Wednesday, December 21, 2005

OmbaOmba

OmbaOmba


Hapa Boston kuna ombaomba kibao! Tena wengi ni wazungu. Hao ombaomba wengi wao ni walevi na watumia madawa y kulevya na wenye ugonjwa wa akili. Miaka nenda, miaka rudi, ombaomba ni hao hao!

Unapita njiani, unasikia “Spare Change”! Utaona mtu kasimama na kikombe chake anakitikisa. Kuna wengine usipowapa kitu wanakutukana matusi ya nguoni. Halafu kuna wale wakali wanakufuata mpaka ndani ya ATM. Basi watu kwa uoga wanatoa walichonacho na kuwapa kwa kuhofiwa kupigwa au kuibiwa.

Haya, lakini ni lazima niongelee kitu ambacho nimeona, na labda wengine hapa USA mmeona. Kuna ubaguzi katika kile watu wanachotoa kwa ombaomba. Tuseme mtoaji ni mzungu, na ombaomba ni mweusi, basi kama atampa kitu anampa vichenji. Huyo huyo mzungu atatoa noti kwa ombaomba mzungu. Nimeshuhudia mara nyingi tu. Nimeona ombaomba wa kizungu wakipewa noti za $1, $5, $10 na hata $20! Lakini mweusi atapewa vichenji, kwa nini? Je, ni kwa vile mzungu anajisikia vibaya kuona mzungu mwenzake katika hali hiyo, hivyo ni jitihada ya kumwinua? Je, ni kwa vile anaona kuwa mweusi ni hali ya kawaida kuwa maskini? Sijui kama tutaelewa sababu.

Halafu utaona weusi wako tayari kutoa kwa yeyote. Atampa mzungu, atampa mweusi lakini mara nyingi nimeona weusi wakisaidia weusi wenzao kuliko mzungu. Kisa, anajua kuwa yule mzungu anaweza kuishi maisha mazuri akitaka maana Marekani maana bado kuna ubaguzi Marekani.

Lakini nisiseme kuwa wazungu wote ni wabaguzi, maana mwaka juzi kuna ombaomba Cambridge, anaitwa Ramsey, alikuwa amesimima pale Memorial Drive. Basi Mzungu jike tajiri kapita ndani ya gari yake ya fahari na kampa noti ya $100. Ndiyo kampa dola mia moja! Halafu mzungu kamwambia Merry Christmas, maana ilikuwa Christmas Eve. Lakini jambo kama hiyo kutokea ni bahati nasibu.

Utaona wazungu wana jaribu kusaidia wazungu wenzao kupata public housing na huduma zingine. Lakini mweusi anaweza kupitwa. Kuna magari ya kuwasaidia zinapita mitaani, lakini hebu cheki, hao ‘volunteers’ wataenda kwa wazungu kwanza halafu mweusi ataambulia kilichobaki.

Ajabu na si kitu cha kushangaza sana ni kuwa hao ombaomba wa kizungu wakienda kuoga, ku-shave, kuchana nywele na kuvaa vizuri, anaweza kupata kazi kabla ya wewe mweusi na digrii zako!

Na kama hamniamini ukipita barbarani tazama mwenyewe. Ngoja niishie kwa leo, na kwa maksudi sijaongelea habari ya welfare, na shelters maana hii blogu ingekuwa ndefu mno!

2 comments:

Jeff Msangi said...

Chemi,
Nadhani tuliopo Marekani ama Canada tutakubaliana na wewe moja kwa moja kwamba kuna ubaguzi bado na kikubwa kabisa kuna OMBAOMBA.Nimewahi kuandika mengi kuhusiana na hali ya umasikini huku magharibi.Wengi huwa wananiona ni mpinga umarekani au uzungu tu kiasi kwamba wachache wanaamini(hususani ambao hawajafika huku).Labda swali moja tunaweza kujiuliza,inakuwaje nchi zenye maendeleo makubwa ya kijamii na viwanda kama hizi zinakuwa na ombaomba na masikini wa kutupwa?Je ni ubepari au kitu gani?

boniphace said...

Jeff nakumbuka nilikuwa pale Washington D.C na hapo usisiseme. Basi kukawa na mtizedi mwenzangu ambaye hakuwahi kukutana na omba omba wa kizungu hivyo akampa vijidola kiasi, si akaja wa kiafrika na kuanza kupaka kuwa kwa nini tunamuacha wakati yeye ni kaka yetu na kumsaidia mzungu ambaye ana ngudu wengi wenye pesa? Ilibidi kumtuliza na kumsaidia pia kinyume na hivyo ilikuwa uchungu sana moyoni mathalani alipozungumzia suala la rangi.

Hili ni blanketi la pili la mataifa haya, nje wanajitangaza kwa blaketi safi lakini ndani wachafu kweli kweli. Na pia huu ndio msingi halisi wa Ubepari maana hawezi kupatikana bepari kama jamii inakaribiana kiuchumi, lazima awepo mmoja mwenye kugawa umaskini ili awe tajiri