Showing posts with label Ali Hassan Mwinyi. Show all posts
Showing posts with label Ali Hassan Mwinyi. Show all posts

Friday, March 13, 2009

Aliyempiga Mzee Ruksa Afungwa Mwaka Moja!


KIJANA IBRAHIM SAIDI A.K.A SULTANI A.KA. USTAADHI AMBAYE LEO AMEHUKUMIWA KIFUNGO CHA MWAKA MMOJA JELA KWA KOSA LA KUMPIGA KOFI HADHARANI RAIS MSTAAFU ALHAJI ALI HASSAN MWINYI WAKATI WA BARAZA LA MAULIDI MNAMO MACHI 10, 2009 KATIKA UKUMBI WA DIAMOND JUBILEE HALL JIJINI DAR.

Hakimu mkazi wa mahakama hiyo Neema Chusi, Amesema kabla ya kusoma hukumu kwamba mahakama imezingatia jinsi mshtakiwa huyo alivyokubali kosa hilo na kuona kwamba anashtahili adhabu hiyo.

Akijitetea kabla ya kuhukumiwa kifungo hicho, mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo, Said alidai kuwa anakiri kufanya kosa hilo na kwamba anakubali kupewa hukumu na mahakama hiyo.

“Mimi ni kiumbe dhaifu, labda nisiiombe mahakama ila nimuombe mwenyezi Mungu Subhana wataallah kama atataka nitapunguziwa adhabu”alisema Said.

Said ambaye kabla ya kuongea maneno hayo alikuwa akizungumza lugha ambayo haikuweza kutambulika na mahakama hivyo kumfanya Hakimu Chusi kumtaka kubadili lugha hiyo ili mahakama iweze kumuelewa.

Baada ya mshtakiwa huyo kuondolewa kizimbani hapo huku akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, ndugu akiwemo mama mzazi wa Said walionekana wakilia nje ya mahakama hiyo.

Thursday, March 12, 2009

Aliyempiga Mwinyi Afungua Mdomo

Wadau, navyoona wasingempa nafasi huyo kijana aongee. Watatokea wengine wenye agenda zao na kufanya fujo. Mshenzi huyo anastahili kipigo cha nguvu! Nchi yetu Tanzania, ni nchi ya amani. Pia tunajivunia kuwa waKristo na waIslamu wanapatana na hakuna bugudha, Wenzetu barani Afrika wanatuonea wivu! Nina hisi huyo kijana katumwa na watu fulani!

****************************************************
Kutoka ippmedia.com

Aliyempiga Mwinyi afungua domo

2009-03-12
Na Waandishi Wetu

Wakati taasisi mbalimbali za kidini, wananchi wa kawaida na Kamati ya Bunge zikilaani kitendo cha Rais Mstaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, kupigwa kofi shavuni, muumini aliyefanya kitendo hicho, Ibrahim Said, ameeleza kuwa alifanya hivyo kupinga matumizi ya kondomu kwa waumini wa dini ya Kiislamu kwa madai kwamba, yanachochea vitendo vya zinaa.

Pia alisema alifanya kitendo hicho kupinga kuwapo kwa umoja kati ya Waislamu na Wakristo wakati wa kusherehekea sikukuu zao (Maulid, Idd, Krismas na Pasaka), uliozungumzwa na Mwinyi katika hotuba zake alizozitoa wakati wa mkesha Jumatatu usiku na kwenye Baraza la Maulid, jijini Dar es Salaam juzi.

Alisema hakuwa na nia ya kumdhuru Mwinyi na wala hamchukii, bali alikuwa na lengo la kufanya kituko chochote ili ujumbe wake uwafikie watu wengi.

Alitoa maelezo hayo alipohojiwa na polisi saa chache baada ya kufanya kitendo hicho wakati Mwinyi alipokuwa akihutubia Baraza la Maulid, katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam juzi jioni.

Kutokana na kitendo hicho, Jeshi la Polisi, jana lilimpeleka kijana huyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa akili na damu ili kubaini kama ana matatizo ya akili au la, kabla ya kufikishwa mahakamani.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kijana huyo, ambaye anajulikana pia kwa jina la `Sultani`, alifanya tukio hilo juzi wakati Mwinyi akihutubia Baraza la Maulid katika ukumbi huo na alikuwa amekaa mstari wa tatu kutoka mbele.

