Tuesday, January 03, 2006

Tupende Urembo Asili

Baada ya kuandika kuhusu matako makubwa, na kusoma feedback yenu, nimeona niongee kuhusu mashindano ya urembo. Asante kaka Ndesanjo kwa kunichokoza!

Hivi karibuni Miss Tanzania 2005, Bi Nancy Sumary alienda kwenye mashindano ya Miss World na kafanikiwa kutwaa taji la Miss Africa. Kwa kweli lazima nimpongeze maana toka mashindano ya Miss Tanzania ifufuliwe miaka ya 90, hakuna Mtanzania aliyefanikiwa kuingia katika raundi za fainali na hata kutwaa taji lolote. Kwa kweli Tanzania imepata sifa kubwa katika dunia ya mashindano ya U-Miss. Pia Tanzania imepata sifa kuwa ina wanawake wazuri, lakini nauliza ni uzuri wa aina gani? Maana sioni kama ni uzuri unayafuata maadili ya kiafrika bali ni uzuri wa kizungu!

Nikitazama picha na kanda za video za Miss Ilala, Miss Kinondoni, Miss Utalii, na mashindano mbalimbali za u-Miss huko Tanzania nashangaa nachoona. Kwa kweli naona wasichana weusi wakijaribu kuiga wazungu! Wengine wanapaka make-ups usoni ambazo zimetengezwa kwa ajili ya wazungu wakati make-up za weusi zipo. Yaani ni vichekesho mpaka wengine wanaonekana vituko. Najua hapo niatambiwa nawaonea wivu lakini si kweli na naomba mnisikilize kabla ya kunipa hukumu.

Kwanza tutazame hao wanaopelekwa na nchi zao katika mashindano hayo. Ukiangalia walio kwenye Miss World na Miss Universe, washindi wote wana hulka (characteristics) za kizungu. Tutazame waafrika wanaoenda, cheki nywele zao, zinafanana na wazungu, yaani zimenyoka kabisa. Na kama tunavyojua, sisi wenye asili ya Afrika nywele zetu ni za kipilipili. Hawa wanaweka dawa au weave! Wanaficha nywele zao za asili, sijui wanazionea haya. Je, wanaona haya kusuka nywele zao au kuonyesha mtindo wa nywele enye asili ya Afrika?

Haya, tutazame shepu zao, wote ni wembamba, hakuna mnene, hata hips za maana hawana. Na kama ana matako ni kiasi, sio ile boxi, wowowo, yokohama inayopendwa Africa. Yaani wanafanya mazeoezi eti kusudi wapunguze matako yao. Na hao weusi kutoka Marekani na Ulaya wanafanya liposuction na surgery kupunguza matako yao asili, eti iwe ya kizungu fleti. Huko Afrika tunasema mtu mwembamba ana shida, hana raha, mgonjwa, lakini mzungu anasema ni uzuri. Na sisi tunaiga! Basi unakuta akina dada hata Tanzania, “Oh nafanya diet!” Kheh! Kisa anataka kufanana na mtu amliyemwona kwenye gazeti. Hawajui kuwa hizo picha zinafanyiwa editing na air brushing. Kwa hiyo dada zetu wanashinda njaa kusudi wawe wembamba! Hawajui kuwa hao wanaofanikiwa kwenda kwenye u-Miss, wanajitapisha, na kujinyima chakula kusudi wasinenepe, na ukweli hawana raha.

Haya tuangalie wanavyotembea na kuongea…wanaongea na kutembea kizungu! Jamani na hata macho hawasahau, maana wanatia contact lenses zenye rangi ya bluu na kijani kusudi wawe na macho ya kizungu! Doh! Matokeo ni kuwa hao siyo watu tena bali na madoli.

Na kuhusu rangi ya ngozi, ni lazima niulize, je, umewahi kuona mshindi mweusi tii? Hao weusi wanaofanikiwa wengi ni weupe. Basi hao dada zetu wanajichibua na madawa ya ajabu. Ubaya ni kuwa usoni wanaonekana weupe lakini miili yao bado rangi yao ya asili. Mwisho wanakuwa na rangi mbili. Halafu wengine baadaye wanajikuta wana kansa ya ngozi shauri ya dawa hizo za kujichibua.

Ubaya ni kuwa kama nchi ya kiafrika inataka kushinda mashindano kama Miss World, Miss Universe ni lazima mtu wao awe Mdoli wa kizungu. Mfano, miaka mingi Nigeria walikuwa wanapeleka mrembo wao ambaye alikuwa mrembo Nigeria lakini mbaya kwa wazungu. Mwaka 2001, waliamua kumpeleka Mdoli wa kizungu, yaani dada fulani, mwembamba, futi sita na kashinda. Na tazama kesi ya aliyeshinda Miss Universe 1996, Miss Venezuela, Bi Alicia Machado…baada ya kashinda, alinenepa kweli! Yaani aliongezeka kama kilo 20! Basi majaji wakasema watamvua taji lake kama hatapungua! Dada wa watu alilia na kusema kachoka kashinda njaa!

Na tuanganlie hatima ya hao wanaoabudu hiyo standard ya kizungu na kuwa wembamba. Wanapambana na magonjwa kama Osteoperosis, yaani ugonjwa wa mifupa kuvunjika kwa urahisi, utapialmlo, na magonjwa wa akili. Ndiyo, mtu ambaye kila saa anawaza kujikondesha na kuwa hatapendwa kama si mwembamba ana ugonjwa wa akili. Je, madaktari huko Tanzania wako tayari kutibu hayo magonjwa wa kisasa?

Mashindano ya U-Miss yataendelea kuwepo, na dada zetu wataendelea kutaka kushindana na kufanana na madoli wa kizungu. Bahati mbaya ndo dunia ya leo. Lakini napendekeza tuwe na mashindano ya Miss Bantu, Miss Tanzania asili pia. Mashindano hayo yawe na nia ya kusifia uzuri asili wa mwanamke wa kiafrika. Tusisahau tulikotoka. Na hao wazungu wakiona tunajipenda basi wao wataanza kuheshimu maadili zetu.

8 comments:

boniphace said...

mjadala mpya huu, sishabikii kabisa haya mashindano ya urembo na wala sitoi pongezi yoyote kwa huyo aliyewakilisha Tanzania. Ametuwakilisha katika lipi alipatikanaje na watanzania walifikiaje muafaka wa kusema anatuwakilisha. Naomba ongeza mada hii mara kwa mara maana Afrika inapoteza dira kwa kuiga kila linaloonekana nje ya mipaka yake.

Mija Shija Sayi said...

Hao waliokaa na kupanga sifa za "Bi Dunia", sijui kama walishirikisha dunia nzima kutengeneza hizo sifa. Dunia ni mchanganyiko wa watu wa aina mbalimbali, warefu, wafupi,wanene,wembamba, mbilikimo,weupe, weusi, vipofu, vilema na wengineo wengi. Sasa iweje warembo wawe ni warefu wembamba na weupe tu? Kuna vilema wengi wazuri tena wenye vipaji ambavyo wewe uliyekamilika humfikii, kuna wafupi na wanene wengi wenye akili na uzuri hadi ukazubaa..., Mimi sielewi mwenzenu.

Ndesanjo aliwahi kuongelea juu ya VITA KUU YA DUNIA, ndio haya haya ya BI DUNIA.

Asante Chemi kwa mada.

mwandani said...

Wale madoli mi nawaona kama waongo, nikisikiliza majibu ya maswali wanavyojibu kwenye mashindano ya kushinda uzuri, kila kitu inakuwa kama wamekariri, wakicheka hawafungui midomo kwa sana.
Halafu wembamba sana. Mie miss Bantu tu, mwisho wa mchezo. yokohama ntalisifia milele yote, au kama wasotho wanavyoita 'mafeshefeshe'

FOSEWERD Initiatives said...

khaa! chemi leo umenifungua macho! yaano kum,be imefikia watu kuvaa lensi ili wawe kama wadachi?

cheers

Chemi Che-Mponda said...

Hey Mark Msaki,

Kwa kweli inasikitisha sana. Unakuta mtu mweusi ana macho ya bluu au kijani unabakia kushangaa. Kumbe ni hizo contact lens za rangi. Zina soko kweli hapa USA, yaani kuna weusi ambao wanataka kuwa 'zungufied' 100%, nywele wana blichi, macho bluu, ngozi imechubuliwa, pua imechongwa kwa surgery, matako yamepunguzwa, doh!

Ndesanjo Macha said...

Yaani vigezo vya mambo yote wanatoa wao. Nasi kama kawaida yetu tunatii na kukubaliana nao. Ni furaha ilioje ninapoona watu wanahoji dunia inayopelekeshwa puta na hawa jamaa wanaoona kuwa mambo yao yote ni ya kidunia na yetu ni ya kishenzi.

mloyi said...

labda hawawajui akina anna, kama wanavyoitwa watu wenye annorexia. wanabidi kufundishwa ili wasijejiangamiza wenyewe.
kazi kwako dada.

Reggy's said...

Warembo wapo. walizaliwa hivyo hivyo na kila mtu ana mrembo wake. HAKUNA HAJA YA KUWASHINDANISHA, kwani wanaoshinda huo urembo kwangu mimi si lolote si chochote.