Showing posts with label Mh. Zitto Kabwe. Show all posts
Showing posts with label Mh. Zitto Kabwe. Show all posts

Saturday, November 12, 2016

Mh. Zitto Kabwe Amkumbuka Marehemu Mh. Samuel Sitta

Mh. Zitto Kabwe akiongea na Mh. Samuel Sitta nje ya Karimjee Hall Miaka ya Nyuma

Makala hii imeandikwa na Zitto Zuberi Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo

ALFAJIRI ya Novemba 7, 2016, tuliamka na kukutana na habari za kusikitisha ya kwamba mzee Samwel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametangulia mbele ya haki.

Mimi, kwa sababu ya heshima zangu kwake, nilikuwa nikimwita Babu. Ninafahamu kwamba alikuwa mgonjwa kwa kitambo kidogo akisumbuliwa na saratani ya tezi dume. Habari hizi zilisambaa kwa kasi kubwa kupitia mitandao ya kijamii. 

Hatimaye taarifa rasmi ikatoka kuthibitisha habari hizo.
Sitta aliitumikia nchi yetu kwa muda mrefu na kwa uadilifu mkubwa sana. Sisi wengine pia kwa kiasi fulani kukua kwetu kisiasa kumetokana na utumishi wake uliotukuka kwa nchi yetu alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Babu yangu huyu ananigusa mimi binafsi moja kwa moja. Alikuwa mtu wangu wa karibu. Tukiwa bungeni akiniandikia kitu alikuwa akitumia neno hilo “babu” kwa mwandiko wake mzuri usiotoka kwenye kumbukumbu zangu kabisa.
Labda siku zijazo, ‘vi- note’ hivi vinaweza kuchapishwa pindi watafiti watakapokuwa wakiandika historia ya nchi yetu na Bunge letu.

Aliniapisha kiapo cha ubunge tarehe 29/12/2005. Maneno ambayo aliniambia baada ya kunikabidhi Kanuni za Bunge na Katiba ya Nchi niliyaandika kwenye daftari langu la kumbukumbu siku hiyohiyo jioni.

Baada ya kula kiapo cha Utii na cha Uaminifu, kawaida wabunge hupewa mkono na mwapishaji na kupewa nyaraka za kazi. Kwa upande wangu, Sitta alinikumbatia na kuniambia “ utakuwa kiongozi muhimu sana kwa nchi yetu. You have a bright future”.

Maneno haya hayajawahi kutoka katika kumbukumbu zangu na kila nikipata misukosuko yangu kisiasa huyakumbuka na wakati mwengine yeye mwenyewe alikuwa akinipigia na kunikumbusha na kunitia moyo. Babu alikuwa mlezi wa wanasiasa vijana.

Sitta pia naweza kusema amenilea kwa kunisomesha. Mwaka 1996 nilikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Galanos jijini Tanga nikisomea mchepuo wa Historia, Jiografia na Uchumi (HGE).
Hali ya hewa ya Tanga haikunipenda, hivyo nikawa naumwa umwa sana. Pia nilitaka kusoma Hesabu badala ya Historia.

Wakati wa likizo ya mwezi Disemba mwaka 1996, nilitoka Tanga nikaenda Dar es Salaam, Wizara ya Elimu kuomba uhamisho kwenda shule yenye Somo la Hesabu, kidato cha Tano na Sita.
Nikakataliwa. Lakini nikaambiwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari wakati ule, Alexander Ndeki, alisoma na Sitta. Kipindi hicho Sitta akiwa Mkurugenzi wa Investments Promotion Centre (IPC) kabla haijabadilishwa jina kuwa Tanzania Investments Centre (TIC).

Nikaenda ofisi za IPC mahala ambapo leo ni CRDB Tawi la Azikiwe. Nilipofika Katibu Muhtasi wake akaniuliza kama nina miadi na bosi wake, nikasema hapana. Akaniambia hawezi kukuona. Nikasisitiza sana na kumlilia dada yule aniruhusu dakika chache tu. Akaniruhusu.

Nilipofika Sitta aliniuliza shida zangu kwa heshima kubwa. Nikamwambia kwamba ninataka kuhama shule. Akaniomba matokeo yangu ya Kidato cha Nne, nikampa maana nilikuwa natembea nayo.
Alipoyasoma akaniambia, “ wewe hupaswi kuhangaika kutafuta shule maana kwa matokeo yako unaweza kusoma shule yeyote nchini ya chaguo lako”.

Akainua simu akampigia Ndeki. Kisha akaniandikia kikaratasi niende wizarani muda uleule. Nilipofika wizarani nikapewa uhamisho kwenda Shule ya Sekondari Mazengo.

Nilipotoka nje ya wizara, nikakutana na kijana mwengine anaomba uhamisho, yeye anatoka Mazengo anataka kwenda Tosamaganga, Iringa. Akaniambia, achana na Mazengo hakuna Mwalimu wa Uchumi na hali ya vyoo ni mbaya sana. Nikarudi kwa Mkurugenzi.

Mzee aliyenipa uhamisho aliponiona narudi na kumwambia sitaki Mazengo akachukua fomu zangu za uhamisho na akachukua ‘whiteout’ akafuta Mazengo na kuweka Tosamaganga huku akisema kwa hasira “ nyie watoto wa wakubwa bwana”.

Sikujali nikaenda zangu Tosa kusoma Uchumi, Jiografia na Hesabu (EGM). Tangu wakati huo, Sitta akaendelea kufuatilia maendeleo yangu shuleni hapo, kisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Taasisi ya InWent nchini Ujerumani.

Nilipotoka Ujerumani kusoma masomo ya Juu ya Biashara ya Kimataifa mwaka 2004, ilipaswa niwe na mradi wa kitaaluma. Nikachagua kuunganisha kampuni za Kijerumani na zile za Tanzania kwa kuandika mradi wa kuchukua wafanyabishiara 20 kutoka Tanzania na kuwaunganisha na wengine 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya.

Ilibidi kupata Taasisi ya Tanzania kwa ajili mradi huo na Sitta akawa mstari wa mbele kuhakikisha mradi unafanikiwa na tukautekeleza kwa umakini kwa msaada wa afisa wa TIC aitwaye Phina Lyimo.

Mwaka mmoja baadaye, tukakutana na Sitta bungeni, yeye akiwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki na mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini. Ulezi wake ukaendelea mpaka mauti yalipomkuta wiki hii. Nimempoteza Babu mlezi.
Sitta alikuwa mwana mageuzi (reformer) na kupitia uanamageuzi wake alifanya mabadiliko makubwa sana katika uendeshaji wa Shughuli za Bunge.

Sisi tuliohudumu kwenye Bunge la Tisa, tukimwita Spika wa Kasi na Viwango, tuliona wenyewe juhudi zake za kuliweka Bunge katika nafasi yake ya Kikatiba. Licha ya kuhakikisha kuwa maslahi ya wabunge yanakuwa yanayolingana na hadhi ya Bunge, alihakikisha pia kuwa Bunge linaisimamia Serikali sawasawa.

Haikuwa kazi rahisi sana kwani kulikuwa na mvutano mkubwa sana kati ya Spika Sitta na Waziri Mkuu, Edward Lowasa, katika kuleta mabadiliko hayo.

Tulikuwa tunaambiwa kuwa mvutano ule ulitokana na tetesi kwamba Sitta ndiye alipaswa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na hivyo kuwa na msuguano na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.
Sio Sitta wala Lowasa ambaye alithibitisha ama kukanusha tetesi zile. Sitta ametangulia mbele ya haki, labda Lowasa ataweza kusemea hili siku za usoni.

Sitta alitumia fursa ya msuguano huo kufanya mabadiliko makubwa ya kanuni za Bunge na kutoa uhuru mpana wa mawazo ndani ya Bunge na kuhakikisha kuwa Taarifa za Kamati za Bunge na hususan Kamati za Usimamizi wa Serikali zinakuwa zinasomwa na kujadiliwa ndani ya Bunge kwa mujibu wa Kanuni.

Wakati wa Bunge la Nane, taarifa za CAG hazikuwahi kusomwa hata mara moja. Ni kutokana na mabadiliko haya ya kanuni ndipo Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC ) ilianzishwa mwezi Machi, mwaka 2008. Nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ile na kuingia kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo kipindi hicho tuliiona kama Kamati ya wabunge wazee.

Namna nilivyoingia kuwa Mwenyekiti wa POAC nayo ni hadithi nyengine ya namna ya malezi ya kiuongozi yaliyofanywa na Spika Sitta.

