
Leo nilienda Boston University kumsikiliza Muongoza Sinema/Mcheza Sinema Spike Lee akiongea kuhusu jinsi alivyokuwa na mafanikio katika sinema Hollywood. Alialikwa na mwanafunzi mweusi ambaye anasoma filamu hapo chuoni. Alivyokubali mwaliko Chuo waliamua kudhamini safari ya Spike.
Wanafunzi wa BU na watu kutoka jamii ya sinema hapa Boston karibu 800 walihudhuria. Ukumbi ulijaa.
Spike aliongea kuhusu jinsi sinema inavyotawala fikra za watu. Alisema lazima uwe mwangalifu unaleta picha gani. Mfano, watu wanaweza kudhani weusi wote ni maskini, wauaji na watumia madawa ya kulevya na wanawake weusi wote wanagawa mavituuz ovyo kutokana na vitu walivyoona kwenye sinema. Alisimulia mkasa wa weusi fulani walioenda Ulaya na kukuta watu walidhani wao wako hivyo kutokana na mambo walioona kwenye sinema.
Alizungumzia jinisi ilivyo ngumu kwa Hollywood kutoa hela kutengeneza sinema inayoleta picha nzuri kuhusu weusi maana hizo picha zinazoleta picha mbaya zinalipa zaidi.
Spike alisema kuwa hivi karibuni ataanza kutengeneza sinema nyingine. Hakusema itahusu nini lakini ametunga yeye mwenyewe.