Showing posts with label Mbeya. Show all posts
Showing posts with label Mbeya. Show all posts

Saturday, April 09, 2016

Waziri Ummy Mwalimu Atembelea Hospitali za Mkoa wa Mbeya

Waziri Ummy Mwalimu atembelea Hospitali za Mkoa wa Mbeya
Na Catherine Sungura, Mbeya
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Mhe. Ummy Mwalimu amefanya ziara katika hospitali zilizopo Mbeya na kuzitaka hospitali zinazotumia mfumo wa ukusanyaji mapato wa kieletroniki wasibweteke na mapato wanayoyakusanya kila siku.
Rai hiyo imetolewa na aziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu wakati alipotembelea hospitali ya rufaa ya kanda ya mjini Mbeya.
Ummy alisema ukusanyaji wa mapato kwa mfumo huu unasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha huduma za afya nchini ikiwemo ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba pamoja na utoaji wa motisha kwa watumishi.
"Bado tunatambua hali ya uhaba wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kuanzia ngazi zote, tukiweza kusimamia vizuri hili tutafanikiwa," alisema.
Aidha alisema wanatarajia katika serikali ya awamu hii bajeti ya dawa itaongezeka zaidi ya mara tatu kulinganisha na bajeti za nyuma, hivyo wameishauri Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wanunue dawa toka kwa wawekezaji wa hapa nchini ambapo itakua na bei nafuu na itaongeza tija na upatikanaji wa dawa kwa haraka.
Waziri Ummy Mwalimu aliutaka Mkoa kufuatilia, kuwafichua na kuwachukulia hatua wale wote watakaojihusisha na wizi wa dawa.
"Tunao watumishi wachache wa afya ambao wanahujumu na kuiba dawa na kuzipeleka kwenye maduka ya dawa binafsi, hao hatutowafumbia macho na kuwapeleka mahakamani"
Kuhusu upungufu wa watumishi wa kada ya afya nchini, Waziri wa afya alisema, nchi ina upungufu wa asilimia 52, hivyo serikali inatarajia kuajiri watumishi takribani elfu kumi hivi karibuni ambao watatawanywa nchi nzima ikiwemo mikoa iliyo pembezoni.
Katika hospitali ya uzazi ya Meta, waziri huyo ameguswa na ufinyu wa wodi za wazazi na kupelekea mama wajawazito na waliojifungua kulala chini na wawili wawili kwenye kitanda kimoja na hivyo kuwataka kufanya haraka ujenzi wa jengo jipya litakaloondoa mrundikano wa mama wajawazito na watoto njiti.
Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya inakusanya kwa mwezi kiasi cha shilingi Milioni mia tano na pia inahudumia mikoa saba nchini na kuhudumia zaidi ya watu milioni mbili.
46e02c3a-bc41-4fed-9ff6-a180f42fa264
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu akisalimia na watumishi mara alipofika kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mbeya.
afc64d2e-46a1-49a8-be9b-59340b6d8a8a
Waziri Ummy akimsalimia mtoto Jenifer Joel (9) mkazi wa Chunya aliyelazwa hospitalini hapo.
5f7ab771-5109-4c0c-95e6-83931c8ec108
Waziri wa afya akimjulia hali mtoto Baraka Jekonia (1) mkazi wa Chunya aliyelazwa wodi ya watoto, Waziri Ummy ameitaka hospitali hiyo kuwachaji pesa wagonjwa wote wanaofika hospitali ya rufaa moja kwa moja bila kupatiwa rufaa kutoka vituo vya afya vilivyopo jirani na wananchi ili kupunguza msongamano kwenye hospitali za rufaa nchini.
8e796dee-b674-43f7-97f8-3bad1046087d
Katika hospitali ya uzazi ya Meta, Waziri Ummy Mwalimu alimsalimia Binti Kanisia Komba aliyejifungua mtoto wa kike katika hospitali hiyo mama wajawazito wote wanatibiwa kwa kadi ya bima ya afya inayodhaminiwa mpango wa kusaidia akina mama wajawazito wa KFW toka Banki ya Ujerumani.
9518e21d-3e1e-43ad-a96a-c9b85ce91018
Hospitali ya Meta tayari imetekeleza maagizo ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ya kutoa kipaumbele kwa wazee wote nchini wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma.
974627cc-137b-436b-996a-f364952f7580
Waziri Ummy akiwasalimia wazazi waliolazwa kwenye moja ya wodi Hospitali ya Meta kutokana na ufinyu wa wodi inawalazimu akinamama wengine kulala chini hospitali hiyo inatarajia kuanza ujenzi wa jengo jipya ambalo litaondoa msongamano wa wazazi hospitalini hapo.
5b44d003-a727-495c-bde5-dea332ef407f
Waziri wa Afya akiwasalimia wagonjwa waliofika Hospitali ya Uzazi ya Meta kupata matibabu.

Saturday, February 21, 2015

Wosia wa Baba Wa Taifa Kuhusu Urais - Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Mei 1, 1995

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alialikwa kuwa Mgeni Rasmi kwenye kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika kitaifa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Mei 1, 1995. Katika hotuba yake alieleza mengi, leo tunachukua kipengele cha urais, alikuwa na haya ya kusema:
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
“Naeleza baadhi ya matatizo ambayo viongozi tutakaowachagua tuwe na hakika iwapo wanayaona hivi kama sisi tunavyoyaona. Yanawauma kama sisi yanavyotuuma na kwamba, watakapofika hapo wanapopataka watusaidie kuyatatua.

“Wanayaona, yanawakera na hata watakapofika hapo, hicho ndicho kitakachowasukuma kutaka kuwa marais wetu na wabunge wetu. “Marekani walikuwa na rais wao kijana mmoja mdogo anaitwa John Kennedy. Walimpiga risasi. Marekani nao ni watu wa ajabu sana! Vijana walilaani tukio hilo kwa kuwa walikuwa wanadhani wamemchagua rais wa umri wa kama miaka arobaini na mitatu au minne hivi.

“Sasa huyo ni kijana, hata kwa hapa Tanzania leo ni kijana. Alipochaguliwa na Marekani akawa rais wao. Katika hotuba yake ya kwanza kabisa aliwambia wananchi wenzake, hasa vijana “Usiulize Marekani itakufanyia nini, jiulize wewe utaifanyia nini Marekani?”.
“Kila anayetaka kuwa mgombea wa urais/ubunge ajiulize ataifanyia nini nchi yake
“Tunataka mtu anayetaka kuwa rais wetu ajiulize anataka kuifanyia nini nchi yetu na sio nchi yetu itamfanyia nini.

“Na tunataka swali hilo ajiulize kila mtu anayetaka kuwa mgombea wa chama cho chote kuwa mbunge/rais: “Kwa nini, kwa dhati kabisa, anaumwa na umasikini wetu na umasikini huo ndiyo unaomsukuma ashughulike na mambo haya ya siasa katika ngazi hiyo ama ya ubunge ama ya urais”. Kama sivyo, hatufai!
“Mtu hapakimbilii Ikulu: Hakuna Biashara Ikulu. Mtu anayetaka kwenda ikulu kutaka faida yo yote ikulu pale, hatufai hata kidogo. Wananchi, mimi nimekaa pale Ikulu kwa muda mrefu zaidi kuliko mwingine ye yote, wala sidhani kuna mtu mwingine anaweza kuzidi muda huo.

“Tayari hapa tumeweka sheria. Kwa mujibu wa sheria, mtu hawezi tena kukaa Ikulu zaidi ya miaka kumi, kipindi ambacho hata hakijafikia nusu ya kipindi nilichokaa. Mimi nimekaa miaka ishirini na tatu!
“Najua, kwa mtu halisi kabisa, Ikulu ni mzigo! Hupakimbilii! Si mahali pa kupakimbilia hata kidogo; huwezi kupakimbilia Ikulu. Unapakimbilia kwenda kutafuta nini?
“Ni mgogoro; ni mzigo mkubwa kabisa! Ukipita barabarani, unakuta watu wana njaa, unaona ni mzigo wako huo. Pazito pale! Huwezi kupakimbilia na watu safi hawapakimbilii.

“Ukiona mtu anapakimbilia, na hasa anapotumia tumia vipesa kwenda Ikulu, huyo ni mtu wa kuogopa kama ukoma!
“Mtu ye yote anayeonekana anapenda sana kwenda Ikulu na hata yupo tayari kununua kura ili kumwezesha kufika Ikulu ni wa kumkwepa kama ukoma. Kwanza, hizo fedha kapata wapi.

“Mtanzania wa leo hawezi kununua watu bila kwanza yeye kununuliwa.
Na kama kanunuliwa, atataka kuzilipaje? Kazipata wapi? Watanzania wote ni masikini tu. Mtanzania anaomba urais wetu kwa hela! Amezipata wapi? “Pili, kama hajanunuliwa, kazipata wapi? Kama kakopa, atarudishaje? Ikulu pana biashara gani mtu akope mamilioni halafu aende ayalipe kwa biashara ya Ikulu? Ikulu mimi nimekaa kwa muda wa miaka ishrini na mitatu.

“Ikulu ni mahali pazito. Kuna biashara gani Ikulu?
“Rushwa na matumizi ya fedha bila utaratiba wakati wa chaguzi: Sisi Waafrika ni watu wa ajabu sana. Unajua ni wadogo, lakini nasema, ni udogo wa mawazo. Umaskini wa mawazo ni umasikini mbaya kupita wote.

“Unaweza ukawa na almasi mfukoni, akaja tapeli na kijiwe kimetengenezwa kama almasi akakuambia “hebu tuone almasi yako. 

Bwana aa! Hii ya kwako sio almasi ni chupa tu, almasi ni hii. Kwanza nipe bwana.” Mkabadilishana. Yeye akachukua almasi yako na akakuachia kichupa na ukatoka hapo unashangilia kama zuzu!
“Sisi hapa Tanzania tulikuwa tumeanza utaratibu ambao ukitumia fedha nje ya fedha za chama na serikali na ukatumia fedha zako mwenywe katika uchaguzi, tunakutoa. Hufai! Huo ndio ulikuwa utaratibu wetu. Tulikuwa tunakuuliza: “hii nchi ya maskini, wewe mwenzetu una mali umeipata wapi?”
“Mali, kwa wakati huo, kwetu sisi ilikuwa ni sifa ya kukunyang’anya uwezo wa kugombea uongozi Tanzania. Tulijua kwamba, kama una mali, utaficha. Leo watu wanasema waziwazi: “Mwalimu uchaguzi wa mwaka huu utapitishwaje?”

“Marekani wanatumia fedha nyingi sana katika uchaguzi. Nyingi sana! Kama Marekani sasa hivi wanazungumza watunge sheria inayofanana na ile mliyoitupa ninyi mnadhani kwa sababu ni mawazo ya masikini, haina maana. “Wakubwa wanayafikiria mawazo hayo sasa hivi. Marekani wanafikiria uwezekano sasa wa kutunga sheria itakayoweka utaratibu wa fedha za ugombeaji kutokana na mfuko mmoja baada ya kugundua kwamba inapokuwa holela na kila mtu akiachiwa lwake, inavuruga.

“Inaleta rushwa kubwa kabisa. Unanunuliwa urais na unaweza kununuliwa na fedha za wauza bangi na wauza baa. Wauza bangi wanaiona hatari hiyo, ninyi haa!“Hapa tulikuwa na utaratibu mzuri kabisa tuliouanzisha mlioutupa, mnafikiri, sisi mwaka huu fedha tu! Uchaguzi wa fedha, mtazipata wapi? Mimi nimetoka juzi tu, mara mmetajirika kiasi hiki!
--

Saturday, November 08, 2014

Basi la Happy Nation yapata Ajali Mbeya!


 Natoa pole kwa waliojeruhwa!

****************************************************



Basi lenye namba T281 ARR mali ya Happy Nation likiwa limepinduka eneo la Meta Igurusi kilometa 54 kutoka Mbeya

Picha na Maelezo Kutoka MBEYA YETU BLOG:



Watu 37 wamenusurika kifo baada ya basi la abiria lenye namba za usajili T 281 ARR aina ya Scania linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam linalomilikiwa na Kampuni  ya Happy Nation kuacha njia na kupinduka eneo la Meta Kata ya Igurusi wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amesema ajali hiyo imetokea leo majira ya saa moja asubuhi  basi hilo likitokea Mbeya baada ya kupasuka gurudumu la mbele kulia kisha kupoteza uelekeo  na baadaye kumgonga mpanda baiskeli na kupinduka.



Msangi amesema baada ya ajali hiyo Dereva wa basi hilo aliyefahamika kwa jina moja la Shabani alikimbia ambapo Jeshi la Polisi linafanya juhudi za kumtafuta ili kueleza sababu za ajali hiyo.



Aidha Msangi amesema katika ajali hiyo kulikuwa na majeruhi 37 wanaume 26 wanawake 10 na mtoto mmoja wa kiume.



Baada ya ajali hiyo majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Chimala ambapo mjeruhi 10 bado wamelazwa na wanne wamekimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi.



Kwa mujibu wa Daktari Mkuu Mahenge wa Hospitali ya Chimala amesema kuwa waliolazwa Hospitalini hapo ni wanaume sita na wanawake wanne na walohamishiwa Rufaa ni wanaume wanne.



Daktari Mahenge amesema kuwa hali za majeruhi 10 walipo Chimala hali zao zinaendelea vema ingawa wanakabiliwa na upungufu wa damu na wameomba msaada katika kitengo cha benki ya Damu salama Mbeya.



Hata hivyo baadhi ya abiria wamelalamikia mwendo kasi wa basi hilo kwani baada ya kutoka kituo kikuu cha Mabasi lilianza kwenda kwa mwendo wa kasi na mara kadhaa walikuwa wakimuonya Dereva lakini alikuwa akikaidi.



Pia walikuwa wakifukazana na mabasi mengine yaliyotokea Mbeya kuelekea Jijini Dar es Salaam hali iliyosababisha basi hilo kupasuka gurudumu la kulia likiwa katika mwendo kasi na kona kali kisha kupinduka.



Wakati huo huo Kamanda Ahmed Msangi amesema  watu wawili wamefariki dunia wilayani Mbozi baada ya roli la mizigo kugongana uso kwa uso na gari linalomilikwa na NSSF.


Msangi amesema bado majina ya waliofariki hayajapatikana na kwamba Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Serikali Mbozi.

KWA PICHA ZAIDI BOFYA HAPA:

Saturday, July 12, 2014

Kuna nini Mbeya? Watu 135 Wameuawa!

Kamanda wa Polisi Mbeya Ahmed Msangi
KWA HISANI YA LUKWANGULE BLOG:

WATU 135 wameuawa katika matukio tofauti yaliyotokea mkoani Mbeya katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Julai mwaka huu.
 
Kiasi hicho cha matukio ya mauaji ni sawa na pungufu ya matukio 21 sawa na asilimia 14 ikilinganisha na yale 156 yaliyotokea katika kipindi kama hicho mwaka jana.
 
Akitoa taarifa ya utendaji wa jeshi la polisi mkoani Mbeya, Kamanda wa polisi mkoani hapa Ahmed Msangi alisema katika takwimu hizo mauaji yaliyotokana na wananchi kujichukulia sheria mikononi yalikuwa 33.
 
Alisema mauaji yaliyosababishwa na imani za kishirikina yalikuwa 23 sawa na matukio ya mauaji yaliyotokana na sababu nyingine huku matukio ya mauaji yaliyosababishwa na wivu au ugoni yalikuwa 20.
 
Matukio ya mauaji yaliyotokana na ugomvi wa majumbani yalikuwa 16, matukio ya ugomvi vilabuni 11 na matukio ya kulipiza kisasi yalikuwa tisa.
Alisema katika kipindi hicho wahamiaji haramu 159 walikamatwa kati yao 152 walikuwa raia wa Ethiopia, 23 raia wa Burundi,10 Wasomali, saba Wapakistani, wawili kutoka Malawi na mmoja akiwa ni raia wa Msumbiji.
 
“Katika kipindi hicho tumeweza kukamata bunduki 19 ambapo gobori zilikuwa 15, bastola mbili zilizotengenezwa kienyeji, Riffle moja na SMG moja. Pia zilikamatwa silaha mbili baada ya majambazi kuuawa katika jaribio la kufanya unyang’anyi. Silaha hizo ni SMG yenye namba 3514 na AK-47 namba 592058 na risasi 25 kwenye magazini,” alisema Kamanda Msangi.
 
Aliongeza kuwa katika kipindi hicho kiasi cha lita 479 za gongo pamoja na mitambo 16 ya kutengenezea pombe hiyo vilikamatwa.
 
Kilo 296 na gramu 678 na miche 314 ya bangi zilikamatwa sambamba na mashamba matatu ya bangi yenye ukubwa wa jumla ya ekari moja na robo.

Wednesday, April 30, 2014

Wajawazito walalamikia ‘Rushwa’ Kituo cha Afya Simambwe

Wajawazito walalamikia ‘Rushwa’ Kituo cha Afya Simambwe 


Mbeya Vijijini


BAADHI ya akinamama na wanakijiji wa baadhi ya vijiji vya Kata ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini wamewalalamikia wauguzi na wahudumu wa afya katika Kituo cha Afya Simambwe kwa kile baadhi yao kuwaomba kitu kidogo (rushwa) hasa kwa wajawazito wanapofika katika kituo hicho kupata huduma.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wanawake kutoka vijiji vinavyohudumiwa na kituo hicho vya Usoha Njiapanda, Shibolya, Simambwe, Garijembe, Ilembo Usafwa, Ngoha na Zunya walisema mjamzito amekuwa akiombwa kutoa shilingi 2000 kila anapojifungulia nyumbani kwa dharura baada ya kushindwa kufika katika kituo hicho.

Mmoja wa akinamama aliyezungumza na mwandishi wa habari hizi ambaye aliomba kutotajwa kwa kuwa huenda akapata taabu kihuduma za afya kituoni hapo, alisema kwa sasa ni jambo la kawaida wahudumu kuwaomba chochote wajawazito kituoni hapo.


“…Unajua vijiji vingi vinavyohudumiwa na kituo hiki vipo mbali na miundombinu ya barabara si mizuri, yaani hakuna usafiri zaidi ya bodaboda ambazo lazima zitoke Simambwe…sasa kutokana na hali hii inatokea mjamzito anajifungulia nyumbani kwa msaada wa wakunga wa jadi, akipeleka mtoto huyo kituo cha afya basi wanamuomba shilingi 2000 haijulikani ya nini, sasa hili si tunaamini sio haki,” alisema mama huyo.


Aidha baadhi ya wanakijiji walikilalamikia kituo hicho kwa kitendo cha kulalamika muda wote hakina dawa huku wahudumu wakiwaelekezwa kwenda kununua dawa jambo ambalo wanahisi kuna mchezo mbaya unafanywa na wahudumu hao.


“Muda wote ukienda kutibiwa utasikia kauli za hakuna dawa tunakuandikia nenda kanunue, tena wengine wanaelekeza hadi maduka ya kununua dawa hizo ndio maana baadhi yetu tunahisi kuna mchezo mbaya (kuhujumu dawa) unaofanywa na baadhi ya wahudumu.,” alisema Mzee aliyejitambulisha kwa jina la Kalamwa.


Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Simambwe, Salome Mwaipopo  alipinga vikali uwepo wa vitendo vya kuomba rushwa kwa watumishi wa kituo hicho na kudai malalamiko kwa wanachi wanaohudumiwa na kituo hicho imekuwa kitu cha kawaida hasa wanapotembelewa na mgeni.


“..Hakuna kitu kama hicho unajua wakazi wengi wa vijiji hivi wamezoea kulalamika hasa wanapotembelewa na mgeni…hakuna wanaoombwa fedha, mjamzito akijifungua nyumbani tunampokea bila masharti na kumpatia huduma anazostahili, si kweli wanachokilalamikia,” alisema Mwaipopo.


Hata hivyo alisema kituo hicho kinahudumia idadi kubwa ya watu zaidi ya uwezo wake jambo ambalo hukifanya kuelemewa kwa idadi ya dawa wanazoletewa, wahudumu na vifaa vingine tiba hivyo kuiomba Serikali kukiongezea mgao wa dawa.

“…Kituo kinahudumia idadi kubwa ya watu kupita uwezo wake hivyo unakuta hata baadhi ya changamoto kama ufinyu wa dawa na wahudumu vinatokana na hali kama hiyo…,” alisema Mganga huyo Mkuu wa Kituo cha Afya Simambwe. 
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa ushirikiano na TGNP

Saturday, November 26, 2011

Tanzia - Annel Mwakipunda Mwaisumo








FAMILIA YA MWAKIPUNDA WA NGAMANGA IPINDA KYELA MKOANI MBEYA WANASIKITIKA KUTANGAZA KIFO CHA MPENDWA WAO ANNEL MWAKIPUNDA MWAISUMO KILICHOTOKEA TAREHE 26/11/2011 DAR ES SALAAM. MAZIKO YATAFANYIKA MOROGORO TAREHE 28/11/2011
HABARI ZIWAFIKIE FAMILIA YA MWAKIPUNDA,FAMILIA YA MWAISUMO,NDUGU,JAMAA NA MARAFIKI POPOTE WALIPO.
BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE MILELE NA MILELE
AMEN

Wednesday, March 03, 2010

Jibu - Ilivyokuwa Safari Yangu Mbeya

Na John Mwaipopo

Nimebahatika kutumiwa e-mail ambayo mwandishi wake ameiita ripoti ya safari yake ya kikazi mkoani Mbeya. Ameituma kwa watu wengi ili kueneza uchafu aliouona mkoani humu. Sina uhakika nani alimpa kazi ya kuandika ripoti yake hii maana nijuavyo riporti ina kitu kinaitwa terms of reference yaani waliokutuma na jinsi walivyokutuma kufanya uchunguzi/utafiti. Lakini haidhuru pia inaweza kuwa ripoti binafsi ya muhusika anayejiita mwanahabari, ingawaje ripoti yenyewe inaonyesha alichokiandika sicho alichotumwa kufanya huko mbeya. Waweza isoma hapa
Awali napenda kumpongeza mwanahabari kwa kuonyesha yale ambayo kwa mtazamo wake hayaonwi ama hayajaonwa na watu wasiowahi kufika Mbeya ila nitachukua fursa kidogo kurekebisha yale ambayo yamewasilishwa ndivyo sivyo. Napenda ijulikane mie ni mkaazi wa mbeya kwa karibu miaka 20 mfululizo isipokuwa nikiwa shule ama vyuoni, ambako nako nilitambulika kuwa natoka Mbeya. Hivyo itambulike nina maslahi na uenyeji/ukaazi wangu hapa Mbeya.

Juhudi hii ni kwa ajili ya kuweka sawa kumbukumbu na taarifa kamili. Pili nadhani itamuongezea ufahamu bwana mwanahabari. Tatu juhudi hii itafanya upotoshajia wa makusudi wa mwanahabari pengine kutokana na wembamba wa uwezo wake wa kufikiri, kupembua na kuchanganua mambo, ujulikane.

Nianze na kunukuu mwanzo wa report yake hii. Nanukuu “Duniani kuna mambo mengi sana.” Nukuu hii inaonyesha jinsi gani huyu mwanahabari (lakini mwanahabari aliyetumwa kwenda kutengeneza mashine mbeya. Habari na umakenika wapi na wapi) alivyo maamuma wa kujua mambo hata yaliyo ndani ya nchi yake. Kwake Mbeya tu ni dunia nyingine kabisa! Kwake ilikuwa safari ya kustaabisha eti. Kwa mtu aliyefanikiwa kusafiri kuliko mwanahabari-makenika Mbeya haitofautiani sana kwa raha na mauzauza utakayoyakuta mikoa mingine, pengine mikoa mingine imeizidi hiyo Mbeya. Nitaonyesha kwa kifupi hapa chini.

Kimojawapo ni uwingi wa makanisa na sehemu za kuabudia hapa Mbeya. Eti kutoka kanisa moja mpaka lingine ni hatua 30! Nimekaa Mbeya karibu miaka 20 sijayaona hayo makanisa na viwanja vya kuabudia vilivyopakana hatua 30 kama mwanahabari-makenika anavyotaka kuwadanganya watu ambao hawajafika Mbeya.

Jambo la msingi lililonisukuma sana kujaribu kujibu ripoti hii ni maambukizi ya ukimwi mkoani Mbeya. Ni kweli Mbeya i miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa maambukizi ya gonjwa hili hatari lakini haiifuatii Johanesburg kwa maambukizi. Hata hapa Tanzania tu haishiki namba moja. Soma hapa uhakikishe. Labdha atuambie takwimu hizi kazipata wapi.

Ingawaje ripoti hii ina nia ya kutukumbusha kujiepudha na kujilinda na ukimwi lakini imejaa kejeli kama vile Mbeya na Ukimwi ni sawa na samaki na maji. Kwa mfano anasema “wenyeji wa hapa wengi hawaamini kama kuna ukimwi. Wanaamini mtu akifariki basi amefariki kutokana na mungu (sic) kumwita amechoka maisha ya dunia , wengine ndio hizo imani zao akifa mwenzao amelogwa na mambo kama hayo .” Hivi tujiulize ni kweli asilimia kubwa ya watu wa Mbeya hawajui lolote kuhusu ukimwi isipokuwa wachache na pengine wageni wanaokuja kutengeneza mashine? Kumbuka hapa alipofikia kabla hajaenda Tukuyu (alikokuita ‘mkoa’ paragrafu ya 32) na Kyela ni mjini ambako ufahamu wa uwepo wa ukimwi ni mkubwa. Au amesahau Mbeya kuna watu wanaotoka mikoa yote ya Tanzania na si kweli kuwa wote wana imani za kizamaani za washamba wa Mbeya? Kuna wachagga, wahaya, wamasai, wasukuma, wakwere n.k. Na kabila lake ‘walistaarabika’ nao wapo wanaishi hapa, na wengine hawana mpango wa kurudi huko kwa ‘wastaarabu’.

Mwanahabari-makenika anaanika kuwa hapa Mbeya “ukikutana na wasichana 5 basi 3 wanamarafiki wa kiume ambao sio wanafunzi wenzao yaani watu wa nje tu , wamachinga na madereva au watu wa shuguli zingine , hii inaadhiri sana hawa vijana utendaji wao madarasani” (para 24). Nadhani anaongelea wanafunzi lakini hajatuambia takwimu hizi amezitoa wapi ama lini yeye binafsi alifanya utafiti huu. Na pia sidhani mmomonyoko huu wa maadaili miongoni mwa wanafunzi uko Mbeya tu. Pengine kwao hamna huu upuuzi, upuuzi ambao katu siupigii upatu kokote kuwako.

Nina mashaka na tabia binafsi za mwanahabari-makenika hususani katika masuala ya ngono. Nadhani ni muumini mkuu wa kuendekeza ngono. Pengine kafikia ushemasi kabisa. Inakuwaje mtu ambaye si muendekeza ngono ukachombezana kwa simu kimahaba na wanawake asiowajua hata wakapanga siku ya kwenda Mbeya ili wakapene hilo joto (para 11) alafu anaingia mitini dakika ya mwisho. Au sitaki nataka? Pia inakuwaje mtu asiye mzinzi akaongea na msichana asiyemjua kwa masaa mawili na wakatongozana (para 38) kisha unajifanya kuingia mitini. Nashawishika kuwa mwanahabari-makenika alikuwa akina sitaki-nataka. Nilidhani mtu asiye mzinzi, kama mwanahabari-makenika anavyotuaminisha, asingejihusisha na mazungumzo yanayoshadidia ngono. Nadhani angekuwa mkali mara moja! Tena katika hili anadiliki kuwadhalilisha wasichana wa Mbeya (pasi na kuwa na uhakina ni wenyeji wa kuzaliwa hapa) kuwa ni heri atongoze ng’ombe au mbuzi kuliko wao! (para 40 & 41).

Katika mambo yote aliyoyaona Mbeya, mazuri na mabaya, aliona la ngono ndio kuu. Afrika Kusini pamoja na kuongoza kwa maambukizi ya ukimwi bado ilionekana inafaa kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia. Safari yote ya Mbeya mwanahabari-makenika ameshindwa kuona mambo chanya kama utekelezaji wa vitendo wa sera ya kilimo kwanza, hakupishana na malori yanayokimbilia Dar es Salaam yakiwa yamesheni vyakula na matunda anuai. Hakushanga hali ya hewa safi tofauti na hali ya Dar es Salaam iliyojaa sumu. Hakuona milima na mabonde yanayohitaji wawekezaji wa aina-aina. Hakuona ukarimu wa watu, wenyeji na wageni. Hakufurahia maji yasiyokatika. Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni.

Hitimisho.

Nina wasiwasi na ufahamu na uwezo wa kufikiri wa mwanahabari-makenika. Sidhani kuwa hajaenda shule kwani kusoma na kuelimika sio lazima vikatangamana. Nadhani ni wakati sote tuliolazimishwa kuisoma (ndio katutumia kwa lazima)ripoti hii tukaiangalia kwa jicho la pili. Hata majibu yangu haya pia yanahitaji upembuzi makini. Sio lazima yakawa ya kweli kwani nimeandika kwa kuzingatia maslahi ya kimkoa zaidi. Lakini nachelea mwanahabari alikuwa na nia ya kuupa mkoa wa taswira potofu zaidi ya ile iliyopo. Ni kweli mawazo yake ni baadhi ya changamoto sio tu katika Mbeya bali pia nchi nzima. Wapi hakuna mauzauza kama haya. Huko Dar es Salaam ambako mwanahabari- makenika anatoka/anaishi ndio usiseme!

Mnaweza kumtebelea John Mwaipopo huko Mwaipopo Blog

Tuesday, March 02, 2010

Ilivyokuwa Safari Yangu Mbeya


Imeandikwa na Mwana Habari
Duniani kuna mambo mengi sana , ambayo mengine ni kama vibaya kuhadithia kwa wengine kama labda ni wenyeji wa huko au labda kama wana mahusiano na kitu hicho inakuwa mbaya haswa kwa wale wasiopenda kujua ukweli wa mambo , lakini wote tunakubaliana kitu kimoja bila kusemeana ukweli hakuna mafanikio yanayoweza kufikiwa na binadamu kwa njia yoyote ile hata kwa nini .

Ntakupa mifano michache mfano huku afrika na sehemu zingine za bara asia na amerika ya kusini , viongozi ni waongo , wamewajengea mpaka watoto wao na vizazi vingine uwongo kiasi kwamba mtu akisema ukweli anaonekana muasi mbaguzi au pengine mchonganishi wanabakia kulalia uongo siku zote hawaendelezi vizazi na watoto wao katika secta ya sayansi na elimu ambayo inahitahi ukweli na uwazi kila kitu uwongo na ulaghai

Hata katika mila na desturi , huku afrika mila na desturi za uongo ni fani , angalia hili suala la ushirikina ?? ushirikina ni mali ya mwafrika na huku imejaa sana lakini ushirikina ni uwongo mtupu ni ujanja ambao mwingine akifundishwa ana adapt na unaweza kutumika kwa faida nyingi tu katika maendeleo na makuzi ya watu wengine hii ni sayansi inayohitaji kuwekwa wazi ila ndio hivyo uwongo umetuzidi mpaka tunajichukia .

Mimi huwa napenda kusema kila ninachojisia kinanivutia na nimeshuhudia mwenyewe kwahiyo sio uwongo napenda kuandika kwa njia ya hadithi au makala kwa watu haswa mafariki zangu , juzi nilikuwa mkoani mbeya na hayo niliyoandika ndio hali halisi ya watu wa mkoa ule wanavyoishi wengi wao hata kama wakikataa na kubisha wanakataa lakini wajomba zao , mama zao , wadogo zao na majirani zao wanaangamia .

Haswa katika hili suala tata la ugonjwa wa ukimwi , huu tuuangalie kwa pande 3 kuu yaani mimi , wewe na yule ( wale ) tuna nafasi gani katika kuendeleza jamii zilizobora ambazo hazisumbuliwi na jinamizi la ugonjwa wa ukimwi wala matatizo yoyote wote wakue vizuri waje kuwa taifa bora watoe mchango kwa majirani zao na vizazi vijavyo ?

Usijali bwana ( KILA MTU NA MAISHA YAKE AU SIO )

Ehe vipi mambo hapo ulipo ??

Hapa ni salama sana , maisha ni bam bam naweza kusema , sasa hivi ni mchana wa saa 6 hivi inaelekea saa 7 kamili , ni lunch time kwa wengine ila mimi huwa nakula chakula cha mchana kuanzia saa 9 hivi au saa 10 jioni halafu usiku huwa sili chakula napenda kula samaki na karanga hiyo ndio furaha ya maisha yangu ya kila siku , kila mtu anaamua na kutenda anachoona kinafaa au sio ?

Basi kipindi hichi cha karibuni wiki hizi 2 nilienda mbeya kwa ajili ya kazi katika offisi moja hili ni shirika la uingereza kazi yake ni kusaidia watu wa manispaa na miji katika ukusanyaji wa kodi na mapato na katika kuwafundisha zaidi kuendana na uchumi wa dunia jinsi unavyokuwa kila siku .

Shiriki hili tuna mkataba nalo wa mambo ya ufundi na shuguli zingine zinazohusu data na ukaguzi wa vifaa vyao vya mawasiliano , kutokana na mkataba huu kila baada ya miezi 3 lazima niende mkoani mbeya angalau kwa wiki moja kuangalia hizo mishine zao n akutatua matatizo yao kama yapo na maisha yanaendelea .

Kwahiyo wiki hizi ndio nilienda mimi na walishanizoea , lakini mwaka huu nilijuwana na dada mmoja hivi anafanya kazi pembeni mwa shirika hili yeye ni mama mahesabu , ananipenda sana mimi na wakati mwingine akinipigia simu huwa ananieleza kuhusu ngono jinsi tukikutana atakavyo nikumbatia , mabusu na mahaba mengine mazito mazito yaani amejichambua sana kuhusu maisha yake kule na anavyonizimia mimi .

Huyu dada alipata taarifa kwamba ntaenda kule , lakini huyu dada sijawahi kukutana nae zaidi ya kuchat nae tu na kuongea katika simu , dada wa watu alijiandaa sana kwa ajili ya kunipokea nikalale kwake yaani kitandani kwake na ile baridi anavyonihadithia anapenda kupata joto langu mambo kama hayo .

Nikatoka zangu huku jumatatu asubuhi saa 12 hivi kwa usafari wa Scandinavia , nilikatiwa tiketi mpaka mbeya lakini nilivyofika iringa pale makambako nilishuka katika gari hilo nikapanda basi lingine nilijua tu huyu dada atakuwa ameshaambiwa naenda na basi gani wakanipokee stendi ya mabasi hapo nilishmkwepa kwa kiasi kikubwa .

Muda wa saa 1 hivi usiku basi lilikuwa limeshaingia mbeya mjini mimi sikwenda kule mwanjelwa nikashukia sehemu moja inaitwa fire , hapo pembeni yake wala sikuchukuwa hoteli , nilipeleka vitu vyangu katika nyumba ndogo za wageni kwanza nione hali ya mambo inavyoenda kabla sijaamua mambo mengine .

Saa 3 hivi usiku ikatimia kama nilivyootea yule dada akanipigia kuniuliza kama nimeshafika mbeya , nilimuuliza amejuaje kama naenda mbeya ? akasema ameambiwa na receptionist wa pale kwa mkuu wa mkoa , kwahiyo hali ikawa hivyo sikuwa na jinsi ya kujitetea .

Lakini niliamua kumdangaya tu , nikamwambia safari imeahirishwa bwana , mpaka tutakapowaambia hapo baadaye mwezi huu kwahiyo nitaenda mkoani singida au mtwara kwa kazi kama hizo “ Ohh yona unasema kweli ? nilivyokuwa nakungoja kwa hamu hivyo nikupe mambo ? na majambo ?”

Basi nilienda kidogo katika internet café kwa ajili ya kumwandikia email yule receptionist wa pale kumweleza hali halisi kisha nikampigia simu kumweleza kuhusu niliandisha katika email kwa kifupi alinielewa kwahiyo kazi ikawa kwake asiseme kama nimekuja mbeya na wala nikifika kule asiniite jina langu akinitaka aniite SHY tu mengine sijui .

Asubuhi yake ikafika yaani jumanne , niliamka katika saa 3 hivi asubuhi , hapo nilienda kuweka vitu vyangu katika hoteli moja eneo la meta mjini mbeya karibu na kituo changu cha kazi nikamuuliza tena yule receptionist kama yule dada anayeningoja yuko karibu au la , kweli yule dada alikuwa mbali kidogo .

Nikatoka hapo kuelekea katika kituo cha kazi kufanya ile iliyonipeleka pale , niliifanya kwa masaa 3 hivi ndio nilimaliza kwahiyo nikarudi zangu katika hoteli , huku nilienda tu kujisafi kwa mara ya pili kubadilisha nguo na kuvaa kama mtoto wa kijiweni halafu nianze kutembelea mitaa ya mji wa mbeya kuongea na watu haswa vijana .

Mbeya kuna mambo ya ajabu na wakati mwingine ya kutisha kama hujazoea , maajabu yake ni kwamba “ HUU NDIO MJI WA PILI KWA WINGI WA MAKANISA BARANI AFRIKA “ Ni mji wenye makanisa mengi kuliko yote Afrika Mashariki Na Kati ,huu wingi wa makanisa yaani ukitembelea hatua 30 unakuta kanisa mbele yako au kama sio kanisa unakuta sehemu ya mahubiri mbele yako hata pembeni yako .

Huu wingi wa makanisa sio hoja kwamba watu wa huku wameshiba neno la mungu kiasi kwamba wanaweza kubadili maisha yao na kuwa mazuri zaidi au kuwa bora zaidi la hasha , wamejawa na neno la mungu mpaka limepasuka yaani wamekinai neno la mungu sasa wanaona kuwa na makanisa ni fasheni .

Huu ndio mji unaoongoza kwa kukua kwa maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi katika afrika ukiachilia jberg , huu unafuatia , kutokana na kwanza uko Mpakani , watu wengi wa afrika ya kusini wanapoingia Tanzania kwa njia ya lami hupitia mbeya kuja dsm , wale wa Zambia nao ni mbeya , Botswana na kadhalika ni mji ulio katika majaribu mengi sana .

Unaona makanisa mengi , watu wengi wameokoka na kadhalika lakini watu wanaangamia kwa ugonjwa wa ukimwi kila kukicha na wenyewe wenyeji wa hapa wengi hawaamini kama kuna ukimwi wanaamini mtu akifariki basi amefariki kutokana na mungu kumwita amechoka maisha ya dunia , wengine ndio hizo imani zao akifa mwenzao amelogwa na mambo kama hayo .

Hapa mjini ukikutana na wasichana 5 basi 3 wanamarafiki wa kiume ambao sio wanafunzi wenzao yaani watu wa nje tu , wamachinga na madereva au watu wa shuguli zingine , hii inaadhiri sana hawa vijana utendaji wao madarasani , maishani na katika maamuzi mengine muhimu katika maisha yao kutokana na nguvu za watu wengine wa nje hawa wafanya biashara .

Mimi hoteli niliyofikia ilikuwa karibu na barabara kidogo , nilikutana na wanamuziki wa bendi ya Akudo Sound , hawa wanamuziki wacheza shoo wao wale wasichana wote ni chini ya miaka 22 , basi hapa katika hii hotel unachukuwa chumba halafu wahudumu wanakuuliza kama unapenda kupata dada wa kuishi nae wakati wote uko hapo katika hoteli .

Yaani huyu msichana atakuwa anakufulia nguo zako ulizokuja nazo na kukunyooshea wakati haupo , anakupa huduma ya ngono ( HII NDIO HUDUMA KUU ) , ukipenda atakuwa anakupikia pamoja na mambo mengine kukuogesha , na vitu kama hivyo , sasa unamwangalia huyu msichana mrembo ( WENGI WAO NI WAREMBO HASWA ) ametulia ana miaka chini ya 25 kwanini anakuja kujiuza huku , amekosa nii maishani mpaka amekuja katika hizi hoteli kujiuza .

Ukikataa kuchukuwa msichana inawezekana usiku wanakusumbua kwa kelele kule katika bar au dirishani mwako , wanakuuliza kama unataka huduma au la , kama hutaki wengine wanaaza kukutusi na maneno mengine ambayo siwezi kuyataja kama wewe shoga nini ? Unaliwa kiboga ? yote haya kisa umemkataa .

Ndio unaweza kuamua kumchukuwa , ukimchukuwa tu ujue sio wewe peke yako uliyemchukuwa labda wiki nzima hajalala kwao au kwake yuko pale anatoa huduma kwa wateja mbali mbali , kila siku yuko katika ngono na mambo mengine yasiyo na msingi kwa binadamu wa kawaida kama ameadhirika basi na wewe uko njiani , safari yako inakuja nap engine unaweza kuadhibiwa zaidi .

Saa zingine unaweza kutoka chumbani kwako katika corridor msichana anaweza kukuvulia chupi ? anakuonyesha alivyoumbika , ni kigiza hivi huoni vizuri lakini ukiona msiri wa chupi unalegea na kuteremka chini utasimama uangalie kunani , wengine utakuta wamesimama katika corridor na nguo zinazoonyesha maungo yao kazi ni kwako wewe mtazamaji yaani mimi niangalie nimekubali nichukuwe mzigo ?

Naweza kukubali , kukubali ni rahisi sana kwasababu inasemekana huyu msichana kukaa nae kwa usiku mmoja ni alfu 2 yaani hii alfu mbili hata kondom yaa maana hupati kama unaamua kulala nae na kutumia kinga , kinga zenyewe haziaminiki ya nini kufanya vile wakati najua wako zaidi yake ? na nikwambie siri wanawake wa mbeya wengi ni wanawake asili ya kiafrika yaani wamejazia ndio hapo sasa mate yanakutoka udenda njee , vishawishi na mambo mengine ya usheee .

Kwahiyo ndio hivyo , kesho yake nilitoka katika hoteli hii nikaenda katika hoteli ingine nikawe huru zaidi kwakuwa nilipenda kupiga picha mji ule wakati wa usiku niwatumie baadhi ya rafiki zangu wengine wanaopenda kujua zaidi kuhusu mji wa mbeya na mambo yake , ndio hivyo niliwakimbia hawa wadada mwaaah .

Siku ya pili ni kwenda kuandika report kuhusu ile kazi ya jana na kufanya majaribio kuhusu mashine zingine , kuwauliza maswali kadhaa kama wanamatatizo yoyote yale na kadhalika , kwahiyo hawakuwa na matatizo yoyote kwahiyo niliwaaga kutoka pale nikaanza safari ya kwenda tukuyu sikuwahi kufika tukuyu nilipenda kufika tu kwa kuwa kuna baadhi ya rafiki zangu wanatokea mkoa huu .

Nilifika pale muda wa saa 9 hivi jioni , nikatafuta sehemu ya kupumzika nikapata nikaenda kuhifadhi vitu vyangu , nikabeba kamera yangu , na kitabu changu kidogo kuanza kwenda mitaani , nilibahatika kuona internet café moja jirani pale , nikaingia ndani mule kufanya shuguli zangu .

Basi nilifika katika internet café hii niliwaambia watu kwamba niko mkoani mbeya sehemu inaitwa tukuyu , kuna baadhi ya watu ni wenyeji wa mkoa wa mbeya tulikuwa tunachat pamoja wengine wanatokea tukuyu na kyela , wakanielekeza makwao niwatembelee na wengine walihitaji salamu kutoka kwao .

Ndio hivyo nilipata marafiki wapya wa mkoani mbeya kw anjia ya mtandao , basi pale nilipokuwa jirani kidogo kama kilometa 10 hivi ndio sehemu ya kwanza nilitakiwa kwenda , nilifanikiwa kwenda mpaka kwa hiyo nyumba niliyoelekezwa na rafiki wa internet niliongea nao na kuwapa namba za simu za huyo ndugu yao aliye majuu , kwingine ni kyela lakini kyela mpaka kesho yake safari yangu ya mwisho .

Muda wa saa 3 hivi usiku nilitoka zangu kule mtaani nikarudi zangu katika nyumba niliyofikia , nilienda kuweka vitu vyangu na nikabadilisha mavazi kama ya kijana mtanashati , mwenye aibu sana , niliyekuwa mpweke nahitaji huduma Fulani ??? huduma ya ……?? Nikakaa pale katika bar , nikaagiza nyama choma nikawa nakula na glasi ya juisi .

Dada mmoja hivi ametokea zake huko sijui wapi akaja pale , akakaa mbele yangu nikamkaribisha vizuri sana kwa roho moja tukaanza kuongea , huyu msichana ni mrembo na amejazia kuanzia kigua , miguu na kadhalika hakika huyu ni masha alah kama nilivyokuambia wasichana wengi wa mkoa wa mbeya wamejazia au sio ?

Mrembo wa watu tukaongea kwa masaa 2 hivi mpaka saa 5 usiku , akaniomba namba ya simu nikampa , pia aliniuliza wapi ninapolala usiku huo , kama niko na mke au mtu maalumu usiku huo , nilimjibu sina niko mwenyewe tu na ninapenda kuwa mwenyewe hivyo hivyo inavutia zaidi au sio ?

Dada wa watu aliondoka , nami niliondoka zangu kurudi katika chumba kwa ajili ya mapumziko ya siku ile , basi nilipofika kule kwa hoteli muda kidogo yule dada aliniandikia sms inasema ‘ DEAR , UKO WAPI NIJE ? NINASIKIA BARIDI SANA NAHITAJI JOTO LAKO “ mhh nikakumbuka ni mambo yale yale nilivyokimbia kule mbeya mjini .

Nami nilimjibu “ JAMANI DEAR MBONA NA MIMI NASIKIA BARIDI NIMEJIFUNGIA CHUMBANI FUNGUO SIJUI IKO WAPI USIJE BWANA “ huyu dada akasoma msg yangu nilipokea jibu lake “ WE XXXNGE SANA , KWANINI ULINITONGOZA ? tukaendelea kubishana katika simu “ AHH NIMEKUTONGOZA ? SI BORA NIKATONGOZA NGOMBE AU MBUZI ? “

DADA : YAANI UNANIJIBU HIVYO ?
YONA : NDIO , BORA NITONGOZE NGOMBE

Basi nilizima ile simu yangu ili niwe huru zaidi nilale , kweli nikalala zangu mpaka usiku saa 10 hivi , nikaamka , nikaenda kwa yule mlinzi wa pale kumwambia anifungulie geti nataka kutoka nje akakataa akasema mpaka nimwambie receptionist wa pale naye alikuwa amelala , basi nilijaribu kumgongea hakuamka .

Uvumilivu ulinishinda , nilienda katika begi langu nikachukuwa vifaa nikatengua kitacha cha mlango wake mpaka ndani kwake nilimkuta yuko juu ya msichana Fulani katika fani ahaha , nilitaka kucheka lakini siku cheka , nilimfuata moja kwa moja mpaka pale nikamfunua shuka lile nikamshuka kitandani na kumpiga teke kidogo akajigonga katika kabati la nguo mule chumbani .

Nikimwomba sasa anifungulie mlango nitoke ndani ya ile hoteli kuna sehemu nataka kwenda , alitaka kuvaa nguo nikazichukuwa nguo pamoja na za yule msichana wote nikazitupa nje ya mlango ili anipe funguo nikafungue mwenyewe , alibisha nilivyomwomba basi nikamfuata tena kumtisha .

Ndio alisalimu amri akanipa funguo zile mimi huyo na begi langu nikatoka nje , nilikuta taxi pale karibu na hoteli lilinikimbiza mpaka kituo cha gari kupata basi la kuelekea kyela nikakata tiketi zangu pale na kupakiza vitu vyangu katika gari lile .

Kyela nilifika salama sana , nikafanya na kutekeleza yaliyonipeleka kule mwisho siku hiyo niliyo usiku nilirudi mbeya mjini ili nijiandae kwa safari ya kurudi zangu mjini dare s salaam kama kawaida , nilifika mbeya mjini katika saa 5 hivi za usiku moja kwa moja nilielekea katika nyumba ya wageni kwenda kupumzika .

Kesho yake ya asbuhi ilikuwa ni saa 11 hivi niliamka mapema nikajiandaa kwenda standi ya basi nikapata basin a safari ya kuja dare s salaam ilianza na kunoga kama kawaid nilifika jiji la mzizima nikiwa salama salmin na mwenye afya tele .

Nilifika muda wa saa 10 hivi , nikaja zangu hapa katika office kuleta report za huko kisha nikakimbilia katika mtando usiku huo huo kwa ajili ya kutuma hizi picha kwa watu Fulani marafiki zangu .

Na huo ndio ukawa mwisho wa safari yangu maridadi mkoani mbeya nilienjoy vya kutosha , karibuni nitaenda mkoani Mtwara , Lindi , Dodoma , Morogoro , Singida na Arusha kwa ajili ya kazi hizi hizi tuone itakuaje

Sikiliza tu