 |
| Wahudumu Maalum wa Mortuary Uganda wakienda kumzika mtu aliyekufa kwa ugonjwa wa Ebola |
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUWEPO KWA MGONJWA WA EBOLA, WILAYA YA KARAGWE MKOA WA KAGERA, TANZANIA
UtanguliziWizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu
tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye vyombo mbali mbali
vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani Karagwe mkoa wa
Kagera.
Mnamo tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na Ustawi Wa
Jamii ilipokea taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya
kuwepo kwa mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa
Ebola, katika hospitali ya Wilaya ya Nyakahanga.
Aidha,taarifa
hiyo ilibainisha kuwa mgonjwa huyo alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye umri
wa miaka (6|) kutoka katika kijiji cha Nyakatundu wilayani Karagwe.
Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali, kulegea, kutokwa damu
puani, kutapika damu, na kukojoa damu.
Maelezo kutoka kwa mama
mzazi zilieleza kuwa mtoto huyu alianza kuugua kuanzia tarehe 30 Agosti
2012, ambapo alipatiwa dawa ya Septrin baada ya hospitali binafsi
kuonyesha kuwa ana ugonjwa wa“Typhoid”.
Uchunguzi wa awali
katika hospitali ya Nyakahanga ulionyesha kuwa mtoto huyu alikuwa
anasumbuliwa na uambukizo kwenye haja ndogo (Urinary Tract
Infection).Vile vile alifanyiwa uchunguzi wa kimaabara na Vipimo vya
malaria, Hepatitis na Typhoid havikuonyesha kuwepo kwa magonjwa haya.
Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka mgonjwa
na mama yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa ajili
ya uangalizi zaidi.
Aidha mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za
wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na
timu ya mkoa wa Kagera imeweza kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina
pamoja na kuchukua sampuli za damu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika
maabara ya Taifa ya uchunguzi wa magonjwa na Maabara za nje ya nchi, ili
kubaini kama ameathirika na ugonjwa wa Ebola.
Timu hiyo ya
wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya mgonjwa huyu kwa sasa imeimarika
ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na kukojoa damu kumekoma pia,
uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha kuwa hana dalili
zozote za ugonjwa wa Ebola.Vile vile hakuna taarifa ya mtu mwingine
yeyote kwenye familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au cha
jirani kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;
- Imepeleka
timu ya wataalamu mbali mbali kutoka Wizarani na mkoa kwa lengo la
kwenda kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa huo.
- Imetoa
elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea ugonjwa wa Ebola pamoja na
dalili za ugonjwa huu, kwa wananchi na watumishi wa afya katika
hospitali ya Nyakahanga
- Kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya Nyakahanga pamoja na maeneo ya mipakani
- Kutoa
matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza sauti na kupitia radioni
(Radio Karagwe) kuhusu ugonjwa huu. Aidha, vipeperushi pia vimetolewa.
HitimishoWizara
inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote
aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa nchini.Aidha, Wizara ya
Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu iwapo utatokea
hapa nchini.
Kwa sasa timu za wataalum zipo katika mikoa ya
Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha, kutoa elimu juu ya
ugonjwa huu kwa wataalamu na kwa wananchi na vilevile kufuatilia ugonjwa
huu sehemu za mipakani.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa
wananchi kutoa taarifa haraka kwenye kituo chochote cha kutolea huduma
za afya, mara wanapoona dalili za ugonjwa huu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano,
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Tarehe 6 Agosti, 2012.