Showing posts with label Tanzania Films. Show all posts
Showing posts with label Tanzania Films. Show all posts

Tuesday, November 10, 2009

IBUA FILMS STAR TANZANIA YAHAMIA MWANZA


Baada ya mchakato mzima wa kuibua vipaji vya wasanii chipukizi wa maigizo yaani IBUA Film Star Tanzania kuanzia Arusha, zoezi zima linahamia Mwanza katika Nyanza Shule ya msingi iliyopo Balewa Road tarehe 14 na 15 Novemba kabla ya kuhamia Dodoma.

Chipukizi waliofanikiwa kuiwakilisha mkoa wa Arusha ni pamoja na Salum Ahmed Shafii, Pauline Edward Munisi, Michael Elias Mrema, Mbara Meena na Enhard Haruna. Kutokana na mwamko mkubwa wa wasanii chipukizi, fomu za kujiunga na shindano la IBUA Film Star Tanzania zinaendelea kutolewa maeneo mbali mbali na mikoa husika. Hii ni kuwawezesha wasanii chipukizi kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wao ya kuendeleza vipaji vyao na kuviacha vikipotea kwa kukosa njia ya kuvikuza. Usaili wa mikoani utaandaliwa vipindi maalum na kuonyeshwa kupitia mojawapo ya runinga hapa nchini.

Taasisi ya YEC Production, inayojihusisha na kukuza na kuibua vipaji kwa vijana katika ulingo wa filamu nchini, imegundua njia pekee ya kuibua vipaji hivyo na kuviokoa visipotee kwa kuanzisha shindano maalum la kusaka vipaji. Washiriki wataonyeshwa kwenye runinga kupitia kipindi maalum ambapo watazamaji watahusishwa kumpata staa halisi wa filamu Tanzania.

Mbali na kuviendeleza vipaji vyao pia washiriki watapata mafunzo katika nyanja zote kuanzia za uandishi wa muongozo (scripting) hadi uigizaji bora na kuwawezesha kufikia malengo yao.

Vigezo vilivyotumika katika kumsaka msanii huyo chipukizi ni kuwa na umri wa miaka 16 ikiwa ni pamoja na uelewa. Hata kutokuonekana katika tamthilia au sinema ya aina fulani hapa nchini hicho pia ni kigezo kimojawapo ambacho ni kizuri, kwani vijana wanaochipukia ndiyo wanahitaji msaada mkubwa katika kuibuliwa vipaji, tofauti na wakongwe ambao tayari wamejitangaza.

YEC, imeahidi kuyaangalia matatizo yanayowakabili wasanii kwa kina na kuahidi kutoyarudia, kama yanavyofanywa na baadhi ya wasanii wakongwe, ndiyo maana wameamua kuingia mikataba ya mwaka mmoja na washindi watakaofika kumi bora, ili kuliepuka tatizo hilo.

Sambamba na mikataba hiyo kwa watakaofika kumi bora, pia watatoa nafasi ya kuwapeleka shule watakaoingia tano bora kwa ajili ya kujiendeleza mambo mbali mbali ya sanaa ambapo atakayeibuka kinara atapewa zawadi nyingine maalum.

Pia mchakato wa kuwapata washindi kumi hadi tano bora utaanzia kwenye 20 bora, ambapo watacheza filamu mbili huku majaji wakiangalia kipaji cha msanii mmoja baada ya mwingine na kuendelea kuchujwa hadi kupatikana mshindi.

Filamu watakayocheza zitakuwa katika mandhari ya mtanzania halisi, huku asilimia 60 ya mauzo ya kazi hizo yatakayopatikana zitakuwa kwa ajili ya wasanii wenyewe.

Kutokana na kuona umuhimu wa suala hilo, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) liliamua kutoa vibali halali vya kuendesha mchakato huo, ikiwa ni pamoja na kupewa baraka na chama cha hakimiliki Tanzania (COSOTA) ya kusimamia kazi hiyo.

Mikoa husika katika mchakato wa kwanza ni Arusha, Mbeya, Zanzibar, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam lakini wigo wa mikoa utaongezeka mwaka hadi mwaka.

Jackline Wolper
Balozi IBUA Film Star Tanzania

Monday, October 05, 2009

IBUA Film Star Awards - Tanzania


WACHEZA FILAMU CHIPUKIZI KUSAKWA TANZANIA

Mchakato wa kutafuta na kuibuwa vipaji vya waigizaji chipukizi linaanza rasmi na litahusisha mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Zanzibar na Dar es Salaam.
Uibuaji na ukuzaji wa vipaji vya wasanii chipukizi wa filamu ambao hawajawahi kushiriki katika filamu au tamthilia yoyote itawahusisha watanzania wenye vigezo vya kuwa na umri wa miaka 16 na kuendelea, awe na akili timamu, awe ni raia wa Tanzania na ajue kusoma na kuandika.
Mchakato utahusisha kufanya usaili katika mikoa husika hadi watakapopatikana kumi bora ambapo washiriki watachuana kumtafuta msanii chipukizi wa filamu Tanzania.
Mwaka huu kampuni mbali mbali zimejitokeza kudhamini mashindano haya lakini yatatajwa hapo baadaye
Mshindi wa IBUA Film Star Tanzania atajinyakulia zawadi ambayo itatangazwa baadae na pia atapata mkataba wa kushiriki filamu mbali mbali za wasanii wa ndani na nje ya nchi.
Mshindi atapatikana kwa kupigiwa kura na wananchi kupitia kipindi maalumu kitakachoonyeshwa hapo baadae.
Fomu za kushiriki shindano la IBUA Film Stars Tanzania zinapatikana mikoa husika kama ifuatavyo Arusha (Club Silk), Mwanza (Salma Cone), Mbeya (CPMTL Stationery mkabala na ofisi ya mkuu wa mkoa), Dodoma (Zunny Ice Cream Parlour), Zanzibar (Ofisi za Zenj FM), Dar es Salaam (TCC Chang’ombe, Shear Illusions mlimani City, Royal Salon Sinza, Zizzou Fashions). Fomu zitaanza kupatikana tarehe 10 Oktoba 2009.
Mwisho wa kuchukua fomu ni tarehe 30 Oktoba 2009 kabla ya kuanza usaili mjini Arusha tarehe 31 Oktoba na 01 Novemba.
Zoezi la usaili litafanyika kabla ya wananchi kupata nafasi ya kutoa maoni na kufanikisha kuwapata washindi.

Jacqueline Wolper
Afisa Uhusiano-YEC PRODUCTION

Wednesday, December 17, 2008

Filamu na Tamthiliya zinapotosha Waadili

(Pichani l-r Kathy Flewellen, Geri Augusto, naWalter Bgoya 1974)

Nakubaliana nao kabisa. Mnakumbuka miaka ya sabini Mwalimu alipopiga maarufuku mtindo wa 'Jiving' na kuimba nyimbo za kizungu. Alisema kuwa si maadili yetu na pia alitaka tukuze utamaduni wa Tanzania. TV na filamu za nje zilikuwa marufuku. Mnakumbuka kulikuwa na censorship board chini ya Tanzania Film Company.

***************************************************************
Na Beda Msimbe (Lukwangule Entertainment Blog)

TAMTHILIYA zinazoonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni, zimeelezwa kuwa ndiyo chanzo cha kuharibu jamii na kusababisha wanajamii wengi kuiga utamaduni wa magharibi badala ya ule wa Tanzania na Afrika.

Hayo yalisemwa na Godfrey Mngereza, kutoka Baraza la Sanaa la Taifa, BASATA wakati akichangia mada kwenye mkutano wa sita wa Sekta ya Utamaduni, unaoendelea kwenye Hoteli ya Oasis mjini Morogoro.

“Ikifika nyakati za usiku, watoto wetu hasa wasichana wamekuwa wakiangalia tamthiliya ambazo nyingi zinakuwa haziko katika maadili ya Kitanzania, hizi ndizo zinasababisha kuporomoka kwa maadili ya kitanzania.

Mngereza alisema kuwa kuna kila sababu ya televisheni mbalimbali kuonyesha tamthiliya zenye kuonyesha maadili na utamaduni wetu. “Mfano, tunataka kuona televisheni ya taifa, TBC1 inapigania maadili mazuri ya utamaduni, lakini si kuwa mfano mbaya katika ujenzi wa maadili,” alisema.

Alisema pia kuwa vibanda vya mitaani vinavyoonyesha sinema, vimekuwa chanzo cha kumomonyoka kwa maadili kwa kuonyesha filamu za ngono. “Utashangaa watoto hawaendi kulala na utasikia wanakwenda kwenye pilau…wenyewe wanaziita hizi filamu za ngono pilau, sasa huwezi kuelewa, lakini wenyewe wameshazipa jina,” alisema.

Naye mtunzi na mchapishaji wa vitabu, Walter Bgoya alisema kuwa Tanzania imeendelea kuwa jalala la filamu za Kinaijeria hata kama hazina ubora na nyingine hazifundishi.
Alisema wasanii wa Tanzania hawana mbinu wala hawawezi kutengeneza filamu bora ndiyo maana kumekuwa na kumwagika kwa filamu hizo. Hata hivyo, alisema kuwa wasanii wa Tanzania wanatakiwa kujifunza zaidi mbinu za kisasa na kuweza kutengeneza filamu bora.

Bgoya alisema kuwa wasanii wa Tanzania hawataki kusoma na kuongeza wigo wa kujifunza. Hii ni wazi kuwa wanatakiwa kusoma sana ili kuweza kutengeneza mwongozo bora utakaotoa filamu bora.

Akizungumzia utandawazi, Katibu Mtendaji Baraza la Sanaa Tanzania , BASATA, Ghonche Materego alisema kuwa Watanzania wameathiriwa na utandawazi na sehemu kubwa huendesha utamaduni kwa kuangalia umagharibi.

“Hata wasanii wa bongo fleva, wamekuwa wakifanya kazi zao kwa kuangalia mitindo ya mataifa ya Magharibi, hatuwezi kukwepa utandawazi, utaendelea kuharibu jamii ya wasanii kwa kuiga.

Saturday, May 03, 2008

Tuzo za Vinara wa Filamu

Press Release kutoka One Game:

Majaji tuzo za Vinara kuanza kazi leo!

Na Mwandishi Wetu

Jopo la majaji wa Tuzo za Vinara wa filamu nchini (Vinara Film Award) leo Jumamosi ya Mei 3, 2008 linatarajiwa kuanza rasmi kazi ya kuziangalia filamu za Kitanzania zinazowania tuzo hizo kabla ya kuzitolea maamuzi.

Mratibu wa One Game Promotion inayoaandaa utolewaji wa tuzo hizo, Khadija Khalili amesema kuwa, majaji hao watatanguliwa na semina ya siku moja kabla ya kuanza zoezi la kuziangalia filamu hizo chini ya usimamizi wa maafisa wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Jopo hilo linaloundwa na wataalamu wa mambo ya filamu nchini wanakutana leo katika hoteli ya Regency ya Mikocheni jijini Dar es Salaam na kuendelea na kazi hiyo kwa siku kadhaa kabla ya kuibuka na majina ya filamu na wasanii walioingia katika makundi ya kuwania tuzo hizo.

"Kikubwa ni kwamba jopo la majaji linategemea kukutana Jumamosi ya Mei 3 (leo) katika hoteli ya Regency Mikocheni kwa ajili ya semina na kuanza kazi ya kuzipitia filamu zilizowasilishwa kwa ajili ya kuwania tuzo za Vinara," alisema Khalili.

Vipengele vinavyoangaliwa ni Filamu Bora ya Mwaka, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kike, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kike, Muongozaji Sinema Bora wa Mwaka, Mchekeshaji Bora wa Mwaka, Mwandishi Bora wa Filamu na Mtunzi Bora wa Filamu.

Vingine ni Filamu Bora ya Kutisha, Muigizaji Mwandamizi Bora wa kike), Muigizaji Bora Mwandamizi wa Kiume, Adui Bora kwenye Filamu, Wimbo Bora wa Mwaka (Sound Track), Mhariri Bora wa Filamu ambao wote watapata tuzo. Pia itatolewa tuzo ya heshima kwa wale waliotoa mchango wao kukuza sanaa nchini.

Wiki iliyopita, Khalili alisema kuwa, zaidi ya filamu sabini zimeingizwa na watengenezaji wa filamu nchini kuwania tuzo hizo.

Filamu zinazowania tuzo hizo ni zile zilizokamilika kutengenezwa Januari 2007 mpaka Machi 31, 2008.

Tuzo hizo zitakazotolewa Mei 30, zimedhaminiwa na Tanzania Breweries Limited (TBL) kupitia bia ya Ndovu Special Malt, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Global Publishers.

Wednesday, March 12, 2008

Tuzo za vinara wa Filamu Tanzania 2008


FOMU ZA KUSHIRIKI TUZO ZA VINARA WA FILAMU TANZANIA KUTOLEWA WIKI HII

Baada ya kufana kwa uzinduzi wa Tuzo za Vinara wa filamu Tanzania,watayarishaji wanaalikwa kujaza fomu za ushiriki ili kuweza kuwasilisha kazi zao katika Tuzo za 2008. Fomu hizi zitapatikana katika ofisi za BASATA (Muulizie Omar Mayanga), Wananchi Wote, Kapico, GMC na Game First Quality.

Baada ya kujaza fomu, watengezaji wa filamu wanatakiwa kurudisha fomu na nakala ya kazi kwenye ofisi za BASATA kwa Omar Mayanga.Utoaji tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania, unalenga katika kuifanya sanaa ya Tanzania kupata nguvu mpya na kuwafanya watengenezaji na wadau sanaa kufanya bidii katika ushindani wa soko la sanaa na hivyo kutengeneza kazi zilizo bora zaidi zinazoweza kuuzika kimataifa ili kuiweka nchi yetu kwenye ramani ya dunia.

Tuzo za Vinara wa Filamu Tanzania pia zinalenga kuwafanya wananchi kuendelea kuwa na mwamko wa kupenda kazi zinazotengenezwa na Watanzania wenzao ili kupata mafunzo mbalimbali yatokanayo na kazi za wasanii na pia kukuza soko kwa faida ya pande zote mbili.

Katika fomu hizo, kutaainishwa mambo muhimu ambayo mtengenezaji wa filamu atapaswa kujaza. Kama vile; Jina kamili la kampuni iliyotengeneza filamu au video na anwani kamili, Jina la Mtayarishaji Mkuu wa filamu (Executive Producer), Jina la Mtayarishaji wa filamu. (Producer), Jina la Mtunzi wa hadithi (Story Writer), Jina la Mwandishi wa skripti (Scriptwriter), Jina la Muongozaji (Director), Jina la Mhariri (Editor), Majina kamili ya wasanii wote waliyoigizia katika filamu husika (Characters), Jina la Muongozaji wa Taa (Lightsman), Jina la Mrekebishaji Sauti (Soundman), Jina la Mpiga Picha (Cameraman), Jina la Meneja wa Mandhari (Location Manager), Jina la Mpangiliaji wa Picha (Cinematographer), Jina la Mtunzi wa Muziki (Music Composer), Jina la Studio iliyofanya/zilizofanya kazi kwa filamu husika.

Fomu itakuwa na maswali mengine kama vile; filamu imetengenezwa lini, mahali ilikotengenezwa, maudhui ya filamu na lugha iliyotumika. Baada ya fomu hizo kujazwa kwa usahihi, zitatumwa kwenye ofisi za waandaji, kwa mkono au njia ya posta kwa anuani kamili ya waandaji. Watengenezaji wa filamu husika watapaswa kuambatanisha na mkanda wa filamu (VHS/DVD/VCD).

Kutakuwa na jopo la majaji wanane (8) watakaochaguliwa na waandaji kwa kushirikiana na Baraza la sanaa la Taifa nchini watakaokuwa na jukumu la kupitia filamu zote na kuzitolea uamuzi. Majina na wasifu za majaji zitawekwa bayana hivi karibuni. Pia vigezo zitakazotumika zitawekwa wazi.
Filamu zitakazoingizwa kuwania tuzo ni zile zilizotengenezwa na Watanzania kuanzia Januari 2007 hadi mwisho wa siku ya kualikwa watengenezaji kuingiza filamu zao ambayo itakuwa 31 Machi 2008.
Kushiriki kwa watengezaji wa filamu itasaidia kupata Filamu Bora ya Mwaka, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora wa Mwaka wa Kike, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kiume, Muigizaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa Kike, Mwongozaji Sinema Bora wa Mwaka, Mchekeshaji Bora wa Mwaka, Mwandishi Bora wa Filamu, Mtunzi Bora wa Filamu, Filamu Bora ya kutisha, Muigizaji Mwandamizii Bora wa kike (supporting actor), Muigizaji Bora Mwandamizi wa Kike; Adui Bora kwenye Filamu,Mhariri Bora wa Filamu na mapambo na maleba ya mwaka.Pia itatolewa tuzo ya heshima kwa wale waliotoa machango wao kukuza sanaa nchini.

Tukio la utoaji wa tuzo hizi limepangwa kufanyika mwezi Mei 2008 na litafanyika kila mwaka.

Msemaji Khadija Khalili-Mratibu