Saturday, December 24, 2016

Unyanyasaji wa Kijinsia: Mchango wa UMIss Tanzania Unaonekana?

Na Elias Muhongo

Tukiwa tunaangalia tangazo la biashara la ‘BIG BOSS’ nikashtukia mwanangu mmoja akilalamika: “Hapo si tunajinyanyasa kweli?”. Nikamuuliza ana maana gani? Akasema “ Baba angalia sana tangazo hilo. Huyu mama anamfahamu boyfriend wake lazima, ndiyo maana alikuwa hakupotea nyumba. Lakini kukutana na harufu ya manukato anayotumia boyfriend wake akaamua kuondoka na aliyejipaka (manukato hayo)? Ni unyanyasaji wa kijinsia na hapo tunajinyanyasa wenyewe”. Mjadala ulikuwa mkali lakini nikomee hapo na kuendeleza mawazo yangu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, hasa unyanyasaji wa wanawake.
Nimeangalia mijadala mingi kipindi hiki na kuilinganisha na kipindi fulani kilichopita. Wakati wa maandalizi ya mkutano wa Beijing 1990, nilishiriki sana maandalizi hayo hapa nchini. Nakumbuka akina mama kufikia hatua ya kuainisha aina mbali mbali za unyanyasaji unaowakabili wanawake. Kupigwa na waume zao. Kusafiri mbali kutafuta maji. Huduma duni za afya wakati wa uzazi na uzazi wa mpango, nakadhalika. Lakini pia walijiambia ukweli mwingine wasiojiambia siku hizi. Walijiambia jinsi inavyokuwa vigumu kukutana na mwanamke aliye madarakani. Jinsi ilivyo vigumu mwanamke kumpigia kura mwanamke mwenzake licha ya wingi wao.
Tulijadili na jinsi katika michezo kama dansi akina mama wanavuliwa nguo na kujianika huku wenzao (wanaume) wanacheza wamejivalia nguo.

Wagombea Miss Tanzania 2009

Ninaamini kuwa huenda baadhi ya manyanyaso yamepungua. Lakini ukichunguza sana utakuta yale wanayojinyanyasa yanaendelea na hayapigiwi kelele kama yale wanayonyanyaswa.
Tuangalie na huu unyanyasaji wa kijinsia kupitia ‘Miss Tanzania’. Nakumbuka katika historia ya Miss Tanzania tangu viruhusiwe baada ya utawala wa Mwalimu Nyerere, naweza kudhibitisha kuwa ni mwaka mmoja ambao Tanzania iliwahi kuwakilishwa na mtanzania halisi licha ya kupingwa na watanzania wengi. Ni mwaka Tanzania ilipowakilishwa na Mtanzania mwenye asili ya India. Huyo alionyesha asili yake na utanzania wake. Lafudhi yake ilikuwa ya mtanzania mwenye asili ya India. Myondoko yake ilikuwa ya Mtanzania mwenye asili ya India. Rangi ya ngozi yake iliwakilisha Mtanzania mwenye asili ya India. Nywele za kichwa chake ziliwakilisha mtanzania mwenye asili ya India.

Nani anitajie mwingine? Anitajie Mis Tanzania ambaye aliiwakilisha Tanzania nje ya Tanzania na waangalizi wakaiona Tanzania? Sitarajii. Maandalizi ya Miss Tanzania yanamuandaa mwakilishi wetu kuuondoa utanzania ndani mwake. Maandalizi huanzia Willayani. Yanapokamilika ngazi ya Taifa mshindi na washiriki wote wanakuwa wamekamuliwa utanzania ndipo (mshindi) anakabidhiwa bendera ya Tanzania kwenda kuwakilisha kitu kisichojulikana. Huwezi kuuona utanzania katika lafudhi yake. Huwezi kuuona utanzania katika myondoko yake (gait). Huwezi kuuona utanzania katika asili ya ngozi yake wala nywele zake. 

Lakini kila mashindano hayo na maandalizi yake yanapokuwepo hukosi kuhisi unyanyasaji wa wazi na wa siri. Mavazi wanayovaa ni unyanyasaji wa ajabu usioendana na Utanzania. Lakini wasikie waandaaji wakijitetea kuwa hakuna eushwa ya ngono zinazoendelea katika shughuli hiyo. Nani haoni kuwa hayo hayawezi kukosekana? Huu wote ni unyanyasaji wa kijinsia unaoendelea kwa hiyari ya wanyanyaswaji na wanaharakati usioweza kupigiwa kelele kwa sababu tu wafadhiri wa miradi ya uanaharakati ndio wadhamini wa unyanyasaji huo.

Kuna wakati niliwahi kufikiri badala ya mashindano ya Miss Tanzania kwa nini kusianzishwe mashindano ysa mapishi ya kitanzania. Inahitaji kuandaa vigezo vya kuamua namna ya kuamua kati ya chakula cha kihaya na kipare. Mpare atapika kande na mhaya ndizi zilizochanganywa magarage mabichi na nyama iliyokauka watu watakula na kuuona utanzania. Ikishindikana basi shindanisha wapishi mbali mbali wa chakula aina moja. Mapishi yetu hayawezi kuchakachuliwa kama ambavyo utamaduni wetu unachakachuliwa kupitia mashindano haya ya Miss Tanzania.

Elisa Muhingo

No comments: