Thursday, May 25, 2006

Taylor Hicks Ashinda American Idol 2006


Taylor Hicks, mwenye mvi na kakitambi kashinda American Idol 2006! Katharine MacPhee aliyefika mbali kwa ajili ya uzuri wake kawa wa pili. Kwa kweli Katharine sikumwona kama ana cha zaidi ila nilimwona kama 'clone' wa waimbaji waimbaji wengine. Taylor ni Taylor, mtu wa aina yake.

Safari ya Taylor mpaka kuwa mshindi ni ndefu. Kwanza Jaji Simon Cowell, hakumtaka. Waliompitisha kwenda Hollywood kwenye mashindano ni majaji Paula Abdul na Randy Jackson.
Kwenye audition Simon alimdhalisha kwa kumwambia unaonekana Mzee, unataka nini hapa.
Lakini lazima niseme kuwa siku zote Taylor alikuwa na heshima kwa wote. Pia hakuficha kuwa ni mpenzi wa muziki wa weusi hasa Ray Charles na Stevie Wonder. Wapenzi wake wanajiita Soul Patrol, na kila akiimba lazima awataje. Utasikia, Soul Patrol, Soul Patrol. Lakini nilijua kuwa anpendwa hasa nilipoona watoto wadogo wanavaa mawigi enye mvi kumwiga na kuona wanamwiga kwenye show ya vichekesho, Saturday Night Live.

Kama mliangalia show jana lazima mlifurahia. Mandisa na Paris walikuwepo pamoja na wenzao waliokuwa katika waimbaji kumi bora mwaka huu. Sijawahi kuona show ya kumaaliza season kama show ya jana. Paris alimba na Al Jarreau, Taylor alimba na Toni Braxton, Elliott alimba na Mary J. Blige, wote kumi bora waliimba na Dionne Warwick! Halafu kwa kumalizia Prince kaimba!

Namtakia mafanikio mema katika uimbaji na pia huu mwaka anayokaa kama American Idol. Kama hakujua utajiri, ataujua sasa.

Nangojea kwa hamu kuona nani atashinda American Idol 2007.

Monday, May 22, 2006

Barbaro Anusurika Kugeuzwa Gundi!





Nadhani kuna wengine hapa mnashangaa naandika kuhusu nini. Ngoja niwaeleze.

Barbaro ni farasi aliyeshinda mashindano ya Kentucky Derby hivi karibuni. Kentucky Derby ni mashindano inayofanyika kila mwaka kwa ajili ya mafarasi. Ni kama Olympiki ya farasi. Watazamaji wanavaa nguo kama vile wanakwenda kwenye arusi au kula chakula White House na MaRais. Hao farasi wana majina yao. Na wenye farasi wanatumia mapesa chungu nzima kumlea na kumfunza kukimbia kwenye mashindano. Ni sifa kubwa kuwa na farasi kwenye haya mashindano. Huwa nangojea kwa hamu Kentucky Derby kusudi nione jinsi hao mafarasi wanavyotembezwa kabla na baada ya shindano. Wanapendeza kweli hasa wakifanya miondoko (trots) yao.

Kama unajua mafarasi gani ni wazuri unaweza kutajirika maana wanawafanyia ‘betting’ (kama kamari, bahati nasibu). Ukicheza combo inayoshinda kwa dola 5 unaweza kutoka na dola zaidi ya 40,000. Halafu mashindano hayo yanakuwa sinema kabisa maana utaona watu wanvyofurahia wakishinda na wanavyolia wakishindwa. Mwaka juzi mzee wa kizungu aliyeonekana mahututi lakini alienda akiwa kwenye kiti cha wagonjwa (wheelchair) alivua Oxygen mask yake na kuanza kurukaruka farasi wake ‘Smarty Jones’ alivyoshinda. Mbona watazamaji walianza kuwa na wasiwasi kuwa atafia hapo kwenye track!

Sasa wiki mbili tu zilizopita Barbaro alishinda Kentucky Derby. Juzi maskini ya Mungu, kavunjika mguu wake vibaya akiwa kwenye mashindano ya Preakness. Loh! Watu walianguka kilio kama vile mtu kafa. Ni hivi, kwa kawaida farasi akivunjika mguu anauliwa mara moja kusudi asiteseke. Na walitakiwa wampeleke pembeni wampige risasi. Halafu nzoga ya farasi inatumika kutengeneza gundi, lakini bila shaka anagezikwa kwa heshima zote za farasi mshindi. Lakini hawakumwua. Badala yake ilitokea gari la wagonjwa (ambulance). Na walimpeleka kwenye hospitali ya wanyama wakubwa. Farasi kama umemona live ni mnyama mkubwa sana. Huko hospitalini walimpiga ma X-ray na kugundua kuwa mguu wake umevunjika vipande vipande. Basi walimfanyia upasuaji na kujaribu kutengeneza huo mguu. Upasuaji huo ulichukua muda wa masaa manane. Alivyotoka, Barbaro kaamka na kutafuta chakula na mabibi pamoja na kuwa na lizinga la POP mguuni. Cha kuchekesha watu walipeleka maua, kadi, mabango yakumtakia afya njema na apone. Huyo mtalaamu wa upasuaji wa wanyama lazima atatafutwa sana na kutengeneza kibunda kwa vile alimfanyia upasuaji mshindi wa Kentucky Derby.

Na nilisahau kuwaeleza, baada ya Barbaro kuumia, mshindi wa Preakness, Bernardini ,hakupata sifa kamili. Macho yote yakawa kwenye hali ya Barbaro. Sasa hali ya Barbaro ni habari kubwa kuliko ushindi wa Bernardini.

Haya sasa Barbaro akipona na akiweza kuishi, hatakuwa anakimbia tena. Kazi yake itakuwa ni kupanda mbegu tu! Watu watakuwa wanalipwa kusudi farasi zao majike yapate nafasi ya kupandwa mbegu na Barbaro aliyeshinda Kentucky Derby 2006!

Najua kuna wanaume lazima wanamwonea wivu! Wanafikiria kazi yake pekee ya kupanda mbegu! Haya tungojee kuona mwakani dunia ya mafarasi itakuwa na drama gani.

Friday, May 19, 2006

Wanaoigiza wabaguzi kwenye sinema si wabaguzi kweli!

Watumwa Marekani 1864


Sijui kama umewahi kuona sinema za Roots na Amistad. Hizo sinema zinahusiana na utumwa Marekani. Zilivyotengenezwa nasikia wazungu waigizaji walikuwa wanaowaombea radhi wachezaji wenzao weusi kwa vile ilibidi watukanwe na wateswe kwenye scene. Nasikia mpaka ikabidi watumie crew weusi kufungwa wachezaji weusi pingu kwa ajili ya hizo scenes kwenye films. Halafu baadaye wakawa wanasema, “I’m so sorry, but that’s not me, I’m just acting!” (yaani samahani, siyo mimi naigiza tu). Wiki hii na mimi nilionja hali hiyo.

Nilienda kwenye audition ya sinema (documentary) inayotengenezwa kwa ajili ya History Channel. Hiyo Sinema itahusu kipindi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Marekani (Civil War) iliyotokea 1861-1865 na kuangamiza mikoa ya kusini mwa nchi. Hicho kipindi kinaitwa Reconstruction (Kujenga upya).

Nikitazama vijana weusi hapa Marekani najiuliza kama wanajua historia yao na mababu zao walitokea wapi. Kwa kweli waliteswa sana na kuishi maisha iliyojaa woga na wasiwasi. Ingekuwa mimi ningesema kila mtu anayesoma shule ya msingi Marekani lazima atazame ile sinema ya Roots. Asante Civil Rights vijana weusi leo wanasoma shule na wazungu, wanakaa na wazungu, na kuingia kwenye restaurants na wazungu, pia wanaweza kwenda kwenye maduka na wazungu. Lakini wengi wa hao vijana hawajui kuwa si miaka mingi iliyopita mtu mweusi hakuwa na haki Marekani. Walikuwa wanauliwa ovyo na wazungu na hakuna aliyejali. Na hao MaKKK (Ku Klux Klan) walikuwa wanaua weusi ovyo, wakiona mweusi ana nyumba nzuri, shule, wanaichoma moto!. Basi hiyo Sinema niliyofanya audition itahusu MaKKK na jinsi walivyofanya komesha maendeleo ya weusi katika enzi za Reconstruction.

Audition enyewe ilifanyika Arlington, Massachusetts, mji ambayo si mbali na Boston. Nilipanda basi na kufika huko mapema tu. Na nawaambia Mungu ni mwema, maana siku ya kwanza waliponiita niliandika anwani walionipa. Nikapoteza ile karatasi na ikabidi nipige simu kuomba anwani tena. Kumbe ile anwani ya kwanza ilikuwa na kosa. Alisema Park St. kumbe ni Park Avenue sehemu tofauti kabisa. Na watu walipotea na wengine hawakuweza kufika kwenye auditions. Lakini nilifika bila taabu!

Nilipofika kulikuwa na mtu ndani, wanamaudition. Sikuweza kumwona lakini nilimsikia akiongea ‘lines’ kwa nguvu na kuaminika kabisa. Jinsi anayochukia weusi na yuko tayari kuwaua. Jamani msishangae maana ilikuwa script enyewe. Basi, yule baba actor alitoka, mtu mzima labda miaka 50, alionekana kushutuka alivyoniona na kawa mwekundu usoni. Kanisalimia vizuri tu halafu kanishika bega kwa urafiki kabisa na kanitazama kama vile ananiomba msamaha, na mimi nilitabasamu kama ishara kumwonyesha asijali na wala asidhanie namchukia.

Line enyewe ni hii: (landowner): “You have been fooled by the damn Yankee lies till you thought you were free, and you got so you could not obey your master. There is no law against killing ( n-words) and I will kill every damned one I have if they do not obey me and work just as hard as they did before the war.”

Basi kulikuwa na kijana mwingine mzungu, mwembamba. Duh, sijui jamaa alikuwa mwoga. Alivyokuwa anatembea hapa na pale na majasho yanamtoka huko anasubiri zamu yake. Halafu kashindwa hata kutamka maneno. Alisoma sehemu ya kwanza nikamsikia Director akisema hatafaa hiyo part kwa hiyo asome nyingine. Kasoma ile nyingine ya kutumia ile tusi ya n-word, na maskini ilimshinda kabisa. Nikajua hajazoea kutumia hiyo neno na nikashukuru lakini nikasema kama ni actor ni lazima uweke maoni yako pembeni na kufanya kama director anvyotaka.

Basi jamaa katoka, nikamwambia ‘Good Luck” (Ukienda kwenye audition ni mila na desturi kumtakia mwenzako heri )!

Basi Director katoka na hakuona mtu. Yule director alikuwa na mshangao mkubwa kutokuona watu maana karibu watu mia walijiandikisha kufika. Headshots zilipangwa kufuatana na time watu waliopangiwa. Yangu haikuwa chini sana.

Kuingia mle, yule Director akawa anaomba msamaha kwa hiyo ‘sensitive’ topiki. Nikamwambia kuwa ninaelewa kuwa kipindi kile kilikuwa ni kigumu.

Basi niliambiwa niseme line, kwa ajili ya kupima ‘delivery’ yangu, yaani jinsi unavyoongea. Basi nikasema. Haya ikaja sehemu mbaya sasa. Hiyo scene inahusu familia ya weusi kuzungukwa na kupigwa na MaKKK. Basi ikabidi nijifanye kama vile nimepigwa na huko mwanangu mwenye miaka sita kapigwa pia. Loh! Nilianguka kilio. Nilikuwa nimaabiwa audition itachuka dakika 5 lakini yangu ilikuwa kama robo saa na niliweza kufanya mengi. Nilivyomaliza Director na msaidizi walitoka na kunipa mkono na kuniuliza kuhusu schedule yangu. Na amini usiamini nilivyotoka na potential actors wengine wakaanza kuja asante cell phones. Jamaa moja kawa analimika kuwa huko Park St. ilikuwa nyumba ya mtu na karibu anga'twe na mbwa.

Nadhani nilfanya vizuri, lakini mjue katika acting, tuko wengi na si ajabu nyuma yangu walikuja actors wazuri zaidi. Ila najua nilikuwa mwanamke wa kwanza mweusi kufanya audition. Pia yote ilikuwa filmed. Kwa hiyo wataweza kupima kutokana na wanachoona kwenye test film. Ujue kuna kitu kinaitwa ‘stage presence’ kwa hiyo mtu anaweza ku-acti lakini asiwe na presence. Kwa kweli acting, na kutengeneza filamu ni kazi ngumu. Msione hivyo.

Nitawajulisha kama nikichaguliwa kuwa kwenye hiyo sinema!

Thursday, May 11, 2006

American Idol Inashangaza Mwaka huu!

kuanzia kushoto (Elliot, Chris, Katharine & Taylor)


Haya wapenzi wa American Idol, pigo lingine! Chris Daughtry, aliyetabiriwa kushinda mwaka huu katolewa jana! Majaji, na watazamaji walibakia kushangaa. Tulisikia watu waliokuwa studi wakilia, "Noooooo!"! Lakini haikufikia mshangao kama siku ile alivyotolewa Dada Mandisa.

Sasa wamebakia Taylor Hicks (mwenye mvi), Eliiot Yamin (MYehudi na anaumwa ugonjwa wa kisukari), na yule dada aliyesoma Boston Conservatory, Katharine MacPhee. Nani atashinda! Inabidi tungojee May 24th kupata jibu.

Lakini ukweli watu wengi wanashangaa maana kwa wanaume waliobakia hakuna ambaye ungeweza kusema atakuwa ni Idol. Kwanza Taylor ana miaka 29 na ana mvi kibao wengine wanamwita, 'The Old Guy' (Mzee). Lakini jamaa ana character, utampenda tu, ni mcheshi sana na lazima akimaliza kuimba utabakia aunatabasamu. Sasa huyo Elliot wengine wamesema ana sura mbaya, halafu wanamchukia kwa vile Myehudi. Ndio Marekani bado kuna chuki dhidi ya waYehudi. Halafu Elliott mara nyingi anaonekana mwoga na kutoka majasho akiimba. Lakini ana sauti nzuri kiasi.

Haya nimchambue huyo Katharine MacPhee. Hao mibaba wa kizungu inasema, "She's Hot!" Yaani mzuri mno! Mara wapambe wa American Idol wamvalishe nguo mbaya mara nini, lakini bado wanasema ni mzuri mno. Ana sauti nzuri kushinda wanawake wa kizungu wote waliokuwepo mwaka huu. Lakini watu wanachoona ni uzuri wake. Na wiki hii Katharine ndo aliimba vibaya kuliko wote. Alisahau na maneno ya wimbo. Lakini kapita shauri ya uzuri.

Wiki iliyopita alitolewa mweusi pekee aliyebaki, Paris Bennett. Huyo alikuwa na sauti nzuri kuliko wote katika mashindano safari hii, lakini nilijua hatafika mbali, maana bibi yake ni mwimbabji mashahuri na anatuzo za Grammy. Watu walikuwa wanalamika kuwa kwa nini Paris awe kwenye show wakati ana ndugu ambao wanaweza kumsaidia kupata mkataba.

Lakini kulikuwa na njama ya kutoa weusi mapema. Mwanaume mwenye sauti bora kuliko wanaume wote, kijana mweusi Gedeon, alitolewa kwenye Top 24. Na watu walisema kuwa si siri kuwa mwaka huu Producers wa show wanataka mwanaume mzungu ashinde. Kwanza walimpampu huyo Ace kuwa sex symbol, mpaka kumfanyia camera angles na ma close up! Lakini hazikusaidia katolewa wiki kadhaaa zilizopita! Jamaa hakuwa na sauti nzuri, na hata huo uzuri wa sura sijaona. Lakini nasikia anatakoa kwenye gazeti la 'Playgirl' kwa hiyo huenda ni kweli ni sex symbol ana uzuri sehemu nyingine.

Haya, tutaona mwaka huu nani atashinda na kuungana na klabu ya American Idols. Washindi wa miaka ya nyuma ni Kelly Clarkson, Ruben Studdard, Fantasia Barrino, na Carrie Underwood.
Ukweli American Idol umekuwa ni nani anapendwa zaidi, na siyo nani ana sauti bora. Mnaonaje?