Showing posts with label Athumani Hamisi. Show all posts
Showing posts with label Athumani Hamisi. Show all posts

Friday, June 08, 2012

TSN Haijamtelekeza Athumani Hamisi

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI: TSN HAIJAMTELEKEZA ATHUMANI HAMISI

Athumani Hamisi Akiongea na Waandishi wa Habari jijin Dar juzi
Tarehe 5 Juni,2012, mfanyakazi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), ambaye amelemaa baada ya kupata ajali ya gari, Bwana Athumani Hamisi, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Maelezo, Dar es Salaam, na kutoa taarifa iliyojenga taswira kuwa ametelekezwa na TSN pamoja na Serikali.

TSN inapenda kufafanua kuwa Serikali na kampuni hii, ambayo ilimwajiri Athumani tarehe 1/09/2006 kama Mpiga picha Mwandamizi, wamemhudumia mfanyakazi huyo kikamilifu tangu alipopata ajali tarehe 12 Septemba, 2008 hadi sasa, na huduma hiyo inaendelea.

Baada ya kutokea ajali hiyo, TSN kama mwajiri ilisimamia matibabu yake ya awali katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa (MOI) mpaka Serikali, kwa kupitia Wizara ya Afya ilipomhamishia Netcare Rehabilitation Hospital nchini Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Serikali ililipia gharama za matibabu yake yote akiwa Afrika Kusini kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi saba, ambayo yanazidi shilingi milioni mia moja. Gharama hizo ni pamoja na ununuzi wa kigari maalum ambacho Athumani anatumia sasa.

TSN kama mwajiri ililipa nauli ya ndege kwenda na kurudi pamoja na posho ya kujikimu ya mgonjwa pamoja na ndugu wasindikizaji ambao ni Bw. Hassan Hussein na Bi. Mirriam Malaquias.Posho ya kujikimu ilikuwa USD 6,210 sawa na Shilingi 9,315,000, na nauli kwa watu watatu ilikuwa ni Shilingi 3,535,869.92. Athumani aliendelea kupatiwa huduma akiwa huko Afrika Kusini kwa gharama za Serikali na TSN mpaka aliporejea nchini tarehe 08/05/2010. Gharama zilizolipwa na kampuni kwa mfanyakazi huyu hadi sasa ni takriban shilingi million 52.

Athumani aliporejea nchini alilakiwa na wafanyakazi na viongozi wa TSN na kupangiwa chumba hoteli ya Holiday Inn wakati utaratibu wa kumtafutia nyumba ya kupanga ukikamilishwa. Kampuni ilitumia kiasi cha Shilingi 1,756,979.50 kulipia hoteli. Baadaye alipelekwa kwenye nyumba ambayo alipangiwa na Kampuni katika eneo la Sinza Vatican ambapo ndipo bado anaishi hadi hivi sasa. Gharama ya nyumba kwa mwaka wa kwanza 2010 ilikuwa ni Shilingi 4,200,000 au Shilingi 350,000 kwa mwezi. Mwaka 201 mwenye nyumba alipandisha kodi hadi 400,000 kwa mwezi ambapo Kampuni ililipia Shilingi 4,800,000. Kodi hiyo imeishia Mei mwaka huu na kampuni imeshafanya mazungumzo na mwenye nyumba ili Athumani aendelee kuishi hapo kwa muda wakati mipango endelevu ya ustawi wake inafanywa kwa kuzingatia taratibu za ajira.

Mnamo tarehe 8/12/2010 Athumani alirudi tena Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi wa maendeleo ya afya yake na matibabu yaligharimiwa na Serikali wakati TSN iligharamia nauli yake na ya muuguzi wake, pamoja na posho ya kujikimu Shilingi 6,300,000/-.

Pamoja na bwana Athumumai kulala kitandani kwa muda wote huo ameendelea kulipwa mshahara kamili bila kukatwa kama mfanyakazi wa kawaida ikiwa ni msaada wa kampuni kwa kuzingatia ulemavu alioupata.Mshahara aliolipwa kwa muda wote aliokuwa anaugua ni kiasi cha shilingi 26,773,000. Vile vile kampuni ilimlipa muuguzi toka Afrika Kusini ambaye alikuwa anamhudumiaa Athumani Rand 12,500 kama mshahara wake.

Kuanzia Januari 2011, mshahara wa Athumani umejumuisha asilimia 15 kama posho ya nyumba ambayo wafanyakazi wote wanalipwa. Aidha Athumani yupo kwenye mpango wa bima ya afya anayolipiwa na kampuni, ambayo inamwezesha yeye na familia yake kuweza kutibiwa katika hospitali yoyote hapa Tanzania. Kampuni inamlipia Shilingi 68,449.20 kila mwezi na bima hiyo ndiyo inayogharamia matibabu yake yote hapa nchini.

Bwana Athumani anapatiwa usafiri na TSN mara mbili kwa wiki kumtoa nyumbani hadi Muhimbili na kurudi kwa ajili ya mazoezi ya viungo.

Imetolewa na

OFISI YA MHARIRI MTENDAJI
08.6.2012

***********************************************************

Kusoma Story Aliyotoa Athumani Hamisi BONGO CELEBRITY , BOFYA HAPA

Monday, September 29, 2008

Athumani Hamisi yuko South Africa kwa Matibabu



Kutoka Lukwangule Blog:

TAARIFA ambazo nimezipata leo mchana ni kuwa Athumani Hamisi ,pichani,ameshaanza kupata matibabu katika hospitali aliyofikishwa, nchini Afrika Kusini.

Matibabu hayo ni pamoja na vipimo vya muhimu kabla ya kumfanyika upasuaji.

Kwa mujibu wa mtu aliyekuwa ananipa habari hizi Athumani ameongezwa damu kwa siku ya leo kwa kuwa aliyokuwa nayo ilionyesha kuwa tatizo kwa madaktari wake.Vinginevyo wamesema hali ni shwari.Nitawapatia maelezo hali ya mpiganaji huyu kwa jinsi inavyowezekana lakini si mara zote.

************************

Wadau tuendelee kumwombea kaka Athumani apate nafuu na aweza kurudi kazini na kuendelea na maisha yake kama hapo awali.

Tuesday, September 16, 2008

Muhimbili Vipi Tena???

Wadau, bila shaka mmefuatilia kwenye blogu mbalimbali habari za ajali ya gari iliyotokea hivi karibuni ambayo wapiga picha na waandishi wa habari waliiumia. Ukagundulika kuwa mashine ya CT Scan hazifanyi kazi katika hospitali za Muhimbili na Aga Khan.

Nauliza hivi, serikali ina hela ya kununua magari ya fahari, ndege na radar, lakini haina pesa za kununua mashine muhimu kama CT Scan? Na nakubaliana na Dr. Faustine, ni aibu kuwa miaka 47 baada ya Uhuru tuko katika hali hii!

****************************************************************

Kutoka Lukwangule Entertainment Blog:

Kuna tatizo gani Muhimbili?

Haya maneno hapa chini nimeyachukua katika blogu ya drfaustine (http://drfaustine.blogspot.com/). Natambua daktari anajua nini anachoandika na yuko serious katika ishu nyingi hasa zinazogusa maisha ya watu na haya ndiyo aliyoandika katika blogu yake. Something shoud be done, lakini sijui nani anatakiwa kufanya hili.Wakati mwingine unabaki ukishangaa. Hebu isomeni . Lukwangule

*******************************************************

Katika pita pita yangu katika Blogu ya Bw Beda Msimbe nimekutana na stori ya kusikitisha na kufedhehesha inayohusu kukosekana kwa huduma ya muhimu ya CT scan.Kwa taarifa zilizopo ni kuwa mashine ya Muhimbili na ile ya Aga Khan zote hazifanyi kazi.Kwa muda mrefu CT Scan ya Muhimbili imekuwa Spana mkononi.

Huduma hii inazalisha fedha nyingi sana. Kipimo si chini ya Tsh 100,000. Fedha hizi zinazotokana na mashine hii zinakwenda wapi?

Kwa taarifa nilizonazo ni kuwa hakuna fungu maalum lililopo kwa ajili ya matengenezo ya mashine hii. Pia mashine hii haina service warranty. Hivyo mashine ikiharibika inaweza kuchukua kipindi kirefu kabla ya kutengenezwa.

Haijulikani ni idadi gani ya wanaopoteza maisha kutokana na kukosekana kwa huduma nyeti kama hii na ile ya kusafisha figo (renal dialysis).

Siku za nyuma nimepiga kelele sana kuhusu suala la renal dialysis. Wataalam tunao, wafadhili wako tayari kutoa vifaa hivi muhimu, Muhimbili wanajivuta kutoa chumba cha kufunga vifaa hivi!

Swali la kujiuliza ni wagonjwa wangapi wenye ndugu wenye uwezo wa kupeleka wagonjwa wao Nairobi na Johannesburg? Hivi hatuoni fedheha miaka 47 ya uhuru bado tunakosa huduma muhimu kama hizi katika hospitali zetu za rufaa?

CT scan sio kipimo cha anasa, ni kipimo cha msingi katika hospitali za rufaa. Mgonjwa kama Bw Athuman Hamisi anakosa kupata matibabu ya msingi kutokana na madaktari kutojua majeraha katika uti wa mgongo yako wapi, kipimo hiki kingesaidia kujua tatizo liko wapi na kuweza kupata tiba stahili.

Watanzania tunaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu.
NB: Nampa pole mdau Athumani Hamisi. Mungu amjalie apone haraka.