Saturday, October 25, 2014

Mh. Shy-Rose Bhanji Ajibu Shutuma Dhidi Yake

Mh. Shy-Rose Bhanji
Mimi Shy-Rose Bhanji, Mbunge wa Afrika Mashariki-Tanzania, ninapinga vikali na kwa nguvu zote shutuma zilizotolewa dhidi yangu kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.
Shutuma hizi hazina ukweli wowote na zinalenga, si kuniharibia, bali kuchafua sifa yangu na utendaji kazi wangu katika Bunge la Afrika Mashariki.
Lengo kuu la shutuma hizo ni kunivunja nguvu na ari ya kutetea maslahi ya nchi yangu na Watanzania wenzangu kwani daima nimekuwa kikwazo na mwiba kwenye ajenda zinazokiuka maslahi ya Tanzania.
Kwa mfano ardhi ya Tanzania kugawiwa kwa wana Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kinyume na Sera ya Tanzania. Nimekuwa miongoni mwa wabunge wa Tanzania tulio mbele katika kulipinga suala hilo. Sishangai likinijengea uadui.
Isitoshe, kwenye ajenda ya kumuondoa madarakani Spika wa EALA, Dk. Margaret Zziwa, nilisimama kidete kwa kutounga mkono kwa sababu halikuwa na maslahi ya Tanzania na yalikuwa kinyume na malengo ya ushirikiano wa Jumuiya nzima.
Hoja ya kumuondoa Spika ilikuwa ni sehemu ya ‘mchezo mchafu’ ya ajenda ya siri ya kumweka kwenye nafasi hiyo mjumbe mwingine kwa maslahi ya wachache.
Jaribio hili la kumuondoka Spika lilifanywa na kushindikana mara tatu baada ya kukosa sahihi za kutosha kutoka Tanzania, ikiwamo ya kwangu.
Baada ya kampeni ya kumwondoa Spika kushindwa, wabunge kadhaa walikuwa wanasusia vikao vya Bunge wakati wameshachukua posho za vikao. Kwa mfano kikao kilichofanyika hivi karibuni hapa Dar es Salaam.
Malumbano ndio yamekuwa yakitawala na kuinyima Bunge akidi ya kuendelea na ajenda za mtangamano. Huu ni usaliti wa wazi kwa nchi zilizowachagua na kuwatuma katika Bunge la EALA.
Ukijaribu kuwaasa kwamba mwenendo huo si sahihi, unageuka kuwa adui.
Na sasa wameamua kunitukana na kuzusha tuhuma kadhaa kupitia mitandao ya kijamii ambako yote ni utunzi wa kisanii usiokuwa na chembe ya ukweli, uhalali wala ushahidi.
Wahenga walisema ‘akutukanaye hakuchagulii tusi’. Walete ushahidi wa tuhuma zote dhidi yangu.
Kwa mfano, shutuma kwamba nililewa pombe ndani ya ndege, kuvunja chupa, kufanya fujo na kufungwa pingu wakati wa safari ya Ubelgiji si kweli hata kidogo.
Kama hizi tuhuma ni za kweli, kwanini hazikupelekwa polisi, serikalini au vyombo vingine vya sheria baada tu ya tukio?
Ijewe wamesubiri wiki mbili baada ya madai hayo ya tukio la kutunga ndipo wajitokeze wakati wa kikao kinachoendelea mjini Kigali, Rwanda? Kwanini wasubiri kikao cha Kigali ndipo uzushi huu utolewe?
Tuhuma kwamba nimewatukana marais wa nchi tatu hazina mashiko isipokuwa kuhalalisha kampeni ya wale wanaonichafua na kuibua chuki kwa maraisi na raia katika nchi za Kenya, Rwanda na Burundi.
Ninayo heshima kubwa sana kwa marais wa nchi zote tano na raia wa nchi wanachama ambako mara zote nimepokewa na kuishi kwa amani na upendo katika nchi hizo. Naahidi kuedeleza heshima hii.
Hainiingii kichwani ni wapi nilipoteza heshima hii isipokuwa kwa wale wasionitakia mema ambao wamekusudia kufanikisha ajenda zao.
Shutuma zote dhidi yangu zimetengenezwa na watu ambao hatushabihiani katika hoja zetu na sishangai kwa hilo.
Mimi ni Mtanzania na ni Mbunge wa Tanzania. Hivyo nina wajibu wa kulinda na kutetea maslahi ya Watanzania ili kuleta mtangamano wenye uwiano sawa kwa nchi zote wanachama.
Ninaahidi nitaendelea kuwatumikia Watanzania kwa nguvu zangu zote na kutoa ushirikiano kwa wabunge wengine wa EALA kwa manufaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nimeyasema haya nikiamini kuwa: “Uongo ukiachwa usemwe mara nyingi unaweza kuaminiwa kuwa ni ukweli.”
Umoja Wetu Ni Nguzo Yetu
Mungu ibariki Afrika Mashariki
Asanteni,
Shy-Rose Bhanji
Mbunge EALA

1 comment:

Anonymous said...

Sidhani kama hii ni njia sahihi ya kujibu tuhuma. Na ni akina nani wanakutuhumu, ni vizuri kulijua hili ili usije ukakuta unatoa nafasi kwa watu kuanza kufuatilia hata yale yaliyo nje ya hili.