Saturday, November 12, 2016

Miss Tanzania 2010, Genevieve Mpangala Kusaidia Kurejesha Heshima ya Elimu Tabora

Mrembo wa taji la Miss Tanzania 2010 Genevieve Mpangala amejitosa kusaidia kurejesha heshima ya mkoa wa Tabora katika elimu hasa kwa wasichana ambao ndio nguzo kubwa kwa familia na maendeleo ya taifa.

Mrembo huyo ameamua kufanya hivyo kwa kutembelea shule mbili za Tabora Girls na Isevya kuongea na wanafunzi, kuwapa moyo na kuangalia matatizo yanayowasumbua katika kujipatia elimu.

Akizungumza na Moblog amesema kwamba amekuwa na masikitiko makubwa na matokeo ya mitihani ya kitaifa ya sekondari kwa miaka mitatu ilhali simulizi za Tabora miaka iliyopita ni za kufurahisha sana uikionesha kwamba mkoa huo ndio kitovu hasa cha elimu.

Anasema ukisoma nyaraka mbalimbali unaona jinsi Tabora ilivyokuwa ngome ya elimu huku watanzania wengi wakifika hapo pia kupata elimu ya sekondari.

Mrembo wa taji la Miss Tanzania 2010, Genevieve Mpangala akizungumza wa shule ya sekondari Tabora Girls hivi karibuni.

“Kwa kweli pamoja na masimulizi mazuri kuhusu elimu Tabora miaka ya 80 na 90 ,nilichagua Tabora girls kwa sababu ni shule aliyosoma mama yangu mzazi form 1 mwaka 1977 mpaka 1980 mpaka na aliisifia sana shule yake hiyo na nikapenda niweze kuwa karibu nao kuhakikisha wanafunzi wote wanamaliza,na Isevya ilikua chaguo la pili kwasababu ilikua ni shule ya kutwa (day) na nilipendelea kuongea na wanafunzi hao” alisema Genevieve.

Mkoa wa Tabora ambao unapatikana kati ya Magharibi ya Tanzania kwenye uwanda wa latitudo 40-70 Kusini na longitudo 310 - 340 mashariki ukipakana na mikoa ya Shinyanga, Katavi, Singida, Kigoma na Dodoma ni mji ulioanzishwa na wafanyabiashara wa Kiarabu kwenye miaka ya 1850 ukijulikana kama Kazeh .

Kihistoria Kazeh ambayo ilikuwa kitovu cha biashara ya utumwa, mwaka 1871 robo ya mji ilichomwa moto na kuvurugwa na mtawala wa wanyamwezi Mirambo .

Ingawa mwaka 1885 hadi 1891 wajerumani walijaribu kutawala, historia zinasema kwamba mji huo ulikuwa na vurugu kubwa lakini baadae ukatawaliwa na wajerumani wakafanya mji wa utawala kabla ya vita kuu ya kwanza kuingia na wao kung’olewa.
Mrembo wa taji la Miss Tanzania 2010 Genevieve Mpangala akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi na mwalimu wao alipofanya ziara shuleni hapo.

Pamoja na historia yenye misukosuko ya Mkoa wa Tabora ambao ni moja ya mikoa yenye eneo kubwa unategemea sana kilimo kufanikisha maisha lakini kwa miaka mingi mkoa umekuwa ukididimia kimaendeleo na kijamii.

Mkoa wa Tabora ambao umekua wa mwisho kwa miaka mitatu mfululizo mwaka 2013,2014 na 2015 unahitaji nguvu kubwa ya kujiondoa katika shida ya kuporomoka katika elimu

Mrembo Genevieve anasema ziara yake katika shule hizo imemfumbua macho na kuona haja kubwa ya kuendelea na programu za kufufua matumaini.

Pamoja na kuwashukuru walimu kwa ushirikiano waliompa aliwataka wanafunzi kuweka mkazo katika imani, matumaini na kutekeleza ndoto zao katika uwanda mkubwa zaidi.
Aidha pamoja na kuzungumza "HAVE FAITH,HOPE FOR MORE AND DREAM EVEN BIGGER", pia aliwaasa kuwa elimu ni msingi mzuri wa maisha na kuwa wasiharakishe na kupotoshwa na mambo ya kidunia kwani haya maisha yapo.

Akiwa na wasichana wa shule ya Tabora Girls walimweleza changamoto wanazokutana nazo ikiwa ni pamoja na kutokuwepo na uzio kwenye shule yao hiyo, uhaba wa vitabu, upungufu wa walimu, uhaba wa upatikanaji wa habari mubashara, kwa wanafunzi kwamba hawana king'amuzi,kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi wanauhitaji wa msaada wa kofia pamoja na mafuta ya kuwakinga na jua.

Matatizo hayo yanatokana zaidi na kwamba wengi wao wanatoka kwenye mazingira duni. Changamoto nyingine ni pamoja na kuwa na zahanati ambayo ina uhaba wa vifaa mfano:vyandarua vya kutosha pamoja na vitanda,pia kwa wanafunzi ambao wanaulemavu wa macho ambao ni hafifu na vipofu kabisa hivyo kuna uhaba wa brail paper.

Ziara fupi ya Mrembo wa Tanzania 2010 Genevieve Mpangala kwa shule mbili za jijini Tabora za Isevya Secondary School na shule ya vipaji maalum ya wanawake Tabora girls.

Amesema katika mazungumzo yake na wanafunzi hao amebaini pia kwamba kutofanya vyema kwa wanafunzi pia kunasababishwa na wanafunzi hao kutumia madawa ya kulevya, utoro, mimba za shuleni na wazazi kuozesha mabinti katika umri mdogo kabla ya wao kumaliza shule.

No comments: