilikuwa script enyewe. Basi, yule baba actor alitoka, mtu mzima labda miaka 50, alionekana kushutuka alivyoniona na kawa mwekundu usoni. Kanisalimia vizuri tu halafu kanishika bega kwa urafiki kabisa na kanitazama kama vile ananiomba msamaha, na mimi nilitabasamu kama ishara kumwonyesha asijali na wala asidhanie namchukia.

Line enyewe ni hii: (landowner): “You have been fooled by the damn Yankee lies till you thought you were free, and you got so you could not obey your master. There is no law against killing ( n-words) and I will kill every damned one I have if they do not obey me and work just as hard as they did before the war.”

Basi kulikuwa na kijana mwingine mzungu, mwembamba. Duh, sijui jamaa alikuwa mwoga. Alivyokuwa anatembea hapa na pale na majasho yanamtoka huko anasubiri zamu yake. Halafu kashindwa hata kutamka maneno. Alisoma sehemu ya kwanza nikamsikia Director akisema hatafaa hiyo part kwa hiyo asome nyingine. Kasoma ile nyingine ya kutumia ile tusi ya n-word, na maskini ilimshinda kabisa. Nikajua hajazoea kutumia hiyo neno na nikashukuru lakini nikasema kama ni actor ni lazima uweke maoni yako pembeni na kufanya kama director anvyotaka.

Basi jamaa katoka, nikamwambia ‘Good Luck” (Ukienda kwenye audition ni mila na desturi kumtakia mwenzako heri )!

Basi Director katoka na hakuona mtu. Yule director alikuwa na mshangao mkubwa kutokuona watu maana karibu watu mia walijiandikisha kufika. Headshots zilipangwa kufuatana na time watu waliopangiwa. Yangu haikuwa chini sana.

Kuingia mle, yule Director akawa anaomba msamaha kwa hiyo ‘sensitive’ topiki. Nikamwambia kuwa ninaelewa kuwa kipindi kile kilikuwa ni kigumu.

Basi niliambiwa niseme line, kwa ajili ya kupima ‘delivery’ yangu, yaani jinsi unavyoongea. Basi nikasema. Haya ikaja sehemu mbaya sasa. Hiyo scene inahusu familia ya weusi kuzungukwa na kupigwa na MaKKK. Basi ikabidi nijifanye kama vile nimepigwa na huko mwanangu mwenye miaka sita kapigwa pia. Loh! Nilianguka kilio. Nilikuwa nimaabiwa audition itachuka dakika 5 lakini yangu ilikuwa kama robo saa na niliweza kufanya mengi. Nilivyomaliza Director na msaidizi walitoka na kunipa mkono na kuniuliza kuhusu schedule yangu. Na amini usiamini nilivyotoka na potential actors wengine wakaanza kuja asante cell phones. Jamaa moja kawa analimika kuwa huko Park St. ilikuwa nyumba ya mtu na karibu anga'twe na mbwa.

Nadhani nilfanya vizuri, lakini mjue katika acting, tuko wengi na si ajabu nyuma yangu walikuja actors wazuri zaidi. Ila najua nilikuwa mwanamke wa kwanza mweusi kufanya audition. Pia yote ilikuwa filmed. Kwa hiyo wataweza kupima kutokana na wanachoona kwenye test film. Ujue kuna kitu kinaitwa ‘stage presence’ kwa hiyo mtu anaweza ku-acti lakini asiwe na presence. Kwa kweli acting, na kutengeneza filamu ni kazi ngumu. Msione hivyo.

Nitawajulisha kama nikichaguliwa kuwa kwenye hiyo sinema!

Thursday, May 11, 2006

American Idol Inashangaza Mwaka huu!

kuanzia kushoto (Elliot, Chris, Katharine & Taylor)


Haya wapenzi wa American Idol, pigo lingine! Chris Daughtry, aliyetabiriwa kushinda mwaka huu katolewa jana! Majaji, na watazamaji walibakia kushangaa. Tulisikia watu waliokuwa studi wakilia, "Noooooo!"! Lakini haikufikia mshangao kama siku ile alivyotolewa Dada Mandisa.

Sasa wamebakia Taylor Hicks (mwenye mvi), Eliiot Yamin (MYehudi na anaumwa ugonjwa wa kisukari), na yule dada aliyesoma Boston Conservatory, Katharine MacPhee. Nani atashinda! Inabidi tungojee May 24th kupata jibu.

Lakini ukweli watu wengi wanashangaa maana kwa wanaume waliobakia hakuna ambaye ungeweza kusema atakuwa ni Idol. Kwanza Taylor ana miaka 29 na ana mvi kibao wengine wanamwita, 'The Old Guy' (Mzee). Lakini jamaa ana character, utampenda tu, ni mcheshi sana na lazima akimaliza kuimba utabakia aunatabasamu. Sasa huyo Elliot wengine wamesema ana sura mbaya, halafu wanamchukia kwa vile Myehudi. Ndio Marekani bado kuna chuki dhidi ya waYehudi. Halafu Elliott mara nyingi anaonekana mwoga na kutoka majasho akiimba. Lakini ana sauti nzuri kiasi.

Haya nimchambue huyo Katharine MacPhee. Hao mibaba wa kizungu inasema, "She's Hot!" Yaani mzuri mno! Mara wapambe wa American Idol wamvalishe nguo mbaya mara nini, lakini bado wanasema ni mzuri mno. Ana sauti nzuri kushinda wanawake wa kizungu wote waliokuwepo mwaka huu. Lakini watu wanachoona ni uzuri wake. Na wiki hii Katharine ndo aliimba vibaya kuliko wote. Alisahau na maneno ya wimbo. Lakini kapita shauri ya uzuri.

Wiki iliyopita alitolewa mweusi pekee aliyebaki, Paris Bennett. Huyo alikuwa na sauti nzuri kuliko wote katika mashindano safari hii, lakini nilijua hatafika mbali, maana bibi yake ni mwimbabji mashahuri na anatuzo za Grammy. Watu walikuwa wanalamika kuwa kwa nini Paris awe kwenye show wakati ana ndugu ambao wanaweza kumsaidia kupata mkataba.

Lakini kulikuwa na njama ya kutoa weusi mapema. Mwanaume mwenye sauti bora kuliko wanaume wote, kijana mweusi Gedeon, alitolewa kwenye Top 24. Na watu walisema kuwa si siri kuwa mwaka huu Producers wa show wanataka mwanaume mzungu ashinde. Kwanza walimpampu huyo Ace kuwa sex symbol, mpaka kumfanyia camera angles na ma close up! Lakini hazikusaidia katolewa wiki kadhaaa zilizopita! Jamaa hakuwa na sauti nzuri, na hata huo uzuri wa sura sijaona. Lakini nasikia anatakoa kwenye gazeti la 'Playgirl' kwa hiyo huenda ni kweli ni sex symbol ana uzuri sehemu nyingine.

Haya, tutaona mwaka huu nani atashinda na kuungana na klabu ya American Idols. Washindi wa miaka ya nyuma ni Kelly Clarkson, Ruben Studdard, Fantasia Barrino, na Carrie Underwood.
Ukweli American Idol umekuwa ni nani anapendwa zaidi, na siyo nani ana sauti bora. Mnaonaje?

Tuesday, April 25, 2006

Miaka baada ya Tukio kaniomba Msamaha!

Nilipokuwa Jeshi ya Kujenga Taifa (JKT) karibu nibakwe na afande Fulani (jina nahifadhi). Lazima niseme kuwa katika kipindi hicho wanaume wengi waliona makambi ya JKT kama ‘buffet’ ya wasichana. Si maafande wa jeshi tu, bali hata viongozi wa serikali walikuwa wanapitia makambi ya JKT kula tani yao!

Mimi nilikuwa Masange JKT, Tabora. Wakati huo huyo jamaa alikuwa ni Kepiteni wa JKT. Nadhani alidhania kwa vile yeye ni kepiteni basi alikuwa na haki ya kutembea na yeyote aliyemtaka. Kwangu aligonga ukuta! Bila shaka alikuwa hajawahi ‘kunyimwa’ mpaka siku hiyo alipokutana na mimi.

Miaka baada ya tukio nikiwa nafanya kazi Daily News mara nyingi nilikuwa napishana naye Posta Mpya. Basi ananisemesha, na mimi namnunia halafu napita zangu kimya bila kumjibu kwa hasira. Siku moja kanisimamisha kaniambia, "Chemi, naomba msamaha, nisemahe tafadhali, kweli nilikukosea!” Aliongeza kuwa miaka mingi imepita hivyo sina sababu ya kuwa na hasira naye! Na mimi nilimjibu, “Mshenzi sana wewe!” nikaenda zangu.

Ikapita kama mwaka nyingine. Jamaa anaendelea kunisalimia kila nikimpita njiani na mimi kwa uchungu bado nikashindwa kusema kitu. Basi nikafikiria alichoniambia Posta Mpya. Lakini nilona kama jambo hilo linamsumbua. Na nikasema kama Bwana Yesu aliweza kusamehe watu kwa madhambi yao kwa nini mimi nisimsamehe. Basi baada ya hapo ikiwa nikimwona na akinisalimia naitika na naendelea zangu na nikaona kidogo hata yeye alikuwa na raha. Lakini bado najiuliza kama kitendo chake kilimsumbua miaka na miaka kama ilivyonisumbua mimi.

Unauliza ilikuaje mpaka nikajikuta kwenye situation ya kubakwa. Au mnasema nilitaka mwenyewe. Ngoja niwaelezee ilivyokuwa. Nilikuwa mhudumu Officer’s Mess, mpishi na msafishaji. Huyo jamaa alikuwa ni mgeni kutoka Makao Makuu ya JKT Dar es Salaam. Kwa kweli sikutaka kufanya kazi pale Mess lakini tulichaguliwa special na Matron, mimi kwa vile niijua kupika vyakula mbalimbali hasa za kizungu. Lakini uzuri wa hiyo kazi ni kuwa uanambulia mabaki ya vyakula (leftovers), na mara nyingine kulikuwa hakuna.

Basi huyo Afande alikaa kambini wiki kadhaa. Katika kumhudumia tukawa tunaongea na mimi nikawa namheshimu kama kaka vile. Wala sikusikia mapenzi yoyote kwake. Basi jioni fulani, kanialika chumbani kwake kunywa soda na biskuti na kwa Maongezi zaidi. Sasa kama ulienda jeshi unajua njaa kali unayokuwa nayo. Nikaenda, kanikaribisha vizuri, nilipewa soda na tukawa tunaongea. Basi nikaona mwenzangu anabadilika ghafla! Mara ananikumbatia kwa nguvu, na kunibusu na mengine. Nikajaribu kuaga lakini jamaa hakuniachia. Baada ya ku-plead naye aniachie, kaniachia. Kaomba msamaha na kaniomba niendelee kukaa nimalize hizo soda alizoninulia. Kama mjinga nikamwamini, nikakaa nakunywa hizo soda. Tukaendelea na Maongezi, kukaa kidogo huyo kanirukia, najaribu kusimama huyo, kanivuta na kuniangusha kitandani! Mimi saa hizo nikawa naogopa kabisa nia yake!

Kaniambia eti, “ukipiga makelele najua nitasema nini! Nyamaza! Huna sababu ya kunikatalia!” LOH! Kanizaba na kibao! Nikamwuliza kwa nini anaifanyia hivyo, na mimi nilikuwa namwona kama kaka yangu!

Hapo sasa ikaniingia. Nabakwa! Loh! Nilimpiga mangumi na mateke lakini jamaa alikuwa na nguvu huyo kachana chupi yangu! Baada ya hapo, jamaa kashika miguu yangu huko anafoka kwa sauti kama vile anatoa amri “panua miguu! PANUA MIGUU!” Huko katoa ume wake uliyosimama kwenye suruali! Basi kuona sipanui jamaa kaongeza makofi na kafanikiwa kupanua miguu yangu! Kuona kafanikiwa kupanua huyo kajaribu kupenya. Ilipogusa kwangu nilipiga kelele cha kufa! Nikasema, “Nakuufaaaa!” Heh! Ghafla jamaa kaniachia kaniambia niende. Alisema, “Nimeigusa na ume wangu, unatosha!” Nenda zako! Na ukimwambia mtu najua nitasema nini!”

Loh nilikimbia bwenini na giza lile la Masange huko nalia. Wenzangu wananiuliza vipi, nikashindwa niseme nini! Kwanza niliona haya! Fikiria, niliona haya (shame)!

Kesho yake nikaenda dispensary na kujiandikisha mgonjwa. Sikwenda kazini Officer's Mess bali nililala bwenini. Siku iliyofuatia huyo Afande mshenzi kapita bwenini kwetu kaulizia hali yangu, na mimi huko natetemeka kwa woga nikashindwa niseme nini. Alininunulia Orange squash na biskuti na kuzileta bwenini. Sitasahau alivyonitazama! Ilikuwa kama vile anapanga jinsi gani atanipata.

Baada ya hapo alimwopoa msichana mwingine na huyo alimkubali kabisa. Akawa analala kabisa huko Officer’s Mess. Hakuna anayemsumbua wakijua ni bibi wa Afisa. Basi, siku za yule jamaa kukaa kambini zikaisha, na yule binti alienda naye Tabora mjini kwa siku kadhaa. Halafu jamaa karudi zake DSM. Yule binti karudi zake kambini! Kumbe alienda bila pass. Alidhania kwa vile yuko na mkubwa hana haja ya pass. Na yule Afande ndo kaondoka kimoja! Maafande waliobakia wacha wamtese huyo binti alivyorudi kambini! Walimtesa kwa Extra drill na mengine mpaka ikabidi Military Police waombe wakuu wamsamehe la sivyo atakufa. Raha yake iliishia kwa suluba! Sijui yule binti alidhania jamaa atamwoa! Kwa nini alimkubali yule mshenzi. Anyway, kila mtu na vyake. Alivyotoka kwenye suluba tulimwuguza! Siku haizkupita na mimi nilitolewa kazi Officer’s Mess na kupelekwa kwenye kikosi cha Ujenzi na lazima nisema hapo nilifurahi sana.

Basi miaka ilipita. Mimi nilikuwa mwandishi wa habari Daily News, tena nilijenga jina. Sasa nikawa napishana na yule jamaa huko kapandishwa cheo na yuko JWTZ. Jamaa anajaribu kunisalimia na mimi napita zangu kimya, namnunia kabisa. Nilimwona mshenzi, mnyama, na kila kitu kibaya ndo ilikuwa yeye! Angefanikiwa kuingiza na kunimwagia uchafu wake ningejiona mchafu mpaka leo! Miaka kama 20 imepita sasa na bado nina uchungu naye.

Jamani nyie wanaume nawaambia kubaka kinaathari zake kwa wanawake. Unataka raha ya dakika na unamwachia mwenzio na uchungu wa maisha! Wengine mpaka wanakuwa wagonjwa wa akili.

Kwa nini nimeamua kuzungumzia kubakwa kwangu hapa, ni kwa sababu naona wasichana wengi wanabakwa, halafu wanaamua kunyamaza kimya. Kisa wakienda polisi na hospitali wanahofia kuambiwa ni Malaya au walitaka wenyewe! Hata mwamanke mwenzako anaweza kukufokea kuwa ulitaka mwenyewe.

Tanzania, wanaume walikuwa na usemi wao kuhusu wanawake na ngono. Walisema eti ukimwomba mwanamke halafu akijibu ndiyo, manake ndiyo atafanya. Akisema labda, manake atafanya, akisema hapana, manake hapana. Lakini jamani tendo si inakuwa tamu kama wote mmekubali? Na kama angefanikiwa kuingiza si angeniumiza sana!

Wengine wanasema ningemshitaki. Je, ningemshitaki ingekuaje? Kwanza jeshini mimi ningepewa Extra Drill mpaka niumie au kufungwa jela ya jeshi iliyojaa maji na mbu kusudi niteswe. Kumbuka ilikuwa Tanzania na yule alikuwa ni Kepiteni wakati huo na mimi nilikuwa Private. Hakuna ambaye angekuwa tayari kunisikia zaidi ya wenzangu maPrivate, na yeye alijua hivyo. SHENZI TAIPU!