Sikuwa nimejaza fomu kuomba Kamati ya POAC. Wakati huo ulikuwa ni wakati wa vuguvugu la Buzwagi (Mkataba wa Madini uliosainiwa kwa siri na Waziri wa Nishati Hotelini nchini Uingereza ).
Nilikuwa mjini Bagamoyo kwenye kazi za Kamati ya Bomani nikiwa na Harrison Mwakyembe na Ezekiel Maige. Spika wa Bunge akanipigia simu, akaniambia “ Babu, kesho kuna uchaguzi wa Kamati za Bunge.

“Nimekuteua Kamati ya POAC ambayo ni kamati mpya itakayokuwa chini ya Kambi ya Upinzani. Najua hukuomba kuwa mjumbe wa kamati hii, lakini nahitaji damu changa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge.

“Naomba unikubalie na kesho uwepo Dar es Salaam kwa ajili ya uchaguzi na ugombee. Utashinda maana nimeshafanya kazi yangu”. Sikuwa na namna ya kukataa japo nilitaka sana kuendelea kuwa Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya Dk. Abdallah Kigoda, ama Kamati ya Nishati na Madini chini ya William Shelukindo.

Ombi la mzee ni amri. Nikawa Mwenyekiti wa POAC na kuwa mmoja wa washauri wakuu wa Spika wa Bunge. Kamati ya PAC ikawa chini ya John Cheyo na Kamati ya LAAC ikawa chini ya Dk. Willibrod Slaa. Ilikuwa ni Bunge lenye meno kwelikweli.

Sitta alikuwa mbabe. Ubabe wake ulimpelekea kufanya maamuzi ambayo wakati mwingine yalimweka kwenye matatizo na wananchi. Mfano mzuri ni suala la Hoja Binafsi ya Buzwagi na Hoja ya Wizi wa Fedha Benki Kuu ( EPA).

Mwanzoni, Spika alikuwa upande wa wabunge wenye hoja hiyo, mimi na Slaa kiasi cha kuziboresha hoja zile kwa kalamu yake mwenyewe. Wabunge wa chama chake hawakuwa wanapenda hoja hizi na hivyo Lowasa akamweka kwenye wakati mgumu sana wa kuegemea upande wa serikali.
Hoja ya Slaa akaitupa kuwa ‘ ni makaratasi ya kuokoteza’. Hoja yangu akaiingiza bungeni na akasimamia kusimamishwa kwangu Bunge.

Wananchi walimkasirikia sana. Siku moja usiku, nikiwa nyumbani kwa Freeman Mbowe Mikocheni, Samwel Sitta, akanipigia simu kulalamika kuwa wafuasi wangu wanamtukana kwa sms. Akaniambia niwakataze. Nilimkubalia tu, lakini sikuwa na uwezo huo.

Spika Samwel Sitta akawa ni Spika pekee wa nchi yetu aliyeshuhudia uundwaji wa Serikali mbili ndani ya miaka mitano ya Uspika wake. Mzee Msekwa yeye alikaa miaka 10 na Waziri Mkuu mmoja, ingawa mwaka 1993-1995 naye aliona mabadiliko ya Mwaziri Wakuu, kutoka John Malecela kwenda kwa Msuya.

Baada ya kujiuzulu kwa Lowasa, Sitta hakurudi nyuma tena. Aliendelea kuwa Spika wa viwango mpaka alipomaliza muda wake katika Bunge la Tisa.
Spika Sitta alikuwa mwepesi kuomba msamaha alipokosea.

Nakumbuka siku moja mwaka 2009 alimfukuza bungeni Cheyo kwa makosa ambayo mzee Cheyo hakufanya. Baadhi yetu tukakasirishwa na kitendo kile.

Nikaenda kumwona Sitta ofisini kumwuliza kulikoni amdhalilishe mwenzake namna ile. Akanieleza kuwa hakuwa sawa na atamwomba radhi Cheyo.

Tukiwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge, kwa ajenda zake za kawaida tu, Sitta akamwomba radhi Cheyo. Nikikumbuka kisa hiki nacheka sana maana Jaji Frederick Werema aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alicheka mpaka kuanguka chini. Sababu?

Sitta aliketi kwenye kiti chake, wenyeviti wote wa Kamati tukiwa tumetulia tuanze kikao. Mzee Sitta akasema “ John, naomba radhi kwa tukio lililotokea bungeni wiki iliyopita.
“Sijui nilikuwa nina nini siku hiyo, nadhani nilisumbuliwa na watu wanaopitapita jimboni kutaka kunitoa, nisamehe mzee mwenzangu”.

Baada ya maneno hayo ukumbi mzima ulitawaliwa na vicheko na Cheyo akamkubalia radhi yake huku naye akicheka na yakaishia hapo. Wazee hawa wawili wameandika pamoja kitabu “ Bunge lenye Meno”. 

Nimwelezeje zaidi Babu? Nimwelezeje zaidi Spika huyu wa Kasi na Viwango? Mwanasiasa shupavu, jasiri, mwenye ngozi ngumu, mbabe, mnyenyekevu inapobidi na mwenye uthubutu.
Tangulia Babu. Tangulia Mtemi wa Unyanyembe Samwel John Sitta. 

Raia Mwema

Tuesday, August 26, 2014

Facebook ya Zitto Kabwe imekuwa Hacked!

Kutoka kwa Maggid Mjengwa - Facebook

*******************************

TAHADHARI: KUNA MTU AMEHACK FACEBOOK ACCOUNT YA ZITTO KABWE

Muda mchache uliopita nimepokea ujumbe kwa anayejifanya Zitto Kabwe ( Impersonate) unaosomeka hapo chini ambao niliutilia mashaka kutoka sentesi ya kwanza. Usome....

"Habari, samahani kwa ujumbe huu endapo kama utakukera ila napenda kukurekebisha lengo kukuweka sawa na kukuepusha katika matatizo. Kuna taarifa umepost katika group ya facebook view timeline kupitia link hii hapa www.facebook-view-timeline.wapka.mobi kiukweli sio taarifa nzuri inaleta uchochez wa vita ya kidini,siasa na mfarakano wa ubaguzi kua makini nimepata taarifa jesh la polisi wanafatilia hz ripot na wapo ktk msako wa kukutafta ili utoe maelezo yakina. Nimezipa hzo hapa www.facebook-view-timeline.wapka.mobi mtu akilogin hapo akiingza email na password anaona yote. Kua makini"

Sunday, June 01, 2014

Mwili wa Mama Yake Mbunge wa Kigoma Zitto Kabwe Wasafirisha Kwenda Kigoma

Zitto kabwe akiwa na Prof  Ibrahimu Lipumba wakati wa kuuaga Mwili wa mama yake kipenzi Bi Shida Salumu aliyefariki leo kabla ya kusafirishwa kwenda Kigoma kwa mazishi
Ndege Ikiandaliwa Ili kuweza Kuingiza Mwili wa Marehemu Mama yake Zitto Kabwe
Waheshimiwa Wabunge na Baadhi ya Viongozi wakibeba Jeneza lililobeba Mwili wa Marehemu Mama Yake Zitto Kabwe Bi Shida Salum  kuingiza kwenye ndege Tayari kwa safari ya kwenda Kigoma Kwenye mazishi
Prof Ibrahimu Lipumba akijadili jambo na Mwezie baada ya kupakia mwili wa marehemu kwenye ndege kuelekea kigoma Kwenye maziko


Rais wa TASWA Juma Pinto akiwa VIP ya Terminal 1 JKN Airport alipokutana na Cardinal Pengo wakati wa kuaga mwili wa Mama yake Zitto Kabwe
KWA HISANI YA: Dj Sek Blog P.O.BOX Dar es salaam IT DEPARTMENT

Mama Mzazi wa Mh. Zitto Kabwe Afariki Dunia

Mh. Zitto Kabwe amefiwa na mama yake mzazi Bi Shida Salum.  Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema mbinguni. Amen.

KUSOMA KUHUSU MAISHA YA BI SHIDA SALUM BOFYA HAPA:

Taarifa kutoka Facebook:

My mother has just passed away. Inna lillah wainna illaih raajiun
Marehemu Bi Shida Salum, alikuwa mama mzazi wa Mh. Zitto Kabwe
 
  Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe Zitto Kabwe akiwa na mama yake Mama Hajjat Shida Salum, enzi za uhai wake.


Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania, (CHAWATA), Shida Salum, ambaye alikuwa mama mzazi wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na

Maendeleo, CHADEMA, aliyekuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Ami, Masaki, Dar es Salaam akisumbuliwa na maradhi ya saratani, ameaga dunia.

Saturday, December 21, 2013

Hotuba ya Mh. Zitto Kabwe Leo Huko Kigoma

 
Mh. Zitto Kabwe - File Photo


HOTUBA YA MH ZITTO Z. KABWE - KIGOMA – 21 DESEMBA 2013

Leo nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si salamu za kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji. Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.
 
Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995. Kabla ya hapo mlitoa madiwani wengi mwaka 1994. Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi zao na wengine hata ndoa zao katika kupata mbegu ya mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.
 
Na nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si maneno tu ambayo ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na maisha niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule ya Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma. Malezi yangu yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma. Nimekuwa nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu. Viatu hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa na Kampuni ya Bora Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga. Mama Coretha hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la hasha! Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili kwenda la tatu. Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana, upendo na hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania. Uwajibikaji kwani alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona kuwa kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote. Jamii hii ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa bidii kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili katika maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya juu sana.
 
Nikiwa nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka niwakumbushe kwa nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia. Demokrasia ina maana pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wananchi. Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha mwananchi kupata huduma zake stahili kama Elimu, Afya, Maji na miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi wanakufa njaa kwa kukosa ajira na kukuza umasikini. Demokrasia inahusu maendeleo. Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa ndege wa Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo cha Usafirishaji Mwandiga. Asije mtu akasema yeye ndio kafanya haya. Haya ni matunda ya nyinyi watu wa Kigoma kupokea demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu bila kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi wenu kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi lazima ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa makuu.
 
Lakini tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi cha utumishi wangu kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka kwenu,nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa Wananchi. Nakumbuka wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna watu hapa nyumbani walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa Taifa' lakini watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na sio Kigoma tu. Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali kuwa na hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani. Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana. Hii ilitokana sio tu na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za Umma. Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia yetu.
Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.
 
Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.
Kutoaminiana. Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi kikubwa. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania kumi, wanane hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. Wananchi wameacha kutuamini wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe kwa wenyewe. Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli umekuwa ni uongo. Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue kudanganya na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli. Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa zetu. Itachukua muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi yetu kama hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa unatengenezwa badala ya kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na kamati maalum iliyoundwa na Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba chini ya kiapo nilisema sina majina ya watu wenye akaunti huko Uswisi. Huu ulikuwa ni uongo. Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa kamati hata nilipokuwa katika mafunzo ya mgambo huko Tanga na nilikutana nao mara nne. Ni uongo kwa sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki wa mali nje ya nchi kinyumecha sheria. Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja majina haya haina maana sina majina, bali ni kwamba ninaheshimu utaratibu na nimeachia vyombo husika vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi nikianza kuchukua majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati hizi muhimu na hata kupelekea mchakato mzima kuvurugika. Sitaingia mtego huu! Lakini hatua hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa mfano uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya KUTOAMINIANA. 
 
Lakini mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na mawazo tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii ni uhaini. Lakini bila kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama imara wala Taifa imara. Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na uhuru wa mawazo. Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na waliojaa woga. Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia. Bila demokrasia ya uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta. Lazima vyama vya siasa, viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.
 
Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli.
Juzi nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa yanayoendelea ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu. Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na mazungumzo. Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule. Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha mawazo tofauti na hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina misingi yake ambayo sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa siasa ni kuwa inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa. Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.
Na hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo! Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi. Ninasukuwa kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu;kila ninapoona akina mama wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana ambao hawana uhakika wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua chai asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi katika hali hii. Alafu nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na utoroshwaji wa pesa zetu. Hebu sasa linganisheni na ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za kimarekani milioni 1315 (bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni  2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania. Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za kitanzania zipatazo trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani milioni 4526 (bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania trilioni 7,286,860,000,000 (trilioni 7.3).  Nimewatajia hapa namba chungu nzima na matrilioni na mabilioni hayaleti maana. Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa - robo yake tuingeweza kujenga barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka Kigoma mpaka Dar-es-salaam! Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha tunapata huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana wetu. Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya maelfu ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi. Pesa hizi zingeweza kuwanunulia watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya viatu. Sasa nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia macho utoroshwaji wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia ya sisi wabunge kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi au msaliti!
 
Lakini naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za kisiasa jambo la msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea bila sababu. Licha ya kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika mambo haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana mawazo yao, ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje ya Serikali na ndani nanje ya nchi yetu. Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra zake zinakuwa huru.
 
Maisha ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa sababu bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna maendeleo. Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko huleta matumaini. Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi hiki kipya. Siasa za kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya kero za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha; ni siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo. Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za mabadiliko; siasa zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania. Mungu ibariki Tanzania.