Sunday, May 11, 2014

Afya ya Vijana Leo ni Mbaya Ukilinganisha na Yetu ZamaniNa Freddy MachaKwa ufupi:
Desturi ya kula inayozagaa nchini kote hususan majiani ni ile iitwayo ‘fast food’ huku Majuu. Ilianzia Marekani.

Tumalizie mada yetu leo iliyoanza wiki tatu zilizopita.
Kitakwimu idadi ya vijana Tanzania ni kubwa zaidi ya wazee, nchi zilizoendelea walipitisha miaka 70 ni wengi sababu ya ubora wa maisha. Lakini hapo hapo Uzunguni yapo ‘mabaya’ yanayostahili kuangaliwa.
Azma ya kutamani ‘maendeleo ya haraka haraka’ bila simile imeanza kuchangia aina ya maradhi ya kisasa. Zamani kisukari, ugonjwa wa moyo au kupoteza nguvu za mapenzi yalikuwa magonjwa ya wazee, walakin leo yanawakaba na kuwasepetua vijana.
Katika makala mbili zilizopita tumejadili namna taratibu nzima ya maisha, siasa- uchumi, elimu na utambuzi yanavyochangia adha hii. Mathalani kama hulali saa nane kwa siku, unaharibu akili, sura, tabia na afya yako.
Kipindi cha miaka 30 iliyopita. kumekuwa na tatizo la Wazungu, hata weusi waliozaliwa huku Majuu, kupungukiwa mbegu za uzazi. Ndoa nyingi zinavunjika. Tatizo hili linaloitwa “low sperm count” au kwa wanawake ‘infertility problems’, limefanyiwa utafiti sana. Mathalan nchini Marekani, imethibitishwa kuwa kutozaa husababishwa na udhaifu wa mayai ukihusisha wote, wanawake na wanaume. Asilimia 30 wanaume na asilimia 30 wanawake wana tatizo hilo.
Sababu zilizotolewa ni pamoja na kurithi hali hiyo, kutokula vyakula asilia, maradhi ya zinaa, uchovu kutokana na kazi na maisha ya kasi sana (“stress”). Tatizo hili lilifikia kilele miaka ya 1980 ambapo wenyeji walipendelea zaidi ndoa na sisi tunaotoka nchi za joto au zinazoendelea.
Kwa nini?
Aina ya maisha (Afrika, Asia na Marekani ya Kusini) ni tofauti na ya Uzunguni. Joto, kutokimbiakimbia ovyo (“stress”), vyakula na hewa safi asilia isiyoathiriwa na moshi, pia mashine za kisasa ni baadhi ya mambo yaliyochangia mbegu, haiba na tabia zetu kimapenzi kuwa bora.
Hivi sasa Wazungu wamegundua kula vyakula asilia (“organic food”) na kufanya mazoezi hustawisha siha ya mapenzi na ngono. Miaka 15 iliyopita vuguvugu la maisha ya siha, limetanda kiasi ambacho maduka yamejazana vyakula asilia vinavyonunuliwa nchi maskini. Mathalan hivi karibuni nilikuwa nakwenda duka moja hapa London kununua nyama ya nyati wa Zimbabwe.
Kwa nini Wazungu wanalipia zaidi vyakula asilia ?
Hapo! Wamegundua njia waliyokuwa wakiipitia baada ya maendeleo ya mashine yaliyoanza karne ya 18 na kufikia kilele karne ya 20 inawaharibia afya na maisha. Sisi tumejaza vitu hivyo, lakini hatuvithamini.
Mwaka 1976 wakati nilipoanza kazi Gazeti la Uhuru, tulikuwa tukila katika vibanda na magenge ya Mama Ntilie. Enzi hizo ubwabwa kwa maharage na ndizi mbivu vilikuwa sehemu mahsusi ya mlo wa mchana. Mwisho wa juma tulipotoka dansini au disko, kando ya barabara yalikaangwa mayai (macho ya ng’ombe) kwa nyanya na vitunguu.


Nilikuwa na rafiki yangu mwanahabari (marehemu) mpigapicha, Awadh Shebe, akiishi Kariakoo. Kila mchana siku za Jumamosi tuliingia Mnazi Mmoja kupata “fruti” yaani bilauri za mseto wa matunda. Leo kinachotiliwa mkazo ni vinywaji vya “kisasa” kama Cocacola, Mirinda kwa “chips” kavu baada ya kazi. Mafuta ya hizo “chips” huwa yameshapikia hata wiki nzima bila kubadilishwa. Sawa kweli?
Desturi ya kula inayozagaa nchini kote hususan majiani ni ile iitwayo ‘fast food’ huku Majuu. Ilianzia Marekani.
Huko ndiko walikojenga maduka na migahawa maarufu ya MacDonalds. Wamarekani haohao wanasemwa hawajui kupika, hawali vyakula asilia. Wanakumbwa na maradhi ya unene na moyo. Haya ndiyo mambo yanayoingia kwetu Afrika. Tena kwa haraka sana.
Je, wangapi leo tunapika nyumbani?
Ni vijana wangapi wanajua kupika msosi ukalika?
Tunakimbilia nyama na ndizi choma tu. Kula nyama choma siyo vibaya hata kidogo. Ubaya imegeuzwa chakula kikuu. Waafrika tunapenda nyama. Twazila kila siku. Nyama nzuri ndiyo. Lakini yanatuponza. Afrika Magharibi na ya Kati wamefikia kula nyama mwitu : panya, nyani na popo! Matokeo ndiyo hiyo Ebola inayoangamiza watu Guinea sasa hivi.
La pili ni ulevi.
Wiki ya jana vyombo vya habari Uzunguni vilitangaza matokeo ya utafiti wa Shirika la ‘Slimming World’ linaloangalia matatizo ya unene kwa walevi 2,000, hapa Uingereza. Kawaida mwanaume anatakiwa asizidishe bia tatu kwa siku, yaani kipimo cha vitengo (“units”), kumi. Ikizidi, mwili hubadilika na kuharibika. Wanawake wanashauriwa vitengo vinane, yaani glasi 2 za mvinyo kama bia mbili. Ulevi unapokiuka vitengo hivyo, mtu hutaka kula zaidi.
Utafiti ulisema, tabia ya kilevi ni kutaka kula ‘chochote kile’ kiwe kibaya au kizuri, kujaza tumbo baada ya kulewa.
Matokeo ni nini? Kutapika, vitambi, ushuzi, unene, harufu mbaya ya mdomo na mwili na mambo kama hayo.
Utafiti wa pili ulichunguza wazee wenye umri wa zaidi ya miaka 60. Ukadadavua kuwa kadri umri unavyokwenda, ndivyo ubongo husinyaa na kupungua uwezo, hii husababisha kusahau, kutofanya mambo sawasawa-yaani ‘dementia’ kwa lugha ya kitaalamu. Utafiti ukashauri kuwa, mazoezi ya viungo kama kutembea (dakika 20 hadi 45 kwa siku), kuogelea, kukimbia na kadhalika kwa watu wa makamo kuimarisha bongo zetu.
Je, yanaathiri vipi vijana?
Vijana leo, (Uzunguni na nyumbani) wanaonyesha dalili za kuwa na matatizo yanayostahili kuwapata wazee. Kwa kuwa bangi ni rahisi kupandisha nishai kuliko pombe (aghali) vijana huanza kuivuta wakiwa wadogo sana. Bangi na dawa za kulevya, humfanya mtumiaji kutojali wakati, kujisikia mzito, mvivu na mwenye usingizi, moyo kukimbia na kadhalika. Bangi inasababisha pia maradhi ya akili (‘schizophrenia’). Ukishazoea sana bangi unakuwa sugu; unataka “kali zaidi.” Unatafuta (‘cocaine’), sindano za ‘heroin’, na kadhalika. Ushetani huu huathiri mzunguko wa damu, jambo linalochangia kupungua nguvu za kufanya mapenzi.
Mwisho, tuangalie ulimbukeni.
Neno hili limetokana na “limbua” au “kulimbuka” yaani mara ya kwanza, kama ua linalochanua. Ulimbukeni ulioenea Tanzania na Afrika unatokana na azma ya kujaribu kupambana na hali duni ya maisha. Kijana anayekua sasa hivi anahitaji uongozi thabiti. Je, ikiwa uongozi bora haupo tutafanyaje? Itabidi tuyakubali maneno ya mwanamuziki wa Kispanyola Manu Chao aliyefanya mahojiano hapa London mwaka 2007 akadai: “Hatuhitaji viongozi. Kila mmoja wetu ahitaji kuwa kiongozi.” Siyo kuvuta bangi na ushetani. Siyo kuwa wavivu. Bali kujituma. Kujielewa sisi nani. Kuipenda nchi yetu; kuipigania. Kujisomea na kujipenda zaidi.

2 comments:

Anonymous said...

Endeleeni kula hambuga na chipsi! Ohooo!

Anonymous said...

Aibu kweli unaende kitandani na puuuu, jamaa kalegea hataki kuamka!