Wednesday, July 13, 2016

Hospitali ya Kutibu Kansa Kujengwa Bukoba

MWEKEZAJI MZAWA AAMUA KUWEKEZA KAGERA KWA KUJENGA    HOSPITALI KUBWA YA KUTIBU MAGONJWA YA KANSA KATIKA MANISPAA YA BUKOBA

Mkoa wa Kagera kupiga hatua kubwa kimaendeleo baada ya kujitokeza mwekezaji mzalendo ambaye ni Mshauri Mkuu wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Company Ltd ya Jijini Dar es Salaam Bwana James Rugemalila kuanza mchakato wa kujenga kituo kikubwa (hospitali) ya magonjwa ya matibabu ya Kansa katika Manispaa ya Bukoba.

Bw. James Rugemalila akiambatana na ujumbe mzito na wataalamu wa afya kutoka nchi mbalimbali alifika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera tarehe 10/07/2015 na kuongea na Katibu Tawala mkoa Bw. Nassor Mnambila ambaye alimhakikishia juu ya kupata ardhi wanayohitaji na kuwa serikali ya mkoa itawaunga mkono katika hatua zote za kupatikana kwa kituo hicho.

Aidha Bw. Rugemalila na ujumbe wake walifika  Manispaa ya Bukoba na kuongea na Kaimu Mkurugenzi Bw. Lukiko Chibunu ambaye pia aliwahakikishia kuwa ardhi ipo na tayari wameitenga kwa ajili ya uwekezaji huo kama walivyoombwa na Bw. Rugemalila na walidhuru eneo husika Mtaa wa Makongo  karibu na Ziwa Victoria.

Ujumbe huo ulilidhishwa na eneo husika pia  Bw. Rugemalila aliambatana na Profesa Anthony Pais Mkuu wa Idara ya Upasuaji kutoka Bangalore India ambaye alisema Tanzania na Mkoa wa Kagera ni muhimu kuwa na kituo hicho kutokana na takwimu za Shirika la Afya ulimwenguni (WHO).

Profesa Pais alisema kuwa wagonjwa wa kansa 35000 wanatambuliwa kila mwaka duniani na asilimia 90%  ya wagonjwa wanatoka duniani kote na wagonjwa 3000 wanatoka Tanzania kila mwaka na hupelekwa nje ya nchi kutibiwa ambapo baada ya kituo hicho kujengwa itakuwa fursa kwa watanzania kupata matibabu hapa hapa nchini  na mkoani Kagera.

Vilevile Profesa Pais alisema kuwa Kampuni ya VIP Engenering and Marketing Ltd iliamua kujenga kituo hicho mkoani Kagera kwasababu walipoonyeshwa eneo la Makongo katika Manispaa ya Bukoba walipendezwa nalo sana pia mkoa wa Kagera umepakana na nchi zote za Afrika Mashariki ambapo ni moja wapo ya fursa katika uwekezaji.

Naye Bw. Anic Kashasha Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano katika Kampuni ya VIP Engineering Ltd alisema kuwa kituo hicho mara baada ya kukamilika kitajulikana kwa jina la (RUTAKWABYERA CANCER HEALTH CENTER) na kitakuwa na hadhi zote  za hali ya juu mpaka kawaida ili kutoa fursa kwa wananchi wote kupata huduma stahili.

Kituo hicho kwa kuanzia kitajengwa na kuanza na vitanda 100 na mara baada ya kukamilika kitakuwa na vitanda 500 pia zitajengwa hosteli za wananchi ambao watakuwa wanawaleta wagonjwa wao kupata mahala pakujihifadhi.  Kitaitwa kituo badala ya hospitali kwani kitakuwa kinaendesha uchunguzi, ugunduzi, na kutoa tiba na elimu juu ya ugonjwa wa Kansa.

Kituo cha Rutakwabyera kinatarajiwa kujengwa ndani ya miaka mitatu kuanzia sasa na gharama za mradi mzima zitajulikana mara baada ya ujenzi kuanza rasmi. Mkoa wa Kagera unazo Nyanja nyingi sana za uwekezaji wazawa na wawekezaji mbalimbali mnakaribishwa kuwekeza Kagera.

No comments: