Sunday, December 06, 2015

Balozi Wilson Masilingi Aanza Ziara ya Kutembelea Vyama Vya Siasa DMV

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Wilson Masilingi leo Jumamosi Desemba 5, 2015 alihudhuria mkutano wa Halmashauri ya CCM tawi la DMV ikiwa ni moja ya ziara zake anazotarajiwa kuzifanya kutembelea matawi ya vyama vya siasa nchiMarekani yenye lengo la kudumisha mshikamano na ushirikiano wa Watanzania bila kujali itikadi za vyama vyao.

Akiongea kwenye mkutano wa Halmashauri ya CCM DMV Mhe. Wilson Masilingi amesema lengo kuu ni kuwa karibu na vyama vya siasa kwa lengo la kuleta umoja na mshikamano ndani ya Jumuiya za Watanzania nchini Marekani na pia kuvitambua kama sehemu na sura ya Diaspora na kutoa wito kwa Watanzania waishio Marekani kuelekeza nguvu katika kuwekeza nyumbani bila kujali ufuasi wa chama unachoamini au kushabikia, wote ni Watanzania.

Mhe. Balozi Wilson Masilingi aliiomba Halmashauri hiyo ya CCM DMV kusaidia katika maendeleo ya Tanzania kwa kupanua wigo wao pamoja na kwamba lengo lao ni siasa na siasa ni sehemu ya maisha ya jamii na maendeleo ya jamii yanategemea siasa, kwa hiyo basi mnaposikia kuna muwekezaji yupo tayari kuwekeza Tanzania msisite Ubalozi upo wazi na utafanya kila liwezekanalo kuhakikisha muwekezaji huyo hapati vikwazo vyovyote.

Mwisho Balozi Wilson Masilingi aliwashukuru Watanzania kwa kuwa mabalozi wazuri nchini Marekani na kuwaasa kuishi kwa kufuata misingi na sheria za nchi ya Marekani.

 Mhe. Balozi Wilson Masilingi akiongea jambo na mwenyekiti wa tawi CCM DMV Bwn. George Sebo kwenye mkutano wa Halmashauri ya CCM DMV siku ya Jumamosi Desemba 5, 2015 mkutano uliofanyika Hampton Inn, College Park, Maryland. Picha na Kwanza Production/Vijimambo Blog
Mkutano ulianza kwa sala na kuwakumbuka wote waliotangulia mbele ya haki.

Mwenyekiti tawi la CCM DMV Bwn. George Sebo akifungua kikao cha Halmashauri ya CCM DMV kilichofanyika siku ya Jumamosi Desemba 5, 2015 katika ukumbi wa Hampton Inn, College Park, Maryland.

No comments: