Saturday, November 19, 2016

Makamu wa Rais Kuzindua Kampeni ya Uchunguzi wa Bure wa Saratani ya Matiti

Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), Dkt.Serafina Mkuwa (kulia), akitoa taarifa kwa wanahabari kuhusu uzinduzi wa kampeni ya uchunguzi na matibabu ya Saratani ya Matiti na mlango wa kizazi mkoani Mwanza.

Kampeni hiyo itazinduliwa kesho katika Uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza na Makamu wa Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan na baadaye kufanyika kwa siku mbili bure.
Na BMG
Kutoka kushoto ni Dkt.Mary Charles ambaye ni Makamu wa Rais MEWATA, Mganga Mkuu mkoa wa Mwanza, Dkt.Leonald Subi, Rais wa MEWATI, Dkt.Serafina Mkuwa, Mwenyekiti Kamati ya Kampeni na Mjumbe kamati tendaji MEWATA, Dkt.Magdalena Lyimo pamoja na Mratibu wa huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Mwanza, Secilia Mrema.
Pia watumishi wa afya mkoani Mwanza wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya kusaidia utoaji wa huduma za uchunguzi wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi
Na George Binagi-GB Pazzo
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Hassan Suluhu, kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa kampeni ya uchunguzi na matibabu ya saratani ya matiti na mlango wa kizazi bila malipo mkaoni Mwanza.

Rais wa Chama cha Madaktari Wanawake nchini MEWATA, Dkt.Serafina Mkuwa, ameyasema hayo hii leo Jijini Mwanza wakati akitoa taarifa ya kampeni hiyo kwa wanahabari.

Amesema baada ya ufunguzi wa kampeni hiyo, akinamama na wasichana mkoani Mwanza, watapata fursa ya kufanya uchunguzi na matibabu ya Saratani ya matiti na mlango wa kizazi kwa muda wa siku mbili ambazo ni kesho na kesho kutwa katika vituo vinne ambavyo ni Uwanja wa Furahisha, Vituo vya Afya Makongoro, Karume pamoja na Igoma Jijini Mwanza ambapo huduma zitakuwa zikitolewa kuanzia majira ya saa moja asubuhi.

Tatizo la saratani ya matiti na mlango wa kizazi bado ni changamoto kubwa mkoani Mwanza ambapo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt.Leonald Subi, anabainisha kwamba takwimu zilizopatikana katika halmashauri za Ukerewe, Buchosa pamoja na Kwimba, zinaonesha kwamba kati ya wanawake 1,294 waliochunguzwa, 58 wanamabadiliko ya awali ya saratani na 18 wanamabadiliko makubwa ya saratani na wamepewa rufaa kwenda hospitali ya rufaa Bugando kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Hata hivyo Dkt.Subi amewahimiza wananchi kuepuka matumizi ya tumbaku, sigara pamoja na pombe kali ambayo huchangia ongezeko la magonjwa ya saratani ya matiti na mlango wa uzazi kwa akinamama huku akiwahimiza kufanya uchunguzi angalau mara moja kwa mwaka ili kubaini tatizo mapema kwani tiba ya mapema husaidia kupambana na magonjwa hayo.

Chama cha Madaktari Wanawake nchini kimeshirikiana na Wizara ya Afya, Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mwanza pamoja na wadau wengine wakiwemo Gender Health, PSI pamoja na Tayoa katika kufanikisha huduma hiyo ya uchunguzi na matibabu ya saratani ya matiti na mlango wa kizazi bila malipo mkoani Mwanza.

No comments: