Showing posts with label Nguvu za Kiume. Show all posts
Showing posts with label Nguvu za Kiume. Show all posts

Sunday, May 11, 2014

Afya ya Vijana Leo ni Mbaya Ukilinganisha na Yetu Zamani



Na Freddy Macha



Kwa ufupi:
Desturi ya kula inayozagaa nchini kote hususan majiani ni ile iitwayo ‘fast food’ huku Majuu. Ilianzia Marekani.

Tumalizie mada yetu leo iliyoanza wiki tatu zilizopita.
Kitakwimu idadi ya vijana Tanzania ni kubwa zaidi ya wazee, nchi zilizoendelea walipitisha miaka 70 ni wengi sababu ya ubora wa maisha. Lakini hapo hapo Uzunguni yapo ‘mabaya’ yanayostahili kuangaliwa.
Azma ya kutamani ‘maendeleo ya haraka haraka’ bila simile imeanza kuchangia aina ya maradhi ya kisasa. Zamani kisukari, ugonjwa wa moyo au kupoteza nguvu za mapenzi yalikuwa magonjwa ya wazee, walakin leo yanawakaba na kuwasepetua vijana.
Katika makala mbili zilizopita tumejadili namna taratibu nzima ya maisha, siasa- uchumi, elimu na utambuzi yanavyochangia adha hii. Mathalani kama hulali saa nane kwa siku, unaharibu akili, sura, tabia na afya yako.
Kipindi cha miaka 30 iliyopita. kumekuwa na tatizo la Wazungu, hata weusi waliozaliwa huku Majuu, kupungukiwa mbegu za uzazi. Ndoa nyingi zinavunjika. Tatizo hili linaloitwa “low sperm count” au kwa wanawake ‘infertility problems’, limefanyiwa utafiti sana. Mathalan nchini Marekani, imethibitishwa kuwa kutozaa husababishwa na udhaifu wa mayai ukihusisha wote, wanawake na wanaume. Asilimia 30 wanaume na asilimia 30 wanawake wana tatizo hilo.
Sababu zilizotolewa ni pamoja na kurithi hali hiyo, kutokula vyakula asilia, maradhi ya zinaa, uchovu kutokana na kazi na maisha ya kasi sana (“stress”). Tatizo hili lilifikia kilele miaka ya 1980 ambapo wenyeji walipendelea zaidi ndoa na sisi tunaotoka nchi za joto au zinazoendelea.
Kwa nini?
Aina ya maisha (Afrika, Asia na Marekani ya Kusini) ni tofauti na ya Uzunguni. Joto, kutokimbiakimbia ovyo (“stress”), vyakula na hewa safi asilia isiyoathiriwa na moshi, pia mashine za kisasa ni baadhi ya mambo yaliyochangia mbegu, haiba na tabia zetu kimapenzi kuwa bora.
Hivi sasa Wazungu wamegundua kula vyakula asilia (“organic food”) na kufanya mazoezi hustawisha siha ya mapenzi na ngono. Miaka 15 iliyopita vuguvugu la maisha ya siha, limetanda kiasi ambacho maduka yamejazana vyakula asilia vinavyonunuliwa nchi maskini. Mathalan hivi karibuni nilikuwa nakwenda duka moja hapa London kununua nyama ya nyati wa Zimbabwe.
Kwa nini Wazungu wanalipia zaidi vyakula asilia ?
Hapo! Wamegundua njia waliyokuwa wakiipitia baada ya maendeleo ya mashine yaliyoanza karne ya 18 na kufikia kilele karne ya 20 inawaharibia afya na maisha. Sisi tumejaza vitu hivyo, lakini hatuvithamini.
Mwaka 1976 wakati nilipoanza kazi Gazeti la Uhuru, tulikuwa tukila katika vibanda na magenge ya Mama Ntilie. Enzi hizo ubwabwa kwa maharage na ndizi mbivu vilikuwa sehemu mahsusi ya mlo wa mchana. Mwisho wa juma tulipotoka dansini au disko, kando ya barabara yalikaangwa mayai (macho ya ng’ombe) kwa nyanya na vitunguu.


Nilikuwa na rafiki yangu mwanahabari (marehemu) mpigapicha, Awadh Shebe, akiishi Kariakoo. Kila mchana siku za Jumamosi tuliingia Mnazi Mmoja kupata “fruti” yaani bilauri za mseto wa matunda. Leo kinachotiliwa mkazo ni vinywaji vya “kisasa” kama Cocacola, Mirinda kwa “chips” kavu baada ya kazi. Mafuta ya hizo “chips” huwa yameshapikia hata wiki nzima bila kubadilishwa. Sawa kweli?
Desturi ya kula inayozagaa nchini kote hususan majiani ni ile iitwayo ‘fast food’ huku Majuu. Ilianzia Marekani.
Huko ndiko walikojenga maduka na migahawa maarufu ya MacDonalds. Wamarekani haohao wanasemwa hawajui kupika, hawali vyakula asilia. Wanakumbwa na maradhi ya unene na moyo. Haya ndiyo mambo yanayoingia kwetu Afrika. Tena kwa haraka sana.
Je, wangapi leo tunapika nyumbani?
Ni vijana wangapi wanajua kupika msosi ukalika?
Tunakimbilia nyama na ndizi choma tu. Kula nyama choma siyo vibaya hata kidogo. Ubaya imegeuzwa chakula kikuu. Waafrika tunapenda nyama. Twazila kila siku. Nyama nzuri ndiyo. Lakini yanatuponza. Afrika Magharibi na ya Kati wamefikia kula nyama mwitu : panya, nyani na popo! Matokeo ndiyo hiyo Ebola inayoangamiza watu Guinea sasa hivi.
La pili ni ulevi.
Wiki ya jana vyombo vya habari Uzunguni vilitangaza matokeo ya utafiti wa Shirika la ‘Slimming World’ linaloangalia matatizo ya unene kwa walevi 2,000, hapa Uingereza. Kawaida mwanaume anatakiwa asizidishe bia tatu kwa siku, yaani kipimo cha vitengo (“units”), kumi. Ikizidi, mwili hubadilika na kuharibika. Wanawake wanashauriwa vitengo vinane, yaani glasi 2 za mvinyo kama bia mbili. Ulevi unapokiuka vitengo hivyo, mtu hutaka kula zaidi.
Utafiti ulisema, tabia ya kilevi ni kutaka kula ‘chochote kile’ kiwe kibaya au kizuri, kujaza tumbo baada ya kulewa.
Matokeo ni nini? Kutapika, vitambi, ushuzi, unene, harufu mbaya ya mdomo na mwili na mambo kama hayo.
Utafiti wa pili ulichunguza wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60. Ukadadavua kuwa kadri umri unavyokwenda, ndivyo ubongo husinyaa na kupungua uwezo, hii husababisha kusahau, kutofanya mambo sawasawa-yaani ‘dementia’ kwa lugha ya kitaalamu. Utafiti ukashauri kuwa, mazoezi ya viungo kama kutembea (dakika 20 hadi 45 kwa siku), kuogelea, kukimbia na kadhalika kwa watu wa makamo kuimarisha bongo zetu.
Je, yanaathiri vipi vijana?
Vijana leo, (Uzunguni na nyumbani) wanaonyesha dalili za kuwa na matatizo yanayostahili kuwapata wazee. Kwa kuwa bangi ni rahisi kupandisha nishai kuliko pombe (aghali) vijana huanza kuivuta wakiwa wadogo sana. Bangi na dawa za kulevya, humfanya mtumiaji kutojali wakati, kujisikia mzito, mvivu na mwenye usingizi, moyo kukimbia na kadhalika. Bangi inasababisha pia maradhi ya akili (‘schizophrenia’). Ukishazoea sana bangi unakuwa sugu; unataka “kali zaidi.” Unatafuta (‘cocaine’), sindano za ‘heroin’, na kadhalika. Ushetani huu huathiri mzunguko wa damu, jambo linalochangia kupungua nguvu za kufanya mapenzi.
Mwisho, tuangalie ulimbukeni.
Neno hili limetokana na “limbua” au “kulimbuka” yaani mara ya kwanza, kama ua linalochanua. Ulimbukeni ulioenea Tanzania na Afrika unatokana na azma ya kujaribu kupambana na hali duni ya maisha. Kijana anayekua sasa hivi anahitaji uongozi thabiti. Je, ikiwa uongozi bora haupo tutafanyaje? Itabidi tuyakubali maneno ya mwanamuziki wa Kispanyola Manu Chao aliyefanya mahojiano hapa London mwaka 2007 akadai: “Hatuhitaji viongozi. Kila mmoja wetu ahitaji kuwa kiongozi.” Siyo kuvuta bangi na ushetani. Siyo kuwa wavivu. Bali kujituma. Kujielewa sisi nani. Kuipenda nchi yetu; kuipigania. Kujisomea na kujipenda zaidi.

Thursday, November 08, 2007

Marudio - Kukosa Nguvu za Kiume si Mwisho wa Dunia!

Kutoka 1/21/06.


Jamani, jamani, jamani, kuna jirani yangu kafa hivi majuzi. Alikuwa ni baba wa makamu, mmarekani mweusi. Alikuwa mcheshi na ilikuwa kila tukionana lazima tusalimiane. Mara ananinunulia kahawa halafu tunakaa namsimulia kuhusu Afrika. Yule baba, alionekana mzima na mwenye afya fiti kabisa. Nilibakia kushangaa kusikia kafa na si kwa ajali. Mke wake alifariki mwaka juzi, lakini miezi ya karibuni alikuwa anaonekana mwenye furaha kwa vile alipata mpenzi, dada mwenye miaka 25 hivi.

Story niliyoskia ni hivi: Kumbe jamaa alikuwa na matatizo ya moyo. Alifia kitandani akiwa kwenye shughuli ya kufanya tendo la ndoa na mpenzi wake. Tena wanasema alifariki mara alipofikia kilele cha tendo. Navyosikia ilikuwa ni ‘massive heart attack’. Kama ni massive bila shaka na utamu wa shughuli hakujua kuwa yuko hatarini.

Nasikia huyo mpenzi wake alipiga sana makelele majirani walipigia simu polisi 911 kwa vile walidhania wameingiliwa na majambazi. Wanasema baba wa watu kamwangukia yule dada na kafa macho wazi.Lakini bado nilikuwa nashangaa maana kama nilivyosema awali, jamaa alionekana kuwa na afya. Kumbe jamaa alikuwa mtumizi wa Viagra, yaani vile vidonge vya kuongeza uume, na kumpa mwanaume uweza wa kufanya tendo la ndoa.

Ndugu zake wanalamika kweli, maana hakuzipata kwa prescription ya daktari, alizaiagiza kwenye mtandao (internet). Kwa kumwangalia alivyofiti nisingefikiria kuwa ana matatizo ya nguvu za kiume. Kumbe mtazame mtu, matatizo yake anayajua mwenyewe na daktari wake.Nikawa najiuliza kama jamaa alijua ana matatizo ya moyo, kwa nini alitumia Viagra. Maana hata tangaza kwenye TV na magazeti wanaonyo kuwa kabla ya kutumia. Halafu pia wanaonya kuwa mwanaume anaweza kupofuka kama anatumia. Lakini wanaume bado wanazitumia!

Na siku hizi dawa za kuongeza nguvu za kiume ziko nyingi kuna Ciallis, Levitra, Yohimbine na mengine. Hizo dawa zina side effects kama kuumwa kichwa, kuharisha, pua kuziba, macho mekundu, tumbo kuumwa na mengine mengi. Pamoja na side effects bado zina soko kubwa. Na zikipigwa marufuku nina amini kuwa watu watatajirika kwa kuzifanyia magendo.

Kwa kweli wanaume wako tayari kufa kama wakishindwa kufanya tendo la ndoa. Nashindwa kuelewa sababu. Yaani tendo la ndoa ni tamu kiasi hicho au wanahofia kuwa kwa vile hawa ‘function’ tena ndo basi si wanaume? Mtu anakuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa ajili ya kufanya tendo la ndoa.

Mwanaume anaambiwa anaweza kupofuka akitumia hiyo dawa lakini bado yuko tayari kuchukua risk. Halafu mwanaume akiitwa ‘hanithi’ yuko tayari kupigana au kuua. Sijui bila kusimamisha anajiona si mtu tena…sielewi kabisa! Nikawa najadiili na marafiki zangu juzi na tulikubaliana kuwa wanaume wako tayari kuchukua ‘risks’ kuliko wanawake.

Yaani mwanaume anaweza kufanya tendo la ndoa hata akijua kuwa kuna hatari ya mwenzake kuwa na ugonjwa wa zinaa na ataambukizwa. Bongo, walikuwa wanasema eti, ‘Ajali Kazini’! Hiyo ajali inaweza kukuua! Sijui hiyo ume ikisimama ndo basi tena, akili zote zinahamia hapo. Nauliza tena, tendo la ndoa ni tamu kiasi kwamba mko tayari kuhatarisha maisha yenu? Kukosa nguvu za kiume zi mwisho wa dunia jamani. Bado tunawahitaji!Lakini nikirudi kwa marehemu jirani yangu, uwongo mbaya, alikuwa anatabasamu ndani ya jeneza lake!

Noti - Nyie wanaume mnaotaka kutumia hizo dawa kawaone daktari wenu kabla ya kuanza kuzitumia.