BURIANI MWANANGU AMINA CHIFUPA: PRINCESS WA TANZANIANa Ummie-Mahfoudha Alley Hamid
Kifo hakina wakati, huruma wala subira, huja kwa saa na muda uliopangwa na mwenyewe Subhana wa Taala Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mwanaadamu hawezi kukipangua. Ya laiti ingelikuwa uwezekano huo upo, basi tungalipangua vifo vya wengi ambao ni vipenzi vyetu kikiwemo hichi cha juzi cha mbunge wa Viti Maalum CCM anaewawakilisha vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Amina Chifupa Mpakanjia.
Wa kale walisema chema hakidumu. Nimeuthibitisha ukweli wa usemi huu kwa kifo cha binti huyu. Marehemu Amina alikuwa na sifa zote za kupendeza. Alikuwa kijana, mrembo, mtanashati, mcheshi, msomi kwa kiasi chake na zaidi ya yote alikuwa mtu wa watu.
Si muda mrefu tangu nimjuwe Marehemu. Nilimsikia sauti yake wakati akiwa mtangazaji wa redio, na nikamjuwa kupitia magazeti na runinga. Nikaja kumjuwa baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa vijana kupitia chama tawala cha CCM. Kabla ya kumjuwa fika, nilikuwa najisemea ki moyo moyo, “Hmmmm, binti kama huyu mwenye sifa zote hizi, kweli atakuwa na uwezo wa kuongea na watu wa hali ya chini anaowawakilisha? Hivi huyu si anaringa na kujiona kuwa hakuna wa kumgusa?” Hakika dhana ni dhambi na kweli nilipata dhambi kwani nilivyomdhania ikawa ni tofauti na nilivyomjua. Ukweli nilijikumbuka mimi enzi zangu nilipokuwa natikisa na namna watu walivyokuwa wanaona najivuna
Nilimwmjuwa Amina kwa muda wa miaka chini ya miwili ya ubunge wake. Aliniita “mama” nikamwitika “mwanangu”. Alikuwa ni mtu “Simpol” kwa lugha ya mjini. Alikuwa mchangamfu na pia alikuwa ni mtu mwenye sikio la kusikiliza watu na shida zao ingawa shida nyengine zilikuwa si rahisi kwake kuzitatua.
Umaarufu, ujana, urembo, wema wake ulimfanya alengwe shabaha na kila chombo cha habari, iwe kwa wema au utelezi alioufanya. Ujana wake ulimfanya awe au afanye mambo mengi ambayo yanafanywa na yalifanywa na wengi ambao walio na umri wake. Binaadamu tunasahau kuwa “ujana ni moshi” na mwishowe hupita tu. Tunasahau kuwa tumepitia hatua zote hizo na zaidi ya hizo katika ujana wetu.
Alifanya mambo ya kawaida ya ujana na urembo, alikuwa mlevi? Sikumfahamu hivyo, mvuta sigara au bangi? Sikumjuwa hivyo, mtumiaji wa madawa ya kulevya? Sikumuona na sidhani kama alikuwa hivyo. Lipi geni alilokuwa nalo Marehemu Amina hata kusakamwa na kudhalillishwa hadi kufikia kupoteza roho yake changa?
Tujiambie na tujiulize, hivi sisi tukiwa kama waandishi wa habari, ni lazima tuwe na habari mbaya (negative) ndio tuandike au ndio ziuzike? Hatuwezi kuwa na upande mzuri (positive) side of issues? Kwa nini muandishi wa habari mwenzetu anaeanza maisha na malengo yake awe ndio chanzo chetu cha habari mbovu zilizopo na zisizokuwepo? Vijarida vya udaku haviuziki bila ya kuwepo uwongo usokifuniko?
Nasema hivi kwa sababu nimesikitishwa na muandishi Eric Shigongo wa gazeti la IJUMAA ambalo slogan yake ni “We belong to God” yaani wao ni waja wa Mungu, na namna alivyomsakama mwana wa watu na kusahau hiyo slogan yake ya kuwa yeye ni mja wa Mungu na Marehemu Amina pia ni mja wa Mungu. Amemuekea makala spesheli ya kumdoboa na kumnazi’i kadmnas bila kimeme. Anamkashifu na kuashiria kuwa Marehemu amefika kumfata kwake na kujitakisha!
Shigongo amemkejeli Marehemu eti asijifananishe na Mhe. Migiro na Mhe. Meghji. Kwa nini iwe vibaya kuwa na malengo? Hata Waheshimiwa hao walimhusudu Margaret Thatcher, Golda Meyer, Bandaranaike, Madeline Albright, Indira Ghandi na Bi Titi hawa wakiwa wachache tu kati ya wengi. Hakuna aliezaliwa na ujuzi usio weza kufikiwa na wengine. Hakuna kati yetu aliejuwa tu bila kuiga au kuweka malengo. Amemkejeli kwa bezo eti hata nae awe katika NEC na awe Mwenyekiti UVCCM. Mbona huyu Mwenyekiti wa sasa nae ni mjumbe wa NEC? Kwa nini kilicho “Good for the goose” kisiwe “Good for the gander?” Au hii ni kwa sababu ya jinsia yake? Kwa Marehemu alijiwekea malengo kuwa “Even the Sky was not the limit” because there is Outer Space after the sky, and may be that is where she wanted to set the limit.
Nathubutu kusema kuwa nilivyomjuwa Marehemu kwa muda mfupi na tukawa karibu sana kiasi cha kuwa wiki haipiti bila kujuliana hali siamini kama alikwenda kwa Shigongo na kukaa kwa saa sita kupindukia usiku wa manane kwa lengo la kutumia ujanajike wake. Maalesh, na iwe kweli kenda kwa lengo hilo, kwani Marehemu Amina atakuwa wa kwanza kujitakisha? Eric Shigongo hajapata kutaka au kutakwa na mwanamke? Anasema alimshikisha Marehemu kitabu kitakatifu ili aape kama aliwahi kutakiwa na Shigongo, na Marehemu akakataa kukishika; jee Shigongo anajuwa sharia za Kiislamu na sababu zinazomfanya mwanamke wa Kiislamu kukataa kushika Mas-hafu kwa sababu na nyakati fulani fulani?
Shigongo ameendelea na makala zake za kashfa juu ya uhusiano wa Marehemu na Mheshimiwa mmoja bungeni, jee tumuite yey ni mtafiti wa habari za ndani za wabunge wote walio bungeni? Ni kweli anajuwa mahusiano binafsi ya baina wabunge wote au alimkandia Marehemu tu? Kama anazijuwa habari zote mbona asiziandike kwa mapana na marefu na akakazania za Marehemu tu? Mbona asitoe habari za kina za huyo mbunge wa kiume na kumuandama Marehemu peke yake? Wangereza wanasema “It takes two to tango and it takes two to quarrel”. Au hii ni ile dhana ya mfumo dume uliotutawala kuwa mwanamke ndie anaefaa kuitwa M……a (siwezi kuliandika hili neno) na mwanamme anafaa uitwa “KIJOGOO”. Kama kazi hii ni ya wawili, vipi iwe sifa kwa mmoja na kashfa kwa mwengine? Shigongo anaogopa mwanmme mwenziwe na akamuonea Marehemu. Au ana ajenda ya siri?
Nimemjuwa Marehemu Amina kwa muda mfupi, na nikajuwa ni mtu mkweli, muaminifu, mwenye ithibati, asiekwenda kinyume na kauli yake. Nasema hivi kwa uthibitisho kamili nilionao binafsi. Miezi michache nyuma alitowa kauli yake kwa mtu mmoja kwamba angempa msaada fulani. Baadhi ya watu hawakupenda Marehemu afanye vile na akawekwa kiti moto na majopo si mawili si matatu, ya watu wazito sana ili aende kinyume na kauli yake ile. Marehemu Amina aliwasikiliza, na baadae akawajibu kuwa hangeweza kwenda kinyume na kauli yake na kwamba kama alivyoahidi, atampa mtu yule msaada wake.
Hapa niliweza kuona tafauti baina ya Marehemu Amina na wanawake na wanaume wengine wengi, wakiwemo vijana kama yeye waliotokea huko Umoja wa vijana CCM, na wanawake na wanaume wakongwe waliokomaa waliotokea katika vilele vikubwa vya Chama. Tafauti ilikuwa wengi wao walitia ulimi puani na kwenda kinyume na walivyotamka, wengine wakawa washiriki wa kumuweka Marehemu kiti moto na kumtishia kuwa wangemfanyia hivi au vile.
Marehemu Alikuwa hamtishi mtu wala hatishiki au kutikisika. Alikuwa ni mtu ambae akishatoa kauli yake, basi hata ashuke malaika gani haibadili abadan. Aliweka msimamo wa kupiga vita madawa ya kulevya kwa nguvu zake zote, jambo ambalo lingemtetemesha mtu mkubwa na mwenye nguvu. Niliwahi kuongea nae na kumwambia “Mwanangu pole pole, wasije wakakudhuru!”. Kauli aliyonijibu ni kuwa amejitolea nafsi yake katika ukweli na haki na chochote kitachomfika ni maktub na hakifutiki. Kweli kilichoandikwa hakifutiki.
Nikiacha hili nitakwenda kwenye utanashati wake ambao ulifika kumponza bungeni kwa kuambiwa na Mheshimiwa Spika atoke nje ya kikao aende akabadili kivazi kwani hakistahili bungeni. Bila kinyongo Marehemu alitoka na tabasamu na akaenda akafanya kama alivyoamriwa. Binafsi wakati huo mimi nilikuwa katika maeneo ya Bunge Dodoma. Kivazi kilichomponza hakikuwa cha uchi au kuvunja heshima, kilikuwa na kidokezo cha kofia ambapo kwa sharia za bungeni tulizorithi kwa wakoloni, kilipaswa kiendane na uvaaji wa gloves na ndipo kiwe kimetimia. Marehemu Amina alitoka nje na akavua kofia ile na kurudi bungeni. Alifika hata kufanyiwa usaili na stesheni moja ya runinga na ilipoletwamada hiyo Marehemu alicheka na kusema kuwa hiyo ilikuwa ni changa-moto ya ukomavu wake na zaidi ya yote ilikuwa ni funzo la kupitia kanuni kabla kutenda jambo.
Wacha niwambie unafiki wa sisi watu. Kwenye runinga nimeona watu wanalia karibu ya kugaragara na kutiririkwa na machozi wakimsifia Marehemu. Jamani wengine katika hao ni wale ambao walichekelea Marehemu alipoamriwa kutoka nje kwa ajili ya kivazi chake, wengi ya hao walidiriki kumbeza na kusema kuwa pale ni pahala pa kazi na si pahala pa fashen na ubishoo. Wengi wetu ambao wakati umeshatupita kushoto na jua limekuchwa tulijisahau kuwa nasi kwa wakati wetu tulipiga vimini na kutesa mjini. Wengi ya wale ambao bado ni vijana walijawa na wivu wa kutomiliki vivazi vya “designer goods” vya Marehemu Amina, au ki maumbile kutopendeza kama yeye. Wivu na choyo vilitutawala na tukasahau kuwa “kila ndege anaruka na ubawa wake na nyota ya mwenzio usiisafiire”.
Kila mtu ana mapungufu yake. Kwa sasa, ilivyo khulka ya binaadamu, utasikia sifa tu atakazo mwagiwa Marehemmu Amina. Kashfa zitatulia kwa wengi wetu kwa ile dhana ya “Never speak evil of the dead”. Bwana Shigongo alisema katika makala yake ya Ijumaa iliopita kuwa anasitisha kuandika mengine kemkem ya Marehemu Amina na kashfa zake kwa vile ni mgonjwa kitandani. Aliahidi kuwa atatuletea uhondo huo baada ya kupona Marehemu Amina. Naomba nimnukuu marehemu bibi yangu ambae alikuwa ndio mentor (muongozi au dira) wangu. Alipokuwa katika “sakarati-l-mauti” nilikuwa namsomea na kumuombea dua huku nikilia na kumwambia “Bibi utapona”. Alinitupia macho akanijibu “Nikipona nimepona, nikifa nimepona”. Nami namuomba bwana Shigongo aliemsakama Marehemu hata wakati alipokuwa mgonjwa mahtuti kitandani, asitunyime conclusion ya uhondo wa hadithi yake tamu maana sasa Mhe. Amina AMEPONA na ni rukhsa kwake kutumalizia makala yake na asituache na shauku na duku duku la kutaka kujuwa kulikoni.
Kwa makala hii namuombea marehemu Amina malazi pema peponi, Mungu amsamehe madhambi yake, ampe kauli thabit, ampe kitaabu chake kwa mkono wa kulia, malaika wema wawe marafiki na wapokezi wake kaburini, apate nuru katika kaburi lake, liwe linatoa harufu ya rehani nasumini na mawaridi, awe mkono wa kulia wa Bwana Mtume siku ya Kiama pamoja na Ma-abrar wema, awape subira wazee wake, mwanawe, marafiki zake na kila aliempenda na aliependwa na Marehemu.
Marehemu Amina namfananisha na Princess Diana wa Uingereza alivyoandamwa na mapaparazi wa ulaya hadi akato(ka)lewa roho yake. Wema, Utanashati,ukarimu, ukweli, huruma, usaidizi na mengi mazuri ya Princess Diana yanafanana na yale ya Mrehemu wetu. Vifo vyao vinatafautiana mazingira lakini vinafanana sababu nazo ni kuandamwa kwa hili na lile. Tarehe pia zinapishana kidogo kama mwezi tu kufikisha miaka kumi kamili.
Diana alikuwa ni Princess wa Uingereza ambae ana andamwa hadi leo miaka 10 baada ya kifo chake. Marehemu Amina ni Princess wetu Tanzania. Natumai Paparazzi wenzangu tutakuwa na hishma za Ki Afrika na utu wa Ki Tanzania na tutamwacha marehemu apumzike kwa amani baada ya kumpa Bwana Shigongo nafasi ya mwisho ya kutueleza yaliyobaki juu ya Marehemu Amina. Baada ya hapo tutamwachia Mungu atamhukumu kwa amali zake nzuri, na zikiwa mbaya atamsamehe.
Naomba kumaliza kwa kunukuu maneno ya Jesus Christ alipowambia Mayahudi walipokuwa wanataka kumpiga mawe Mary Magdalene kwa sabau eti alikuwa mzinzi. Jesus aliwaambi hivi: “Let that among you with no sin cast the first stone”. Yaani naanze kati yenu yule asie na dhambi kutupa jiwe la kwanza. Jee tupo kati yetu tulio malaika bila dhambi? Tukumbuke kuwa mtu akimyooshea mwenziwe kidole kimoja, basi vidole vine vinamgeukia yeye na kumsuta. Upo Bwana Shigongo?
Briani mwanangu Princess Amina. Mungu akulaze pema peponi Amin.
Wakatabahu
Mahfoudha Alley Hamid
E mail:
umimah@zanlink.com