Hata hivyo, alisema licha ya kumpeleka Muhimbili, wanatarajia kumfikisha mahakamani leo baada ya jalada la kesi yake kukamilika.

Alisema baada ya kufanya tukio hilo, kijana huyo alifikishwa kituo cha Polisi cha Salander Bridge na baadaye alihamishiwa kituo cha Polisi Kati kwa mahojiano.

``Nilimhoji kijana huyu ambapo katika maelezo yake alisema kuwa, yeye hakuwa na nia ya kumdhuru Mwinyi na hamchukii bali alikuwa na lengo la kufanya kituko chochote kile ili ujumbe wake uwafikie watu wengi. Alidai hakubaliani na hotuba za viongozi wa Kiislamu zinazosisitiza Waislamu na Wakristo kushirikiana kama vile kusherehekea kwa pamoja sikukuu za Maulid, Idd, Pasaka na Krismas,`` Kova alisema akimkariri kijana huyo.

Kova alisema kijana huyo aliendelea kumweleza kuwa, kwa maoni yake sikukuu za Kiislamu wanasherehekea wenyewe na Wakristo hivyo hivyo na sio kwa pamoja.

Kuhusu kondomu, Kova alimkariri kijana huyo akieleza kwamba, anapinga matumizi ya mpira huo kwa madai kwamba kuhimiza matumizi yake ni kuhalalisha uzinifu kwa Waislamu.

Hata hivyo, Kamanda Kova alisema katika mahojiano naye alimuuliza kwa nini aliamua kutumia njia hiyo kufikisha ujumbe wake, na yeye alieleza kuwa ujumbe wake usingefika kwa sababu ni mtu mdogo mwenye hadhi ya chini hivyo ungechelewa.

Akisimulia zaidi tukio hilo, Kamanda Kova alisema siku ya tukio kijana huyo alinyanyuka kwenye eneo alilokuwa amekaa muda mfupi baada ya waandishi wawili wa televisheni kurekebisha vipaza sauti vyao mbele ya Mwinyi, naye akijifanya anafanya hivyo (kurekebsiha kipaza sauti), lakini akaishia kumpiga kofi kiongozi huyo mstaafu.

``Mtu huyu baada ya kufika pale mbele alijifanya anarekebisha vipaza sauti kama walivyofanya waandishi, na alisogea karibu zaidi na Sheikh Mkuu na kujifanya anaongea naye ndipo aliponyanyua mkono wake wa kulia na kupiga kipaza sauti alichokuwa akikitumia Mwinyi na kiganja cha mkono sehemu ya nyuma ulimpata kwenye shavu la kulia,`` alisema.

Alisema kufuatia tukio hilo, uchunguzi unaendelea kufanyika ili kujua kama alitumwa na mtu au kikundi fulani au ni mwanaharakati.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Kova alisema wataangalia uwezekano wa waandishi wa habari pindi wanapohudhuria kazi za viongozi kuwa na kadi maalum za kuwatambulisha ili mtu yeyote asije akaonekana kama mwandishi.

Kamati ya Bunge ya Ulinzi, Bakwata walaani
Wakati kijana huyo akijieleza, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Jumuiya inayoratibu safari za Hijja na Umra ya Taibah pamoja na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), zimelaani vikali kitendo cha Mwinyi kushambuliwa na kijana huyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Wilson Masilingi alisema analaani vikali kitendo hicho kwa vile kimelitia taifa aibu.

``Nalaani vikali, kwani ni aibu. Ninawaomba wananchi watoe ushirikiano ili kitendo kama hicho kisijirudie katika siku za usoni,`` alisema Masilingi, ambaye pia ni Mbunge wa Muleba Kusini (CCM).

Hata hivyo, alisema hajui mazingira ya tukio hilo na kwamba, waliokuwapo katika eneo la tukio wana nafasi nzuri ya kueleza kama kuna uzembe wowote uliofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama, na kutoa mwanya kwa mtuhumiwa kumshambuliwa Mwinyi.

Kutokana na hali hiyo, alishauri marais wote wastaafu waongezewe ulinzi kwa kuwa jambo hilo ni haki yao na ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kuwasibu baadaye kutokana na kufanyiwa vitendo vya kihuni kama hicho.

``Marais wastaafu wanastahili kuongezewa ulinzi. Ni haki yao. Kwani anaweza kutokea mwendawazimu katika dunia ya sasa, akaleta fedheha,`` alisema Masilingi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taibah, Sheikh Ali Mubarak, alisema kitendo cha kushambuliwa kwa Mwinyi ni cha kulaaniwa na Watanzania wote wanaopenda amani na kuvumiliana katika masuala ya kila aina kwa vile kitendo hicho ni cha kinyama.

Sheikh Mubarak alisema mbali ya kuwa ni cha kinyama, kitendo hicho ni kinyume cha utamaduni wa Watanzania, hivyo kinapaswa kulaaniwa na kudhibitiwa ili kisitokee tena.

``Uongozi wote wa Taibah umepokea kwa masikitiko makubwa tukio la kushambuliwa kwa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi wakati akihutubia maelfu ya waumini wa Kiislamu jana (juzi) ukumbi wa Diamond Jubilee. Kitendo hicho kwa vyovyote vile ni cha kulaaniwa na jumla ya Watanzania wanaopenda amani na kuvumiliana katika masuala ya kila aina,`` alisema Sheikh Mubarak.

Kutokana na hali hiyo, aliishauri serikali kuchukua hatua dhidi ya kitendo hicho ili kupata undani wa tukio lenyewe.

Alisema Taibah inampa pole Mwinyi, serikali na uongozi wake kwa vile inaamini kuwa kiongozi huyo ni mzee mwenye busara na anayetegemewa.

Naye Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Suleiman Gorogosi, alisema jana kuwa Bakwata inalaani vikali kitendo cha kushambuliwa Mwinyi kwa vile kitendo hicho ni cha kihuni na ni kinyume cha mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Hata hivyo, Gorogosi ambaye pia ni Sheikh wa Bakwata Mkoa wa Lindi, alisema bado wana wasiwasi huenda mtuhumiwa aliyefanya kitendo hicho, ana matatizo ya akili, ingawa alisema kuwa uongozi wa Bakwata haumjui.

Kanisa lapigwa na butwaa
Nao viongozi wa dini nchini, wamesema kitendo cha Rais Mstaafu Mwinyi kupigwa kibao jukwaani, kimeidhalilisha Tanzania na kuwafedhehesha wananchi wote.

Aidha, wamesema kutokana na kitendo hicho hivi sasa ipo haja kupima na kutathimini kiwango cha amani na utulivu nchini.

Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Mhashamu Methodius Kilaini, alisema kitendo hicho hakikumvunjia heshima na kumdhalilisha Mwinyi pekee bali Watanzania wote.

Alisema kwa kifupi Kanisa nchini limepigwa na butwaa na kubaki na mshangao.

``Lakini pamoja na hayo yote tunampa pole nyingi Mzee Mwinyi. Tunamtaka asifadhaishwe na kitendo hicho,`` alisema.

Kilaini alisema jambo hilo linashangaza zaidi na kulifanya Kanisa liwe kama limemwagiwa maji, hasa ikizingatiwa kuwa kitendo hicho kimefanyika katika shughuli za kidini.

Hata hivyo, alisema pamoja na dosari hiyo, bado anaamini kwamba Watanzania hawajawa na tabia ya hujuma na kujitoa mhanga kama hiyo.

``Naomba suala hili lichukuliwe kama ajali tu, kwa vile siamini kwamba hali ya amani katika nchi yetu imefikia hapo,`` alisema.

Askofu huyo alisema hakuna jambo lolote baya ambalo alizungumza Rais Mwinyi ambalo lilifanya iwe sahihi apigwe.

``Lakini jambo hili sasa lisipotazamwa kwa makini, mambo ya dini yatakuwa sio ya kuaminika tena kama ilivyozoeleka,`` alisema.

Alisema kitendo hicho kinaweza kuwaweka viongozi mbali na wananchi kwa kuhofia usalama wao.

Askofu Kilaini aliwataka Watanzania hasa watu wa dini, kujenga utamaduni wa kuheshimiana na kuvumiliana hata kama mtu anazungumza au anatoa msimamo ambao hukubaliani nao.

Naye Askofu Dk. Stephen Munga wa KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki, alisema wakati Kanisa limebaki mdomo wazi, kuna haja ya vyombo vya dola kuchunguza kwa kina jambo hilo na kulikomesha.

Alisema haelewi hasa lengo la muumini huyo lilikuwa nini, lakini akasisitiza kwamba huenda kuna kikundi au watu wapo nyuma ya `mbabe` huyo.

``Kama yale mambo ya kujitoa mhanga yameshaanza kuota hapa petu, basi ni ishara kwamba Watanzania tunaelekea gizani, jambo hili haliashirii mema katika nchi yetu,`` alisema.

Askofu Munga alisema Kanisa limepigwa na butwaa na kujiuliza kuwa mtu huyo aliyefanya kitendo hicho, amezaliwa katika nchi gani?

``Jambo hili lina maswali mengi kuliko majibu, kweli kijana wa Kitanzania aliyezaliwa hapa, hajui wala hajaona ustaarabu wetu wa kuwaheshimu viongozi kama ni Mtanzania, basi anao uovu mkali kichwani pake, ambao amepandikizwa na kikundi fulani. Haya kama kweli ni punguani kama wengine wanavyosema, huo upunguani umeanza lini, tunaambiwa amekuwa akihudhuria ibada zote za Maulidi, kwanini upunguani wake ukamsubiri hadi Mwinyi aongee? Kwa nini huo upunguani haujaonekana kwingineko? Ndio maana tunasema jambo hili lina maswali mengi kuliko majibu,`` alisema.

Hata hivyo, Dk. Munga alionya kwamba suala hilo ni kubwa hivyo lisitolewe majibu rahisi kwamba mhusika ni punguani.

Alimtaka Mzee Mwinyi kutofadhaika na kukata tamaa kwa vile bado Watanzania wengi wanamheshimu, kutokana na mchango wake mkubwa wa kisiasa, kujamii, kiuchumi na kiutamaduni alioutoa wakati wa uongozi wake.

UVCCM walaani
Baraza Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), limetoa tamko la kulaani kitendo cha kupigwa kwa Rais Mstaafu Mwinyi, kilichotokea juzi wakati wa sherehe za Baraza la Maulidi.

Akitoa tamko hilo jana kwa waandishi wa habari kwa niaba ya Baraza hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya UVCCM, Masauni Yusuf Masauni, alikiita kitendo hicho kuwa ni cha kihuni, udhalilishaji, fedheha na utovu wa nidhamu.

Alisema kwa kauli moja Baraza hilo limesikitishwa na kitendo hicho, hasa ukizingatia kuwa kimefanywa na kijana wa Kitanzania ambaye amewaaibisha vijana wote wa Tanzania, kwa kuonyesha kuwa hawana nidhamu.

``Kwa ujumla Baraza limepokea kwa masikitiko makubwa kitendo hicho cha kihuni, udhalilishaji na cha fedheha alichofanyiwa kiongozi wetu mpendwa Mzee wetu Alhaji Ali Hassan Mwinyi,`` alisema Masauni.

Aliongeza kuwa kitendo hicho kilichofanywa na kijana huyo ni kinyume cha maadili ya dini zote na utamaduni wa Kitanzania kwa wazee wetu, viongozi na jamii kwa ujumla.

Kutokana na kitendo hicho, Baraza hilo limeitaka serikali ufanyike uchunguzi wa kina na wa haraka ili kubaini nia ya kitendo hicho cha kihuni na hatua kali za kisheria dhidi ya mhusika, zichukuliwe mara moja.

Pia alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama viimarishe ulinzi kwa viongozi wastaafu na waliopo madarakani, ili kusiwe na matukio ya namna hiyo tena.

Baraza Kuu la Jumuiya ya Umoja wa Vijana lilikutana mjini Dodoma kwa muda wa siku sita kujadili mambo mbali mbali yanayohusu mustakabali wa CCM.

Mbeya nao waja juu
Wananchi wakiwemo viongozi wa dini mkoa wa Mbeya wameelezea kusikishwa na tukio la kupigwa kibao Rais Mstaafu Mwinyi ambapo wamewatupia lawama walinzi wake kwamba walikuwa wazembe kwa kushindwa kumlinda kwa umakini kiongozi huyo.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti walisema tukio la kupigwa Rais Mwinyi limeiweka nchi katika kashifa mbaya mbele ya uso wa dunia na Tanzania kuonekana ni nchi isiyokuwa makini katika kuwalinda viongozi wake.

Mmoja wa wananchi hao, Abdallah Bugano, akizungumza na Nipashe alisema mazingira ya jinsi tukio lilivyotokea yanaonyesha kuwa walinzi wa Rais Mwinyi hawakuwa makini na ndiyo maana mtu aliyefanya kituko hicho aliweza kujipenyeza hatimaye kumnasa kibao kiongozi huyo.

``Tukio hili walinzi wa Rais Mwinyi ni wazembe sana, kwanini yule kijana alikwenda pale kama vile anataka kurekebisha vipaza sauti, ina maana hakukuwa na watu maalum wanaojulikana waliowekwa kuifanya kazi ya mitambo, huu ni uzembe,`` alisema Bugano.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste mkoa wa Mbeya, Askofu Amos Igundu, alisema Wakristo wamelipokea tukio hilo kwa maskikitiko makubwa na kwamba kuna haja kwa vyombo vya usalama kujipanga upya kwa namna ya kuimarisha ulinzi kwa viongozi wakuu, hususani kwenye mikutano ama sherehe zinazojumuisha watu wengi.

Askofu Igundu alisema tukio hilo limeitia doa nchi na hivyo ni jukumu la vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina sababu za kijana huyo kuamua kuchukua hatua ya kumpiga kibao Rais Mstaafu Mwinyi.

Naye Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Albert Mgumba akizungumza na Nipashe kwa simu akiwa wilayani Kyela, alisema kitendo kilichofanywa na kijana aliyempiga kibao Rais mstaafu Mwinyi ni utovu wa nidhamu na kwamba inabidi achukuliwe hatu kali.

Imeandaliwa na Muhibu Said, Romana Malya, Simon Mhina, Mary Edward na Thobias Mwanakatwe.

SOURCE: Nipashe

Wednesday, March 11, 2009

Aliyempiga Mzee Ruksa!


Pichani ni mtuhumiwa Ibrahim Said Sultan maarufu kama (Ustaadh) ambaye alimzaba Rais Mstaafu, Alii Hassan Mwinyi kibao akiwa jukwaani akihubiri kwenye sherehe za Maulidi.

Cheki wananchi walivyo na hasira! Mzee Ruksa anapendwa! Bahati katoka na uhai wake hapo!

Kwa habari na picha zaidi mtembelee Kaka Michuzi:

Mzee Ruksa Apigwa Kofi Jukwaani!


Hivi kama Rais Mstaafu, Mzee Mwinyi si ana kuwa na wanausalama wake? Halafu ajabu wanakataa kuwa jambo hiyo ilitokea...wakati waandishi wa haabri wengi walishuhudia!

********************************************************************
Kutoka Ippmedia.com

Rais Mwinyi apigwa kofi jukwaani

2009-03-11
Na Muhibu Said

Rais Mstaafu Rais Ali Hassan Mwinyi jana alipigwa kofi la shavuni na muumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Maulidi mara baada ya kuwataka Waislamu kujikinga na Ukimwi kwa kutumia kondomu kuliko kuwaambukiza watu gonjwa hilo hatari kwa jamii.

Rais Mwinyi ambaye pamoja na mambo mengine, alizungumzia masuala ya uchumi yanayoikumba nchi, alianza kuzungumzia vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, kwa kusema kuwa zinaa katika Uislamu ni jambo haramu moja kwa moja.

Mwinyi aliendelea kudai kuwa mtu akifanya zinaa, kwa kutumia mpira (kondomu), atakuwa amefanya dhambi moja, lakini akifanya bila kutumia mpira, mtu huyo ni dalali wa kutembeza zinaa na Ukimwi.

Baada ya hapo akauliza mashekhe, kwamba kufanya dhambi Mungu anaweza akasamehe, lakini yule ambaye atafanya dhambi bila kondomu, bora ni vipi?

Mwinyi akaendelea kusema: ``Dharura ya mtu asiyeweza kujizuia na kufanya zinaa, mashekh na maulamaa tufanyeje hapo?``

Baada ya kusema hivyo, akatoka muumini mmoja akapanda jukwaani na kumpiga Rais Mwinyi kofi upande wa shavu la kuume, akapepesuka almanusra aanguke na kuokolewa na maafisa usalama.

Hali hiyo ilisababisha Mwinyi asitishe hotuba yake baada ya maafisa wa usalama na polisi kuvamia jukwaa na kumkamata mtuhumiwa aliyefanya kitendo kisicho cha kiuungwana.

Katika harakati za kumkamata, askari hao walianza kumpiga na ukumbi ukapatwa na taharuki kubwa.

Baada ya kumdhibiti mtu huyo ambaye alitia dosari sherehe hizo zilizokuwa zimeandaliwa vizuri, wanausalama hao walimpakia kwenye gari na kuondoka naye.

Baadhi ya waumini walitaka kukimbia, wengine wakaenda kuwasaidia maafisa usalama kumkabili mtu huyo aliyempiga Rais Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa.

Miongoni mwa watu waliomkabili kijana huyo ni pamoja na viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na waumini wengine.

Taharuki hiyo ilisababisha waandishi ambao walikuwa wakifuatilia shughuli nzima ya Baraza la Maulidi, baadhi kutaka kukimbia na wengine kujua kulikoni.

Hali hiyo ilidumu kwa muda wa dakika mbili, huku viongozi wa Bakwata wakiwatuliza watu kutulia ili shughuli iendeleee.

Nipashe jana iliwasiliana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, juu ya tukio hilo lakini akasema kwamba amewasiliana na Kamanda wa Polisi Ilala, na tukio hilo halijatokea.

Nipashe ilipomuuliza kwamba mbona waandishi wa habari wameshuhudia tukio hilo, na pia Kaimu Mufti, Sheikh Suleiman Gorogosi, amewaomba waumini radhi kwa rabsha iliyotokea, Kamanda Kova alisema`` ``Wasiliana na Kamanda wa Ilala kwa habari zaidi.``

Akiomba radhi, Sheikh Gorogosi alisema mtu aliyefanya kitendo hicho cha aibu ni kichaa. Hadi tunakwenda mitamboni jina la mtu huyo lilikuwa halijajilikana.
Baada ya hapo, Mwinyi aliendelea kuhutubia.

Baada ya hapo, Nipashe iliwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, ambaye alisema kwamba alikuwa hana taarifa kamili kwa kuwa alikuwa katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

``Ndio naelekea huko sasa hivi baada ya kuambiwa na askari waliokuwa huko Diamond Jubilee kupata habari kamili,`` alisema Shilogile.

Rais Mwinyi ni rais mstaafu anayependwa na wananchi kwa kiwango kikubwa, na kila anapohudhuria hafla mbalimbali amekuwa akishangiliwa kwa nguvu kutokana na mchango wake katika kubadili hali ya mambo nchini.

Ilikuwa ni chini utawala wake, akiwa Rais wa awamu ya tatu mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa yalianza kutekelezwa nchini ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Jina la Mzee Ruksa alipachikwa baada ya kuwa mkali kutokana na vitendo vya baadhi ya watu kuvamia na kuvunja mabucha ya nyama ya nguruwe, akiwakanya na kusema kwamba kila mtu ana ruksa ya kula atakacho.

Kutokana na utaratibu wa utawala wa kuachia wananchi uhuru wa kufanya watakalo ilimradi hawavunji sheria, alijiziolea umaarufu mkubwa na kupachikwa jina la Mzee Ruksa.

SOURCE: Nipashe