Wednesday, September 25, 2013

Al Shaabab ni Nani?Al Shaabab Ni Nani? ( Makala Raia Mwema)

Na Maggid Mjengwa,

ULIMWENGU umepatwa na mshtuko mkubwa kwa kuona picha za tukio kubwa la kigaidi kwenye moja ya maduka makubwa jijini Nairobi. Hili ni shambulio kubwa la kigaidi kupata kutokea Afrika Mashariki tangu lile la mwaka 1998. Na ajabu ya kihitoria ni kuwa matukio mengi ya kigaidi yametokea katika mwezi wa Septemba.

La Nairobi ni shambulizi la kigaidi la kulaaniwa vikali na wapenda amani wote ulimwenguni. Hata hivyo, moja ya tafsiri ya vitendo vya kigaidi tunavyovishuhudia Nairobi ni kuwepo kwa hali ya vita vya kigaidi vyenye kuendeshwa kwenye maeneo ya mijini (Urban terrorism).

Ni shambulizi lenye athari mbaya kiuchumi si tu kwa nchi ya Kenya, bali hata majirani zake ikiwemo Tanzania. Ni shambulizi lililowaogopesha wageni wengi wakiwamo wawekezaji pia. Kwamba Al Shabaab inalenga pia nchi za Magharibi. Hivyo basi, hata raia wake. Kunahitajika jitihada za pamoja kuwaondoa hofu watu wa mataifa ya nje, kuwa kilichotokea Nairobi kitadhibitiwa kwa njia zote, kisitokee tena.
Na hakika, aina hii ya ugaidi ni ngumu sana kudhibitika hatakama nchi ina jeshi kubwa na lenye vifaa vya kisasa. Inahitaji ushiriki wa raia wema katika kutoa taarifa za wahalifu hata kabla hawajafanya matendo yao maovu. Inahitaji pia maandalizi makini, ya kuwa na vikosi vilivyo tayari wakati wote kukabiliana na matukio kama haya.

Ni dhahiri, kuwa mbinu inazotumika kikundi cha kigaidi cha Al Shaabab ambacho maana hasa ya jina hilo ni ' Vijana', ni moja ya changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Al Shabaab iliundwa mwaka 2006. Kinasemekana kuwa na wapiganaji wenye silaha wapatao 10,000. Al Shabaab katika miaka ya karibuni wamepoteza maeneo mengi ya mijini waliyokuwa wakiyadhibiti, ikiwamo mji wa Kismayu ambao majeshi ya Kenya yaliudhibiti baada ya kuwasambaratisha Al Shabaab. Kwa sasa Al Shabaab bado wana nguvu maeneo ya vijijini katika Somalia.

Kufuatia Kenya kujiingisha kijeshi kupanbana na Al Shaabab, kikundi hicho kimeifanya Kenya kuwa adui na kutangaza wazi azma yake ya kuishambulia Kenya. Mwezi Aprili mwaka huu watu watano walipoteza maisha nchini Kenya baada ya wapiganaji wa Al Shabaab kuingia kwa nguvu wakiwa na silaha kwenye mgahawa mmoja kwenye mji wa Garissa nchini Kenya.

Mwaka 2012 ndipo Al Shabaab walipojiunga rasmi na mtandao wa kigaidi wa Al qaida chini ya kiongozi wa Al qiada, Ayman al- Zawahiri.
Hakika, hapa duniani matukio ya kigaidi yameongezeka.
Kwa faida ya wasomaji, nitaanza kwa kuangalia chimbuko la ugaidi kihistoria. Ni rahisi kusema kwamba ulimwengu umebadilika baada ya ugaidi wa Septemba 11 mwaka 2001 kule Marekani. Kwamba ugaidi umesogea karibu zaidi katika fikra zetu. Watanzania bado tunakumbuka tukio la shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la Ubalozi wa Marekani jijini Dar Es Salaam Agosti 7, 1998.

Sura ya ugaidi imeonekana vema zaidi miongoni mwa walimwengu. Bila shaka, picha ya filamu ya televisheni yenye kuonesha majengo mawili ya World Trade Centre kule Marekani yakitunguliwa na kuanguka, zimeonwa na takribani asilimia 75 ya watu wa ulimwengu huu. Katika hili la kuchambua ugaidi, hebu
basi tuanze na kujiuliza; Ugaidi ni nini?

Itakumbukwa wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano walipokutana Dodoma mwaka 2002 walipitisha Muswaada wa Ugaidi. Wabunge wetu walitumia muda mwingi sana kujadili tafsiri ya neno "ugaidi".
Kwa kifupi, ugaidi ukitafsiri kutoka neno la Kiingereza "Terrorism" tunapata maana ya "hofu". Neno la Kiingereza "Terror" lina maana ya hali ya "kutisha".

Vitendo vya kigaidi hutumiwa na mtu au makundi ya watu ili kuwaingizia watu hofu ndani ya mioyo yao na pengine hata kuchukua madaraka ya kisiasa. Ugaidi ni njia ya mnyonge na hata mwenye nguvu kutimiza malengo yake. Hili litafafanulika zaidi kadri utakapofuatilia maandiko haya.

Kihistoria tunaona kuwa, vitendo vingi vya kigaidi humu duniani vimefanywa pia na dola zilizo madarakani kwa minajili ya kuendelea kushika hatamu za dola. Mathalan, msemo wa " Utawala dhalimu" kwa tafsiri ya Kiingereza "Terror regime" hutumika tunapoielezea dola yenye kutumia mabavu na nguvu nyingi kupita kiasi. Dola au mtawala asiyezingatia sheria wala haki za kibinadamu.

Msamiati huu wa utawala dhalimu unatokana na lugha ya Kifaransa na una chimbuko la Mapinduzi ya Wananchi kule Ufaransa kati ya mwaka 1789 hadi 1799. Utawala dhalimu wenye kutisha" la terreur" ulikuwepo kule Ufaransa kunako miaka ya kati ya 1792 hadi 1794. Katika kipindi hicho watu takribani 40,000, wengi wao wakiwa wakulima na wahunzi waliuawa.

Mifano ya tawala dhalimu na za kutisha katika sehemu nyingine za dunia ni kama Urusi ya zamani chini ya dikteta Stalin, utawala wa Kinazi wa Ujerumani kati ya 1933-1945 chini ya Fashisti Hittler.
Katika Afrika, tuna pia mifano kadhaa ya tawala dhalimu na za kutisha ambazo kimsingi ni tawala za kigaidi. Uganda ya Idd Amin, Afrika ya Kati ya Bokassa, Zaire ya Mobutu, na nchi nyingine nyingi. Hizi zilikuwa tawala dhalimu.

Ugaidi kimsingi ni ile hali ya mtu, kikundi au dola, kwa maana ya taifa,kutumia nguvu nje ya wigo wa sheria ili kufikia malengo yao. Mwenye kuendesha vitendo vya kigaidi huchagua watu wake watakaoathirika na vitendo hivyo. Si lazima mtu au watu hao watakaoathirika wawe ni wahusika wa moja kwa moja wa mgogoro husika, isipokuwa, waathirika mara nyingi huchaguliwa na huonekana kama wawakilishi wa malengo ambayo magaidi wanataka kuyafikia.

Malengo au sababu za ugaidi zaweza kuwa ni za kidini, kijamii na kisiasa.
Ugaidi huwa wa kimataifa pale tukio la kigaidi linapofanywa nje ya mipakaya yule anayatenda tendo la kigaidi, au raia wa nchi moja wanapokuwawalengwa na kauthirika na tendo la kigaidi katika nchi ya tatu, mathalan,magaidi kutoka Colombia wanapofanya tendo la kigaidi dhidi ya raia waUingereza katika nchi ya Zambia.

0754 678 252, http://mjengwablog.com

No comments: