Showing posts with label CUF. Show all posts
Showing posts with label CUF. Show all posts

Friday, February 07, 2014

Muungano

Mungu Ibariki Jamhuri ya Muungano ya Tanzania!  Hii picha inasema mengi, Nimeitoa Facebook.


Thursday, March 28, 2013

Mazishi ya Mh. Khamis Yatakuwa Kesho Mjini Pemba


The Late Honourable Salim Hemed Khamis (MP Chambani Pemba -CUF)

MAZISHI ya aliyekuwa Mbunge wa CUF, Jimbo la Chambani Pemba kisiwani Zanzibar, Marehemu, Salim Hemed Khamis,  (62), yanataraji kufanyika kesho  (Ijumaa Machi 29, 2013) mchana mjini Pemba.

Tarifa za awali kutoka Chama cha Wananchi CUF, zinasema kuwa Mwili wa Marehemu, Khamis utaagwa kesho asubuhi kuanzia majira ya saa 2:30-4:00 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo Viongozi mbalimbali wa kitaifa na Kimataifa pamoja na wananchi na Wanachama wa CUF watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa Marehemu.

Taarifa hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julis Mtatiro inasema kuwa Msafara utaondoka Karimjee saa 4:00 kuelekea uwaja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo Msafara wa Ndege 2 utaondoka kwenda Pemba.

Saa saba mchana mazishi yatafanyika huko Pemba na maazishi hayo yataongozwa na Viongozi wa serikali, Wabunge na CUF.

Mtatiro amewaomba wanachama nba wafuasi wa CUF jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuuga mwili wa Mbunge huyo aliyefikwa na umauti akiwa kazini katika vikao vya Kamati za Bunge, ambapo Marehemu alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

***************************************************************************

KUTOKA MICHUZI BLOG:

Pichani ni Baadhi ya Maofisa wa Ofisi Ndogo ya Bunge,wakimsaidia kwa kumbeba Mbunge wa Chambani,Bwa.SalimHemed Khamis,mara baada ya kuanguka ghafla hapo jana jijini Dar akiwa katika vikao vya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kukimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu ya haraka.



======= ====== ======

Habari zilizoifikia Globu ya Jamii hivi punde inaelezwa kuwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Chambani-Pemba, Salim Hemed Khamis,ambaye hapo jana alianguka ghafla jijini Dar Es Salaam alipokuwa akihudhuria vikao vya kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kukimbizwa hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu, amefariki dunia muda mfupi uliopita katika Hospitali hiyo ya Taifa ya Muhimbili,aidha chanzo cha habari hizi kimeongeza kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa Marehemu kuelekea Pemba kwa mazishi zinafanyika.Tutazidi kuwafahamisha zaidi kadiri ya habari zitakavyokuwa zikiingia.
Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema Peponi-Amin

***************************************

WADAU NINA SWALI.  Hivi huko Bungeni, hakuna Stretcher ya kubeba wagonjwa?  Je, hakuna watu wa First Aid?   Hii ni mwaka 2013, wanatakiwa wawe na wahudumu wa afya, ambulance, wahudumu onsite. Watu wawepo wanaoelewa jinsi ya kubeba wagonjwa. Na hasa huko Bungeni waBunge wengi wana umri mkubwa na matatatizo ya kiafya.  - Chemi

Saturday, January 08, 2011

TAMKO LA CUF KUHUSU MAANDAMANO YA CHADEMA ARUSHA

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)

VYOMBO VYA DOLA VINAHATARISHA AMANI YA NCHI.

CUF - Chama Cha Wananchi kimeumizwa sana na kitendo cha kinyama kilichofanywa na jeshi la polisi na serikali ya chama cha mapinduzi kuwapiga na kuwaumiza viongozi, wanachama na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) na wananchi mbalimbali wapenda demokrasia na haki ndani ya nchi yetu waliokuwa wakiandamana kwa amani jijini Arusha jana tarehe 05 Januari 2011. Tunalaani vikali kukamatwa na kwenda kuhojiwa kwa Wabunge wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa Taifa Mhe. Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai , Mhe. Godbless Lema Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Joseph Selasini Mbunge wa Rombo na Mhe. Philemon Ndesamburo, Mbunge wa Moshi Mjini.

CUF inaamini kuwa CHADEMA kama chama cha siasa kilichosajiliwa kihalali ndani ya nchi yetu kilikuwa na haki ya kikatiba na kisheria ya kufanya maandamano yao ya amani ambayo mwanzoni tayari jeshi la polisi jijini Arusha kupitia kwa kamanda wa polisi wa mkoa lilishaahidi kutoa ulinzi wa kuyaweka maandamano hayo salama.

Jeshi la Polisi na Serikali ndiyo wanaostahili kulaumiwa kwa uvunjifu wa amani uliotokea Arusha. Ushahidi wa kimazingira unaonyesha wazi kuwa amri ya kusitisha maandamano iliyotolewa na IGP saa chache kabla hayajafanyika ilitokana na shinikizo za kisiasa. Hoja iliyotolewa kuwa taarifa za kiintelijensia zinaonyesha kutakuwa na uvunjifu wa amani na ndiyo maana maandamano yanazuiliwa ni usanii mtupu. Kama kweli polisi wana taarifa za kiintelijensia kuwa kuna watu watavunja amani basi wazitumie taarifa hizo kuwadhibiti watu hao na siyo kuyasitisha maandamano na kuwanyima wananchi uhuru wa kisheria wa kufanya maandamano.

Nchi hii inapaswa kuongozwa na katiba na sheria na Watanzania tusikubali Serikali iliyoko madarakani kutumia vyombo vya dola kuua uhuru na demokrasia ya nchi yetu.

Hivi sasa jeshi la polisi limekuwa mstari wa mbele kuzuia kila aina ya madai yanayotolewa na vyama ili mwisho wa siku jeshi lifanye kazi yake kuu ya kulinda CCM na utawala wao kijeuri na kisanii. Haiwezekani kila watu wakitaka kuandamana jeshi la polisi lianzishe hoja ati “kwa sababu za ki-intelijensia” maandamano hayo yanafutwa. Hizi taarifa za ki-intelijensia ni zipi?

CUF inaamini kuwa polisi na serikali ya CCM wanataka kutumia kitisho cha ugaidi kilichozikumba Kenya na Uganda kama sababu ya kupinga mikusanyiko mikubwa ya kisiasa kwa lengo la kuitetea Serikali. Lazima tujiulize,hivi magaidi wakitaka kulipua Tanzania mbona kuna sehemu nyingi sana ambazo wanaweza kufanya hivyo bila kusubiri maandamano ya CHADEMA au CUF au vyama vingine?

Hivi tujiulize kama kweli pana tishio la ugaidi iweje mechi za mpira ziendelee bila kuzuiwa na polisi? Mikusanyiko yote inafanyika isipokuwa maandamano ya vyama vya siasa tu? Hawa magaidi walio tishio kwa jeshi la polisi wanaotaka kulipua maandamano peke yake wametokea wapi? Kwa nini nchi hii iendeshwe kisanii na kiujanja ujanja namna hii? Kwa nini serikali inaogopa maandamano?

CUF inalaani ukatili waliofanyiwa wakazi wa Arusha katika maandamano ya CHADEMA na kuwa ukatili huo hauvumiliki na unahatarisha amani na utulivu wa kweli wa nchi yetu.

Ukatili huu hauna tofauti na ule tuliofanyiwa CUF – Chama cha Wananchi tarehe 28/12/2010 ambapo maandamano ya amani yaliyokuwa yaongozwe na Kaimu naibu katibu mkuu Julius Mtatiro yalipigwa marufuku ghafla na kisha mamia na mamia ya polisi wakisheheni silaha za kila aina wakaanza kuwapiga na kuwakamata wafuasi wa CUF na wananchi wengine walioshiriki katika maandamano yale. Kitendo kile ambacho polisi walikifanya kimetia doa kubwa sana jeshi la polisi linaloongozwa na kiongozi tunayemheshimu IGP Said Mwema.

Kitendo hiki cha pili kilichofanyika Arusha kinazidi kuharibu kabisa sifa na uaminifu ambao vyama vya siasa vilikuwa nao juu ya IGP Mwema. Ni muhimu sana kwa taifa letu kwa IGP Said Mwema kulinda heshima yake na asikubali kutumiwa kisiasa kukandamiza demokrasia ndani ya nchi.

Chama cha wananchi CUF kinaamini kuwa ustawi wa demokrasia, utawala bora, usawa, maendeleo ya nchi yetu na amani ya nchi havitaletwa kwa mtutu wa bunduki wala mabomu wala kila aina ya nguvu, hata kama CCM wataendelea na mbinu zao za kuwadhibiti wapinzani hatutokaa kimya na wala hatutoacha kutumia fursa za kikatiba kutoa maoni yetu kwa njia ya amani kama walivyofanya CHADEMA tarehe 05/01/2011 na CUF tarehe 28/12/2011.

Tunaamini walichokuwa wakipigania CHADEMA jijini Arusha ni kitu cha msingi sana,walikuwa wakipinga kitendo cha kukiuka demokrasia katika uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha. CHADEMA hawakuwa na budi kutumia njia za kidemokrasia kuonyesha kutokukubali na kutotambua utaratibu huo wa kinyemela ulioendeshwa na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kwa manufaa ya CCM.

CUF inawapa pole wahanga wote waliopigwa na kuumizwa na mabomu, risasi, maji ya kuwasha n.k katika tukio hilo la kihistoria la kudai haki ya wanyonge jijini Arusha. CUF iko pamoja nao katika kuendelea kupigania haki. CUF inawapa pole viongozi wote wa CHADEMA waliokamatwa katika maandamano ya Arusha na tunawataka waendelee na juhudi za kupigania ukombozi kama inavyofanya CUF.

CUF inamtaka Rais Jakaya kikwete kutumia busara za hali ya juu sana katika kuendesha nchi katika kipindi hiki ambacho anamalizia miaka yake mitano ya mwisho. Rais Kikwete ana fursa ya kujenga misingi imara ya demokrasia ili akitoka madarakani akumbukwe kwa mambo ya heri na siyo kwa mambo ya shari.

Kukaa kimya kwa Rais wakati polisi wanatumia nguvu kubwa kuua demokrasia ndani ya nchi kunaashiria kuwa wanatimiza amri ya Rais.

Pamoja na mambo yote hayo CUF inawataka Watanzania kuendelea kutuunga mkono ili tuweze kuendeleza mapambano ya kudai demokrasia na maendeleo ya kweli ya nchi yetu kama chama mbadala kitakachomkomboa Mtanzania.

Mwisho tunawataka wakazi wote wa Arusha, Dar es salaam na mikoa mingine wazidi kuungana na CUF na wadau wengine wote muhimu katika madai mazito ya kudai katiba mpya.

CUF inaamini suluhisho la sehemu kubwa ya ukatili unaofanywa sasa ni kukosekana kwa katiba mpya itakayotoa mwongozo sahihi wa taifa letu. Tofauti na sasa ambapo jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola vinaweza kufanya lolote wanalotaka juu ya maisha ya watanzania huku katiba ikiwalinda au wanaivunja na hakuna mwenye mamlaka ya kuwauliza.

Tanzania inahitaji Katiba Mpya ya Wananchi wenyewe na Tume Huru ya Uchaguzi. Tamko la Rais la kuunda Tume Maalum ya Katiba na ishara nzuri ukilinganisha na matamko ya awali ya Waziri wa Sheria na Katiba. Hata hivyo ni muhimu Rais akawafafanulia Watanzania kuwa lengo la mchakato mzima ni kupata Katiba Mpya yenye misingi imara ya demokrasia itakayotokana na ushiriki wa wadau wote. CUF inawaomba na kuwasisitiza Watanzania watuunge mkono sana ili tuhakikishe kwa pamoja tunapata katiba itakayoandikwa upya na kubeba matumaini ya Watanzania na siyo kuwekwa viraka kwa katiba iliyopo.

Imetolewa na

Prof Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti - CUF.
06 Januari 2011.
Dar es salaam.

Tuesday, August 26, 2008

Kongamano la CUF

CUF waandaa kongamano la ukosefu wa uongozi na hatma ya Tanzania

Chama Cha Wananchi
Office of The Secretary General
P.O. Box 10979
Dar Es Salaam, Tanzania
www.cuftz.info
www.hakinaumma.wordpress.blog

TAREHE: 26/08/2008

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU: KONGAMANO LA KITAIFA KUJADILI
UKOSEFU WA UONGOZI NA HATIMA YA TANZANIA

Imetolewa na Mbaralah Maharagande,
Mkurugenzi Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma.

Nchi yetu inapita katika moja ya kipindi kigumu katika historia yake tokea ilipopata Uhuru mwaka 1961. Hali ya uchumi ni ngumu sana huku gharama za maisha zikipanda kwa kasi ya ajabu chini ya falsafa ya ari, nguvu, na kasi mpya. Tofauti za kipato na kiwango cha maisha kati ya matajiri wachache na walalahoi walio wengi inazidi kuongezeka. Migomo ya wafanyakazi na wanafunzi imekuwa ni jambo la kawaida hivi sasa.

Nyufa katika Muungano wetu zinazidi kukua na hata kutishia uhai wa Muungano wenyewe. Migawanyiko ya kidini inaonekana kuzidi kujikita. Mpasuko wa Kisiasa Zanzibar umeshindwa kupatiwa jibu huku uchaguzi mkuu wa 2010 ukiwa unakaribia. Serikali inaonekana kuzidiwa nguvu katika mapambano dhidi ya ufisadi na sasa mafisadi wanaonekana kutamba. Taifa linakwenda bila ya Dira wala Mwelekeo unaoeleweka. Wananchi wanaonekana kukata tamaa.

Matatizo haya kwa kiasi kikubwa yanaonekana kusababishwa na ukosefu wa uongozi thabiti, makini na adilifu. Hii si hali nzuri na tusipokuwa makini Taifa litayumba sana. Wazalendo wakweli wa Tanzania hawapaswi kukaa kimya na kusubiri matokeo ambayo kwa vyovyote vile hayawezi kuwa mazuri.

The Civic United Front (Chama Cha Wananchi-CUF) kikiwa chama makini kikuu cha upinzani nchini, kinachotegemewa na Watanzania walio wengi, kimeandaa kongamano maalum kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu hali hii ya ukosefu wa uongozi na athari zake kwa hatima ya Tanzania. Kongamano hilo litafanyika siku ya Alhamis, tarehe 28 Agosti, 2008, kuanzia saa 3.30 asubuhi katika ukumbi wa Diamond Jubilee, mjini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Mhe. Prof. Ibrahim Lipumba, atawasilisha mada kuhusu UKOSEFU WA UONGOZI NA HATIMA YA TANZANIA na baadaye washiriki watapata nafasi ya kuichambua mada hiyo na kutoa maoni na mtazamo wao.

CUF imewaalika watu mbali mbali kushiriki katika kongamano hilo wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa, wahariri na waandishi wa vyombo vya habari, taasisi za kiraia na kijamii, viongozi wa kidini, wasomi na wataalamu, maofisa wa kibalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

HAKI SAWA KWA WOTE
Mbaralah Maharagande,
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mahusiano ya Umma.

0773 062 577

Wednesday, August 15, 2007

Rais Kikwete azungumzia Muafaka kati ya CUF na CCM


TAARIFA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KUHUSU MAZUNGUMZO YA MUAFAKA KATI YA CUF NA CCM

Tarehe 7 Agosti, 2007, Mwenyekiti wa Chama cha Civic United Front (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alitoa tamko la kuelezea kukwama kwa mazungumzo ya muafaka kati ya Chama chake na Chama cha Mapinduzi (CCM). Katika tamko hilo, Profesa Lipumba alielezea nia yake na ya Chama chake ya kujiondoa katika mazungumzo hayo ifikapo tarehe 15 Agosti 2007.

Napenda kukumbusha kwamba chimbuko la mazungumzo yanayoendelea sasa ni ahadi niliyoitoa kwa Watanzania wakati nilipohutubia Bunge tarehe 30 Desemba, 2005. Niliahidi kuwa nitakuwa tayari kuchukua hatua za kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Kwa ajili hiyo, nilielezea nia yangu ya kusaidia kuanzisha na kuwezesha mjadala juu ya mustakabali wa kisiasa Zanzibar.

Ahadi hiyo niliitoa kwa dhati ya moyo wangu nikiamini kwamba hakuna tofauti zozote za kisiasa na kijamii katika nchi yetu au baina yetu au katika jamii zetu ambazo haziwezi kumalizwa kwa njia ya mazungumzo. Imani hiyo bado ninayo leo na nitaendelea kuwa nayo daima.Ilichukua muda kwa mazungumzo baina ya CCM na CUF kuanza. Hii ilisababishwa na haja ya kufanya mashauriano mapana baina na miongoni mwa wadau wa pande zote husika ndani ya Chama cha Mapinduzi na wenzetu wa CUF.

Mashauriano haya yalichukua muda kidogo zaidi ndani ya CCM kwa sababu utamaduni na mfumo wetu wa demokrasia ndani ya Chama cha Mapinduzi unatuwajibisha kuwa na mashauriano mapana na ya kina katika ngazi mbalimbali za uongozi na vikao vya Chama.

Nafurahi kuwa kazi hiyo ilikamilika vizuri na tukafikia maelewano ya dhati kuwa CCM ifanye mazungumzo na CUF.Baada ya hapo, Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ilimuagiza Katibu Mkuu wa CCM kuwasiliana na Katibu Mkuu wa CUF na kumuomba akubali kushiriki katika mazungumzo baina ya vyama vyetu. Tulifarijika sana kwamba baada ya maombi hayo ya CCM wenzetu wa CUF walikubali kukaa pamoja nasi katika meza ya mazungumzo.Tarehe 17 Januari, 2007, Makatibu Wakuu wa vyama vya CUF na CCM wakakutana na mchakato wa mazungumzo ukaanza. Baada ya kikao hicho cha mwanzo, kila upande ukaunda timu yake ya kushiriki katika mazungumzo hayo.

Tarehe 01 Februari, 2007 Kamati yetu ya Pamoja ilifanya mkutano wake wa kwanza ambapo walikubaliana kuwa jambo la mwanzo la kufanya ni kwa kila upande kutengeneza mapendekezo yake ya mambo unayotaka yazungumzwe, yaani yawe kwenye Ajenda ya Mazungumzo. Baada ya hapo yalifanyika majadiliano mazuri na katika mazingira ya kidugu, ajenda ya pamoja ya mazungumzo ikatengenezwa.
Ajenda hiyo ilikuwa na mambo matano makubwa kama ifuatavyo:
1. Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 na taathira zake;
2. Usawa na haki katika kuendesha siasa;
3. Masuala ya utawala ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
4. Njia za kuimarisha mazingira ya maelewano ya kisiasa na uendeshaji wa uchaguzi huru na wa haki Zanzibar; na,
5. Utaratibu wa kutekeleza Programu ya Utekelezaji wa Makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo haya.

Tangu mazungumzo haya yaanze mwezi Januari mwaka huu, Kamati yetu ya Pamoja imefanya vikao 12 na wametumia siku 43 za mazungumzo. Pia Makatibu Wakuu nao wamekutana mara mbili kutafuta ufumbuzi wa yale mambo yaliyohitaji kufanywa nao. Tulikubaliana kuwa mazungumzo ya msingi yatafanywa na Kamati lakini pale ambapo Kamati itakwama Makatibu Wakuu waingilie kati kutoa mwongozo. Ukweli kwamba wamekutana mara mbili tu ni dalili kwamba mambo yanakwenda vizuri.

Hatua kubwa imefikiwa na mafanikio ya kuridhisha yamepatikana. Kuna mambo kadhaa makubwa na ya msingi ambayo pande hizi mbili zimekwishakubaliana. Katika ajenda tano za mazungumzo, ajenda tatu, yaani ajenda ya Usawa na Haki katika Kuendesha Siasa, Masuala ya Utawala ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Njia za Kuimarisha Mazingira ya Maelewano ya Kisiasa na Uendeshaji wa Uchaguzi Huru na wa Haki Zanzibar, zimejadiliwa na pande zote mbili zimefikia maelewano mazuri.Kwa upande wa ajenda ya kwanza inayohusu Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 na Taathira Zake, mazungumzo yamefanyika na maelewano yamepatikana kwa mambo kadhaa.

Yapo mambo mawili matatu ambayo bado maelewano hayajafikiwa. Hatuna budi tuendelee kuyazungumza mpaka tutakapopata maelewano ya pamoja. Jambo moja kubwa ambalo wawakilishi wa vyama vyetu bado wanaendelea kujadiliana na ambalo bado halijakamilika ni lile linalohusu namna ya kutengeneza mazingira yatakayowezesha vyama vya siasa Zanzibar, hususan CUF na CCM, kuishi na kuendesha shughuli zao kwa pamoja katika hali ya maelewano na mazingira ya amani na utulivu.

Mazungumzo kuhusu kipengele hiki yamechukua muda na muafaka bado haujafikiwa. Kwa maoni yangu imekuwa hivyo kwa sababu ya umuhimu wake na umakini unaotakiwa katika uchambuzi wa hoja na kufikia uamuzi. Katika mazungumzo kuna mambo rahisi yanayochukua muda mfupi kujadiliwa na kufikiwa makubaliano na kuna mambo magumu yanayochukua muda mrefu. Huu ndiyo uzoefu wa vyama vyetu katika mazungumzo tuliyofanya huko nyuma na hata kwa mazungumzo haya.

Kwa sababu hiyo, sisi wa upande wa CCM, hatudhani kama tumefikia mahali pa kusema kuwa mambo yameshindikana na hivyo mazungumzo yavunjike. Hatujafikia hatua hiyo hata kidogo. Ni maoni yangu na ya Chama cha Mapinduzi kuwa tuendelee kuzungumza na kila upande uboreshe hoja zake za kuushawishi upande mwingine. Tupo kwenye mazungumzo kwa ajili hiyo. Tupo kufanya hivyo. Naamini kwamba, kama ambavyo tumepata maelewano katika maeneo mengine ambayo yalikuwa magumu, hata kwa haya yaliyobakia hatimaye tutaafikiana.

Wahenga walisema: “Penye nia pana njia”. Maadam sote nia tunayo, jawabu muafaka kwetu sote na kwa nchi yetu tutalipata.Nawasihi wenzetu wa CUF wasijiondoe kwenye mazungumzo haya na badala yake tuendelee kuzungumza. Tunazungumza kwa sababu tuna tatizo tunalolitafutia ufumbuzi. Kuacha kuzungumza si jawabu kwani tutakuwa tunaacha kulipatia ufumbuzi tatizo linalotusibu sote.

Tutarudi kule tulikokuwa, yaani kwenye uhasama, shutuma zisizoisha, kubaguana, kutozikana na hata kutosalimiana au kuchekeana. Tutaendelea na utamaduni mbaya wa kuzifanya tofauti zetu za kisiasa kuwa ni chanzo cha uadui, chuki na hivyo kuhatarisha amani, utulivu na umoja wa taifa letu na watu wake.Ni kweli, mazungumzo ni lazima yawe na ukomo. Na sisi wote tungependa yafikie mwisho wake mapema inavyowezekana.
Lakini, ukomo wa mazungumzo ni lazima utokane na ridhaa ya pamoja ya pande zote na hasa kwamba ajenda zote zimepata nafasi ya kujadiliwa kwa kina na maelewano yamefikiwa. Ukomo wa mazungumzo usiotokana na hayo ni kuahirisha tatizo litakalokuja kujitokeza na kutudhuru wote siku za usoni. Shabaha yetu katika mazungumzo haya ni kupata ufumbuzi wa kudumu na endelevu kwa matatizo yanayotukabili katika uwanja wa kisiasa nchini.

Tunafanya yote hayo ili kujihakikishia amani, utulivu, mshikamano na umoja wa taifa letu na watu wake vinaendelea kuwepo daima dumu.Napenda kumaliza kama nilivyoanza kwa kukumbusha kwamba mazungumzo haya yametokana na ahadi yangu na ya CCM. Ahadi hiyo ni ya dhati na niliitoa kwa kujiamini na kwa kuamini kuwa hii ndiyo njia pekee iliyo bora kuliko zote ya kushughulikia tofauti zetu.

Kwa msingi huo, ningependa na CCM ingependa kuona mazungumzo haya yanaendelea na yanazaa matunda tunayoyatarajia sote. Nawasihi wenzetu wa CUF tuungane kuhakikisha tunafanikiwa. Tusikubali mazungumzo yavunjike kwani gharama ya kuvunjika kwa mazungumzo haya ni mbaya na haina maslahi kwa taifa letu na watu wake. Itahatarisha amani na utulivu wa nchi yetu.
Ikulu, Dar es Salaam.
14 Agosti, 2007